سُورَةُ التكوير
Sura At-Takwir
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 81:1١
Jua litakapo kunjwa! [1]
Tanbihi
[1] Jua litakapo kunjwa na mwangaza wake ukafutwa,
- 81:2٢
Na nyota zikazimwa! [2]
Tanbihi
[2] Na nyota ikazimwa nuru yao,
- 81:3٣
Na milima ikaondolewa! [3]
Tanbihi
[3] Na milima ikaondoshwa hapo ilipo,
- 81:4٤
Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe, [4]
Tanbihi
[4] Na ambao wa kuchukua mimba wakaharibu mimba zao,
- 81:5٥
Na wanyama wa mwituni wakakusanywa! [5]
Tanbihi
[5] Na nyama mwitu wakusanywe kutoka vichakani mwao na mashimoni mwao, hawajijui hawajitambui kwa wingi wa kufazaika.
- 81:6٦
Na bahari zikawaka moto! [6]
Tanbihi
[6] Na bahari zikawa zinawaka moto,
- 81:7٧
Na nafsi zikaunganishwa! [7]
Tanbihi
[7] Na roho zikaunganishwa na viwiliwili vyao,
- 81:8٨
Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa! [8]
Tanbihi
[8] Na mtoto wa kike aliye zikwa hai, akaulizwa kwa kumliwaza yeye, na kumshutumu aliye mzika hai,
- 81:9٩
Kwa kosa gani aliuliwa? [9]
Tanbihi
[9] Kwa makosa gani kauliwa, naye hana dhambi? (Ilikuwa ada ya makafiri wa Kiarabu kabla ya Uislamu kuwazika watoto wao wa kike nao wahai! Baadhi ya Mabaniani wanawauwa watoto wao wa kike hata hivi leo huko India!!)
- 81:10١٠
Na madaftari yatakapo enezwa, [10]
Tanbihi
[10] Na nyaraka zilizo andikwa ndani vitendo vya watu zikakunjuliwa wakati wa hisabu.
- 81:11١١
Na mbingu itapo tanduliwa, [11]
Tanbihi
[11] Na mbingu itapo ondoshwa pahala pake,
- 81:12١٢
Na Jahannamu itapo chochewa, [12]
Tanbihi
[12] Na Moto ukawashwa kwa mwako mkali,
- 81:13١٣
Na Pepo ikasogezwa, [13]
Tanbihi
[13] Na Pepo ikajongezwa ikawa karibu,
- 81:14١٤
Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha. [14]
Tanbihi
[14] Yatakapo tokea yote hayo, basi hapo tena kila nafsi itajua nini iliyo tanguliza, ikiwa kheri au shari.
- 81:15١٥
Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma, [15]
Tanbihi
[15] Naapa kiapo cha mkazo kwa nyota ambazo zinanywea zinapo chomoza, na hapo mwanga wake huwa khafifu,
- 81:16١٦
Zinazo kwenda, kisha zikajificha, [16]
Tanbihi
[16] Zenye kwenda na hujificha wakati wa kuchwa kwake, kama paa wanapo jificha kwenye mapango yao.
- 81:17١٧
Na kwa usiku unapo pungua, [17]
Tanbihi
[17] Na kwa usiku linapo pungua giza lake wakati unapo malizika.
- 81:18١٨
Na kwa asubuhi inapo pambazuka, [18]
Tanbihi
[18] Na kwa asubuhi unapo anza mwangaza wake na ukavuma upepo wake,
- 81:19١٩
Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, [19]
Tanbihi
[19] Hakika Qur'ani bila ya shaka ni kauli ya Mjumbe anaye toka kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mwenye kuhishimiwa kwake,
- 81:20٢٠
Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi, [20]
Tanbihi
[20] Mwenye nguvu katika kutekeleza waajibu wake, mwenye cheo na daraja mbele ya Mwenyezi Mungu Mwenye Kiti cha Enzi.
- 81:21٢١
Anaye t'iiwa, tena muaminifu. [21]
Tanbihi
[21] Tena ni mwenye kut'iiwa, na muaminifu wa kuchukua wahyi miongoni wa walio juu.
- 81:22٢٢
Na wala huyu mwenzenu hana wazimu. [22]
Tanbihi
[22] Na huyo Mtume wenu ambaye ni mwenzenu, mnaye mjua kuwa ana akili timamu, si mwendawazimu.
- 81:23٢٣
Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi. [23]
Tanbihi
[23] Na ninaapa kuwa Muhammad s.a.w. bila ya shaka alimwona Jibrili katika upeo wa macho kwa mujibu wa inavyo onekana.
- 81:24٢٤
Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu. [24]
Tanbihi
[24] Na Muhammad si bakhili wa kufikisha wahyi na kuwafunza watu.
- 81:25٢٥
Wala hii si kauli ya Shetani maluuni. [25]
Tanbihi
[25] Wala huu wahyi (ufunuo) ulio teremshwa juu yake si kauli ya Shetani aliye fukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.
- 81:26٢٦
Basi mnakwenda wapi? [26]
Tanbihi
[26] Basi njia gani iliyo ya uwongofu zaidi kuliko hii mnayo ifuata?
- 81:27٢٧
Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. [27]
Tanbihi
[27] Qur'ani si chochote ila ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote.
- 81:28٢٨
Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa. [28]
Tanbihi
[28] Kwa anaye taka, miongoni mwenu, kusimama sawa kufikilia haki na kweli.
- 81:29٢٩
Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. [29]
Tanbihi
[29] Na nyinyi hamwezi kutaka kitu ila anapo taka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย