Quran Touch

Juzuu 30 (Amma)

An-Naba 78:1 – An-Naas 114:6 · 564 aya

Aa
Neno kwa neno

  1. Sura An-Naba

    سُورَةُ النبإ
  2. 78:1
    ۝١

    WANAULIZANA nini? [1]

    Tanbihi

    [1] Wanaulizana nini hao makafiri?

  3. 78:2
    ۝٢

    Ile khabari kuu! [2]

    Tanbihi

    [2] Wanaulizana khabari kubwa, khabari ya kufufuliwa,

  4. 78:3
    ۝٣

    Ambayo kwayo wanakhitalifiana. [3]

    Tanbihi

    [3] Ambayo wao wamezama ndani yake kukhitalifiana baina ya wenye kuikataa na wenye kuitilia shaka.

  5. 78:4
    ۝٤

    La! Karibu watakuja jua. [4]

    Tanbihi

    [4] Kuwazuia kuulizana huko wanaambiwa kuwa watakuja ujua ukweli wa mambo hapo watapo ona kufufuliwa kumetokea khasa.

  6. 78:5
    ۝٥

    Tena la! Karibu watakuja jua. [5]

    Tanbihi

    [5] Tena kuwazuia, watakuja jua itapo wateremkia adhabu.

  7. 78:6
    ۝٦

    kaKwani hatukuifanya ardhi ma tandiko? [6]

    Tanbihi

    [6] Kwani wao hawaoni Ishara za uweza wetu kwamba Sisi tumeifanya ardhi imetandikwa upatikane utulivu juu yake na iwezekane kutembea juu yake?

  8. 78:7
    ۝٧

    kama Na milima vigingi? [7]

    Tanbihi

    [7] Na tukaifanya milima ni vigingi vya ardhi vya kuituliza? Sehemu ya gamba gumu lilio juu ya ardhi linfikilia kiasi ya kilomita 60 unene wake, na inazidi mikunjo, mifimbi, inapanda juu kuwa milima, na huteremka chini kuwa ni vina vya bahari; na hiyo hulingana kwa sababu ya uzito unao patikana kutokana na milima. Na kulingana huko hakuharibiki ila kwa kubugunyika, kwani gamba kavu la ardhi linazuiliwa na milima, kama vigingi vinavyo zuilia khema. (Rejea Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 7 ya Surat Qaf).

  9. 78:8
    ۝٨

    Na tukakuumbeni kwa jozi? [8]

    Tanbihi

    [8] Na tukakuumbeni kwa jozi, wanaume na wanawake?

  10. 78:9
    ۝٩

    Na tukakufanya kulala kwenu ni mapumziko? [9]

    Tanbihi

    [9] Na tukafanya kulala kwenu ni mapumziko ya machofu ya kazi? Kulala usingizi ni kusita nishat'i ya sehemu ya ubongo yenye kutambua na kuwa macho. Yaani gamba la ubongo, au kupunguka nishat'i yake kwa wingi, ukilinganisha na daraja za nishat'i ya sehemu za viungo vilio baki. Na kwa hivyo kunapunguka nguvu na joto la mwili, tena mwili hapo wakati wa usingizi hupata kutua na kupumzika baada ya kuhangaika viungo au akili au vyote viwili. Basi kazi za kimwili zote hupunguka isipo kuwa kazi za kusaga chakula, na kupitisha mkojo katika mafigo, na kutoka majasho katika ngozi, kwani yakisita hayo hupatikana madhara juu ya maisha ya mtu. Ama kuvuta pumzi huko nako hupunguka, na huwa ni kwa ndani zaidi, na huwa kwa kifua zaidi kuliko kwa tumbo. Na mpigo wa mishipa hupungua kasi kwa kunavyo tokana na moyo, na hudhoofika mkazano wa musulo (muscular tension), na kwa hivyo huwa taabu kupata harakati za kinyume. Na yote haya ni ili binaadamu apate kupumzika wakati wa kulala.

  11. 78:10
    ۝١٠

    Na tukaufanya usiku ni nguo? [10]

    Tanbihi

    [10] Na tumeufanya usiku ni sitara kwenu kwa kiza kinacho kufunikeni.

  12. 78:11
    ۝١١

    Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha? [11]

    Tanbihi

    [11] Na tumeufanya mchana ni wakati wa kuhangaika kwenu kutafuta cha kukusaidieni katika maisha yenu.

  13. 78:12
    ۝١٢

    Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu? [12]

    Tanbihi

    [12] Na tumesimamisha juu yenu mbingu saba zenye nguvu madhubuti.

  14. 78:13
    ۝١٣

    Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto; [13]

    Tanbihi

    [13] Na Sisi tumeliumba jua lenye mwangaza na linalo waka. Makusudio ya Assiraj Alwahhaaj, Taa yenye mwanga na joto, ni Jua. Na hayo kama ilivyo thibiti katika sayansi kuwa daraja ya joto la uso wake inafika daraja 6000. Ama kati yake daraja yake inazidi daraja 30 milioni kwa sababu ya mdidimizo mkubwa unao patikana juu ya madda ziliomo ndani yake. Na jua linatoa nishat'i hizi zifuatazo: 9 katika 100 ya miale ya Ultraviolet rays, 46 katika 100 ya miale ya mwangaza, 45 katika 100 miale ya joto, au Infra red rays. Na kwa hivyo hii Aya tukufu imeliita kuwa ni Taa yenye mwangaza na joto.

  15. 78:14
    ۝١٤

    Na tukateremsha maji yanayo anguka kwa kasi kutoka mawinguni, [14]

    Tanbihi

    [14] Na tumeteremsha kutokana na mawingu yaliyo karibia kunyesha maji yenye kumiminika kwa nguvu. Mvua ndio kitu pekee kinacho toka asli yake maji matamu katika ardhi. Na asli ya mvua ni kukusanyika vijisehemu vya maji yanayo panda kutoka baharini, na maziwa na mito, yakakusanyika kama mawingu na yakageuka chembe za mvua au vipande vya barafu, na khatimaye yakaanguka kwa sura ya mvua au theluji.

  16. 78:15
    ۝١٥

    Ili tutoe kwayo nafaka na mimea. [15]

    Tanbihi

    [15] Ili tutoe kwa maji haya nafaka na mimea kuwa ni chakula kwa ajili ya watu na wanyama.

  17. 78:16
    ۝١٦

    Na mabustani yenye miti iliyo kamatana. [16]

    Tanbihi

    [16] Na mabustani yenye miti iliyo fungamana na matawi yake yameingiliana.

  18. 78:17
    ۝١٧

    Hakika siku ya uamuzi imewekewa wakati wake, [17]

    Tanbihi

    [17] Hakika siku ya uamuzi baina ya viumbe imewekewa miadi ilio kwisha kadiriwa kwa ajili ya kufufuliwa.

  19. 78:18
    ۝١٨

    Siku litapo pulizwa barugumu, nanyi mtakuja kwa makundi, [18]

    Tanbihi

    [18] Siku litakapo pulizwa barugumu na kufufuliwa watu, mtakuja kwenye mkutano makundi kwa makundi.

  20. 78:19
    ۝١٩

    Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango. [19]

    Tanbihi

    [19] Na mbingu zitapasuliwa kila upande hata zitakuwa ni milango milango.

  21. 78:20
    ۝٢٠

    Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi. [20]

    Tanbihi

    [20] Na milima itaondolewa baada ya kung'olewa mwahala mwake, na kuvurugwa, ikawa unaiona kama sura ya milima na hali hiyo ni kifusi tu kilicho rindikwa, kama uonavyo mangati, sarabi, unaona kama sura ya maji nayo si maji.

  22. 78:21
    ۝٢١

    Hakika Jahannamu inangojea! [21]

    Tanbihi

    [21] Hakika Jahannamu imekuwa kama ni kitu kinacho ngojea, walinzi wake wanawangojea watu watakao kuja kuingia.

  23. 78:22
    ۝٢٢

    Kwa walio asi ndio makaazi yao, [22]

    Tanbihi

    [22] Yawe ni marejeo na mafikio kwa wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu.

  24. 78:23
    ۝٢٣

    Wakae humo karne baada ya karne, [23]

    Tanbihi

    [23] Watakaa humo dahari baada ya dahari.

  25. 78:24
    ۝٢٤

    Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji, [24]

    Tanbihi

    [24] Hawataonja humo hata chembe ya upepo wa kuburudisha joto lake, wala kinywaji cha kupoza kiu chao.

  26. 78:25
    ۝٢٥

    Ila maji yamoto sana na usaha, [25]

    Tanbihi

    [25] Lakini watakunywa maji yalio pita ukomo kwa umoto wake, na usaha unao miminika kutokana na ngozi za watu wa Motoni.

  27. 78:26
    ۝٢٦

    Ndio jaza muwafaka. [26]

    Tanbihi

    [26] Malipo ya kuwafikiana na vitendo vyao viovu.

  28. 78:27
    ۝٢٧

    Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu. [27]

    Tanbihi

    [27] Kwani hao hawakutaraji kuwa itakuwapo kuhisabiwa, hata watende ya kuwaokoa humo.

  29. 78:28
    ۝٢٨

    Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu. [28]

    Tanbihi

    [28] Wakazikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuthibitisha kufufuliwa kwa mkadhibisho mkali.

  30. 78:29
    ۝٢٩

    Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika. [29]

    Tanbihi

    [29] Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.

  31. 78:30
    ۝٣٠

    Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu! [30]

    Tanbihi

    [30] Basi onjeni, wala hampati kwetu ila kuzidishiwa adhabu tu.

  32. 78:31
    ۝٣١

    Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu, [31]

    Tanbihi

    [31] Hakika wenye kumcha Mola wao Mlezi watapata kuokoka na adhabu, na wataipata Pepo,

  33. 78:32
    ۝٣٢

    Mabustani na mizabibu, [32]

    Tanbihi

    [32] Na mabustani yenye matunda, na mizabibu mizuri,

  34. 78:33
    ۝٣٣

    Na wake walio lingana nao, [33]

    Tanbihi

    [33] Na wanawari walio watipwatipwa wa hirimu yao,

  35. 78:34
    ۝٣٤

    Na bilauri zilizo jaa, [34]

    Tanbihi

    [34] Na bilauri safi zilizo jaa pomoni,

  36. 78:35
    ۝٣٥

    Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo, [35]

    Tanbihi

    [35] Hawasikii huko Peponi upuuzi wala uwongo.

  37. 78:36
    ۝٣٦

    Malipo kutoka kwa Mola wako Mlezi, kipawa cha kutosha. [36]

    Tanbihi

    [36] Ni malipo kutokana na Mola wako Mlezi, kwa fadhila yake na ihsani ya kutosha.

  38. 78:37
    ۝٣٧

    Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, Arrahman, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake! [37]

    Tanbihi

    [37] Mola Mlezi wa mbinguni na duniani na vilio baina yao, ambaye rehema yake imeenea juu ya kila kitu. Hapana yeyote mwenye madaraka ya kusema mbele yake.

  39. 78:38
    ۝٣٨

    Siku atakapo simama Roho na Malaika kwa safu. Hawatasema ila Mwingi wa rehema aliye mruhusu, na atasema yaliyo sawa tu. [38]

    Tanbihi

    [38] Siku atakapo simama Jibrili na Malaika walio teuliwa nao wamenyenyekea, hasemi mmoja wao ila akipewa idhini na Arrahman, Mwingi wa rehema, kuwa aseme, naye atasema lilio sawa tu.

  40. 78:39
    ۝٣٩

    Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anaye taka na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi [39]

    Tanbihi

    [39] Hiyo ndiyo siku isiyo na shaka. Basi atakaye na ashike njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi arejee kwa Imani, na a'mali njema.

  41. 78:40
    ۝٤٠

    Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapo ona yaliyo tangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: Laiti ningeli kuwa udongo! [40]

    Tanbihi

    [40] Hakika Sisi tumekuhadharisheni na adhabu itakayo tokea karibu, siku atakapo angalia mtu vitendo vyake vilivyo tangulizwa na mikono yake, na atakapo sema kafiri kwa kutamani kuokoka: Laiti ningeli bakia udongo baada ya kufa, nisifufuliwe wala nisihisabiwe!

  42. Sura An-Naazi'aat

    سُورَةُ النازعات
  43. 79:1
    ۝١

    Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu! [1]

    Tanbihi

    [1] Ninaapa kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuving'oa vitu kutokana na pahala pao kwa nguvu,

  44. 79:2
    ۝٢

    Na kwa wanao toa kwa upole! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuvitoa vitu kwa utaratibu na ulaini,

  45. 79:3
    ۝٣

    Na wanao ogelea! [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwa kila kilicho pewa mbio za kutekeleza kazi yake kwa sahala na wepesi.

  46. 79:4
    ۝٤

    Wakishindana mbio! [4]

    Tanbihi

    [4] Na kwa vinavyo shindania kutimiza waajibu ulio twikwa juu yao kushindania kwa juhudi,

  47. 79:5
    ۝٥

    Wakidabiri mambo. [5]

    Tanbihi

    [5] Na vinavyo dabiri, kupanga, mambo na kuyaendesha kwa mujibu wa vilivyo khusishwa,

  48. 79:6
    ۝٦

    Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka! [6]

    Tanbihi

    [6] Bila ya shaka Saa ya Kiyama itafika; hiyo siku ambayo mpulizo wa mwanzo wa barugumu utavitikisa viumbe vyote,

  49. 79:7
    ۝٧

    Kifuate cha kufuatia. [7]

    Tanbihi

    [7] Na mpulizo huo utafuatiwa na wa pili ambao ndio utakao kuwa wa kufufuliwa watu.

  50. 79:8
    ۝٨

    Siku hiyo nyoyo zitapiga piga! [8]

    Tanbihi

    [8] Siku hiyo nyoyo zitapapatika kwa khofu.

  51. 79:9
    ۝٩

    Macho yatainama chini! [9]

    Tanbihi

    [9] Macho ya watu yatakuwa na huzuni, manyonge.

  52. 79:10
    ۝١٠

    Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza? [10]

    Tanbihi

    [10] Watu hawa husema duniani kwa kukanya kufufuliwa: Ati tutarudishwa sisi baada ya kwisha kufa, tuumbwe tena kama tulivyo kuwa?

  53. 79:11
    ۝١١

    Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa? [11]

    Tanbihi

    [11] Tukisha kuwa mafupa yaliyo chakaa, ati tutarejeshwa tufufuliwe upya?

  54. 79:12
    ۝١٢

    Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara! [12]

    Tanbihi

    [12] Wanasema, kwa kukanya na kejeli: Kurejea huko kama kukitokea basi ni marejeo ya khasara, na sisi si watu wa kukhasiri.

  55. 79:13
    ۝١٣

    Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu, [13]

    Tanbihi

    [13] Msidhani kurejea huko ni kuzito. Kwani hayo ni ukelele mmoja tu,

  56. 79:14
    ۝١٤

    Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano! [14]

    Tanbihi

    [14] Mara maiti wote watahudhurishwa kwenye ardhi ya mkusanyiko!

  57. 79:15
    ۝١٥

    Je! Imekufikia hadithi ya Musa? [15]

    Tanbihi

    [15] Ewe Muhammad! Imekufikilia hadithi ya Musa,

  58. 79:16
    ۝١٦

    Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T'uwaa, akamwambia: [16]

    Tanbihi

    [16] Alipo mwita Mola wake Mlezi katika bonde lilio takaswa, linalo itwa "T'uwa"?

  59. 79:17
    ۝١٧

    Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri [17]

    Tanbihi

    [17] Akaambiwa: Nenda kwa Firauni aliye pindukia mpaka katika udhalimu.

  60. 79:18
    ۝١٨

    Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa? [18]

    Tanbihi

    [18] Umwambie: Je! Huelekei kut'ahirika?

  61. 79:19
    ۝١٩

    Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha. [19]

    Tanbihi

    [19] Na mimi nikuongoze upate kumjua Mola wako Mlezi, umwogope.

  62. 79:20
    ۝٢٠

    Basi alimwonyesha Ishara kubwa. [20]

    Tanbihi

    [20] Musa akamwonyesha Firauni miujiza mikubwa.

  63. 79:21
    ۝٢١

    Lakini aliikadhibisha na akaasi. [21]

    Tanbihi

    [21] Lakini Firauni alimkadhibisha Musa kwa aliyo kuja nayo, na akamuasi kwa aliyo mwitia.

  64. 79:22
    ۝٢٢

    Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi. [22]

    Tanbihi

    [22] Kisha akamgeuzia mgongo, akenda kujitahidi kumpinga.

  65. 79:23
    ۝٢٣

    Akakusanya watu akanadi. [23]

    Tanbihi

    [23] Akawakusanya wachawi, na akawaita watu,

  66. 79:24
    ۝٢٤

    Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa. [24]

    Tanbihi

    [24] Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa.

  67. 79:25
    ۝٢٥

    Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo. [25]

    Tanbihi

    [25] Mwenyezi Mungu akampa adhabu kwa kauli yake ya mwisho, nayo ni vile kusema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa. Na akampa adhabu kwa kauli yake ya mwanzo, nayo ni kumkadhibisha Musa a.s.

  68. 79:26
    ۝٢٦

    Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa. [26]

    Tanbihi

    [26] Hakika katika hadithi hiyo yapo mawaidha kwa mwenye kumkhofu Mwenyezi Mungu.

  69. 79:27
    ۝٢٧

    Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga! [27]

    Tanbihi

    [27] Enyi mnao kanya kufufuliwa! Kukuumbeni nyinyi ni taabu zaidi au kuziumba mbingu, kuzikusanya sehemu zake zilio tawanyika mbali mbali,

  70. 79:28
    ۝٢٨

    Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri. [28]

    Tanbihi

    [28] Na kunyanyua kimo chake, na zikakaa sawa hazina tafauti wala ila?

  71. 79:29
    ۝٢٩

    Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake [29]

    Tanbihi

    [29] Na akatia kiza katika usiku wake, na akautokeza mchana wake ukawa na mwangaza?

  72. 79:30
    ۝٣٠

    Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi. [30]

    Tanbihi

    [30] Na ardhi baada ya hayo akaikunjua, na akaisawazisha, ikasilihi kukaliwa na watu wake?

  73. 79:31
    ۝٣١

    Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake, [31]

    Tanbihi

    [31] Akatoa ndani yake maji yake yanayo tibuka katika chemchem zake, na ikamiminika mito yake, na ikawa na mimea yake ya chakula kwa ajili ya watu na wanyama;

  74. 79:32
    ۝٣٢

    Na milima akaisimamisha, [32]

    Tanbihi

    [32] Na milima akaithibitisha imara

  75. 79:33
    ۝٣٣

    Kwa nafuu yenu na mifugo yenu. [33]

    Tanbihi

    [33] Kwa ajili ya manufaa yenu na wanyama wenu mnao wafuga!

  76. 79:34
    ۝٣٤

    Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa, [34]

    Tanbihi

    [34] Kitakapo fika Kiyama ambacho vitisho vyake vitaenea kote,

  77. 79:35
    ۝٣٥

    Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya, [35]

    Tanbihi

    [35] Siku atakapo kumbuka mtu vitendo vyake vya kheri au shari,

  78. 79:36
    ۝٣٦

    Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona, [36]

    Tanbihi

    [36] Na Jahannamu ikadhihirishwa wazi, akaiona kila mwenye macho kuwa ndio malipo,

  79. 79:37
    ۝٣٧

    Basi ama yule aliye zidi ujeuri, [37]

    Tanbihi

    [37] Basi ama mwenye kupita mpaka kwa maasi yake,

  80. 79:38
    ۝٣٨

    Na akakhiari maisha ya dunia, [38]

    Tanbihi

    [38] Na akajichagulia nafsi yake maisha yanayo pita njia,

  81. 79:39
    ۝٣٩

    Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake! [39]

    Tanbihi

    [39] Basi Moto wa Jahannamu unao babua upepo wake ndio makaazi yake wala hana mengineyo.

  82. 79:40
    ۝٤٠

    Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, [40]

    Tanbihi

    [40] Na ama mwenye kukhofu ukubwa na utukufu wa Mola wake Mlezi, na akaizuia nafsi yake na matamanio ya kumpumbaza,

  83. 79:41
    ۝٤١

    Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake! [41]

    Tanbihi

    [41] Basi huyo nyumba ya neema ya Peponi ndio makaazi yake, wala hana penginepo.

  84. 79:42
    ۝٤٢

    Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini? [42]

    Tanbihi

    [42] Ewe Muhammad! Wanakuuliza, ati, khabari za Saa ya Kiyama, itakuwa lini?

  85. 79:43
    ۝٤٣

    Una nini wewe hata uitaje? [43]

    Tanbihi

    [43] Ujuzi wa hayo hauko kwako hata uwatajie.

  86. 79:44
    ۝٤٤

    Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake. [44]

    Tanbihi

    [44] Ujuzi wa hayo uko kwa Mola wako Mlezi tu, si kwa mwenginewe. (Nabii Isa a.s. ambaye Wakristo wanasema ni Mwana wa Mungu, au ndiye Mungu, pia anasimuliwa katika Biblia kuwa hakuijua Saa na Siku ya Kiyama. Injili ya Mathayo inanukulu maneno ya Yesu: "Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.")

  87. 79:45
    ۝٤٥

    Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu. [45]

    Tanbihi

    [45] Kwani waajibu wako ni kuwaonya wanao khofu si kuwatangazia wakati wake.

  88. 79:46
    ۝٤٦

    Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake. [46]

    Tanbihi

    [46] Na wao siku watakayo iona hiyo Saa ya Kiyama ni kama kwamba hawakuishi duniani zaidi kuliko jioni moja tu, au mchana wake.

  89. Sura Abasa

    سُورَةُ عبس
  90. 80:1
    ۝١

    Alikunja kipaji na akageuka! [1]

    Tanbihi

    [1] Uso wake ulitaghayari kwa kuchukia na akageuka,

  91. 80:2
    ۝٢

    Kwa sababu alimjia kipofu! [2]

    Tanbihi

    [2] Kwa sababu kamjia kipofu anamuuliza khabari ya Dini yake.

  92. 80:3
    ۝٣

    Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika? [3]

    Tanbihi

    [3] Na wewe unajuaje, pengine huyo kipofu atatakasika kwa atayo yapata kwako,

  93. 80:4
    ۝٤

    Au atawaidhika, na mawaidha yamfae? [4]

    Tanbihi

    [4] Au atawaidhika na mawaidha yamfae.

  94. 80:5
    ۝٥

    Ama ajionaye hana haja! [5]

    Tanbihi

    [5] Ama yule anaye jiona ametosheka kwa mali yake na nguvu zake,

  95. 80:6
    ۝٦

    Wewe ndio unamshughulikia? [6]

    Tanbihi

    [6] Wewe ndio unamkabili na unamshughulikia kumfikishia wito wako.

  96. 80:7
    ۝٧

    Na si juu yako kama hakutakasika. [7]

    Tanbihi

    [7] Na wewe una lawama gani ikiwa yeye hakutakasika kwa Imani?

  97. 80:8
    ۝٨

    Ama anaye kujia kwa juhudi . [8]

    Tanbihi

    [8] Ama anaye kukimbilia kutafuta ilimu na uwongofu,

  98. 80:9
    ۝٩

    Naye anaogopa! [9]

    Tanbihi

    [9] Naye anamkhofu Mwenyezi Mungu .

  99. 80:10
    ۝١٠

    Ndio wewe unampuuza? [10]

    Tanbihi

    [10] Wewe unampuuza.

  100. 80:11
    ۝١١

    Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana. [11]

    Tanbihi

    [11] Hakika Aya hizi ni mawaidha.

  101. 80:12
    ۝١٢

    Basi anaye penda akumbuke. [12]

    Tanbihi

    [12] Mwenye kutaka atawaidhika kwa Qur'ani.

  102. 80:13
    ۝١٣

    Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa, [13]

    Tanbihi

    [13] Nayo Qur'ani imo katika kurasa zilizo tukuzwa kwa Mwenyezi Mungu,

  103. 80:14
    ۝١٤

    Zilizo inuliwa, zilizo takaswa. [14]

    Tanbihi

    [14] Zina cheo cha juu, na pahala palipo tukuka, zimetakasika na kila upungufu.

  104. 80:15
    ۝١٥

    Zimo mikononi mwa Malaika waandishi, [15]

    Tanbihi

    [15] Katika mikono ya Malaika ambao Mwenyezi Mungu amewafanya ndio mabalozi baina yake na Mitume wake;

  105. 80:16
    ۝١٦

    Watukufu, wema. [16]

    Tanbihi

    [16] Walio bora, wema.

  106. 80:17
    ۝١٧

    Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha? [17]

    Tanbihi

    [17] Ameangamia mwanaadamu! Nini kilicho mfanya akufuru na hali Mwenyezi Mungu amemfanyia hisani zote hizi?

  107. 80:18
    ۝١٨

    Kwa kitu gani amemuumba? [18]

    Tanbihi

    [18] Hakumbuki yeye kaumbwa kutokana na nini?

  108. 80:19
    ۝١٩

    Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria. [19]

    Tanbihi

    [19] Kutokana na maji ya kudharauliwa Yeye Mwenyezi Mungu alimwanzisha kumuumba akamjaalia apitie daraja mbali mbali za kukua.

  109. 80:20
    ۝٢٠

    Kisha akamsahilishia njia. [20]

    Tanbihi

    [20] Kisha akamfanyia nyepesi njia ya kufikia Imani, na akamfunza njia hiyo.

  110. 80:21
    ۝٢١

    Kisha akamfisha, akamtia kaburini. [21]

    Tanbihi

    [21] Kisha akamfisha na akamtukuza kwa kumtia kaburini.

  111. 80:22
    ۝٢٢

    Kisha apendapo atamfufua. [22]

    Tanbihi

    [22] Na tena akipenda atamhuisha baada ya kufa kwake.

  112. 80:23
    ۝٢٣

    La! Hajamaliza aliyo muamuru. [23]

    Tanbihi

    [23] Ni kweli mwanaadamu, juu ya kuwa umri wake mrefu duniani, hakutimiza aliyo amrishwa na Mwenyezi Mungu katika mambo ya Imani na ut'iifu.

  113. 80:24
    ۝٢٤

    Hebu mtu na atazame chakula chake. [24]

    Tanbihi

    [24] Hebu mtu na aangalie shani ya chakula chake - vipi tulivyo kipanga na kumsahilishia!

  114. 80:25
    ۝٢٥

    Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu, [25]

    Tanbihi

    [25] Ni Sisi tumeiteremsha mvua kutoka mbinguni, ikateremka.

  115. 80:26
    ۝٢٦

    Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, [26]

    Tanbihi

    [26] Tena tukaipasua pasua ardhi kwa ajili ya mimea.

  116. 80:27
    ۝٢٧

    Kisha tukaotesha humo nafaka, [27]

    Tanbihi

    [27] Tukaotesha humo nafaka ambazo watu huzila na huweka akiba.

  117. 80:28
    ۝٢٨

    Na zabibu, na mimea ya majani, [28]

    Tanbihi

    [28] Na mizabibu na mimea ya majani inayo liwa mibichi.

  118. 80:29
    ۝٢٩

    Na mizaituni, na mitende, [29]

    Tanbihi

    [29] Na mizaituni mizuri, na mitende yenye kuzaa,

  119. 80:30
    ۝٣٠

    Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara, [30]

    Tanbihi

    [30] Na mabustani yaliyo songamana matawi ya miti yake,

  120. 80:31
    ۝٣١

    Na matunda, na malisho ya wanyama; [31]

    Tanbihi

    [31] Na matunda ya kustaladhi nayo, na malisha ya kula nyama hoa (mifugo).

  121. 80:32
    ۝٣٢

    Kwa manufaa yenu na mifugo yenu. [32]

    Tanbihi

    [32] Tumeotesha yote hayo kwa ajili ya faida yenu na wanyama wenu wa kufuga.

  122. 80:33
    ۝٣٣

    Basi utakapo kuja ukelele, [33]

    Tanbihi

    [33] Basi utakapo kuja ukelele wa Kiyama utakao tia uziwi masikio,

  123. 80:34
    ۝٣٤

    Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, [34]

    Tanbihi

    [34] Siku mtu atakapo mkimbia ndugu yake,

  124. 80:35
    ۝٣٥

    Na mamaye na babaye, [35]

    Tanbihi

    [35] Na mama yake, na baba yake,

  125. 80:36
    ۝٣٦

    Na mkewe na wanawe. [36]

    Tanbihi

    [36] Na mkewe, na wanawe!

  126. 80:37
    ۝٣٧

    Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha [37]

    Tanbihi

    [37] Kila mmojapo katika hawa atakuwa na jambo lake la kumshughulisha!

  127. 80:38
    ۝٣٨

    Siku hiyo ziko nyuso zitazo nawiri, [38]

    Tanbihi

    [38] Zipo nyuso siku hii zenye mwangaza,

  128. 80:39
    ۝٣٩

    Zitacheka, zitachangamka; [39]

    Tanbihi

    [39] Zenye kung'ara na kufurahi kwa neema za Mwenyezi Mungu.

  129. 80:40
    ۝٤٠

    Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi, [40]

    Tanbihi

    [40] Na nyuso nyengine siku hii zina vumbi zimesawijika.

  130. 80:41
    ۝٤١

    Giza totoro litazifunika, [41]

    Tanbihi

    [41] Zimegubikwa na kiza na weusi.

  131. 80:42
    ۝٤٢

    Hao ndio makafiri watenda maovu [42]

    Tanbihi

    [42] Wenye nyuso hizi ni makafiri wapotovu, ambao walio kuwa hawabali maasi waliyo kuwa wakiyatenda.

  132. Sura At-Takwir

    سُورَةُ التكوير
  133. 81:1
    ۝١

    Jua litakapo kunjwa! [1]

    Tanbihi

    [1] Jua litakapo kunjwa na mwangaza wake ukafutwa,

  134. 81:2
    ۝٢

    Na nyota zikazimwa! [2]

    Tanbihi

    [2] Na nyota ikazimwa nuru yao,

  135. 81:3
    ۝٣

    Na milima ikaondolewa! [3]

    Tanbihi

    [3] Na milima ikaondoshwa hapo ilipo,

  136. 81:4
    ۝٤

    Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe, [4]

    Tanbihi

    [4] Na ambao wa kuchukua mimba wakaharibu mimba zao,

  137. 81:5
    ۝٥

    Na wanyama wa mwituni wakakusanywa! [5]

    Tanbihi

    [5] Na nyama mwitu wakusanywe kutoka vichakani mwao na mashimoni mwao, hawajijui hawajitambui kwa wingi wa kufazaika.

  138. 81:6
    ۝٦

    Na bahari zikawaka moto! [6]

    Tanbihi

    [6] Na bahari zikawa zinawaka moto,

  139. 81:7
    ۝٧

    Na nafsi zikaunganishwa! [7]

    Tanbihi

    [7] Na roho zikaunganishwa na viwiliwili vyao,

  140. 81:8
    ۝٨

    Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa! [8]

    Tanbihi

    [8] Na mtoto wa kike aliye zikwa hai, akaulizwa kwa kumliwaza yeye, na kumshutumu aliye mzika hai,

  141. 81:9
    ۝٩

    Kwa kosa gani aliuliwa? [9]

    Tanbihi

    [9] Kwa makosa gani kauliwa, naye hana dhambi? (Ilikuwa ada ya makafiri wa Kiarabu kabla ya Uislamu kuwazika watoto wao wa kike nao wahai! Baadhi ya Mabaniani wanawauwa watoto wao wa kike hata hivi leo huko India!!)

  142. 81:10
    ۝١٠

    Na madaftari yatakapo enezwa, [10]

    Tanbihi

    [10] Na nyaraka zilizo andikwa ndani vitendo vya watu zikakunjuliwa wakati wa hisabu.

  143. 81:11
    ۝١١

    Na mbingu itapo tanduliwa, [11]

    Tanbihi

    [11] Na mbingu itapo ondoshwa pahala pake,

  144. 81:12
    ۝١٢

    Na Jahannamu itapo chochewa, [12]

    Tanbihi

    [12] Na Moto ukawashwa kwa mwako mkali,

  145. 81:13
    ۝١٣

    Na Pepo ikasogezwa, [13]

    Tanbihi

    [13] Na Pepo ikajongezwa ikawa karibu,

  146. 81:14
    ۝١٤

    Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha. [14]

    Tanbihi

    [14] Yatakapo tokea yote hayo, basi hapo tena kila nafsi itajua nini iliyo tanguliza, ikiwa kheri au shari.

  147. 81:15
    ۝١٥

    Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma, [15]

    Tanbihi

    [15] Naapa kiapo cha mkazo kwa nyota ambazo zinanywea zinapo chomoza, na hapo mwanga wake huwa khafifu,

  148. 81:16
    ۝١٦

    Zinazo kwenda, kisha zikajificha, [16]

    Tanbihi

    [16] Zenye kwenda na hujificha wakati wa kuchwa kwake, kama paa wanapo jificha kwenye mapango yao.

  149. 81:17
    ۝١٧

    Na kwa usiku unapo pungua, [17]

    Tanbihi

    [17] Na kwa usiku linapo pungua giza lake wakati unapo malizika.

  150. 81:18
    ۝١٨

    Na kwa asubuhi inapo pambazuka, [18]

    Tanbihi

    [18] Na kwa asubuhi unapo anza mwangaza wake na ukavuma upepo wake,

  151. 81:19
    ۝١٩

    Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, [19]

    Tanbihi

    [19] Hakika Qur'ani bila ya shaka ni kauli ya Mjumbe anaye toka kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mwenye kuhishimiwa kwake,

  152. 81:20
    ۝٢٠

    Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi, [20]

    Tanbihi

    [20] Mwenye nguvu katika kutekeleza waajibu wake, mwenye cheo na daraja mbele ya Mwenyezi Mungu Mwenye Kiti cha Enzi.

  153. 81:21
    ۝٢١

    Anaye t'iiwa, tena muaminifu. [21]

    Tanbihi

    [21] Tena ni mwenye kut'iiwa, na muaminifu wa kuchukua wahyi miongoni wa walio juu.

  154. 81:22
    ۝٢٢

    Na wala huyu mwenzenu hana wazimu. [22]

    Tanbihi

    [22] Na huyo Mtume wenu ambaye ni mwenzenu, mnaye mjua kuwa ana akili timamu, si mwendawazimu.

  155. 81:23
    ۝٢٣

    Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi. [23]

    Tanbihi

    [23] Na ninaapa kuwa Muhammad s.a.w. bila ya shaka alimwona Jibrili katika upeo wa macho kwa mujibu wa inavyo onekana.

  156. 81:24
    ۝٢٤

    Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu. [24]

    Tanbihi

    [24] Na Muhammad si bakhili wa kufikisha wahyi na kuwafunza watu.

  157. 81:25
    ۝٢٥

    Wala hii si kauli ya Shetani maluuni. [25]

    Tanbihi

    [25] Wala huu wahyi (ufunuo) ulio teremshwa juu yake si kauli ya Shetani aliye fukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.

  158. 81:26
    ۝٢٦

    Basi mnakwenda wapi? [26]

    Tanbihi

    [26] Basi njia gani iliyo ya uwongofu zaidi kuliko hii mnayo ifuata?

  159. 81:27
    ۝٢٧

    Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. [27]

    Tanbihi

    [27] Qur'ani si chochote ila ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote.

  160. 81:28
    ۝٢٨

    Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa. [28]

    Tanbihi

    [28] Kwa anaye taka, miongoni mwenu, kusimama sawa kufikilia haki na kweli.

  161. 81:29
    ۝٢٩

    Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. [29]

    Tanbihi

    [29] Na nyinyi hamwezi kutaka kitu ila anapo taka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  162. Sura Al-Infitaar

    سُورَةُ الإنفطار
  163. 82:1
    ۝١

    Mbingu itapo chanika! [1]

    Tanbihi

    [1] Itakapo pasuka mbingu,

  164. 82:2
    ۝٢

    Na nyota zitapo tawanyika! [2]

    Tanbihi

    [2] Na nyota zitakapo pukutika na kutawanyika,

  165. 82:3
    ۝٣

    Na bahari zitakapo pasuliwa! [3]

    Tanbihi

    [3] Na bahari zikafurika na kuingiliana kwa kuondoka viziwizi baina yao,

  166. 82:4
    ۝٤

    Na makaburi yatapo fukuliwa! [4]

    Tanbihi

    [4] Na makaburi yakafunuliwa na wakatoka maiti walio kuwamo,

  167. 82:5
    ۝٥

    Hapo kila nafsi itajua ilicho tanguliza, na ilicho bakisha nyuma. [5]

    Tanbihi

    [5] Hapo basi kila nafsi itajua nini kheri au shari iliyo tanguliza na iliyo chelewesha.

  168. 82:6
    ۝٦

    Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu? [6]

    Tanbihi

    [6] Ewe mwanaadamu! Kitu gani kilicho kukhadaa wewe na Mola wako Mlezi Mtukufu hata ukafanya jeuri ya kwenda kumuasi? (Ni dhaahiri kuwa Sayyid Abdulla bin Ali bin Nassir aliye tunga utenzi wa Kiswahili maarufu uitwao Al Inkishaf aliiwaza Aya hii alipo tunga ubeti huu: Moyo wangu nini huzundukani Likughurielo hela ni nni? Hunelezi nami kalibaini Liwapo na sura nisikataye )

  169. 82:7
    ۝٧

    Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha! [7]

    Tanbihi

    [7] Mungu wako huyo ndiye aliye kuumba nawe hukuwa chochote, akakuumba na viungo vya kukuletea manufaa, akakufanya umenyooka kwa umbo sawa sawa.

  170. 82:8
    ۝٨

    Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga. [8]

    Tanbihi

    [8] Akakujenga na akakuleta katika sura yoyote aliyo itaka.

  171. 82:9
    ۝٩

    Sivyo hivyo! Bali nyinyi mnaikanusha Siku ya Malipo. [9]

    Tanbihi

    [9] Hamwachi? Bali nyinyi mnakadhibisha malipo ya Siku ya Kiyama!

  172. 82:10
    ۝١٠

    Na hakika bila ya shaka wapo walinzi juu yenu, [10]

    Tanbihi

    [10] Na hakika wapo juu yenu Malaika walinzi, ambao ni waheshimiwa kwetu,

  173. 82:11
    ۝١١

    Waandishi wenye hishima, [11]

    Tanbihi

    [11] Wanasajili vitendo vyenu vyote mvitendavyo, vya kheri na shari.

  174. 82:12
    ۝١٢

    Wanayajua mnayo yatenda. [12]

    Tanbihi

    [12] Wanayajua mnayo yafanya ya kheri na ya shari

  175. 82:13
    ۝١٣

    Hakika wema bila ya shaka watakuwa katika neema, [13]

    Tanbihi

    [13] Hakika wale walio ni wa kweli katika Imani yao wapo katika neema kubwa.

  176. 82:14
    ۝١٤

    Na hakika waovu bila ya shaka watakuwa Motoni; [14]

    Tanbihi

    [14] Na hakika walio iacha amri ya Mwenyezi bila ya shaka watakuwa katika Moto unao unguza,

  177. 82:15
    ۝١٥

    Wataingia humo Siku ya Malipo. [15]

    Tanbihi

    [15] Wataingia humo Siku ya Malipo.

  178. 82:16
    ۝١٦

    Na hawatoacha kuwamo humo. [16]

    Tanbihi

    [16] Na wala hawatatoka katika Jahannamu!

  179. 82:17
    ۝١٧

    Na nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani? [17]

    Tanbihi

    [17] Na nini kitakujuvya ni nini hiyo Siku ya Malipo, na mambo yake yamepindukia ujuzi wako na fikra zako?

  180. 82:18
    ۝١٨

    Tena nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani? [18]

    Tanbihi

    [18] Tena ni nini kitacho kujuvya ni nini hiyo Siku ya Malipo kwa vitisho vyake na shida zake?

  181. 82:19
    ۝١٩

    Siku ambayo nafsi haitakuwa na madaraka yoyote juu ya nafsi; na amri yote siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu tu. [19]

    Tanbihi

    [19] Siku ambayo nafsi haitakuwa na mamlaka yoyote juu ya nafsi ya kuifaa au kuidhuru; na amri yote siku hiyo itakuwa ni ya Mwenyezi Mungu peke yake!

  182. Sura Al-Mutaffifin

    سُورَةُ المطففين
  183. 83:1
    ۝١

    Ole wao hao wapunjao! [1]

    Tanbihi

    [1] Wataangamia wanao punja,

  184. 83:2
    ۝٢

    Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe. [2]

    Tanbihi

    [2] Ambao wakijipimia wenyewe kwa watu hujitwalia ya kutosha na kuzidi,

  185. 83:3
    ۝٣

    Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza. [3]

    Tanbihi

    [3] Na wakiwapimia watu kwa vipimo au mizani huwapunguzia haki yao wanayo stahiki, kwa dhulma!

  186. 83:4
    ۝٤

    Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa . [4]

    Tanbihi

    [4] Hivyo haiwapitikii katika akili zao hawa wanao punja wenzao kwamba watakuja fufuliwa,

  187. 83:5
    ۝٥

    Katika Siku iliyo kuu! [5]

    Tanbihi

    [5] Katika siku ya vitisho vikuu?

  188. 83:6
    ۝٦

    Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote? [6]

    Tanbihi

    [6] Siku watapo simama watu kwa amri ya Mola Mlezi wa walimwengu wote na hukumu yake?

  189. 83:7
    ۝٧

    Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin. [7]

    Tanbihi

    [7] Wacheni kupunja, na kughafilika na kufufuliwa! Kwani hakika waliyo andikiwa wakosefu katika a'mali zao mbovu, bila ya shaka yamo katika Sijjin.

  190. 83:8
    ۝٨

    Unajua nini Sijjin? [8]

    Tanbihi

    [8] Na nini kitakujuvya nini hiyo Sijjin?

  191. 83:9
    ۝٩

    Kitabu kilicho andikwa. [9]

    Tanbihi

    [9] Hicho ni Kitabu kilicho pigwa mistari baina ya maandishi yake.

  192. 83:10
    ۝١٠

    Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha! [10]

    Tanbihi

    [10] Wataangamia wanao kadhibisha siku itapo kuwa kufufuliwa na kuhisabiwa.

  193. 83:11
    ۝١١

    Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo. [11]

    Tanbihi

    [11] Ambao wanaikanusha Siku ya Malipo.

  194. 83:12
    ۝١٢

    Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi. [12]

    Tanbihi

    [12] Na wala haikanushi Siku ya Malipo ila kila mwenye kupindukia mipaka mwingi wa madhambi.

  195. 83:13
    ۝١٣

    Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale! [13]

    Tanbihi

    [13] Na akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu zenye kutaja kuwepo malipo husema: Huo ni uwongo wa walio tangulia!

  196. 83:14
    ۝١٤

    Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma. [14]

    Tanbihi

    [14] Ewe uliye kiuka mipaka! Wacha kauli hiyo potovu. Bali nyoyo za wenye kupindukia mipaka imegubikwa na ukafiri na maasi waliyo yatenda.

  197. 83:15
    ۝١٥

    Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi. [15]

    Tanbihi

    [15] Hakika ni kweli kuwa hao wanao kadhibisha watazuiliwa siku hiyo rehema ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya maasi waliyo yachuma.

  198. 83:16
    ۝١٦

    Kisha wataingia Motoni! [16]

    Tanbihi

    [16] Kisha hakika hao bila ya shaka wataingia Motoni.

  199. 83:17
    ۝١٧

    Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha. [17]

    Tanbihi

    [17] Kisha wataambiwa kwa kuwakebehi: Hii basi ndiyo adhabu inayo kuteremkieni ambayo mlikuwa mkiikanusha duniani!

  200. 83:18
    ۝١٨

    Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I'liyyin. [18]

    Tanbihi

    [18] Ni hakika kuwa vitendo vya watu wema bila ya shaka vimeandikwa katika I'liyyin.

  201. 83:19
    ۝١٩

    Na nini kitakacho kujuvya nini I'liyyin? [19]

    Tanbihi

    [19] Na nini cha kukujuvya nini I'liyyin?

  202. 83:20
    ۝٢٠

    Kitabu kilicho andikwa. [20]

    Tanbihi

    [20] Hicho ni Kitabu kilicho andikwa wazi maandishi yake,

  203. 83:21
    ۝٢١

    Wanakishuhudia walio karibishwa. [21]

    Tanbihi

    [21] Wanakihudhurisha na kukihifadhi Malaika walio kurubishwa.

  204. 83:22
    ۝٢٢

    Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema. [22]

    Tanbihi

    [22] Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema za Peponi,

  205. 83:23
    ۝٢٣

    Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia. [23]

    Tanbihi

    [23] Juu ya viti vya enzi, wakiziangalia neema na ukarimu alio wakirimu Mwenyezi Mungu.

  206. 83:24
    ۝٢٤

    Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema, [24]

    Tanbihi

    [24] Utaona katika nyuso zao uchangamfu na mng'aro wa neema.

  207. 83:25
    ۝٢٥

    Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri, [25]

    Tanbihi

    [25] Wakinyweshwa kinywaji safi kilicho hifadhiwa;

  208. 83:26
    ۝٢٦

    Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana. [26]

    Tanbihi

    [26] Kuhifadhiwa huko hakukuzidisha ila uzuri wake. Na kupata neema hizo, basi, na washindanie wanao shindana.

  209. 83:27
    ۝٢٧

    Na mchanganyiko wake ni Tasniim, [27]

    Tanbihi

    [27] Cha kuchanganyia kinywaji hicho ni maji ya Tasniim ya Peponi,

  210. 83:28
    ۝٢٨

    Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa. [28]

    Tanbihi

    [28] Nayo ni chemchem wanao inywa walio kurubishwa si wengineo, katika watu wa Peponi.

  211. 83:29
    ۝٢٩

    Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini. [29]

    Tanbihi

    [29] Wale walio kuwa wakibeba madhambi kuipingia Dini walikuwa wakiwacheka kuwakejeli Waumini duniani.

  212. 83:30
    ۝٣٠

    Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana. [30]

    Tanbihi

    [30] Na wakipita Waumini mbele yao basi wao hukonyezana kwa kuwabeza.

  213. 83:31
    ۝٣١

    Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi. [31]

    Tanbihi

    [31] Na hao wakosefu wakirejea kwa ahali zao hurejea kwa furaha na kuona ladha kwa vile kuwakejeli Waumini.

  214. 83:32
    ۝٣٢

    Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea. [32]

    Tanbihi

    [32] Na wakiwaona Waumini husema: Ama hakika hawa wamepotea kweli kwa kumuamini Muhammad.

  215. 83:33
    ۝٣٣

    Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao. [33]

    Tanbihi

    [33] Wala hao wakosefu hawakutumwa wawe wa kuwahukumu Waumini kwa kuwaongoza au kuwapoteza, wala kuwa ni walinzi wa vitendo vyao.

  216. 83:34
    ۝٣٤

    Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri, [34]

    Tanbihi

    [34] Basi Siku ya Malipo walio amini watakuwa ndio wa kuwacheka hao makafiri kwa kuwalipizia kile kicheko chao na kejeli yao ya duniani.

  217. 83:35
    ۝٣٥

    Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia. [35]

    Tanbihi

    [35] Ilhali wako juu ya vitanda na matakia watakuwa Waumini wakiziangalia neema za Mwenyezi Mungu alizo wapa.

  218. 83:36
    ۝٣٦

    Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda? [36]

    Tanbihi

    [36] Je! Makafiri watalipwa huko Akhera kwa waliyo yatenda duniani?

  219. Sura Al-Inshiqaaq

    سُورَةُ الإنشقاق
  220. 84:1
    ۝١

    Itapo chanika mbingu! [1]

    Tanbihi

    [1] Mbingu itapo chanika, ikaamrishwa iondoke,

  221. 84:2
    ۝٢

    Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza! [2]

    Tanbihi

    [2] Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi na ikamt'ii, na ndio maelekeo yake isikie na kut'ii,

  222. 84:3
    ۝٣

    Na ardhi itakapo tanuliwa! [3]

    Tanbihi

    [3] Na ardhi ikazidi upana wake kwa kulazwa milima na kuondolewa kifusi chake,

  223. 84:4
    ۝٤

    Na kuvitoa vilivyo kuwa ndani yake, ikawa tupu! [4]

    Tanbihi

    [4] Na ardhi ikatoa nje maiti na khazina ziliyo kuwamo ndani yake, na ikaachana navyo vyote hivyo,

  224. 84:5
    ۝٥

    Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza! [5]

    Tanbihi

    [5] Na ikamwelekea Mola wake Mlezi kwa kuzidi kutanuka kwake na kutoa vilio kuwemo ndani yake na kuachana navyo, na hayo ni haki yake kuwa. Yakitokea yote hayo yaliyo tangulia kusimuliwa basi kila mtu atapata malipo ya vitendo vyake.

  225. 84:6
    ۝٦

    Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta. [6]

    Tanbihi

    [6] Ewe mtu! Hakika wewe unafanya juhudi katika vitendo vyako vikufikishie lengo lako. Basi utakuja kukutana na Mola wako Mlezi kwa a'mali yako, naye atakulipa kwayo.

  226. 84:7
    ۝٧

    Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia! [7]

    Tanbihi

    [7] Ama mwenye kupewa daftari la vitendo vyake kwa mkono wake wa kulia

  227. 84:8
    ۝٨

    Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi! [8]

    Tanbihi

    [8] Basi atahisabiwa kwa hisabu nyepesi,

  228. 84:9
    ۝٩

    Na arudi kwa ahali zake na furaha. [9]

    Tanbihi

    [9] Na atarejea kwa jamaa zake Waumini naye furahani.

  229. 84:10
    ۝١٠

    Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, [10]

    Tanbihi

    [10] Ama mwenye kupewa daftari lake kwa mkono wa kushoto wake nyuma ya mgongo wake kwa kudharauliwa shani yake,

  230. 84:11
    ۝١١

    Basi huyo ataomba kuteketea. [11]

    Tanbihi

    [11] Huyo atatamani ajiue,

  231. 84:12
    ۝١٢

    Na ataingia Motoni. [12]

    Tanbihi

    [12] Na ataingia Motoni aungulie mbali!

  232. 84:13
    ۝١٣

    Hakika alikuwa furahani kati ya jamaa zake. [13]

    Tanbihi

    [13] Kwani huyo hakika duniani alikuwa furahani kati ya jamaa zake akitanaamu na pumbao alilo kuwa nalo hata akapuuza a'mali ya kuitenda kwa mustakabali wake.

  233. 84:14
    ۝١٤

    Huyo hakika alidhani kuwa hatarejea tena. [14]

    Tanbihi

    [14] Hakika huyo alidhani kuwa kabisa hatorejea kwa Mwenyezi Mungu akamhisabu.

  234. 84:15
    ۝١٥

    Kwani? Hakika Mola wake Mlezi alikuwa akimwona! [15]

    Tanbihi

    [15] Bali atarejea, na atahisabiwa! Kwani Mola wake Mlezi alikuwa anamwona vyema yeye na vitendo vyake.

  235. 84:16
    ۝١٦

    Basi ninaapa kwa wekundu wa jua linapo kuchwa, [16]

    Tanbihi

    [16] Basi naapa kiapo cha mkazo kwa wekundu wa mbingu baada ya kuchwa jua!

  236. 84:17
    ۝١٧

    Na kwa usiku na unavyo vikusanya, [17]

    Tanbihi

    [17] Na kwa usiku na unavyo vikusanya vyote katika giza lake, wanaadamu, wanyama na vyenginevyo!

  237. 84:18
    ۝١٨

    Na kwa mwezi unapo pevuka, [18]

    Tanbihi

    [18] Na mwezi unapo kamilika kupevuka na kutimia nuru yake,

  238. 84:19
    ۝١٩

    Lazima mtapanda t'abaka kwa t'abaka! [19]

    Tanbihi

    [19] Hapana shaka yoyote mtakutana na hali baada ya hali, baadhi yake zina shida zaidi kuliko nyenginezo, za kufa na kufufuliwa na vitisho vya Kiyama.

  239. 84:20
    ۝٢٠

    Basi wana nini hawaamini? [20]

    Tanbihi

    [20] Wana nini hawa makafiri yanayo wazuia wasimuamini Mwenyezi Mungu na kufufuliwa baada ya kuwekwa wazi dalili zake zote za kuwajibika kwake?

  240. 84:21 ۩ Sijida
    ۝٢١

    Na wanapo somewa Qur'ani hawasujudu? [21]

    Tanbihi

    [21] Na pindi wakizisikia Aya za Qur'ani hawasujudu wakanyenyekea?

  241. 84:22
    ۝٢٢

    Bali walio kufuru wanakanusha tu. [22]

    Tanbihi

    [22] Bali watu hawa, kwa ukafiri wao, wanakanusha kwa inadi na kutakabari kuikataa Haki!

  242. 84:23
    ۝٢٣

    Na Mwenyezi Mungu anajua wanayo yadhamiria. [23]

    Tanbihi

    [23] Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kabisa hayo wanayo yadhamiria katika nyoyo zao.

  243. 84:24
    ۝٢٤

    Basi wabashirie adhabu chungu! [24]

    Tanbihi

    [24] Basi wabashirie, kwa kejeli, kuwa watapata adhabu ya kutia uchungu.

  244. 84:25
    ۝٢٥

    Isipo kuwa wale walio amini na wakatenda mema; hao watakuwa na ujira usio malizika. [25]

    Tanbihi

    [25] Lakini walio amini na wakatenda mema watapata, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ujira usio wakatikia na wala usio kuwa na hisabu juu yao.

  245. Sura Al-Burooj

    سُورَةُ البروج
  246. 85:1
    ۝١

    Naapa kwa mbingu yenye Buruji! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa mbingu yenye Buruj au Manaazil, njia au vituo ambavyo nyota hupitia katika nyendo zake, Buruuj au Manaazil ndio huu mkusanyiko wa nyota unao onekana kwa sura namna mbali mbali mbinguni. Hizo Buruuj zimegawika sehemu kumi na mbili ambazo ardhi inazipitia inapo lizunguka jua.

  247. 85:2
    ۝٢

    Na kwa siku iliyo ahidiwa! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa Siku iliyo ahidiwa kuwa ndiyo Siku ya Hisabu na Malipo,

  248. 85:3
    ۝٣

    Na kwa shahidi na kinacho shuhudiwa! [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwa viumbe watao hudhuria Siku hiyo wakaona vitisho na ajabu zitakazo kuwepo,

  249. 85:4
    ۝٤

    Wameangamizwa watu wa makhandaki. [4]

    Tanbihi

    [4] Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani watu walio chimba khandaki katika ardhi,

  250. 85:5
    ۝٥

    Yenye moto wenye kuni nyingi! [5]

    Tanbihi

    [5] Wakawasha moto kuwatumbukiza ndani yake Waumini ili kuwatesa,

  251. 85:6
    ۝٦

    Walipo kuwa wamekaa hapo! [6]

    Tanbihi

    [6] Na wao wamekaa ukingoni mwake wakishuhudia mateso yanayo wapata Waumini.

  252. 85:7
    ۝٧

    Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini. [7]

    Tanbihi

    [7] Na wao wapo hapo wamehudhuria kwenye mateso wanayo watendea Waumini.

  253. 85:8
    ۝٨

    Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa! [8]

    Tanbihi

    [8] Na hapana walilo lichukia kwa hao Waumini ila ni kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu ambaye adhabu yake huogopwa, Msifiwa anaye tarajiwa thawabu zake.

  254. 85:9
    ۝٩

    Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu. [9]

    Tanbihi

    [9] Ambaye, peke yake, ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi anashuhudia yote wayatendayo Waumini na makafiri na atawalipa kwayo.

  255. 85:10
    ۝١٠

    Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua. [10]

    Tanbihi

    [10] Hakika walio watia matatani Waumini wanaume na Waumini wanawake kwa maudhi na kuwaadhibu kwa moto, kisha wasitubu na kurejea nyuma watapata Akhera adhabu ya Jahannamu kwa ukafiri wao, na watapata adhabu ya kuunguzwa kwa kule kuwaunguza moto Waumini.

  256. 85:11
    ۝١١

    Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa. [11]

    Tanbihi

    [11] Hakika hao walio kusanya kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu vitendo vyema watapata Mabustani yapitayo mito kati yake. Neema hiyo waliyo lipwa ni kufuzu kukubwa.

  257. 85:12
    ۝١٢

    Hakika kutesa kwa Mola wako Mlezi ni kukali. [12]

    Tanbihi

    [12] Hakika mshiko wa Mola wako Mlezi kuwashika majabari umefika ukomo kwa ukali wake

  258. 85:13
    ۝١٣

    Yeye ndiye anaye anzisha na ndiye anaye rejeza tena, [13]

    Tanbihi

    [13] Ni Yeye peke yake ndiye Mwenye kuanza kuumba, na kisha ni Yeye anaye rejeza tena,

  259. 85:14
    ۝١٤

    Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi, [14]

    Tanbihi

    [14] Na Yeye ni Mwingi wa msamaha kwa mwenye kutubu na akarejea, na Mwingi wa mapenzi kwa mwenye kumpenda na akamt'ii.

  260. 85:15
    ۝١٥

    Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu, [15]

    Tanbihi

    [15] Yeye ndiye Mwenye Kiti cha Enzi na Mwenye kukimiliki, na Mkuu kwa dhati yake na sifa zake.

  261. 85:16
    ۝١٦

    Atendaye ayatakayo. [16]

    Tanbihi

    [16] Ni Mtendaji kwa alitakalo, na hendi kinyume na uweza wake yeyote anaye taka.

  262. 85:17
    ۝١٧

    Je! Zimekuwasilia khabari za majeshi? [17]

    Tanbihi

    [17] Je! Imekujia, ewe Muhammad, hadithi ya kile kikundi kilicho a'si katika mataifa yaliyo kwisha pita?

  263. 85:18
    ۝١٨

    Ya Firauni na Thamudi? [18]

    Tanbihi

    [18] Kaumu ya Firauni na Thamudi na yaliyo washukia katika malipo ya kushikilia kwao upotovu?

  264. 85:19
    ۝١٩

    Lakini walio kufuru wamo katika kukadhibisha. [19]

    Tanbihi

    [19] Bali hao makafiri katika kaumu yako ni shadidi zaidi katika kukukadhibisha kuliko hawa walivyo wakadhibisha Mitume wao.

  265. 85:20
    ۝٢٠

    Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka. [20]

    Tanbihi

    [20] Na Mwenyezi Mungu anawaweza hao, na anawajua vilivyo.

  266. 85:21
    ۝٢١

    Bali hii ni Qur'ani tukufu [21]

    Tanbihi

    [21] Bali hii ulio waletea ni Qur'ani tukufu inadhihirisha hoja za ukweli wako.

  267. 85:22
    ۝٢٢

    Katika Ubao Ulio Hifadhiwa. [22]

    Tanbihi

    [22] Imo katika Ubao Ulio Hifadhiwa, hapana uwezo unao weza kuipotoa au kuigeuza

  268. Sura At-Taariq

    سُورَةُ الطارق
  269. 86:1
    ۝١

    Naapa kwa mbingu na Kinacho kuja usiku! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa mbingu na nyota inayo tokeza usiku!

  270. 86:2
    ۝٢

    Na nini kitakacho kujuulisha ni nini hicho Kinacho kuja usiku? [2]

    Tanbihi

    [2] Na kitu gani kitakujuvya ukweli wa nyota hii? Ni hiyo inayotoa mwanga wake katika giza.

  271. 86:3
    ۝٣

    Ni Nyota yenye mwanga mkali. [3]

    Tanbihi

    [3] Na kitu gani kitakujuvya ukweli wa nyota hii? Ni hiyo inayotoa mwanga wake katika giza.

  272. 86:4
    ۝٤

    Hapana nafsi ila inayo mwangalizi. [4]

    Tanbihi

    [4] Hapana nafsi ila inayo mlinzi wa kuiangalia na kudhibiti vitendo vyake.

  273. 86:5
    ۝٥

    Hebu naajitazame mwanaadamu ameumbwa kwa kitu gani? [5]

    Tanbihi

    [5] Basi naafikiri mtu, yeye kaumbwa kutokana na nini?

  274. 86:6
    ۝٦

    Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa! [6]

    Tanbihi

    [6] Ameumbwa mtu kutokana na maji yanayo toka kwa nguvu.

  275. 86:7
    ۝٧

    Yatokayo baina ya mifupa ya mgongo na mbavu. [7]

    Tanbihi

    [7] Maji haya yanatoka baina ya uti wa mgongo na mbavu za mwanamume na mwanamke. S'ULB ni sehemu za uti wa mgongo; na TARAAIB ni mafupa ya vifua, yaani mbavu. Masomo ya watoto wanapo kuwa ndani ya matumbo ya mama zao (Embryology). yamedhihirisha kuwa viini vya vyombo vya uzazi na mkojo katika mtoto ndani ya tumbo la mama yake vinadhihiri baina ya khalaya (cells) za mishipa itakayo kuwa mafupa ya uti wa mgongo, na baina ya khalaya zitakazo kuwa mafupa ya kifua. Mafigo hubakia pahala pake, na kokwa huteremka kwenye pahala pake pa kawaida katika pumbu wakati wa kuzaliwa. Na juu ya kuteremka kokwa chini mishipa inayo inywesha damu maisha yake yote inatokana na mishipa ya mafigo. Hali kadhaalika mishipa ya Navo inayo peleka kuhisi na ikasaidia kuzalisha vitu vya uhai na yaliyo khusiana na hayo kama maji yanayo toka kwenye mshipa wa kifua wa kumi unao tokana na ubongo wa uti wa mgongo kwenye kipingili cha kumi na kumi na moja. Yaliyo wazi kutokana na hayo ni kwamba vyombo vya uzazi na vinavyo lisha vyombo hivyo, na vyombo vya damu, vipo katika kiwiliwili baina ya uti wa mgongo na mbavu.

  276. 86:8
    ۝٨

    Hakika Yeye ana uweza wa kumrudisha. [8]

    Tanbihi

    [8] Hakika Mwenyezi Mungu aliye muumba hivi hapo mwanzo, bila ya shaka ni Muweza wa kumuumba tena baada ya kufa kwake.

  277. 86:9
    ۝٩

    Siku zitakapo dhihirishwa siri. [9]

    Tanbihi

    [9] Siku dhamiri zitapo fanyiwa mtihani, na zitengwe mbali mbali baina ya ziliyo kuwa nzuri na ziliyo kuwa mbovu.

  278. 86:10
    ۝١٠

    Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi. [10]

    Tanbihi

    [10] Basi hapana mtu wakati huo ataye kuwa na nguvu ya kujikinga nafsi yake, wala hatakuwa na msaidizi wa kumnusuru.

  279. 86:11
    ۝١١

    Naapa kwa mbingu yenye marejeo! [11]

    Tanbihi

    [11] Naapa kwa mbingu yenye mvua inayo rejea na kuja mara kwa mara!

  280. 86:12
    ۝١٢

    Na kwa ardhi inayo pasuka! [12]

    Tanbihi

    [12] Na ardhi inayo pasuka kwa kuchipuka mimea!

  281. 86:13
    ۝١٣

    Hakika hii ni kauli ya kupambanua. [13]

    Tanbihi

    [13] Hakika hii Qur'ani ni yenye kupambanua baina ya kweli na uwongo.

  282. 86:14
    ۝١٤

    Wala si mzaha. [14]

    Tanbihi

    [14] Wala haina nuksani yoyote ya mchezo au maskhara.

  283. 86:15
    ۝١٥

    Hakika wao wanapanga mpango. [15]

    Tanbihi

    [15] Hakika hao wanao ikadhibisha Qur'ani wanaipangia njama kutaka kuiharibia, njama zenye kufikia ukomo!

  284. 86:16
    ۝١٦

    Na Mimi napanga mpango. [16]

    Tanbihi

    [16] Lakini Mimi nitawalipa, na nitavipambanisha hivyo vitimbi vyao kwa vitimbi madhubuti ambavyo hawataweza kujikinga navyo.

  285. 86:17
    ۝١٧

    Basi wape muhula makafiri - wape muhula pole pole. [17]

    Tanbihi

    [17] Basi wangojee hao makafiri! Wape muhula wa karibu mpaka nikuamrishe amri gani kali ya kuwatendea.

  286. Sura Al-A'laa

    سُورَةُ الأعلى
  287. 87:1
    ۝١

    Litakase jina la Mola wako Mlezi aliye juu kabisa! [1]

    Tanbihi

    [1] Litakase jina la Mola wako Mlezi lilio tukufu na kila kitu kisicho kuwa kinaelekeana nalo.

  288. 87:2
    ۝٢

    Aliye umba, na akaweka sawa! [2]

    Tanbihi

    [2] Aliye umba kila kitu, na akajaalia uumbaji wote sawa sawa katika hukumu na kupangana.

  289. 87:3
    ۝٣

    Na ambaye amekadiria na akaongoa,. [3]

    Tanbihi

    [3] Na akakadiria kwa kila kitu kwa mujibu wa maslaha yake, na akakiongoza.

  290. 87:4
    ۝٤

    Na aliye otesha malisho! [4]

    Tanbihi

    [4] Na ambaye akatoa kwenye ardhi mimea namna mbali mbali ya kuwalisha wanyama.

  291. 87:5
    ۝٥

    Kisha akayafanya makavu, meusi. [5]

    Tanbihi

    [5] Na akaifanya mimea hiyo baada ya kuwa kijani imestawi, ikakauka na imekuwa myeusi!

  292. 87:6
    ۝٦

    Tutakusomesha wala hutasahau! [6]

    Tanbihi

    [6] Ewe Muhammad! Sisi tutakujaalia uwe ni mwenye kuisoma Qur'ani kwa ufunuo kutoka kwetu, na wala hutosahau utacho kihifadhi.

  293. 87:7
    ۝٧

    Ila akipenda Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye anayajua yaliyo dhaahiri na yaliyo fichikana. [7]

    Tanbihi

    [7] Isipo kuwa anacho taka Mwenyezi Mungu ukisahau, kwani hakika Yeye Mtukufu anayajua wanayo yadhihirisha waja wake na wanayo yaficha, ikiwa maneno au vitendo.

  294. 87:8
    ۝٨

    Na tutakusahilishia yawe mepesi. [8]

    Tanbihi

    [8] Na tutakuwezesha kupita njia ya kufikilia kwa wepesi mambo yako yote.

  295. 87:9
    ۝٩

    Basi kumbusha, kama kukumbusha kunafaa. [9]

    Tanbihi

    [9] Basi wakumbushe watu ikiwa kukumbusha kutaleta manufaa, kwani inavyo faa ndio kuwanafiisha.

  296. 87:10
    ۝١٠

    Atakumbuka mwenye kuogopa. [10]

    Tanbihi

    [10] Watanafiika kwa ukumbusho wako wanao mwogopa Mwenyezi Mungu.

  297. 87:11
    ۝١١

    Na atajitenga mbali nayo mpotovu, [11]

    Tanbihi

    [11] Na atajitenga na ukumbusho mpotovu anaye shikilia kufanya inda na ukafiri.

  298. 87:12
    ۝١٢

    Ambaye atauingia Moto mkubwa. [12]

    Tanbihi

    [12] Ambaye ataingia kwenye Moto mkubwa ulio andaliwa kuwa ndio malipo yake.

  299. 87:13
    ۝١٣

    Tena humo hatakufa wala hawi hai. [13]

    Tanbihi

    [13] Tena hatokufa huko Motoni akapumzika kwa kifo, wala hawi hai kwa uhai wa kustarehe nao.

  300. 87:14
    ۝١٤

    Hakika amekwisha fanikiwa aliye jitakasa. [14]

    Tanbihi

    [14] Hakika amefuzu mwenye kujisafisha na ukafiri na maasi.

  301. 87:15
    ۝١٥

    Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akaswali. [15]

    Tanbihi

    [15] Na akalikumbuka jina la Muumba wake kwa moyo wake na ulimi wake, na akaswali kwa unyenyekevu kama itakikanavyo.

  302. 87:16
    ۝١٦

    Lakini nyinyi mnakhiari maisha ya dunia! [16]

    Tanbihi

    [16] Bali nyinyi hamfanyi hayo yanayo pelekea kufanikiwa, lakini katika hima zenu mnatanguliza maisha ya duniani kuliko ya Akhera.

  303. 87:17
    ۝١٧

    Na Akhera ni bora na yenye kudumu zaidi. [17]

    Tanbihi

    [17] Na Akhera ni bora kuliko dunia, kwa usafi wa neema zake, na ni yenye kubaki na kudumu zaidi.

  304. 87:18
    ۝١٨

    Hakika haya yamo katika Vitabu vya mwanzo, [18]

    Tanbihi

    [18] Hakika haya yote yaliyo tajwa katika Sura hii bila ya shaka yamethibitishwa katika Vitabu vya zamani,

  305. 87:19
    ۝١٩

    Vitabu vya Ibrahimu na Musa. [19]

    Tanbihi

    [19] Vitabu vya Ibrahimu na Musa; kwani haya yamewafikiana na mafunzo ya dini zote na yamesajiliwa katika Vitabu vya mbinguni.

  306. Sura Al-Ghaashiya

    سُورَةُ الغاشية
  307. 88:1
    ۝١

    Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza? [1]

    Tanbihi

    [1] Je! Ewe Muhammad! Imepata kukujia hadithi ya Kiyama ambacho kwa vitisho vyake kitawafanya watu wazimie?

  308. 88:2
    ۝٢

    Siku hiyo nyuso zitainama! [2]

    Tanbihi

    [2] Siku hiyo ya Kiyama zitakuwepo nyuso zimedhalilika,

  309. 88:3
    ۝٣

    Zikifanya kazi, nazo taabani. [3]

    Tanbihi

    [3] Zimechoka, taabani kwa shughuli na mashaka ya Motoni,

  310. 88:4
    ۝٤

    Ziingie katika Moto unao waka . [4]

    Tanbihi

    [4] Zinaingia kwenye Moto unao waka kwa nguvu!

  311. 88:5
    ۝٥

    Zikinyweshwa kutoka chemchem inayo chemka. [5]

    Tanbihi

    [5] Wananywesha maji yanayo toka kwenye chemchem inayo tokota.

  312. 88:6
    ۝٦

    Hawatakuwa na chakula isipo kuwa kichungu chenye miba. [6]

    Tanbihi

    [6] Hawana chakula ila chakula kiovu kabisa, anaadhibika mwenye kukila.

  313. 88:7
    ۝٧

    Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa. [7]

    Tanbihi

    [7] Hakileti nafuu yoyote katika mwili, wala hakiondoi njaa.

  314. 88:8
    ۝٨

    Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu. [8]

    Tanbihi

    [8] Na pia zitakuwapo nyuso zenye kutoa nuru Siku ya Kiyama, kwa malipo ya vitendo vyao walivyo fanya duniani.

  315. 88:9
    ۝٩

    Zitakuwa radhi kwa juhudi yao! [9]

    Tanbihi

    [9] Hao watakuwa wameridhia kwa watayo yapata katika Pepo iliyo juu kwa pahala na cheo.

  316. 88:10
    ۝١٠

    Katika Bustani ya juu. [10]

    Tanbihi

    [10] Katika Pepo iliyo juu kwa pahala na cheo.

  317. 88:11
    ۝١١

    Hawatasikia humo upuuzi.Humo imo chemchem inayo miminika. [11]

    Tanbihi

    [11] Humo halisikilizani neno la upuuzi.

  318. 88:12
    ۝١٢

    Humo imo chemchem inayo miminika. [12]

    Tanbihi

    [12] Humo mna chemchem isiyo katika.

  319. 88:13
    ۝١٣

    Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa, [13]

    Tanbihi

    [13] Humo vitakuwamo viti vilivyo nyanyuliwa kwa cheo na kwa hakika, kama ni ziada ya neema.

  320. 88:14
    ۝١٤

    Na bilauri zilizo pangwa, [14]

    Tanbihi

    [14] Na bilauri (gilasi) zilio wekwa mbele yao,

  321. 88:15
    ۝١٥

    Na matakia safu safu, [15]

    Tanbihi

    [15] Na mito na matakia yalio pangwa kwa safu.

  322. 88:16
    ۝١٦

    Na mazulia yaliyo tandikwa. [16]

    Tanbihi

    [16] Na mazulia mengi yaliyo tandazwa hapo barazani.

  323. 88:17
    ۝١٧

    Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa? [17]

    Tanbihi

    [17] Je! Wanapuuza kuzingatia Ishara, basi hebu na wamuangalie ngamia, vipi alivyo umbwa kwa namna ya peke yake kwa uweza wa Mwenyezi Mungu? Katika kuumbwa ngamia zipo Ishara na miujiza yenye kuthibitisha uweza wa Mwenyezi Mungu ambao yafaa wenye kuzingatia wauzingatie. Katika sifa zake zinazo onekana ni hizo zinazo mfanya kweli awe ni jahazi ya jangwani. Macho yake yamenyanyuka yako juu ya kichwa, na yanaelekea nyuma, na tena yana kope za kuyakinga na mchanga na vumbi. Kadhaalika pua na masikio yamefunikwa na nywele kwa sababu hiyo hiyo. Ukivuma mdharuba wa mchanga pua hufunga na masikio hupinda, juu ya kuwa tokea hapo ni madogo na si yenye kudhihiri mno, ukilinganisha na mwili wake. Ama miguu ni mirefu kwa kusaidia wepesi wa kwenda, pamoja na kunasibiana na urefu wa shingo yake. Ama nyayo ni pana zimetanda kwa ukhafifu ili kumwezesha ngamia kwenda juu ya mchanga laini. Na ngamia kwa jumla chini ya kifua chake na chini ya viungo vyake vya miguu pana kama mito inayo msaidia ngamia kupiga magoti na kulala juu ya ardhi ngumu na imoto, kama vile vile pande zote mbili za mkia wake yapo manyoya marefu ya kumlinda sehemu zake za nyuma na vitu vya kumuudhi. Ama vipawa alivyo pewa ngamia kwa ajili ya kazi yake ni vya ajabu zaidi. Siku za baridi hahitajii maji, bali anaweza asinywe maji muda wa miezi miwili mfululizo, ikiwa chakula kimajimaji na laini, au wiki mbili ikiwa kikavu. Pia anaweza kustahamili kiu hata siku za joto muda wa wiki au wiki mbili, na hupungua muda huo zaidi ya thuluthi mbili ya uzito wake. Na anapo yapata maji huyagugumia maji kwa wingi mno arejeshe uzito wake wa zamani kwa dakika chache tu. Na ngamia hayarimbiki maji katika tumbo lake kama ilivyo kuwa ikidhaniwa, bali katika mfumo wa mwili wake, na huyatumia kwa uangalifu mkubwa mno. Kwa hivyo kabisa hapumui kama anavyo pumua mbwa, mathalan, wala hatoi pumzi kwa mdomo wake, wala hatoki majasho kwenye ngozi yake ila kwa uchache kabisa. Na hayo ni kuwa daraja ya joto ya mwili wake inakuwa chini sana asubuhi mapema. Kisha hupanda kidogo kidogo zaidi ya daraja sita kabla ya kuhitajia kuipoza kwa jasho na kutoa mvuke. Na juu ya maji mengi mno yanayo toka katika mwili baada ya kiu kirefu kwa hakika uzito wa damu hauathiriki ila kwa kiasi tu, na kwa hivyo kiu hakina athari kitu juu yake. Na imethibiti mafuta ya nunudu yaliyo khaziniwa kwa ajili ya nishat'i yanamkifu kumkinga na machungu ya njaa, lakini hayamfaidishi sana kwa haja ya maji ambayo ni lazima kwa mwili wake. Na bado wataalamu wangali wanagundua mapya katika ngamia kila wakichungua ya kuhakikisha hadhi aliyo mpa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atazamwe katika uumbaji wake wa muujiza.

  324. 88:18
    ۝١٨

    Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa? [18]

    Tanbihi

    [18] Na waizingatie mbingu wanayo iona daima, vipi ilivyo nyanyuliwa huko mbali bila ya nguzo!

  325. 88:19
    ۝١٩

    Na milima jinsi ilivyo thibitishwa? [19]

    Tanbihi

    [19] Na milima wanayo ikwea mpaka wakafika vileleni kwake, vipi ilivyo simamishwa kwa urefu, imeshikamana na ardhi, haiyumbi wala haitikisiki!

  326. 88:20
    ۝٢٠

    Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa? [20]

    Tanbihi

    [20] Na ardhi wanayo ikalia na kuyendea juu yake, vipi ilivyo kunjuliwa na kutandazwa! Mara nyingi katika Qur'ani tukufu inatajwa kuwa ardhi "imekunjuliwa". Na makusudio ya hayo ni kuwa ardhi ijapo kuwa ni duara kama mpira kwa sura yake, lakini inavyo onekana kwa watazamao ni kuwa imekunjuliwa. Na haya hayagongani na yaliyo thibitishwa na sayansi katika jambo lolote.

  327. 88:21
    ۝٢١

    Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji. [21]

    Tanbihi

    [21] Basi kumbusha kwa wito wako, kwani kazi yako muhimu ni kufikisha wito tu.

  328. 88:22
    ۝٢٢

    Wewe si mwenye kuwatawalia. [22]

    Tanbihi

    [22] Hukuwa mtawala juu yao.

  329. 88:23
    ۝٢٣

    Lakini anaye rudi nyuma na kukataa, [23]

    Tanbihi

    [23] Lakini miongoni mwao ataye puuza na akakataa,

  330. 88:24
    ۝٢٤

    Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa kabisa! [24]

    Tanbihi

    [24] Basi Mwenyezi Mungu atampa adhabu iliyo kubwa kabisa, isiyo kuwa na ya kuipita.

  331. 88:25
    ۝٢٥

    Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao. [25]

    Tanbihi

    [25] Hakika ni kwetu Sisi marejeo yao kwa kifo na kufufuliwa, wala hapana penginepo isipo kuwa kwetu.

  332. 88:26
    ۝٢٦

    Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabu yao! [26]

    Tanbihi

    [26] Tena ni juu yetu Sisi tu peke yetu kuwahisabia na kuwalipa.

  333. Sura Al-Fajr

    سُورَةُ الفجر
  334. 89:1
    ۝١

    Naapa kwa alfajiri! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa mwangaza wa asubuhi unapo ufukuza usiku.

  335. 89:2
    ۝٢

    Na kwa masiku kumi! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa masiku kumi yaliyo tukuzwa na Mwenyezi Mungu. (Na hayo ni masiku kumi ya mwanzo wa Mwezi wa Alhaj, Mfungo Tatu).

  336. 89:3
    ۝٣

    Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja! [3]

    Tanbihi

    [3] Na shafi' yaani hisabu inayo gawika kwa mbili, kama 4, 6, 8 n.k. na witri, yaani isiyo gawika kwa mbili, kama 1, 3, 5 n.k. katika kila kitu.

  337. 89:4
    ۝٤

    Na kwa usiku unapo pita! [4]

    Tanbihi

    [4] Na kwa usiku unapo pita kwa kwenda ulimwengu kwa namna ya ajabu.

  338. 89:5
    ۝٥

    Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili? [5]

    Tanbihi

    [5] Je! Katika vitu vilivyo tajwa vinavyo onekana kwa akili hapana kiapo cha kukinaisha?

  339. 89:6
    ۝٦

    Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A'di? [6]

    Tanbihi

    [6] Kwani hujui jinsi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu yake kaumu ya Hud, ?

  340. 89:7
    ۝٧

    Wa Iram, wenye majumba marefu? [7]

    Tanbihi

    [7] Watu wa Iram wenye majengo marefu?

  341. 89:8
    ۝٨

    Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi? [8]

    Tanbihi

    [8] Ambayo haikupata kujengwa mfano wake kwa umadhubuti na ujenzi katika nchi.

  342. 89:9
    ۝٩

    Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni? [9]

    Tanbihi

    [9] Kwani hukujua jinsi Mola wako Mlezi alivyo teremsha adhabu yake kwa Thamudi, kaumu ya Saleh, walio chonga majabali kujengea nyumba zao huko bondeni?

  343. 89:10
    ۝١٠

    Na Firauni mwenye vigingi? [10]

    Tanbihi

    [10] Au kwani hukujua vipi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu yake Firauni mwenye majeshi yaliyo upa nguvu ufalme wake kama vigingi vinavyo simamisha makhema?

  344. 89:11
    ۝١١

    Ambao walifanya jeuri katika nchi? [11]

    Tanbihi

    [11] Ambao walipita mipaka katika nchi?

  345. 89:12
    ۝١٢

    Wakakithirisha humo ufisadi? [12]

    Tanbihi

    [12] Na wakazidisha kufanya uharibifu kwa ukafiri na udhalimu?

  346. 89:13
    ۝١٣

    Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu. [13]

    Tanbihi

    [13] Basi Mola wako Mlezi aliwateremshia adhabu kali ya kuwaunguza.

  347. 89:14
    ۝١٤

    Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia. [14]

    Tanbihi

    [14] Hakika Mola wako Mlezi anaviangalia vitendo vya watu, na anawahisabia, na atakuja kuwalipa kwavyo.

  348. 89:15
    ۝١٥

    Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu! [15]

    Tanbihi

    [15] Ama mtu akijaribiwa na Mola wake Mlezi na akamkirimu, na akamneemesha kwa mali na cheo na nguvu, basi husema kwa kughurika na hayo: Mola wangu Mlezi amenitukuza kwa kuwa ninastahiki haya!

  349. 89:16
    ۝١٦

    Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge! [16]

    Tanbihi

    [16] Na pindi Mola wake Mlezi akimjaribu mtu kwa kumdhikisha riziki, basi hughafilika na hikima ya hayo na husema: Mola wangu Mlezi kanidhalilisha!

  350. 89:17
    ۝١٧

    Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima, [17]

    Tanbihi

    [17] Wacheni mtindo huo! Mambo siyo hayo kama msemavyo; bali nyinyi hamumkirimu yatima;

  351. 89:18
    ۝١٨

    Wala hamhimizani kulisha masikini; [18]

    Tanbihi

    [18] Wala hamhimizani kuwalisha masikini;

  352. 89:19
    ۝١٩

    Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa, [19]

    Tanbihi

    [19] Na mnakula mali ya urithi kwa pupa, hamchagui linalo faa na lisilo faa.

  353. 89:20
    ۝٢٠

    Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi. [20]

    Tanbihi

    [20] Na mnayapenda mali mno, yanayo kupelekeeni kupapatika katika kuyakusanya na ubakhili wa kuyatumia.

  354. 89:21
    ۝٢١

    Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande, [21]

    Tanbihi

    [21] Wacheni vitendo hivyo! Kwani inakungojeeni siku itapo lazwa ardhi iwe sawa sawa,

  355. 89:22
    ۝٢٢

    Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu, [22]

    Tanbihi

    [22] Na aje Mola wako Mlezi kama anavyo stahiki kuja kwake Subhanahu na Malaika waje kwa safu safu;

  356. 89:23
    ۝٢٣

    Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? [23]

    Tanbihi

    [23] Na siku hiyo iletwe Jahannamu, nyumba ya adhabu, siku hiyo yatapo tokea hayo mwanaadamu atakumbuka aliyo yaharibu - lakini wapi! Kukumbuka huko kumfae nini, na wakati umekwisha pita?

  357. 89:24
    ۝٢٤

    Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu! [24]

    Tanbihi

    [24] Atasema kwa majuto: Laiti ningeli jitangulizia katika dunia vitendo vyema vya kunifaa katika maisha ya Akhera!

  358. 89:25
    ۝٢٥

    Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake. [25]

    Tanbihi

    [25] Siku hiyo zitakuwa hali hizi, haadhibu mtu kama adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala hafungi mtu kama afungavyo Yeye.

  359. 89:26
    ۝٢٦

    Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake. [26]

    Tanbihi

    [26] Siku hiyo zitakuwa hali hizi, haadhibu mtu kama adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala hafungi mtu kama afungavyo Yeye.

  360. 89:27
    ۝٢٧

    Ewe nafsi iliyo tua! [27]

    Tanbihi

    [27] Ewe nafsi uliye tulia juu ya Haki!

  361. 89:28
    ۝٢٨

    Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. [28]

    Tanbihi

    [28] Rejea kwenye radhi ya Mola wako Mlezi nawe uradhi kwa neema ulio pewa, nawe umemridhisha kwa a'mali uliyo ikadimisha.

  362. 89:29
    ۝٢٩

    Basi ingia miongoni mwa waja wangu, [29]

    Tanbihi

    [29] Basi ingia katika kundi la waja wangu walio wema!

  363. 89:30
    ۝٣٠

    Na ingia katika Pepo yangu. [30]

    Tanbihi

    [30] Na ingia katika Pepo yangu, nyumba ya neema ya milele!

  364. Sura Al-Balad

    سُورَةُ البلد
  365. 90:1
    ۝١

    Naapa kwa Mji huu! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kiapo cha mkazo kwa mji wa Makka, mji mtakatifu;

  366. 90:2
    ۝٢

    Nawe unaukaa Mji huu. [2]

    Tanbihi

    [2] Na wewe unaishi katika mji huu, unauzidisha utukufu wake na cheo chake.

  367. 90:3
    ۝٣

    Na naapa kwa mzazi na alicho kizaa. [3]

    Tanbihi

    [3] Na naapa kwa mzazi na anacho kizaa, na kwa hao wawili ndio jinsi inahifadhika na maendeleo yanabakia.

  368. 90:4
    ۝٤

    Hakika tumemuumba mtu katika taabu. [4]

    Tanbihi

    [4] Hakika Sisi tumemuumba mtu katika mashaka na taabu tangu mwanzo wake mpaka kumalizika mambo yake.

  369. 90:5
    ۝٥

    Ati anadhani hapana yeyote ataye muweza? [5]

    Tanbihi

    [5] Je! Anadhani mtu aliye umbwa katika mashaka haya kuwa hapana awezae kumdhalilisha?

  370. 90:6
    ۝٦

    Anasema: Nimeteketeza chungu ya mali. [6]

    Tanbihi

    [6] Anasema: Nimetumia katika kupambana na Muhammad s.a.w. na kuupinga wito wake mali mengi ukiyakusanya pamoja.

  371. 90:7
    ۝٧

    Ati anadhani ya kuwa hapana yeyote anaye mwona? [7]

    Tanbihi

    [7] Ati anadhani kwamba mambo yake hayo yamefichikana, hayajui yeyote hata huyo aliye muumba?

  372. 90:8
    ۝٨

    Kwani hatukumpa macho mawili? [8]

    Tanbihi

    [8] Kwani Sisi hatukumuumba na macho mawili ya kutazamia,?

  373. 90:9
    ۝٩

    Na ulimi, na midomo miwili? [9]

    Tanbihi

    [9] Na ulimi na midomo miwili ili aweze kutamka na kusema sawa?

  374. 90:10
    ۝١٠

    Na tukambainishia zote njia mbili? [10]

    Tanbihi

    [10] Na tukamwonyesha njia ya kheri na ya shari, na tukamtengenezea aweze kuchagua mojawapo?

  375. 90:11
    ۝١١

    Lakini hakujitoma kwenye njia ya vikwazo vya milimani. [11]

    Tanbihi

    [11] Basi huyo hakunafiika kwa tuliyo mtengenezea, wala hakuivuka njia ya milimani inayo mzuia asifikie uwokovu, nayo ni choyo wa nafsi yake.

  376. 90:12
    ۝١٢

    Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani? [12]

    Tanbihi

    [12] Na kitu gani kitakufunza nini huko kujitoma kwenye njia ya milimani?

  377. 90:13
    ۝١٣

    Kumkomboa mtumwa; [13]

    Tanbihi

    [13] Kumkomboa mtu kutokana na utumwa,

  378. 90:14
    ۝١٤

    Au kumlisha siku ya njaa [14]

    Tanbihi

    [14] Au kumlisha siku ya njaa

  379. 90:15
    ۝١٥

    Yatima aliye jamaa, [15]

    Tanbihi

    [15] Yatima aliye jamaa wa kumliwaza kwa ujamaa na ufakiri.

  380. 90:16
    ۝١٦

    Au masikini aliye vumbini. [16]

    Tanbihi

    [16] Au masikini mwingi wa haja na kufakirika.

  381. 90:17
    ۝١٧

    Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana. [17]

    Tanbihi

    [17] Tena awe pamoja na hayo miongoni mwa wenye Imani wanao usiana na wenzao kwa subira na kuoneana huruma.

  382. 90:18
    ۝١٨

    Hao ndio watu wa kheri wa kuliani. [18]

    Tanbihi

    [18] Hao wanao sifika kwa sifa hizi, ndio watu wa kheri, wa mkono wa kulia.

  383. 90:19
    ۝١٩

    Lakini walio zikataa Ishara zetu, hao ndio watu wa shari wa kushotoni. [19]

    Tanbihi

    [19] Na walio zikataa dalili tulizo zisimamisha kuthibitisha Haki kutoka na Kitabu na hoja zake, hao ndio wapotovu watu waovu walio kosa kheri na watapata adhabu.

  384. 90:20
    ۝٢٠

    Juu yao utakuwa Moto ulio fungiwa kila upande. [20]

    Tanbihi

    [20] Juu yao utakuwa Moto ulio bebeana na milango yake ikafungwa.

  385. Sura Ash-Shams

    سُورَةُ الشمس
  386. 91:1
    ۝١

    Naapa kwa jua na mwangaza wake! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa jua na mwangaza wake na kuchomoza kwake na kwa joto lake!

  387. 91:2
    ۝٢

    Na kwa mwezi unapo lifuatia! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa mwezi unapo lifuata na likawa nyuma yake kwa kutoa mwangaza baada ya kuchwa jua,

  388. 91:3
    ۝٣

    Na kwa mchana unapo lidhihirisha! [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwa mchana unapo lidhihirisha jua, likaonekana wazi halikufichikana.

  389. 91:4
    ۝٤

    Na kwa usiku unapo lifunika! [4]

    Tanbihi

    [4] Na kwa usiku unapo lifunika jua, ukawa mwangaza wake hauonekani.

  390. 91:5
    ۝٥

    Na kwa mbingu na kwa aliye ijenga! [5]

    Tanbihi

    [5] Na kwa mbingu na kwa Mweza Mtukufu aliye inyanyua na akaijenga kwa hikima yake.

  391. 91:6
    ۝٦

    Na kwa ardhi na kwa aliye itandaza! [6]

    Tanbihi

    [6] Na kwa ardhi na kwa Mweza Mtukufu aliye ikunjua kwa kila upande, na akaitengeneza kwa ajili ya utulivu, na akaifanya kama tandiko.

  392. 91:7
    ۝٧

    Na kwa nafsi na kwa aliye itengeneza! [7]

    Tanbihi

    [7] Na kwa nafsi, na aliye iumba na akaiweka sawa, kwa kuipa nguvu,

  393. 91:8
    ۝٨

    Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake! [8]

    Tanbihi

    [8] Akaifunza jema na baya, na akaipa uweza wa kutenda itakayo katika hayo,

  394. 91:9
    ۝٩

    Hakika amefanikiwa aliye itakasa! [9]

    Tanbihi

    [9] Hakika amefuzu mwenye kuisafisha nafsi yake kwa ut'iifu na vitendo vya kheri.

  395. 91:10
    ۝١٠

    Na hakika amekhasiri aliye iviza. [10]

    Tanbihi

    [10] Na hakika amekhasiri mwenye kuzificha fadhila zake, na akayaua matayarisho aliyo umbwa nayo ya kutenda kheri.

  396. 91:11
    ۝١١

    Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao, [11]

    Tanbihi

    [11] Kina Thamudi walimkanusha Nabii wao kwa upotovu wao na jeuri zao,

  397. 91:12
    ۝١٢

    Alipo simama mwovu wao mkubwa, [12]

    Tanbihi

    [12] Alipo gutuka mwovu wao mkubwa kabisa kutaka kumchinja ngamia.

  398. 91:13
    ۝١٣

    Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake. [13]

    Tanbihi

    [13] Saleh, Mtume wa Mwenyezi Mungu, akawaambia: Mwachilieni huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ale maridhawa katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, na tahadharini msimzuie maji katika siku yake aliyo wekewa.

  399. 91:14
    ۝١٤

    Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa. [14]

    Tanbihi

    [14] Wakamkadhibisha Mtume wao katika hilo onyo lake, wakamchinja. Mola wao Mlezi akazibomoa nyumba zao kwa sababu ya dhambi zao; akazisawazisha na ardhi!

  400. 91:15
    ۝١٥

    Wala Yeye haogopi matokeo yake. [15]

    Tanbihi

    [15] Wala Yeye Mwenyezi Mungu hakhofu matokeo ya adhabu hiyo, kwani hiyo ni malipo ya haki kwa yale waliyo yatenda.

  401. Sura Al-Lail

    سُورَةُ الليل
  402. 92:1
    ۝١

    Naapa kwa usiku unapo funika! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa usiku kinapo enea kiza chake!

  403. 92:2
    ۝٢

    Na mchana unapo dhihiri! [2]

    Tanbihi

    [2] Na naapa kwa mchana unapo zagaa mwangaza wake!

  404. 92:3
    ۝٣

    Na kwa Aliye umba dume na jike! [3]

    Tanbihi

    [3] Na naapa kwa Mjuzi aliye umba viwili viwili, dume na jike, katika kila vinavyo zaliwa!

  405. 92:4
    ۝٤

    Hakika juhudi zenu bila ya shaka ni mbali mbali. [4]

    Tanbihi

    [4] Hakika juhudi zenu bila ya shaka zimekhitalifiana; kwani wapo wenye kubahatika katika juhudi zao, na wako wasio bahatika.

  406. 92:5
    ۝٥

    Ama mwenye kutoa na akamchamngu! [5]

    Tanbihi

    [5] Ama mwenye kutoa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na akamkhofu Mola wake Mlezi, na kwa hivyo akaepuka anayo yakataza,

  407. 92:6
    ۝٦

    Na akaliwafiki lilio jema! [6]

    Tanbihi

    [6] Na akayakinika kufuata fadhila njema, nayo ni Imani kumuamini Mwenyezi Mungu kwa kumjua,

  408. 92:7
    ۝٧

    Tutamsahilishia yawe mepesi. [7]

    Tanbihi

    [7] Basi Sisi tutamtengenezea awe katika khulka ya wepesi na raha kwa kumwongoza kwenye njia ya kheri.

  409. 92:8
    ۝٨

    Na ama mwenye kufanya ubakhili, na asiwe na haja ya wenzake! [8]

    Tanbihi

    [8] Ama mwenye kufanya ubakhili kwa mali yake asitoe haki ya Mwenyezi Mungu iliomo humo, na akawa hana haja na yatokayo kwa Mwenyezi Mungu,

  410. 92:9
    ۝٩

    Na akakanusha lilio jema! [9]

    Tanbihi

    [9] Na akakadhibisha khulka nzuri,

  411. 92:10
    ۝١٠

    Tutamsahilishia yawe mazito! [10]

    Tanbihi

    [10] Basi huyo tutamtengenezea khulka ambayo inapelekea uzito na mashaka ya milele.

  412. 92:11
    ۝١١

    Na mali yake yatamfaa nini atapo kuwa anadidimia? [11]

    Tanbihi

    [11] Na kitu gani katika adhabu ambacho hayo mali yake yataweza kumkinga nacho, atapo teketea yeye mwenyewe mzima?

  413. 92:12
    ۝١٢

    Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu. [12]

    Tanbihi

    [12] Hakika ni juu yetu, Sisi, kwa kufuatana na hikima yetu, ndio tuwabainishie viumbe njia ya uwongofu.

  414. 92:13
    ۝١٣

    Na hakika ni yetu Sisi Akhera na dunia. [13]

    Tanbihi

    [13] Na juu yetu Sisi peke yetu, bila ya shaka, hili jambo la kuendesha yaliomo duniani na Akhera.

  415. 92:14
    ۝١٤

    Basi nakuonyeni na Moto unao waka! [14]

    Tanbihi

    [14] Ndio maana tukakutieni khofu ya Moto unao waka na kuripuka!

  416. 92:15
    ۝١٥

    Hatauingia ila mwovu kabisa! [15]

    Tanbihi

    [15] Hawauingii kwa kudumu ila kafiri

  417. 92:16
    ۝١٦

    Anaye kadhibisha na kupa mgongo. [16]

    Tanbihi

    [16] Aliye ikadhibisha Haki na akazipuuza Ishara za Mola wake Mlezi.

  418. 92:17
    ۝١٧

    Na mchamngu ataepushwa nao, [17]

    Tanbihi

    [17] Na atakuwa mbali na huo Moto aliye mwingi wa kujikinga na ukafiri na maasi,

  419. 92:18
    ۝١٨

    Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa. [18]

    Tanbihi

    [18] Amabye hutoa mali yake wakati wa nafasi ili kujisafisha na uchafu wa ubakhili, na najsi ya uchoyo.

  420. 92:19
    ۝١٩

    Na wala si kwa kuwa yupo yeyote aliye mfanyia hisani ndio anamlipa. [19]

    Tanbihi

    [19] Na mtoaji huyu si kama anaye mtu yeyote ambaye ndio anamlipa kwa neema aliyo mfanyia zamani,

  421. 92:20
    ۝٢٠

    Ila ni kutaka radhi ya Mola wake Mlezi aliye juu kabisa. [20]

    Tanbihi

    [20] Bali anatoa hicho kwa kutafuta radhi ya Mola wake Mlezi Mtukufu tu.

  422. 92:21
    ۝٢١

    Naye atakuja ridhika! [21]

    Tanbihi

    [21] Na bila ya shaka atakuja pata kutoka kwa Mola wake Mlezi anacho kitaka kwa njia za ukamilifu kabisa, hata itimie radhi kwake.

  423. Sura Ad-Dhuhaa

    سُورَةُ الضحى
  424. 93:1
    ۝١

    Naapa kwa mchana! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa wakati wa kupanda juu jua, na ni wakati wa uchangamfu na kazi!

  425. 93:2
    ۝٢

    Na kwa usiku unapo tanda! [2]

    Tanbihi

    [2] Na naapa kwa usiku unapo tulia na ukatanda kote kiza chake!

  426. 93:3
    ۝٣

    Mola wako Mlezi hakukuacha, wala hakukasirika nawe. [3]

    Tanbihi

    [3] Ewe Muhammad! Mola wako Mlezi hakukuacha, wala hakukuchukia.

  427. 93:4
    ۝٤

    Na bila ya shaka wakati ujao utakuwa bora kwako kuliko ulio tangulia. [4]

    Tanbihi

    [4] Na matokeo ya mambo yako, mwisho wake, yatakuwa bora kuliko mwanzo wake.

  428. 93:5
    ۝٥

    Na Mola wako Mlezi atakupa mpaka uridhike. [5]

    Tanbihi

    [5] Na ninaapa kuwa bila ya shaka hapo Mola wako Mlezi atakupa kheri za duniani na Akhera hata utaridhia.

  429. 93:6
    ۝٦

    Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? [6]

    Tanbihi

    [6] Kwani hakukukuta wewe yatima unahitaji wa kukutunza naye akakupa makaazi ya kukuhifadhi kwa mwenye kukuangalia vyema kwa mambo yako?

  430. 93:7
    ۝٧

    Na akakukuta umepotea akakuongoa? [7]

    Tanbihi

    [7] Na akakuona umebabaika hukukinaika na itikadi zilizo kuzunguka, naye akakuongoa kwenye Njia ya Haki?

  431. 93:8
    ۝٨

    Akakukuta mhitaji akakutosheleza? [8]

    Tanbihi

    [8] Akakukuta fakiri wa mali naye akakutajirisha kwa kukupa riziki?

  432. 93:9
    ۝٩

    Basi yatima usimwonee! [9]

    Tanbihi

    [9] Ikiwa hii ndiyo hali yetu nawe, basi yatima usimdhili,

  433. 93:10
    ۝١٠

    Na anaye omba au kuuliza usimkaripie! [10]

    Tanbihi

    [10] Na mwenye kuomba au kuuliza usimjibu kwa ukavu,

  434. 93:11
    ۝١١

    Na neema za Mola wako Mlezi zisimlie. [11]

    Tanbihi

    [11] Na ama neema za Mola wako Mlezi zitangaze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kuwa ndio kudhihirisha neema.

  435. Sura Ash-Sharh

    سُورَةُ الشرح
  436. 94:1
    ۝١

    Hatukukunjulia kifua chako? [1]

    Tanbihi

    [1] Hakika tumekukunjulia kifua chako kwa kuwa tulitia ndani yake Uwongofu na Imani.

  437. 94:2
    ۝٢

    Na tukakuondolea mzigo wako! [2]

    Tanbihi

    [2] Na tumekupunguzia mizigo iliyo kuwa mizito juu ya mgongo wako, kwa kukuunga mkono na kukusahilishia mambo yako,

  438. 94:3
    ۝٣

    Ulio vunja mgongo wako? [3]

    Tanbihi

    [3] Ambayo yalikuwa ni mazito juu ya mgongo wako.

  439. 94:4
    ۝٤

    Na tukakunyanyulia utajo wako? [4]

    Tanbihi

    [4] Na tumelitukuza jina lako, tukalifanya linatajwa na ulimi wa kila Muumini pamoja na jina letu.

  440. 94:5
    ۝٥

    Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi! [5]

    Tanbihi

    [5] Hizo ni baadhi ya neema zetu juu yako. Basi kuwa na yakini na uweza wa Mwenyezi Mtukufu, kwani pamoja na uzito upo wepesi mwingi unao kuja nao.

  441. 94:6
    ۝٦

    Hakika pamoja na uzito upo wepesi. [6]

    Tanbihi

    [6] Hakika pamoja na uzito (wakati huo huo ijapo kuwa wewe hujui), upo wepesi mwingi vile vile.

  442. 94:7
    ۝٧

    Na ukipata faragha, fanya juhudi. [7]

    Tanbihi

    [7] Basi ukipata nafasi katika kazi ya kuwalingania watu, na mambo yaliyo khusiana na Jihadi, endelea na jitihada ya ibada na jishughulishe nafsi yako katika hayo.

  443. 94:8
    ۝٨

    Na Mola wako Mlezi ndio mshughulikie. [8]

    Tanbihi

    [8] Kwa Mola wako Mlezi tu ndio uelekee kwa kumwomba na kumhitajia.

  444. Sura At-Tin

    سُورَةُ التين
  445. 95:1
    ۝١

    Naapa kwa tini na zaituni! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa tini na zaituni, kwa baraka zao na ubora wa manufaa yao.

  446. 95:2
    ۝٢

    Na kwa Mlima wa Sinai! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa mlima ambao juu yake ndio Mwenyezi Mungu alimsemeza Musa.

  447. 95:3
    ۝٣

    Na kwa mji huu wenye amani! [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwa huu mji mtukufu wa Makka, ambao anaushuhudia utukufu wake mwenye kwenda uzuru, na anapata amani mwenye kuuingia.

  448. 95:4
    ۝٤

    Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa. [4]

    Tanbihi

    [4] Kwa hakika bila ya shaka yoyote Sisi tumemuumba mtu amesimama sawa kwa umbo bora kabisa lilio nyooka, na akasifika kwa sifa nzuri kabisa.

  449. 95:5
    ۝٥

    Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini! [5]

    Tanbihi

    [5] Kisha tukamteremsha cheo mpaka akawa ni wa chini kabisa katika hao walioko chini, kwa kuacha kufanya waajibu wa hayo tuliyo muumbia.

  450. 95:6
    ۝٦

    Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha. [6]

    Tanbihi

    [6] Lakini walio amini na wakatenda vitendo vyema, hao basi watapata ujira usio wakatikia wala kuwapungukia.

  451. 95:7
    ۝٧

    Basi ni kipi baadaye kitacho kukukadhibishia malipo? [7]

    Tanbihi

    [7] Basi kitu gani kinacho kupelekea kukadhibisha kufufuliwa na kulipwa baada ya kuwekwa wazi uweza wetu wa hayo?

  452. 95:8
    ۝٨

    Kwani Mwenyezi Mungu si muadilifu kuliko mahakimu wote? [8]

    Tanbihi

    [8] Kwani Mwenyezi Mungu aliye yatenda hayo tuliyo kueleza si muadilifu kuliko mahakimu wote kwa kufanya na kupanga?

  453. Sura Al-Alaq

    سُورَةُ العلق
  454. 96:1
    ۝١

    Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba! [1]

    Tanbihi

    [1] Ewe Muhammad! Soma unayo funuliwa kwa kufunguliwa kwa Jina la Mola wako Mlezi ambaye ni Yeye tu peke yake ndiye Mwenye uweza wa kuumba.

  455. 96:2
    ۝٢

    Amemuumba binaadamu kwa tone la damu! [2]

    Tanbihi

    [2] Amemuumba mtu kwa ukamilifu wa mwili wake na ilimu kutokana na kipande cha damu ambacho hakina chochote cha kupelekea kujiona bora.

  456. 96:3
    ۝٣

    Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! [3]

    Tanbihi

    [3] Endelea na kusoma, na Mola wako Mlezi aliye Karimu kushinda wote, atakutukuza wala hatakudharau.

  457. 96:4
    ۝٤

    Ambaye amefundisha kwa kalamu. [4]

    Tanbihi

    [4] Yeye ndiye ambaye aliye mfunza mtu kuandika kwa kalamu, na wala kwanza hakuwa anajua hayo.

  458. 96:5
    ۝٥

    Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui. [5]

    Tanbihi

    [5] Amemfunza mtu yasiyo kuwa yanampitia katika mawazo yake.

  459. 96:6
    ۝٦

    Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri. [6]

    Tanbihi

    [6] Ni hakika kweli mtu hupindukia mpaka na hupanda kiburi mbele ya Mola wake Mlezi

  460. 96:7
    ۝٧

    Akijiona katajirika. [7]

    Tanbihi

    [7] Anapo jiona si mhitaji, katajirika.

  461. 96:8
    ۝٨

    Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo. [8]

    Tanbihi

    [8] Ewe Muhammad! Hakika ni kwa Mola wako Mlezi peke yake ndiyo yako marejeo ya wote kwa kufufuliwa na kulipwa.

  462. 96:9
    ۝٩

    Umemwona yule anaye mkataza. [9]

    Tanbihi

    [9] Je! Umemwona huyu jeuri

  463. 96:10
    ۝١٠

    Mja anapo sali? [10]

    Tanbihi

    [10] Anaye mzuia mja asisali anapo taka kusali?

  464. 96:11
    ۝١١

    Umeona kama yeye yuko juu ya uwongofu? [11]

    Tanbihi

    [11] Hebu niambie khabari za jeuri huyu kama yeye yumo katika uwongofu katika huku kuzuia kwake,

  465. 96:12
    ۝١٢

    Au anaamrisha uchamngu? [12]

    Tanbihi

    [12] Au kwamba ndio anaamrisha uchamngu katika hayo anayo amrisha!

  466. 96:13
    ۝١٣

    Umeona kama yeye akikanusha na anarudi nyuma? [13]

    Tanbihi

    [13] Niambie khabari za huyu mwenye kukataza anapo yakadhibisha aliyo kuja nayo Mtume, na akapuuza Imani na vitendo vyema!

  467. 96:14
    ۝١٤

    Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona? [14]

    Tanbihi

    [14] Hivyo hajui kwamba Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zake, naye atamlipa kwazo?

  468. 96:15
    ۝١٥

    Kwani! Kama haachi, tutamkokota kwa shungi la nywele! [15]

    Tanbihi

    [15] Kwa kumkemea huyu mwenye kuzuia, anaambiwa kama hakuacha hayo anayo yafanya, basi hapana shaka tutamkokota kwa nguvu tukimshika kwa shungi lake la nywele mpaka Motoni!

  469. 96:16
    ۝١٦

    Shungi la uwongo, lenye makosa! [16]

    Tanbihi

    [16] Hilo shungi lilio juu ya uso wake mwenye kuropokwa uwongo na mwenye athari za ukosefu!

  470. 96:17
    ۝١٧

    Basi na awaite wenzake! [17]

    Tanbihi

    [17] Basi yeye awaite wenziwe na watu wa baraza lake wawe ndio wasaidizi duniani au Akhera.

  471. 96:18
    ۝١٨

    Nasi tutawaita Mazabania! [18]

    Tanbihi

    [18] Sisi tutawaita askari wetu wamsaidie Muhammad na walio pamoja naye, na wapambane na huyo mwenye kukanya na wasaidizi wawasukume kwenye Jahannamu!

  472. 96:19 ۩ Sijida
    ۝١٩

    Hasha! Usimt'ii! Nawe sujudu na ujongee! [19]

    Tanbihi

    [19] Kumnyamazisha huyu mwenye kuzuia, wewe usimkubalie kwa hayo anayo kukataza nayo, na dumu juu ya Swala zako, na endelea na sijida zako, na jijongeze kwa Mola wako Mlezi kwa hivyo.

  473. Sura Al-Qadr

    سُورَةُ القدر
  474. 97:1
    ۝١

    Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu. [1]

    Tanbihi

    [1] Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani katika usiku wa Cheo na Utukufu.

  475. 97:2
    ۝٢

    Na nini kitacho kujuulisha nini Laylatul Qadri? [2]

    Tanbihi

    [2] Na kitu gani kitakufunza ni nini usiku huo wa Cheo na Utukufu?

  476. 97:3
    ۝٣

    Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. [3]

    Tanbihi

    [3] Usiku wa Qadr na Sharaf, Cheo na Utukufu, ni bora kuliko miezi elfu, kwa kuwa umekhusika kwa kuteremka ndani yake Qur'ani tukufu.

  477. 97:4
    ۝٤

    Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo. [4]

    Tanbihi

    [4] Huteremka Malaika na Jibrili katika usiku huo mpaka kwenye ardhi kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa sababu ya kila jambo.

  478. 97:5
    ۝٥

    Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri. [5]

    Tanbihi

    [5] Na wameaminika na maudhi na uovu. Hali inabaki hivyo mpaka mapambazuko ya alfajiri.

  479. Sura Al-Bayyina

    سُورَةُ البينة
  480. 98:1
    ۝١

    Hawakuwa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina waache walio nayo mpaka iwajie bayana! [1]

    Tanbihi

    [1] Hawakuwa walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake miongoni mwa Mayahudi na Wakristo, na miongoni mwa washirikina, waache kughafilika kwao na ujinga wao kuto ijua Haki mpaka iwajie hoja ya kukata.

  481. 98:2
    ۝٢

    Yaani Mtume aliye toka kwa Mwenyezi Mungu anaye wasomea kurasa zilizo takasika! [2]

    Tanbihi

    [2] Na hoja hiyo ni Mtume aliye tumwa kutokana na Mwenyezi Mungu awasomee kurasa zilizo takasika na upotovu,

  482. 98:3
    ۝٣

    Ndani yake mna maandiko yaliyo nyooka. [3]

    Tanbihi

    [3] Ndani yake zimo hukumu zilizo sawa zenye kutamka kwa haki na kwa yaliyo ndiyo.

  483. 98:4
    ۝٤

    Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu ila baada ya kuwajia hiyo bayana. [4]

    Tanbihi

    [4] Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu katika Mayahudi na Wakristo, ila baada ya kuwajia hiyo hoja iliyo wazi yenye kuonyesha ya kwamba Muhammad ndiye huyo Mtume wa Mwenyezi Mungu aliye ahidiwa katika Vitabu vyao.

  484. 98:5
    ۝٥

    Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti. [5]

    Tanbihi

    [5] Na hawakulazimishwa jambo katika walio lazimishwa ila iwe ibada yao kwa Mwenyezi Mungu ni kumsafia Yeye Dini, waache upotovu wasimame sawa kwenye Haki, na wazihifadhi Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Mila Iliyo Nyooka.

  485. 98:6
    ۝٦

    Hakika walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu kabisa. [6]

    Tanbihi

    [6] Hakika wale walio kufuru katika Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu, wala hawatatoka humo. Hao ndio waovu wa viumbe kwa itikadi na vitendo.

  486. 98:7
    ۝٧

    Hakika walio amini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe. [7]

    Tanbihi

    [7] Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda vitendo vyema, hao ndio bora ya viumbe kwa itikadi na vitendo.

  487. 98:8
    ۝٨

    Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yu radhi nao, na wao waradhi naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi. [8]

    Tanbihi

    [8] Malipo yao Akhera kwa Imani na vitendo vyema walivyo vitanguliza, ni Mabustani ya kudumu yenye kupitiwa na mito kati yake, watakaa humo milele. Mwenyezi Mungu amepokea a'mali zao, na wao watamshukuru kwa hisani yake aliyo wafanyia. Hiyo ndiyo jaza ya mwenye kuiogopa adhabu ya Mola wake Mlezi, akaamini na akatenda mema.

  488. Sura Az-Zalzala

    سُورَةُ الزلزلة
  489. 99:1
    ۝١

    Itakapo tetemeshwa ardhi kwa mtetemeko wake! [1]

    Tanbihi

    [1] Ikitisika ardhi kwa mtikiso mkubwa, na ikasukika kwa ukomo wa kutisika na kusukika kunako mkinika na ikaweza kuchukua!

  490. 99:2
    ۝٢

    Na itakapo toa ardhi mizigo yake! [2]

    Tanbihi

    [2] Na ardhi ikatoa yote yaliomo katika ndani ya tumbo lake, ikiwa khazina au maiti walio kwisha zikwa!

  491. 99:3
    ۝٣

    Na mtu akasema: Ina nini? [3]

    Tanbihi

    [3] Na binaadamu akasema kwa kushtuka na khofu: Ardhi hii ina nini hata inatikisika hivi, na inatoa vilivyomo tumboni mwake, ndio Saa imefika?

  492. 99:4
    ۝٤

    Siku hiyo itahadithia khabari zake. [4]

    Tanbihi

    [4] Siku hiyo ardhi itamsimulia mtu khabari zake zilio mshitua,

  493. 99:5
    ۝٥

    Kwa sababu Mola wake Mlezi ameifunulia! [5]

    Tanbihi

    [5] Kwani Mlezi wake na Muumba wake atakuwa kaifunulia, kaipa Wahyi, na kaiamuru itetemeke na ijisuke suke, ndio ikafanya upesi kutekeleza amri.

  494. 99:6
    ۝٦

    Siku hiyo watu watatoka kwa mfarakano wakaonyweshwe vitendo vyao! [6]

    Tanbihi

    [6] Siku hiyo watu watatoka makaburini mbio, nao wamo katika mtafaruku, wapate kuziona hisabu zao na malipo yao aliyo waahidi Mwenyezi Mungu.

  495. 99:7
    ۝٧

    Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona! [7]

    Tanbihi

    [7] Basi mwenye kufanya hata kitu chenye uzito wa punje ya mchanga cha kheri ataiona katika daftari lake, na atapata malipo yake.

  496. 99:8
    ۝٨

    Na anaye tenda chembe ya uovu atauona! [8]

    Tanbihi

    [8] Na mwenye kufanya shari ya uzito wa chembe ya mchanga ataiona kadhaalika, na atapata malipo yake. Wala Mola wako Mlezi hatamdhulumu yeyote.

  497. Sura Al-Aadiyaat

    سُورَةُ العاديات
  498. 100:1
    ۝١

    Naapa kwa farasi wendao mbio wakipumua, [1]

    Tanbihi

    [1] Ninaapa kwa farasi wa Jihadi wendao mbio, na huku pumzi zao zinasikilizana kwa sauti inayo itwa "Dh'abh'an".

  499. 100:2
    ۝٢

    Na wakitoa moto kwa kupiga kwato zao chini, [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa farasi hao ambao hutoa cheche za moto zinapo gonga kwato zao kwenye ardhi wanapo kwenda.

  500. 100:3
    ۝٣

    Wakishambulia wakati wa asubuhi, [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwa farasi hao wanao washambulia maadui asubuhi kabla jua halijachomoza;

  501. 100:4
    ۝٤

    Huku wakitimua vumbi, [4]

    Tanbihi

    [4] Wakatimua mavumbia mengi, farasi hao, kati ya makundi ya maadui!

  502. 100:5
    ۝٥

    Na wakijitoma kati ya kundi, [5]

    Tanbihi

    [5] Ikawa vumbi limewagubika maadui hata wakaingiwa kiwewe na kufazaika.

  503. 100:6
    ۝٦

    Hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila kwa Mola wake Mlezi! [6]

    Tanbihi

    [6] Hakika mwanaadamu ni mwingi wa kuzikufuru neema za Mola wake Mlezi ambazo hazikadiriki.

  504. 100:7
    ۝٧

    Na hakika yeye mwenyewe bila ya shaka ni shahidi wa hayo! [7]

    Tanbihi

    [7] Na hakika yeye mwenyewe bila ya shaka atakuwa mwingi wa kuja jishuhudia huko Akhera kwa kuungama madhambi yake.

  505. 100:8
    ۝٨

    Naye hakika bila ya shaka ana nguvu za kupenda mali! [8]

    Tanbihi

    [8] Na hakika yeye kwa uchoyo na kuyapenda mali alio nayo, ni bakhili, hatoi kama inavyo mwajibikia katika mali yake.

  506. 100:9
    ۝٩

    Kwani hajui watakapo fufuliwa waliomo makaburini? [9]

    Tanbihi

    [9] Kwani hajui mwisho wa hali yake, hata hajui wakitolewa maiti waliomo makaburini,

  507. 100:10
    ۝١٠

    Na yakakusanywa yaliomo vifuani? [10]

    Tanbihi

    [10] Na vikakusanywa viliomo vifuani navyo vimekwisha sajiliwa katika madaftari yao, yakiwa mema au mabaya waliyo yatenda?

  508. 100:11
    ۝١١

    Kuwa hakika Mola wao Mlezi siku hiyo bila ya shaka atakuwa na khabari zao wote! [11]

    Tanbihi

    [11] Kwamba hakika Mlezi wao na Muumba wao bila ya shaka anajua vyema vitendo vyao na malipo yao Siku ya Kufufuliwa na Kulipwa.

  509. Sura Al-Qaari'a

    سُورَةُ القارعة
  510. 101:1
    ۝١

    Inayo gonga! [1]

    Tanbihi

    [1] AL-QAARIA'H, Inayo gonga, ni Kiyama, ambacho kinaanza kwa mpulizo wa mwanzo wa barugumu, na kinaishia itapo katwa hukumu baina ya watu.

  511. 101:2
    ۝٢

    Nini Inayo gonga? [2]

    Tanbihi

    [2] Kitu gani kilicho cha ajabu zaidi katika ukuu wake, na khatari zake na kitisho chake!

  512. 101:3
    ۝٣

    Na nini kitacho kujuilisha nini Inayo gonga? [3]

    Tanbihi

    [3] Na kitu gani kitacho kujuulisha hali ya AL-QAARIA'H katika kitisho chake juu ya nafsi za watu?

  513. 101:4
    ۝٤

    Siku ambayo watu watakuwa kama nondo walio tawanyika; [4]

    Tanbihi

    [4] Siku hiyo watu watakuwa kama vipepeo kwa wingi na kuhangaika kulia na kushoto, madhaifu na wanyonge!

  514. 101:5
    ۝٥

    Na milima itakuwa kama sufi zilizo chambuliwa! [5]

    Tanbihi

    [5] Na milima itakuwa kama sufi iliyo tiwa rangi na kuchambuliwa kwa kutapanyika vipande mbali mbali na kupeperuka katika anga huku na huku.

  515. 101:6
    ۝٦

    Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, [6]

    Tanbihi

    [6] Ama yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, mema yake yakapindukia kuliko maovu yake,

  516. 101:7
    ۝٧

    Huyo atakuwa katika maisha ya kupendeza. [7]

    Tanbihi

    [7] Basi huyo atakuwa na maisha yatayo mridhisha mwenyewe, na nafsi yake itue.

  517. 101:8
    ۝٨

    Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, [8]

    Tanbihi

    [8] Na ama ambaye mizani yake itakuwa nyepesi, na maovu yake yakazidi kuliko mema yake,

  518. 101:9
    ۝٩

    Huyo maskani yake yatakuwa Moto wa Hawiya! [9]

    Tanbihi

    [9] Basi makaazi yake yatakuwa Jahannamu.

  519. 101:10
    ۝١٠

    Na nini kitacho kujuilisha nini hiyo? [10]

    Tanbihi

    [10] Na nini cha kukujuulisha ni nini Hawiya?

  520. 101:11
    ۝١١

    Ni Moto mkali! [11]

    Tanbihi

    [11] Moto ulio mkali, hapana moto unao fikilia ukali wake, hata ukichochewa vipi na kutiwa kuni gani!

  521. Sura At-Takaathur

    سُورَةُ التكاثر
  522. 102:1
    ۝١

    Kumekushughulisheni kutafuta wingi, [1]

    Tanbihi

    [1] Yamekushughulisheni mkaacha kutimiza yaliyo waajibu na ya ut'iifu kule kujitapa kwenu kwa wana na wafwasi, na kujifakhiri kwa mali, na hisabu, na nasaba, mpaka yakusibuni mauti!

  523. 102:2
    ۝٢

    Mpaka mje makaburini! [2]

    Tanbihi

    [2] Mpaka yakusibuni mauti!

  524. 102:3
    ۝٣

    Sivyo hivyo! Mtakuja jua! [3]

    Tanbihi

    [3] Hakika mtakuja jua matokeo ya upumbavu wenu na mapuuza yenu.

  525. 102:4
    ۝٤

    Tena sivyo hivyo! Mtakuja jua! [4]

    Tanbihi

    [4] Na hakika bila ya shaka mtakuja jua natija ya hayo!

  526. 102:5
    ۝٥

    Sivyo hivyo! Lau mngeli jua kwa ujuzi wa yakini, [5]

    Tanbihi

    [5] Ama kwa hakika lau mngeli jua kwa yakini uovu wa mwisho wenu bila ya shaka mngeli ogopa huko kushindania kurindika mali, na mngeli jitengenezea Akhera yenu.

  527. 102:6
    ۝٦

    Basi bila ya shaka mtaiona Jahannamu! [6]

    Tanbihi

    [6] Nakuapieni na nakutilieni mkazo, enyi watu, kwamba hakika nyinyi mtakuja ushuhudia Moto unao waka.

  528. 102:7
    ۝٧

    Tena, bila ya shaka, mtaiona kwa jicho la yakini. [7]

    Tanbihi

    [7] Kisha ninaapa na natilia mkazo kwamba mtauona wazi na kwa yakini.

  529. 102:8
    ۝٨

    Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. [8]

    Tanbihi

    [8] Tena naapa na natilia mkazo kwamba hakika nyinyi mtahisabiwa kwa neema mlizo deka nazo na mkazistarehea.

  530. Sura Al-Asr

    سُورَةُ العصر
  531. 103:1
    ۝١

    Naapa kwa Zama! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa Zama kwa sababu ya maajabu mengi na mazingatio yaliomo ndani yake.

  532. 103:2
    ۝٢

    Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika khasara, [2]

    Tanbihi

    [2] Hakika kila binaadamu bila ya shaka yumo katika namna fulani au fulani ya kukhasiri, kwa mujibu wa anavyo ghilibiwa na pumbao na matamanio.

  533. 103:3
    ۝٣

    Ila wale walio amini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri. [3]

    Tanbihi

    [3] Isipo kuwa wale walio muamini Mwenyezi Mungu na wakatenda mema, na wakadumu juu ya ut'iifu, na wakasemezana na kuusiana kwa kushikamana na Haki, kwa itikadi, na maneno, na vitendo. Na wakausiana wasubiri na wavumilie mashaka yanayo wapata wenye kushikamana na Dini. Basi hao ndio wenye kusalimika na hiyo khasara, wenye kufanikiwa duniani na Akhera.

  534. Sura Al-Humaza

    سُورَةُ الهمزة
  535. 104:1
    ۝١

    Ole wake kila safihi, msengenyaji! [1]

    Tanbihi

    [1] Atapata adhabu kali na maangamio huyo ambaye mtindo wake ni kuwafedhehi watu kwa kauli au kwa ishara, au kuwasengenya kuwavunjia hishima zao.

  536. 104:2
    ۝٢

    Aliye kusanya mali na kuyahisabu. [2]

    Tanbihi

    [2] Ambaye amekusanya chungu ya mali na akawa kazi yake kuyahisabu tu, kwa kuona ladha huko kuhisabu.

  537. 104:3
    ۝٣

    Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele! [3]

    Tanbihi

    [3] Anadhani huyo kuwa mali yake yatamweka milele duniani, na yatamkinga na hayo anayo yachukia?

  538. 104:4
    ۝٤

    Hasha! Atavurumishwa katika H'ut'ama. [4]

    Tanbihi

    [4] Na aache dhana hiyo! Wallahi! Hapana shaka yoyote kwa vitendo vyake viovu hivyo atakuja tumbukizwa katika Moto unao vuruga kila kinacho tupwa humo!

  539. 104:5
    ۝٥

    Na nani atakujuvya ni nini H'ut'ama? [5]

    Tanbihi

    [5] Na kitu gani kitacho kujuvya nini ukweli wa Moto huu wa H'ut'ama?

  540. 104:6
    ۝٦

    Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa. [6]

    Tanbihi

    [6] Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa kwa amri yake, na daima unawaka!

  541. 104:7
    ۝٧

    Ambao unapanda nyoyoni. [7]

    Tanbihi

    [7] Ambao unafikilia nyoyoni na kuzizunguka nyoyo.

  542. 104:8
    ۝٨

    Hakika huo utafungiwa nao [8]

    Tanbihi

    [8] Huo utakuwa umefungwa milango yake, na wao watakuwa wamefungwa humo ndani

  543. 104:9
    ۝٩

    Kwenye nguzo zilio nyooshwa. [9]

    Tanbihi

    [9] Kwenye maguzo yaliyo nyooka. Hawawezi kutaharaki, wala kutoka.

  544. Sura Al-Fil

    سُورَةُ الفيل
  545. 105:1
    ۝١

    Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo? [1]

    Tanbihi

    [1] Hakika, ewe Muhammad, unajua kwa ujuzi usio ingiliwa na shaka yoyote, alivyo fanya Mola wako Mlezi kuwafanyia wale watu wenye tembo (ndovu), wakataka kuishambulia Nyumba takatifu ya Al-Kaaba.

  546. 105:2
    ۝٢

    Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? [2]

    Tanbihi

    [2] Unajua ya kwamba hakika Mwenyezi Mungu amejaalia juhudi yao kutaka kuibomoa Al-Kaaba ivize na ipotelee mbali. Juhudi yao ikapeperuka, na wao wasipate makusudio yao.

  547. 105:3
    ۝٣

    Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi, [3]

    Tanbihi

    [3] Na Mwenyezi Mungu aliwasalitisha na majeshi ya ndege yaliyo watokea makundi kwa makundi yakifuatana, na yakawazunguka kila upande.

  548. 105:4
    ۝٤

    Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni, [4]

    Tanbihi

    [4] Wakiwatupia mawe kutoka Jahannamu.

  549. 105:5
    ۝٥

    Akawafanya kama majani yaliyo liwa! [5]

    Tanbihi

    [5] Akawafanya kama majani ya mimea yaliyo sibiwa yakatilifu.

  550. Sura Quraish

    سُورَةُ قريش
  551. 106:1
    ۝١

    Kwa walivyo zoea Maqureshi, [1]

    Tanbihi

    [1] Hebu staajabuni kwa yanayo walazimu Makureshi! Kuwalazimu safari za musimu wa baridi kwenda Yaman,

  552. 106:2
    ۝٢

    Kuzoea kwao safari za siku za baridi na siku za joto. [2]

    Tanbihi

    [2] Na safari za musimu wa joto kwenda Shamu, kufanya biashara na kutafuta riziki kwa utulivu na amani. (Hizo safari za biashara za Yaman ndizo zilizo waleta Waarabu Afrika Mashariki kwa maelfu ya miaka, na zikauleta Uislamu pande za Afrika kabla ya kuenea Arabuni. Kwani nchi za Afrika Mashariki zilikaliwa na Waarabu kwa maelfu ya miaka. Soma Periplus of the Erythrean Sea, na East Africa and Its Invaders ya Prof. Coupland, na vitabu vya Sir John Gray na Dr. L.W. Hollingsworth.)

  553. 106:3
    ۝٣

    Basi nawamuabudu Mola Mlezi wa Nyumba hii, [3]

    Tanbihi

    [3] Basi wamtakasie ibada Mola Mlezi wa Nyumba hii aliye wawezesha kuzifanya hizi safari mbili.

  554. 106:4
    ۝٤

    Ambaye anawalisha wasipate njaa, na anawalinda na khofu. [4]

    Tanbihi

    [4] Ambaye anawalisha wasione njaa, na hali wao wamo katika bonde lisio na makulima, na akawalinda na khofu na watu wengine pembezoni mwao wananyakuliwa.

  555. Sura Al-Maa'un

    سُورَةُ الماعون
  556. 107:1
    ۝١

    Je! Umemwona anaye kadhibisha Malipo? [1]

    Tanbihi

    [1] Unamjua anaye kanusha malipo na hisabu ya Akhera?

  557. 107:2
    ۝٢

    Huyo ndiye anaye msukuma yatima, [2]

    Tanbihi

    [2] Ukitaka kumjua basi ni huyo ambaye anaye msukuma yatima kwa nguvu, na anamtumilia mabavu, na anamdhulumu,

  558. 107:3
    ۝٣

    Wala hahimizi kumlisha masikini. [3]

    Tanbihi

    [3] Na wala hahimizi kulishwa masikini.

  559. 107:4
    ۝٤

    Basi, ole wao wanao swali, [4]

    Tanbihi

    [4] Maangamio yatawashukia wanao sali na wakasifika kwa sifa hizi, na wakaghafilika na Swala zao wasinafiike nazo.

  560. 107:5
    ۝٥

    Ambao wanapuuza Sala zao; [5]

    Tanbihi

    [5] Maangamio yatawashukia wanao swali na wakasifika kwa sifa hizi, na wakaghafilika na Swala zao wasinafiike nazo.

  561. 107:6
    ۝٦

    Ambao wanajionyesha, [6]

    Tanbihi

    [6] Ambao huonyesha kwa watu vitendo vyao, ili wapate cheo katika nyoyo za hao watu, na wasifiwe.

  562. 107:7
    ۝٧

    Nao huku wanazuia msaada. [7]

    Tanbihi

    [7] Na huku wanazuia hisani zao na msaada wao kwa watu

  563. Sura Al-Kawthar

    سُورَةُ الكوثر
  564. 108:1
    ۝١

    Hakika tumekupa kheri nyingi. [1]

    Tanbihi

    [1] Sisi hakika tumekupa kheri nyingi za daima katika dunia na Akhera.

  565. 108:2
    ۝٢

    Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi. [2]

    Tanbihi

    [2] Ilivyo kuwa umepewa hayo, basi dumisha Swala kwa Mola wako Mlezi kwa usafi kabisa, na uchinje dhabihu wako kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa aliyo kupa ya ukarimu, na akakukhusisha wewe khasa kwa kukupa kheri.

  566. 108:3
    ۝٣

    Hakika anaye kuchukia ndiye aliye mpungufu. [3]

    Tanbihi

    [3] Hakika huyo anaye kuchukia ndiye aliye katika na kila kheri.

  567. Sura Al-Kaafiroon

    سُورَةُ الكافرون
  568. 109:1
    ۝١

    Sema: Enyi makafiri! [1]

    Tanbihi

    [1] Ewe Muhammad! Sema: Enyi makafiri, mlio shikilia juu ya ukafiri wenu.

  569. 109:2
    ۝٢

    Siabudu mnacho kiabudu; [2]

    Tanbihi

    [2] Mimi simuabudu mnaye muabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu.

  570. 109:3
    ۝٣

    Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu. [3]

    Tanbihi

    [3] Wala nyinyi si wenye kumuabudu huyo ambaye mimi namuabudu, naye ni Mwenyezi Mungu wa pekee.

  571. 109:4
    ۝٤

    Wala sitaabudu mnacho abudu. [4]

    Tanbihi

    [4] Wala mimi si mwenye kuabudu mfano wa ibada yenu, kwani nyinyi ni washirikina.

  572. 109:5
    ۝٥

    Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu. [5]

    Tanbihi

    [5] Wala nyinyi si wenye kuabudu mfano wa ibada yangu, kwani hii ni Tawhidi, ibada ya Mungu Mmoja.

  573. 109:6
    ۝٦

    Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu. [6]

    Tanbihi

    [6] Nyinyi mna dini yenu mnayo itakidi, na mimi nina Dini yangu aliyo niteulia Mwenyezi Mungu niishike.

  574. Sura An-Nasr

    سُورَةُ النصر
  575. 110:1
    ۝١

    Itakapo kuja nusura ya Mwenyezi Mungu na ushindi, [1]

    Tanbihi

    [1] Ikithibiti nusura ya Mwnyezi Mungu na ushindi kwako na kwa Waumini,

  576. 110:2
    ۝٢

    Na ukaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu kwa makundi, [2]

    Tanbihi

    [2] Na ukawaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi,

  577. 110:3
    ۝٣

    Zitakase sifa za Mola wako Mlezi, na umwombe msamaha; hakika Yeye ndiye anaye pokea toba. [3]

    Tanbihi

    [3] Basi mshukuru Mola wako Mlezi, na Sabbih' , Mtakase kwa sifa zake, na mtake akusamehe wewe na umma wako, kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kupokea toba za waja wake. Maoni ya wataalamu juu ya Surat Annas'r:- Sura hii tukufu inaashiria kugomboka kwa Makka. Na sababu khasa iliyo pelekea kugomboka Makka ni Maqureshi walipo vunja mkataba wa amani wa Hudaibiya kwa kuwashambulia kabila ya Khuzaa', ambao walikuwa wana masikilizano na Mtume s.a.w., na wakawasaidia Bani Bakri katika hayo. Yalipo tokea hayo Mtume akaona waliyo yafanya Maqureshi kuvunja mapatano imembidi ende kuigomboa Makka. Basi akakusanya jeshi la nguvu lenye wapiganaji elfu kumi. Akenda mwezi wa Ramadhani katika mwaka wa nane wa Hijra (Desemba mwaka 630 B.K.) Akawazuia watu wake wasipigane ila wakilazimishwa. Na Mwenyezi Mungu alipenda aingie Nabii na jeshi lake Makka bila ya vita. Na kwa hivi akapata ushindi mkubwa kabisa katika taarikhi ya wito wa Kiislamu, bila ya vita. Na Mwenyezi Mungu akamwezesha kusimamisha dola ya kwanza duniani bila ya vita na bila ya kumwagwa damu. Na huo ugombozi wa Makka ulikuwa na athari za kufikia mbali kwa pande za Dini na siyasa, kwani ilikuwa ni kuung'oa upagani, kuabudu masanamu, katika ngome yake kubwa, kwa kuvunjwa masanamu yaliyo simamishwa katika Al-kaaba, na yakaondolewa mapicha na masanamu yaliyo kuwemo. Na kwa kuingia Makka kwenye boma la Uislamu Nabii s.a.w. aliweza kuzishinda kabila zote zilizo bakia katika Hijazi, ambazo zilizo kuwa zina kani za kijahiliya, kama Hawazan na Thaqif. Mwenyezi Mungu akamwezesha kusimamisha dola si juu ya kabila wala nchi bali juu ya Imani, nayo ni Imani ya Kiislamu, na bendera ya Kiislamu

  578. Sura Al-Masad

    سُورَةُ المسد
  579. 111:1
    ۝١

    Imeangamia mikono ya Abu Lahab, na yeye pia ameangamia. [1]

    Tanbihi

    [1] Imeteketea mikono ya Abu Lahab iliyo kuwa ikiwaudhi Waislamu, na yeye mwenyewe amehiliki pia.

  580. 111:2
    ۝٢

    Hayatamfaa mali yake, wala alivyo vichuma. [2]

    Tanbihi

    [2] Hayatolindwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu mali yake aliyo kuwa nayo, wala cheo chake alicho kichuma.

  581. 111:3
    ۝٣

    Atauingia Moto wenye mwako. [3]

    Tanbihi

    [3] Ataingia katika Moto unao waka, aungue.

  582. 111:4
    ۝٤

    Na mkewe, mchukuzi wa kuni, [4]

    Tanbihi

    [4] Na ataingia pia kwenye Moto mkewe huyo aliye kuwa akibeba masengenyo baina ya watu, kama alivyo ingia yeye (mumewe).

  583. 111:5
    ۝٥

    Shingoni mwake iko kamba iliyo sokotwa. [5]

    Tanbihi

    [5] Juu ya shingo yake itakuwa kamba ya mtende ya kumtesa.

  584. Sura Al-Ikhlaas

    سُورَةُ الإخلاص
  585. 112:1
    ۝١

    Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee. [1]

    Tanbihi

    [1] Ewe Muhammad! Hao wanao sema kwa kejeli, "Tusifie Mola wako Mlezi.": waambie: Yeye ni Mwenyezi Mungu wa pekee hapana mwenginewe, wala hana mshirika.

  586. 112:2
    ۝٢

    Mwenyezi Mungu Mkusudiwa. [2]

    Tanbihi

    [2] Mwenyezi Mungu Mwenye kukusudiwa peke yake katika haja zote, na yote yanayo takikana.

  587. 112:3
    ۝٣

    Hakuzaa wala hakuzaliwa. [3]

    Tanbihi

    [3] Hana mtoto wala hakuzaliwa na baba wala mama,

  588. 112:4
    ۝٤

    Wala hana anaye fanana naye hata mmoja. [4]

    Tanbihi

    [4] Wala hana yeyote aliye mshabihi, au mfano wake.

  589. Sura Al-Falaq

    سُورَةُ الفلق
  590. 113:1
    ۝١

    Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko, [1]

    Tanbihi

    [1] Sema najikinga na Mola Mlezi wa asubuhi inapo pambazuka kutokana na usiku.

  591. 113:2
    ۝٢

    Na shari ya alivyo viumba, [2]

    Tanbihi

    [2] Na shari ya kila chenye shari katika viumbe, ambavyo hapana wa kuzuia shari yao ila Mwenye kumiliki amri yao.

  592. 113:3
    ۝٣

    Na shari ya giza la usiku liingiapo, [3]

    Tanbihi

    [3] Na shari ya usiku unapo kuwa totoro.

  593. 113:4
    ۝٤

    Na shari ya wanao pulizia mafundoni, [4]

    Tanbihi

    [4] Na shari ya anaye pita baina ya watu kwa sababu ya kuwafisidi.

  594. 113:5
    ۝٥

    Na shari ya hasidi anapo husudu. [5]

    Tanbihi

    [5] Na shari ya hasidi anaye tamani iondoke neema kwa wengine.

  595. Sura An-Naas

    سُورَةُ الناس
  596. 114:1
    ۝١

    Sema: Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu, [1]

    Tanbihi

    [1] Sema: Najikinga na Mola Mlezi wa wanaadamu, Mwenye kuendesha mambo yao.

  597. 114:2
    ۝٢

    Mfalme wa wanaadamu, [2]

    Tanbihi

    [2] Mfalme wa wanaadamu, kwa ufalme ulio timia, kuwamiliki wote wafalme wao na maraia.

  598. 114:3
    ۝٣

    Mungu wa wanaadamu, [3]

    Tanbihi

    [3] Mungu wa wanaadamu, Mwenye uweza kwa kuwasarifu kwa ukamilifu atakavyo.

  599. 114:4
    ۝٤

    Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannas, [4]

    Tanbihi

    [4] Na shari ya mwenye kutia wasiwasi watu, ambaye hurudi nyuma ukiomba msaada kwa Mwenyezi Mungu dhidi yake.

  600. 114:5
    ۝٥

    Anaye tia wasiwasi katika vifua vya watu, [5]

    Tanbihi

    [5] Ambaye hutia kwa kificho katika vifua vya watu ya kuwaachisha wasende kwenye njia ya uwongofu.

  601. 114:6
    ۝٦

    Kutokana na majini na wanaadamu. [6]

    Tanbihi

    [6] Kutokana na majini na wanaadamu.

Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani