سُورَةُ المرسلات
Sura Al-Mursalaat
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 77:1١
Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole! [1]
Tanbihi
[1] Naapa kwa Aya zilizo tumwa kwa ulimi wa Jibrili kumpelekea Muhammad kwa upole wa kawaida na kheri,
- 77:2٢
Na zinazo vuma kwa kasi! [2]
Tanbihi
[2] Na kwa Aya zenye kuzitwaa kwa nguvu dini nyengine zote za uwongo zikizipeperushia mbali,
- 77:3٣
Na zikaeneza maeneo yote! [3]
Tanbihi
[3] Na kwa Aya zenye kueneza hikima na uwongofu katika nyoyo za walimwengu kwa uenezi mkubwa mno,
- 77:4٤
Na zinazo farikisha zikatawanya! [4]
Tanbihi
[4] Na zenye kufarikisha baina ya kweli na uwongo kwa mfarakano ulio wazi kabisa,
- 77:5٥
Na zinazo peleka mawaidha! [5]
Tanbihi
[5] Na zenye kuwapa watu mawaidha ya kuwanufaisha,
- 77:6٦
Kwa kuudhuru au kuonya, [6]
Tanbihi
[6] Ili iwe ni udhuru kwao na onyo wasiwe na hoja,
- 77:7٧
Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa! [7]
Tanbihi
[7] Hakika haya mliyo ahidiwa ya kuja Kiyama kwa yakini yatatimia tu bila ya shaka yoyote.
- 77:8٨
Wakati nyota zitakapo futwa, [8]
Tanbihi
[8] Basi nyota zitapo ondolewa kabisa,
- 77:9٩
Na mbingu zitakapo pasuliwa, [9]
Tanbihi
[9] Na mbingu zitapo pasuka,
- 77:10١٠
Na milima itakapo peperushwa, [10]
Tanbihi
[10] Na milima ikavurugwa na ikapeperushiwa mbali na upepo,
- 77:11١١
Na Mitume watakapo wekewa wakati wao, [11]
Tanbihi
[11] Na Mitume wakawekewa wakati maalumu wahudhurie kwa ajili ya kuwatolea ushahidi kaumu zao.
- 77:12١٢
Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo? [12]
Tanbihi
[12] Kwa ajili ya siku gani yametayarishwa mambo haya makubwa makubwa?
- 77:13١٣
Kwa siku ya kupambanua! [13]
Tanbihi
[13] Kwa ajili ya siku watakapo pambanuliwa baina ya viumbe.
- 77:14١٤
Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni nini? [14]
Tanbihi
[14] Na nini cha kukujuvya ina nini hiyo siku ya kupambanua?
- 77:15١٥
Ole wao, siku hiyo hao wanao kanusha! [15]
Tanbihi
[15] Ni maangamio ya milele siku hiyo kwa hao wanao kadhibisha walio waahidi Mitume!
- 77:16١٦
Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia? [16]
Tanbihi
[16] Kwani hatukuwaangamiza mataifa ya zamani yaliyo kadhibisha,
- 77:17١٧
Kisha tukawafuatilizia walio fuatia? [17]
Tanbihi
[17] Na kisha tukawafuatilizia hao wenginewe tukawateketeza hali kadhaalika,
- 77:18١٨
Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu! [18]
Tanbihi
[18] Kwa madhambi waliyo yafanya na walivyo mkataa Mwenyezi Mungu?
- 77:19١٩
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [19]
Tanbihi
[19] Siku hiyo ni siku ya kuteketezwa walio kadhibisha, kama tulivyo waahidi.
- 77:20٢٠
Kwani hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa? [20]
Tanbihi
[20] Kwani hatukukuumbeni kutokana na maji yaliyo dhalili, nayo ni manii,
- 77:21٢١
Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti? [21]
Tanbihi
[21] Na tukayaweka maji haya katika pahala patulivu,
- 77:22٢٢
Mpaka muda maalumu? [22]
Tanbihi
[22] Mpaka kutimilia kuumbwa kwake na kutengenezwa kwake kwa muda anao ujua Mwenyezi Mungu.
- 77:23٢٣
Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria. [23]
Tanbihi
[23] Nasi tukaweka vipimo katika kuumbwa kwake, na kutengenezwa kwake, na kutoka kwake. Basi wabora wa kupima na kukadiria ni Sisi.
- 77:24٢٤
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [24]
Tanbihi
[24] Ole wao hao wanao kadhibisha neema za kuumba na kukadiria.
- 77:25٢٥
Kwani hatukuifanya ardhi yenye kukusanya [25]
Tanbihi
[25] Kwani hatukuifanya ardhi kuwa imekusanya juu ya mgongo wake
- 77:26٢٦
Walio hai na maiti? [26]
Tanbihi
[26] Viumbe vilivyo hai visio hisabika, na vilio kufa visio kadirika,
- 77:27٢٧
Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu? [27]
Tanbihi
[27] Na tukaweka milima iliyo thibiti imara mirefu, na tukakunywesheni maji matamu?
- 77:28٢٨
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [28]
Tanbihi
[28] Wataangamia siku hiyo hao wanao kadhibisha neema hizi!
- 77:29٢٩
Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha! [29]
Tanbihi
[29] Siku ya kupambanua wataambiwa makafiri: Nendeni huko Motoni mliko kuwa mkikukanusha.
- 77:30٣٠
Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu! [30]
Tanbihi
[30] Nendeni kwenye joto la moshi wa Jahannamu ulio gawika kwa ukubwa wake mapande matatu.
- 77:31٣١
Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako. [31]
Tanbihi
[31] Hapana cha kujikinga na joto la siku hiyo, wala kivuli hicho hakipunguzi joto la mwako hata kidogo.
- 77:32٣٢
Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba! [32]
Tanbihi
[32] Moto huo hutupa macheche yenye ukubwa kama majumba,
- 77:33٣٣
Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano! [33]
Tanbihi
[33] Au utaona hayo macheche kama ngamia weusi wenye kuingia rangi ya manjano.
- 77:34٣٤
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [34]
Tanbihi
[34] Wataangamia siku hiyo wanao kanusha kwamba hizi ndizo sifa za Moto.
- 77:35٣٥
Hii ni siku ambayo hawatatamka kitu, [35]
Tanbihi
[35] Haya uliyo simuliwa yatatokea katika siku ambayo hawatatamka kitu cha kuwanufaisha,
- 77:36٣٦
Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru. [36]
Tanbihi
[36] Wala hawatakuwa na idhini ya kutamka, wala hawatatoa udhuru, kwani hawana udhuru.
- 77:37٣٧
Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! [37]
Tanbihi
[37] Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha siku hii.
- 77:38٣٨
Hii ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia. [38]
Tanbihi
[38] Hii ndiyo siku ya kufafanua baina ya mwenye ukweli, na mwenye uwongo, kwa kuwa kila mmoja atalipwa kwa mujibu wa anavyo stahiki. Enyi mnao mkadhibisha Muhammad! Tumekujaalieni nyinyi na walio kutangulieni walio kadhibisha mfano wenu,
- 77:39٣٩
kiwa mnayo hila, nifanyieni hila Mimi! [39]
Tanbihi
[39] Kama mnayo hila ya kujikinga na adhabu basi fanyeni hila hiyo. Basi njooni muepukane na adhabu yangu.
- 77:40٤٠
Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! [40]
Tanbihi
[40] Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha ahadi ya Mwenyezi Mungu.
- 77:41٤١
Hakika wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem, [41]
Tanbihi
[41] Hakika wachamngu wenye kujikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu watakuwa katika kivuli kikubwa, na chemchem zinazo miminika,
- 77:42٤٢
Na matunda wanayo yapenda, [42]
Tanbihi
[42] Na matunda wanayo yaonea ladha, na wanayo yapenda,
- 77:43٤٣
Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda. [43]
Tanbihi
[43] Wataambiwa kwa kuamkiwa na kukirimiwa: Kuleni na mnywe chakula na vinywaji kwa starehe kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kuwa mkivitenda duniani.
- 77:44٤٤
Hakika ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema. [44]
Tanbihi
[44] Hakika Sisi huwalipa mfano wa malipo hayo matukufu watu wema.
- 77:45٤٥
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [45]
Tanbihi
[45] Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha Pepo.
- 77:46٤٦
Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu! [46]
Tanbihi
[46] Na makafiri wataambiwa: Kuleni na mjistareheshe kwa starehe isiyo baki muda mrefu, kwani hakika nyinyi ni wakosefu kwa kumshirikisha kwenu Mwenyezi Mungu.
- 77:47٤٧
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [47]
Tanbihi
[47] Wataangamia siku hiyo wanao ikadhibisha neema.
- 77:48٤٨
Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami. [48]
Tanbihi
[48] Na wakiambiwa: Swalini kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na mnyenyekeeni Yeye, hawanyenyekei wala hawaswali; bali hushikilia kiburi chao!
- 77:49٤٩
Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [49]
Tanbihi
[49] Wataangamia siku wanao kadhibisha amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake.
- 77:50٥٠
Basi maneno gani baada ya haya watayaamini? [50]
Tanbihi
[50] Basi maneno gani hawa watayaamini ikiwa hawaiamini Qur'ani, na hali hii ni muujiza ulio toka mbinguni?
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย