سُورَةُ النبإ
Sura An-Naba
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 78:1١
WANAULIZANA nini? [1]
Tanbihi
[1] Wanaulizana nini hao makafiri?
- 78:2٢
Ile khabari kuu! [2]
Tanbihi
[2] Wanaulizana khabari kubwa, khabari ya kufufuliwa,
- 78:3٣
Ambayo kwayo wanakhitalifiana. [3]
Tanbihi
[3] Ambayo wao wamezama ndani yake kukhitalifiana baina ya wenye kuikataa na wenye kuitilia shaka.
- 78:4٤
La! Karibu watakuja jua. [4]
Tanbihi
[4] Kuwazuia kuulizana huko wanaambiwa kuwa watakuja ujua ukweli wa mambo hapo watapo ona kufufuliwa kumetokea khasa.
- 78:5٥
Tena la! Karibu watakuja jua. [5]
Tanbihi
[5] Tena kuwazuia, watakuja jua itapo wateremkia adhabu.
- 78:6٦
kaKwani hatukuifanya ardhi ma tandiko? [6]
Tanbihi
[6] Kwani wao hawaoni Ishara za uweza wetu kwamba Sisi tumeifanya ardhi imetandikwa upatikane utulivu juu yake na iwezekane kutembea juu yake?
- 78:7٧
kama Na milima vigingi? [7]
Tanbihi
[7] Na tukaifanya milima ni vigingi vya ardhi vya kuituliza? Sehemu ya gamba gumu lilio juu ya ardhi linfikilia kiasi ya kilomita 60 unene wake, na inazidi mikunjo, mifimbi, inapanda juu kuwa milima, na huteremka chini kuwa ni vina vya bahari; na hiyo hulingana kwa sababu ya uzito unao patikana kutokana na milima. Na kulingana huko hakuharibiki ila kwa kubugunyika, kwani gamba kavu la ardhi linazuiliwa na milima, kama vigingi vinavyo zuilia khema. (Rejea Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 7 ya Surat Qaf).
- 78:8٨
Na tukakuumbeni kwa jozi? [8]
Tanbihi
[8] Na tukakuumbeni kwa jozi, wanaume na wanawake?
- 78:9٩
Na tukakufanya kulala kwenu ni mapumziko? [9]
Tanbihi
[9] Na tukafanya kulala kwenu ni mapumziko ya machofu ya kazi? Kulala usingizi ni kusita nishat'i ya sehemu ya ubongo yenye kutambua na kuwa macho. Yaani gamba la ubongo, au kupunguka nishat'i yake kwa wingi, ukilinganisha na daraja za nishat'i ya sehemu za viungo vilio baki. Na kwa hivyo kunapunguka nguvu na joto la mwili, tena mwili hapo wakati wa usingizi hupata kutua na kupumzika baada ya kuhangaika viungo au akili au vyote viwili. Basi kazi za kimwili zote hupunguka isipo kuwa kazi za kusaga chakula, na kupitisha mkojo katika mafigo, na kutoka majasho katika ngozi, kwani yakisita hayo hupatikana madhara juu ya maisha ya mtu. Ama kuvuta pumzi huko nako hupunguka, na huwa ni kwa ndani zaidi, na huwa kwa kifua zaidi kuliko kwa tumbo. Na mpigo wa mishipa hupungua kasi kwa kunavyo tokana na moyo, na hudhoofika mkazano wa musulo (muscular tension), na kwa hivyo huwa taabu kupata harakati za kinyume. Na yote haya ni ili binaadamu apate kupumzika wakati wa kulala.
- 78:10١٠
Na tukaufanya usiku ni nguo? [10]
Tanbihi
[10] Na tumeufanya usiku ni sitara kwenu kwa kiza kinacho kufunikeni.
- 78:11١١
Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha? [11]
Tanbihi
[11] Na tumeufanya mchana ni wakati wa kuhangaika kwenu kutafuta cha kukusaidieni katika maisha yenu.
- 78:12١٢
Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu? [12]
Tanbihi
[12] Na tumesimamisha juu yenu mbingu saba zenye nguvu madhubuti.
- 78:13١٣
Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto; [13]
Tanbihi
[13] Na Sisi tumeliumba jua lenye mwangaza na linalo waka. Makusudio ya Assiraj Alwahhaaj, Taa yenye mwanga na joto, ni Jua. Na hayo kama ilivyo thibiti katika sayansi kuwa daraja ya joto la uso wake inafika daraja 6000. Ama kati yake daraja yake inazidi daraja 30 milioni kwa sababu ya mdidimizo mkubwa unao patikana juu ya madda ziliomo ndani yake. Na jua linatoa nishat'i hizi zifuatazo: 9 katika 100 ya miale ya Ultraviolet rays, 46 katika 100 ya miale ya mwangaza, 45 katika 100 miale ya joto, au Infra red rays. Na kwa hivyo hii Aya tukufu imeliita kuwa ni Taa yenye mwangaza na joto.
- 78:14١٤
Na tukateremsha maji yanayo anguka kwa kasi kutoka mawinguni, [14]
Tanbihi
[14] Na tumeteremsha kutokana na mawingu yaliyo karibia kunyesha maji yenye kumiminika kwa nguvu. Mvua ndio kitu pekee kinacho toka asli yake maji matamu katika ardhi. Na asli ya mvua ni kukusanyika vijisehemu vya maji yanayo panda kutoka baharini, na maziwa na mito, yakakusanyika kama mawingu na yakageuka chembe za mvua au vipande vya barafu, na khatimaye yakaanguka kwa sura ya mvua au theluji.
- 78:15١٥
Ili tutoe kwayo nafaka na mimea. [15]
Tanbihi
[15] Ili tutoe kwa maji haya nafaka na mimea kuwa ni chakula kwa ajili ya watu na wanyama.
- 78:16١٦
Na mabustani yenye miti iliyo kamatana. [16]
Tanbihi
[16] Na mabustani yenye miti iliyo fungamana na matawi yake yameingiliana.
- 78:17١٧
Hakika siku ya uamuzi imewekewa wakati wake, [17]
Tanbihi
[17] Hakika siku ya uamuzi baina ya viumbe imewekewa miadi ilio kwisha kadiriwa kwa ajili ya kufufuliwa.
- 78:18١٨
Siku litapo pulizwa barugumu, nanyi mtakuja kwa makundi, [18]
Tanbihi
[18] Siku litakapo pulizwa barugumu na kufufuliwa watu, mtakuja kwenye mkutano makundi kwa makundi.
- 78:19١٩
Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango. [19]
Tanbihi
[19] Na mbingu zitapasuliwa kila upande hata zitakuwa ni milango milango.
- 78:20٢٠
Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi. [20]
Tanbihi
[20] Na milima itaondolewa baada ya kung'olewa mwahala mwake, na kuvurugwa, ikawa unaiona kama sura ya milima na hali hiyo ni kifusi tu kilicho rindikwa, kama uonavyo mangati, sarabi, unaona kama sura ya maji nayo si maji.
- 78:21٢١
Hakika Jahannamu inangojea! [21]
Tanbihi
[21] Hakika Jahannamu imekuwa kama ni kitu kinacho ngojea, walinzi wake wanawangojea watu watakao kuja kuingia.
- 78:22٢٢
Kwa walio asi ndio makaazi yao, [22]
Tanbihi
[22] Yawe ni marejeo na mafikio kwa wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu.
- 78:23٢٣
Wakae humo karne baada ya karne, [23]
Tanbihi
[23] Watakaa humo dahari baada ya dahari.
- 78:24٢٤
Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji, [24]
Tanbihi
[24] Hawataonja humo hata chembe ya upepo wa kuburudisha joto lake, wala kinywaji cha kupoza kiu chao.
- 78:25٢٥
Ila maji yamoto sana na usaha, [25]
Tanbihi
[25] Lakini watakunywa maji yalio pita ukomo kwa umoto wake, na usaha unao miminika kutokana na ngozi za watu wa Motoni.
- 78:26٢٦
Ndio jaza muwafaka. [26]
Tanbihi
[26] Malipo ya kuwafikiana na vitendo vyao viovu.
- 78:27٢٧
Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu. [27]
Tanbihi
[27] Kwani hao hawakutaraji kuwa itakuwapo kuhisabiwa, hata watende ya kuwaokoa humo.
- 78:28٢٨
Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu. [28]
Tanbihi
[28] Wakazikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuthibitisha kufufuliwa kwa mkadhibisho mkali.
- 78:29٢٩
Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika. [29]
Tanbihi
[29] Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.
- 78:30٣٠
Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu! [30]
Tanbihi
[30] Basi onjeni, wala hampati kwetu ila kuzidishiwa adhabu tu.
- 78:31٣١
Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu, [31]
Tanbihi
[31] Hakika wenye kumcha Mola wao Mlezi watapata kuokoka na adhabu, na wataipata Pepo,
- 78:32٣٢
Mabustani na mizabibu, [32]
Tanbihi
[32] Na mabustani yenye matunda, na mizabibu mizuri,
- 78:33٣٣
Na wake walio lingana nao, [33]
Tanbihi
[33] Na wanawari walio watipwatipwa wa hirimu yao,
- 78:34٣٤
Na bilauri zilizo jaa, [34]
Tanbihi
[34] Na bilauri safi zilizo jaa pomoni,
- 78:35٣٥
Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo, [35]
Tanbihi
[35] Hawasikii huko Peponi upuuzi wala uwongo.
- 78:36٣٦
Malipo kutoka kwa Mola wako Mlezi, kipawa cha kutosha. [36]
Tanbihi
[36] Ni malipo kutokana na Mola wako Mlezi, kwa fadhila yake na ihsani ya kutosha.
- 78:37٣٧
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, Arrahman, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake! [37]
Tanbihi
[37] Mola Mlezi wa mbinguni na duniani na vilio baina yao, ambaye rehema yake imeenea juu ya kila kitu. Hapana yeyote mwenye madaraka ya kusema mbele yake.
- 78:38٣٨
Siku atakapo simama Roho na Malaika kwa safu. Hawatasema ila Mwingi wa rehema aliye mruhusu, na atasema yaliyo sawa tu. [38]
Tanbihi
[38] Siku atakapo simama Jibrili na Malaika walio teuliwa nao wamenyenyekea, hasemi mmoja wao ila akipewa idhini na Arrahman, Mwingi wa rehema, kuwa aseme, naye atasema lilio sawa tu.
- 78:39٣٩
Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anaye taka na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi [39]
Tanbihi
[39] Hiyo ndiyo siku isiyo na shaka. Basi atakaye na ashike njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi arejee kwa Imani, na a'mali njema.
- 78:40٤٠
Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapo ona yaliyo tangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: Laiti ningeli kuwa udongo! [40]
Tanbihi
[40] Hakika Sisi tumekuhadharisheni na adhabu itakayo tokea karibu, siku atakapo angalia mtu vitendo vyake vilivyo tangulizwa na mikono yake, na atakapo sema kafiri kwa kutamani kuokoka: Laiti ningeli bakia udongo baada ya kufa, nisifufuliwe wala nisihisabiwe!
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย