Quran Touch

سُورَةُ الفجر

Sura Al-Fajr

Sura 89 · 30 aya · Ya Makka · Juzuu 30 · Msahafu Ukurasa 593–594 · Hizb 60

Sikiliza sura nzima Msomaji: Mishary Rashid Alafasy
Aa
Neno kwa neno

  1. 89:1
    ۝١

    Naapa kwa alfajiri! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa mwangaza wa asubuhi unapo ufukuza usiku.

  2. 89:2
    ۝٢

    Na kwa masiku kumi! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa masiku kumi yaliyo tukuzwa na Mwenyezi Mungu. (Na hayo ni masiku kumi ya mwanzo wa Mwezi wa Alhaj, Mfungo Tatu).

  3. 89:3
    ۝٣

    Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja! [3]

    Tanbihi

    [3] Na shafi' yaani hisabu inayo gawika kwa mbili, kama 4, 6, 8 n.k. na witri, yaani isiyo gawika kwa mbili, kama 1, 3, 5 n.k. katika kila kitu.

  4. 89:4
    ۝٤

    Na kwa usiku unapo pita! [4]

    Tanbihi

    [4] Na kwa usiku unapo pita kwa kwenda ulimwengu kwa namna ya ajabu.

  5. 89:5
    ۝٥

    Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili? [5]

    Tanbihi

    [5] Je! Katika vitu vilivyo tajwa vinavyo onekana kwa akili hapana kiapo cha kukinaisha?

  6. 89:6
    ۝٦

    Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A'di? [6]

    Tanbihi

    [6] Kwani hujui jinsi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu yake kaumu ya Hud, ?

  7. 89:7
    ۝٧

    Wa Iram, wenye majumba marefu? [7]

    Tanbihi

    [7] Watu wa Iram wenye majengo marefu?

  8. 89:8
    ۝٨

    Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi? [8]

    Tanbihi

    [8] Ambayo haikupata kujengwa mfano wake kwa umadhubuti na ujenzi katika nchi.

  9. 89:9
    ۝٩

    Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni? [9]

    Tanbihi

    [9] Kwani hukujua jinsi Mola wako Mlezi alivyo teremsha adhabu yake kwa Thamudi, kaumu ya Saleh, walio chonga majabali kujengea nyumba zao huko bondeni?

  10. 89:10
    ۝١٠

    Na Firauni mwenye vigingi? [10]

    Tanbihi

    [10] Au kwani hukujua vipi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu yake Firauni mwenye majeshi yaliyo upa nguvu ufalme wake kama vigingi vinavyo simamisha makhema?

  11. 89:11
    ۝١١

    Ambao walifanya jeuri katika nchi? [11]

    Tanbihi

    [11] Ambao walipita mipaka katika nchi?

  12. 89:12
    ۝١٢

    Wakakithirisha humo ufisadi? [12]

    Tanbihi

    [12] Na wakazidisha kufanya uharibifu kwa ukafiri na udhalimu?

  13. 89:13
    ۝١٣

    Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu. [13]

    Tanbihi

    [13] Basi Mola wako Mlezi aliwateremshia adhabu kali ya kuwaunguza.

  14. 89:14
    ۝١٤

    Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia. [14]

    Tanbihi

    [14] Hakika Mola wako Mlezi anaviangalia vitendo vya watu, na anawahisabia, na atakuja kuwalipa kwavyo.

  15. 89:15
    ۝١٥

    Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu! [15]

    Tanbihi

    [15] Ama mtu akijaribiwa na Mola wake Mlezi na akamkirimu, na akamneemesha kwa mali na cheo na nguvu, basi husema kwa kughurika na hayo: Mola wangu Mlezi amenitukuza kwa kuwa ninastahiki haya!

  16. 89:16
    ۝١٦

    Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge! [16]

    Tanbihi

    [16] Na pindi Mola wake Mlezi akimjaribu mtu kwa kumdhikisha riziki, basi hughafilika na hikima ya hayo na husema: Mola wangu Mlezi kanidhalilisha!

  17. 89:17
    ۝١٧

    Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima, [17]

    Tanbihi

    [17] Wacheni mtindo huo! Mambo siyo hayo kama msemavyo; bali nyinyi hamumkirimu yatima;

  18. 89:18
    ۝١٨

    Wala hamhimizani kulisha masikini; [18]

    Tanbihi

    [18] Wala hamhimizani kuwalisha masikini;

  19. 89:19
    ۝١٩

    Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa, [19]

    Tanbihi

    [19] Na mnakula mali ya urithi kwa pupa, hamchagui linalo faa na lisilo faa.

  20. 89:20
    ۝٢٠

    Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi. [20]

    Tanbihi

    [20] Na mnayapenda mali mno, yanayo kupelekeeni kupapatika katika kuyakusanya na ubakhili wa kuyatumia.

  21. 89:21
    ۝٢١

    Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande, [21]

    Tanbihi

    [21] Wacheni vitendo hivyo! Kwani inakungojeeni siku itapo lazwa ardhi iwe sawa sawa,

  22. 89:22
    ۝٢٢

    Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu, [22]

    Tanbihi

    [22] Na aje Mola wako Mlezi kama anavyo stahiki kuja kwake Subhanahu na Malaika waje kwa safu safu;

  23. 89:23
    ۝٢٣

    Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? [23]

    Tanbihi

    [23] Na siku hiyo iletwe Jahannamu, nyumba ya adhabu, siku hiyo yatapo tokea hayo mwanaadamu atakumbuka aliyo yaharibu - lakini wapi! Kukumbuka huko kumfae nini, na wakati umekwisha pita?

  24. 89:24
    ۝٢٤

    Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu! [24]

    Tanbihi

    [24] Atasema kwa majuto: Laiti ningeli jitangulizia katika dunia vitendo vyema vya kunifaa katika maisha ya Akhera!

  25. 89:25
    ۝٢٥

    Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake. [25]

    Tanbihi

    [25] Siku hiyo zitakuwa hali hizi, haadhibu mtu kama adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala hafungi mtu kama afungavyo Yeye.

  26. 89:26
    ۝٢٦

    Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake. [26]

    Tanbihi

    [26] Siku hiyo zitakuwa hali hizi, haadhibu mtu kama adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala hafungi mtu kama afungavyo Yeye.

  27. 89:27
    ۝٢٧

    Ewe nafsi iliyo tua! [27]

    Tanbihi

    [27] Ewe nafsi uliye tulia juu ya Haki!

  28. 89:28
    ۝٢٨

    Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. [28]

    Tanbihi

    [28] Rejea kwenye radhi ya Mola wako Mlezi nawe uradhi kwa neema ulio pewa, nawe umemridhisha kwa a'mali uliyo ikadimisha.

  29. 89:29
    ۝٢٩

    Basi ingia miongoni mwa waja wangu, [29]

    Tanbihi

    [29] Basi ingia katika kundi la waja wangu walio wema!

  30. 89:30
    ۝٣٠

    Na ingia katika Pepo yangu. [30]

    Tanbihi

    [30] Na ingia katika Pepo yangu, nyumba ya neema ya milele!

Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani

Soma kwa lugha nyingine

EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย