Quran Touch

Juzuu 29 (Tabarak)

Al-Mulk 67:1 – Al-Mursalaat 77:50 · 431 aya

Aa
Neno kwa neno

  1. Sura Al-Mulk

    سُورَةُ الملك
  2. 67:1
    ۝١

    AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. [1]

    Tanbihi

    [1] Ametukuka, na amezidi baraka zake Mwenye kumiliki peke yake uwezo wa kuendesha mambo ya viumbe vyote. Na Yeye, juu ya kila kitu, anao uwezo ulio timia.

  3. 67:2
    ۝٢

    Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha. [2]

    Tanbihi

    [2] Ambaye ndiye aliye umba mauti na uhai kwa makusudio anayo yataka Yeye, ili akufanyieni mtihani ni yupi katika nyinyi anaye fanya vitendo sawa, na mwenye niya safi. Na Yeye ni Mwenye kushinda, wala hashindiki kwa kitu, Mwenye msamaha kwa wenye upungufu.

  4. 67:3
    ۝٣

    Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote? [3]

    Tanbihi

    [3] Yeye ndiye aliye zizua mbingu saba zilizo pandana kwa mpango mmoja sawa sawa. Huoni tafauti yoyote katika uundaji wa Mwenyezi Mungu, ambaye rehema yake imeenea kwenye viumbe vyake vyote. Basi hebu tazama tena, unaona khitilafu yoyote?

  5. 67:4
    ۝٤

    Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka. [4]

    Tanbihi

    [4] Kisha tazama tena, na tena! Jicho lako linakurejea mwenyewe bila ya kugundua aibu yoyote, nalo limechoka.

  6. 67:5
    ۝٥

    Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu. [5]

    Tanbihi

    [5] Na hakika Sisi tumeipamba mbingu hii ya karibu, unayo iona kwa macho, tumeipamba kwa nyota zinazo ng'aa. Na tumefanya katika hizo vimondo vya kuwapopolea mashetani; na Akhera tumewaandalia adhabu ya moto unao waka. Mbingu ni kila kilicho juu yetu kikatufunika. Amesema Ibn Sayyidih: Hiyo ni bahari ya anga na vyombo vyote viliomo ndani yake na vimondo. Na sura wanayo iona wakaazi wa duniani katika masiku yaliyo safi ni kama qubba la kibuluu lilio pambwa kwa nyota na sayari kama kwamba ni taa, kama unavyo ziona nyota za mkia, au vimondo, vinakwenda angani vikiungua huko juu ya ardhi. Na hilo qubba la kibuluu si chochote ila ni matokeo ya mwangaza wa jua na nyota pamoja na takataka za vumbi zinazo ning'inia katika hewa, na sehemu za hewa molecules zinazo tawanyika. Haya mbali na yanayo onekana katika mwangaza nafsi yake ambayo huipamba mbingu hii ya karibu, kama vile zile rangi nzuri nzuri za wakati wa kuchwa jua, au wakati wa kuchomoza jua alfajiri, na mianga ya njia za nyota, miangaza ya kaskazini, na miangaza ya katika sehema za Polar regions. Na hayo yote yanayo onekana ni matokeo ya kuingiliana mwanga pamoja na funiko la anga la ardhi na uwanja wake wa smaku, magnetic field.

  7. 67:6
    ۝٦

    Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo! [6]

    Tanbihi

    [6] Na kwa ajili ya wasio muamini Mola wao Mlezi tumewawekea adhabu ya Jahannamu. Na huo ndio mwisho muovu kweli kwao.

  8. 67:7
    ۝٧

    Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka. [7]

    Tanbihi

    [7] Wakitiwa humo watasikia sauti mbaya ya kuchusha, na huo moto unatokota kwa ukali,

  9. 67:8
    ۝٨

    Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji? [8]

    Tanbihi

    [8] Unakaribia kukatika na kutawanyika kwa wingi wa kuwaghadhibikia. Kila likitumbukizwa kundi mojapo kati yao walinzi wake huwauliza kwa kuwakejeli: Kwani hakukujieni Mtume kukuhadharisheni na mkutano wa siku hii ya leo?

  10. 67:9
    ۝٩

    Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa! [9]

    Tanbihi

    [9] Na wao watajibu: Ametujia mwonyaji, lakini sisi tulimkanusha tukamwambia mwongo, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakukuteremshia chochote wewe wala Mitume wenginewe. Nyinyi mnao dai Utume si chochote ila ni watu walio potoka, na mko mbali na haki.

  11. 67:10
    ۝١٠

    Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni! [10]

    Tanbihi

    [10] Na watasema: Lau kuwa tulikuwa tunasikia kama inavyo faa asikie mwenye kutaka ukweli wa mambo, au tunafikiri tunayo itiwa, tusinge kuwa miongoni mwa watu wa Motoni.

  12. 67:11
    ۝١١

    Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni! [11]

    Tanbihi

    [11] Basi wataungama kukadhibisha kwao na kukufuru kwao. Watu wa Motoni wamepotelea mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu!

  13. 67:12
    ۝١٢

    Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa. [12]

    Tanbihi

    [12] Hakika wenye kumkhofu Mola wao Mlezi, na hali wao hawamwoni, watafutiwa madhambi yao, na watapata thawabu kubwa kwa mema yao.

  14. 67:13
    ۝١٣

    Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. [13]

    Tanbihi

    [13] Na ficheni kauli yenu, au itangazeni. Yote mawili kwa Mwenyezi Mungu ni sawa, kwani Yeye ni Mkuu wa kuyazunguka yote kwa kuyajua, Mjuzi wa vinavyo ficha vifua.

  15. 67:14
    ۝١٤

    Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari? [14]

    Tanbihi

    [14] Kwani Muumba si Mwenye kujua mambo yote ya waja wake? Na Yeye ni Mjuzi wa dogo na kubwa

  16. 67:15
    ۝١٥

    Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa. [15]

    Tanbihi

    [15] Yeye ndiye aliye ifanya ardhi dhalili inakut'iini. Basi tembeeni pande zake kote kote. Na kuleni katika riziki zake zinazo toka ndani yake. Na kwake Yeye peke yake ndio kufufuliwa na kulipwa.

  17. 67:16
    ۝١٦

    Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika! [16]

    Tanbihi

    [16] Je! Mmejiaminisha na Mwenye Ufalme wa mbinguni, kuwa hatakukatieni ardhi, akakuchukulieni kwa ghafla kwa mtikiso mkubwa?

  18. 67:17
    ۝١٧

    Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu? [17]

    Tanbihi

    [17] Bali, mmejiaminisha na Mwenye Ufalme wa mbinguni, kuwa hatakupelekeeni upepo wa kukupopoeni kwa changarawe? Hapo basi mtakijiua kitisho cha onyo langu kwenu!

  19. 67:18
    ۝١٨

    Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu? [18]

    Tanbihi

    [18] Na hakika walikwisha wakanusha Mitume wao hao walio kuwa kabla ya kaumu yako. Basi ghadhabu yangu juu yao ilikuwa hali gani kwa nilivyo waangamiza na kuwashika!

  20. 67:19
    ۝١٩

    Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu. [19]

    Tanbihi

    [19] Wameingia upofu? Wala hawakuwaangalia ndege walio juu yao, vipi wanavyo kunjua mbawa zao mara kwa mara, na mara nyingine wakizikunja? Hapana anaye washikilia wasianguke ila Mwingi wa Rehema. Hakika Yeye ni Mwingi wa ujuzi na khabari kwa kila kitu. Anakipa kila kitu jambo kwa mujibu wa maslaha yake. Kukunjua huku ni kukunjua ndege mbawa zake bila ya kuziendesha. Katika kuruka kwa ndege ipo miujiza ambayo haikufahamika baadhi yake ila baada ya kuendelea ilimu ya kuruka na nadhariya ya kutembea katika hewa. Lakini katika yanayo staajabisha ni kupita ndege katika anga na mbawa zote mbili zimetulia mpaka apite upeo wa macho. Na ilimu imevumbua kuwa ndege wanao kunjua mbawa zao hupanda juu ya mikondo ya hewa inayo saidia inayo timbuka ama kwa kupigana dafrau na kiziwizi fulani au kwa kunyanyuka nguzo za hewa imoto. Ukiwa upepo ni mzuri hizo nguzo za hewa husimama wima na ndege hupaa kwa namna ya mzunguko kama skurubu. Na ukiwa mkali hizo nguzo hugeuka kuelekea juu na ndege huruka bila ya kupiga mbawa kwa njia ya sawa moja kwa moja na kufikia mbali. Na ndege kwa jumla wana sifa maalumu, katika hizo ni kuwa ni wepesi, na wana umbo la nguvu, na nyoyo zao ni madhubuti, na kadhaalika mzunguko wao wa damu, na vyombo vya kuvutia pumzi, na namna lilivyo pimika umbo lao, na vikawa sawa sawa viwiliwili vyao kwa kusahilisha kuruka katika hewa. Na sifa hizi Mwenyezi Mungu Mjuzi Mwenye kuona kawajaalia ndege , kwa ajili ya kuwahifadhi hao ndege katika hewa pale wanapo kunjua mbawa zao au wanapo zikunja. Ama videge vidogo vinavyo tegemea kuruka kwao juu ya mbio, hivyo hupiga mbawa zao kwa chini na mbele ili vipate kujisukuma na kupaa. Na hayo ni dharura kwa sababu ya kuruka kwao. Kisha huzikunja mbawa zao, lakini nao wanabaki kuwa wanaruka kwa zile nguvu za msukumo wao. Na hivyo linawafikiana umbo lao hao ndege wa kila namna na muundo wa kifundi wa miili yao kwa kuwazesha kuruka na kujilinda sawa wakati wa kuruka.

  21. 67:20
    ۝٢٠

    Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu. [20]

    Tanbihi

    [20] Bali ni nani huyo mwenye nguvu kwenu atakaye kulindeni na adhabu asiye kuwa Mwenyewe Arrahman, Mwingi wa Rehema? Makafiri hawamo ila katika udanganyifu tu kwa hayo wanayo yadhania.

  22. 67:21
    ۝٢١

    Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki. [21]

    Tanbihi

    [21] Bali ni nani huyo atakaye kuruzukuni kwa yanayo kupeni uhai wenu na starehe zenu, ikiwa Mwenyezi Mungu akizuia riziki zake asikupeni? Bali makafiri wamekakamia katika kutakabari kwao na kuikimbia Haki.

  23. 67:22
    ۝٢٢

    Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka? [22]

    Tanbihi

    [22] Je! Hali itageuka? Mwenye kwenda akijikwaa na kusinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi katika mwendo wake, au yule anaye tembea sawasawa kwenye njia isiyo kwenda upogo?

  24. 67:23
    ۝٢٣

    Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu. [23]

    Tanbihi

    [23] Sema: Huyo aliye kuumbeni nanyi hamjakuwa chochote, na akakupeni usikizi na kuona, na fahamu ambazo ni sababu za vitendo vyenu na uwongofu wenu - ama ni kuchache mno kushukuru kwenu kwa neema hizi kumshukuru huyo aliye kupeni.

  25. 67:24
    ۝٢٤

    Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa. [24]

    Tanbihi

    [24] Sema: Huyo ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake Yeye peke yake ndio mtarejea kwa ajili ya kukuhisabuni na kukulipeni.

  26. 67:25
    ۝٢٥

    Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli? [25]

    Tanbihi

    [25] Na wanasema wanao kanya kufufuliwa: Yatatokea lini haya ya kukusanywa watu? Twambieni yatakuwa lini, kama nyinyi mnasema kweli!

  27. 67:26
    ۝٢٦

    Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha. [26]

    Tanbihi

    [26] Ewe Muhammad! Sema: Ujuzi wa hayo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Ama mimi ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji tu.

  28. 67:27
    ۝٢٧

    Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba. [27]

    Tanbihi

    [27] Watakapo yaona hayo yaliyo ahidiwa yapo karibu nao, nyuso za makafiri zitajaa huzuni na unyonge, na wataambiwa kwa kuwakejeli na kuwatia uchungu: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyataka yaje kwa haraka!

  29. 67:28
    ۝٢٨

    Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu? [28]

    Tanbihi

    [28] Sema: Nambieni, ikiwa Mwenyezi Mungu akinifisha mimi na Waumini walio pamoja nami, kama mnavyo tamani yawe, au akaturehemu akaakhirisha ajali yetu, na akatusamehe asituadhibu, maana itakuwa katuokoa katika hali zote mbili, basi nani atakaye wakinga makafiri na adhabu chungu wanayo istahiki kuipata kwa sababu ya ukafiri wao, na kudanganyika kwao na miungu yao?

  30. 67:29
    ۝٢٩

    Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri. [29]

    Tanbihi

    [29] Yeye huyo ndiye Arrahman, Mwingi wa Rehema, tunaye msadiki sisi, na nyinyi hamumsadiki. Yeye tu peke yake ndiye tunaye mtegemea, na nyinyi mnawategemea wenginewe. Mtakuja jua itakapo teremka adhabu ni kundi gani kati yetu lilio tengeka mbali na Haki.

  31. 67:30
    ۝٣٠

    Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atakueleteeni maji yanayo miminika? [30]

    Tanbihi

    [30] Sema: Hebu nipeni khabari, maji yenu yakitoweka chini ya ardhi msiweze kuyapata kwa namna yoyote, ni nani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni maji ya dhaahiri yanayo miminika anayo weza kuyapata kila atakaye?

  32. Sura Al-Qalam

    سُورَةُ القلم
  33. 68:1
    ۝١

    Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo! [1]

    Tanbihi

    [1] Nuun, ndio harufi ya N, iliyo anzia Sura hii ni kama kupinzana na hao wanao kadhibisha, na ili kuwazindua wenye kusadiki. Naapa kwa kalamu wanayo andikia Malaika na wenginewe, na hayo mambo ya kheri na manufaa wanayo yaandika,

  34. 68:2
    ۝٢

    Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu. [2]

    Tanbihi

    [2] Hakika wewe, na Mwenyezi Mungu amekuneemesha kwa kukupa Unabii, si mchachefu wa akili, wala mpumbavu wa mawazo.

  35. 68:3
    ۝٣

    Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika. [3]

    Tanbihi

    [3] Na hakika unapata thawabu kubwa zisio katika kwa ajili ya kufikisha Ujumbe.

  36. 68:4
    ۝٤

    Na hakika wewe una tabia tukufu. [4]

    Tanbihi

    [4] Na hakika wewe bila ya shaka umeshikamana na sifa nzuri kabisa na vitendo vizuri kabisa alivyo kuumba navyo Mwenyezi Mungu.

  37. 68:5
    ۝٥

    Karibu utaona, na wao wataona! [5]

    Tanbihi

    [5] Karibuni hivi, ewe Muhammad, utaona, na makafiri wataona,

  38. 68:6
    ۝٦

    Ni nani kati yenu aliye pandwa na wazimu. [6]

    Tanbihi

    [6] Ni nani kati yenu aliye mwenda wazimu.

  39. 68:7
    ۝٧

    Hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye ajuaye zaidi nani aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka. [7]

    Tanbihi

    [7] Hakika Mola wako Mlezi, Yeye ndiye Mwenye kumjua zaidi aliye iacha Njia yake, na Yeye ndiye Mwenye kuwajua zaidi wenye akili walio ongoka kumwendea Yeye.

  40. 68:8
    ۝٨

    Basi usiwat'ii wanao kadhibisha. [8]

    Tanbihi

    [8] Basi usiyaache uliyo nayo ya kuwapinga wanao kanusha.

  41. 68:9
    ۝٩

    Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie. [9]

    Tanbihi

    [9] Wanatamani lau ungeli kuwa laini kwao katika baadhi ya mambo, ili na wao wawe laini kwako, kwa tamaa upate kurudishiana nao. (Neno lililo tumiwa hapo "Tud- hinu fayud-hinuun", maana yake khasa "Upake mafuta na wao wapake mafuta". Kiswahili husema: Kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa. Yaani kumpa sifa za uwongo, kumfanyia unaafiki. Kwa Kiarabu ni "Mudaahana". Kupakana mafuta)

  42. 68:10
    ۝١٠

    Wala usimt'ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa, [10]

    Tanbihi

    [10] Wala usiache mwendo wako ulio nao kwenda kinyume na kila mwingi wa viapo, mtu wa kudharauliwa,

  43. 68:11
    ۝١١

    Mtapitapi apitae akifitini. [11]

    Tanbihi

    [11] Mtapitapi mwenye kueneza aibu za watu, mwenye kuwasengenya watu, kuwasema kwa siri, mwenye kutwaa maneno baina ya watu kwa sababu ya kuwafisidi,

  44. 68:12
    ۝١٢

    Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi, [12]

    Tanbihi

    [12] Mwingi wa kupinga kila la kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi,

  45. 68:13
    ۝١٣

    Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu. [13]

    Tanbihi

    [13] Mgumu wa moyo, mwenye tabia ya ukavu, muovu maarufu kwa shari, juu ya sifa hizo mbovu alizo nazo.

  46. 68:14
    ۝١٤

    Ati kwa kuwa ana mali na watoto! [14]

    Tanbihi

    [14] Ati kwa kuwa anajiona yeye ana mali na watoto wengi! Amezikadhibisha Aya zetu na amezipuuza.

  47. 68:15
    ۝١٥

    Anapo somewa Aya zetu, husema: Hizi ni simulizi za uwongo za watu wa zamani! [15]

    Tanbihi

    [15] Akisomewa Qur'ani husema: Hivi ni visa vya uwongo vya watu wa kale!

  48. 68:16
    ۝١٦

    Tutamtia kovu juu ya pua yake. [16]

    Tanbihi

    [16] Tutambandika alama juu ya pua yake ya kumganda, apate kufedheheka mbele za watu.

  49. 68:17
    ۝١٧

    Hakika tumewajaribu hawa kama tulivyo wajaribu wale wenye shamba, walipo apa kwamba watayavuna mazao yake itakapo kuwa asubuhi. [17]

    Tanbihi

    [17] Sisi tumewafanyia mtihani watu wa Makka kwa kuwapa neema, nao wakazikufuru; kama tulivyo wafanyia mtihani hao watu wenye shamba, walipo chukua kiapo kuwa watakwenda vuna mazao ya shamba lao asubuhi mapema,

  50. 68:18
    ۝١٨

    Wala hawakusema: Mungu akipenda! [18]

    Tanbihi

    [18] Wala wasimkumbuke Mwenyezi Mungu, wakafunganisha hilo jambo lao na kupenda kwake.

  51. 68:19
    ۝١٩

    Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala! [19]

    Tanbihi

    [19] Basi ikaliteremkia shamba hilo balaa kubwa ilio toka kwa Mola wako Mlezi, na hali wao wamelala.

  52. 68:20
    ۝٢٠

    Likawa kama usiku wa giza. [20]

    Tanbihi

    [20] Likawa hilo shamba kama usiku wa giza kwa masaibu yalio lifikia.

  53. 68:21
    ۝٢١

    Asubuhi wakaitana. [21]

    Tanbihi

    [21] Asubuhi wakawa wanaitana:

  54. 68:22
    ۝٢٢

    Ya kwamba nendeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna. [22]

    Tanbihi

    [22] Amkeni mapema mwende kondeni kwenu kama mmeazimia kuvuna.

  55. 68:23
    ۝٢٣

    Basi walikwenda na huku wakinong'onezana, [23]

    Tanbihi

    [23] Wakatoka, nao wakinong'ona kuambizana:

  56. 68:24
    ۝٢٤

    Ya kuwa leo hata masikini mmoja asikuingilieni. [24]

    Tanbihi

    [24] Msimwachie masikini yeyote kukuingilieni leo!

  57. 68:25
    ۝٢٥

    Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimio hilo. [25]

    Tanbihi

    [25] Wakenda hapo asubuhi mpaka kwenye shamba lao, na azma yao ovu hiyo, na wao ni wenye uwezo kaamili wa kutenda hayo kwa kujigamba kwao.

  58. 68:26
    ۝٢٦

    Basi walipo liona, wakasema: Hakika tumepotea! [26]

    Tanbihi

    [26] Walipo liona limekuwa jeusi limeungua, walisema nao wamebabaika: Hakika sisi bila ya shaka tumepotea. Hili silo shamba letu!

  59. 68:27
    ۝٢٧

    Bali tumenyimwa! [27]

    Tanbihi

    [27] Bali ndilo shamba letu! Na sisi tumenyimwa!

  60. 68:28
    ۝٢٨

    Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu? [28]

    Tanbihi

    [28] Alisema aliye kuwa muadilifu wao na mbora wao akiwalaumu: Sikukwambieni mlipo kuwa mnasemezana kuwanyima masikini, hebu hamumkumbuki Mwenyezi Mungu mkaiacha niya yenu?

  61. 68:29
    ۝٢٩

    Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu. [29]

    Tanbihi

    [29] Wakasema walipo rejea kwenye uwongozi wao: Tunamtakasa Mwenyezi Mungu kuwa katudhulumu kwa yaliyo tusibu. Hakika sisi wenyewe ndio tumejidhulumu kwa makusudio yetu maovu.

  62. 68:30
    ۝٣٠

    Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao. [30]

    Tanbihi

    [30] Wakawa wanaelekeana wao kwa wao wakilaumiana,

  63. 68:31
    ۝٣١

    Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka! [31]

    Tanbihi

    [31] Wakisema: Huku ni kuhiliki kwetu! Hakika sisi tulikuwa tumepita mipaka katika dhulma zetu.

  64. 68:32
    ۝٣٢

    Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. [32]

    Tanbihi

    [32] Asaa Mola wetu Mlezi akatupa badala lilio bora kuliko hili shamba letu. Hakika sisi tunamtaka Mola wetu Mlezi peke yake atupe msamaha na malipo.

  65. 68:33
    ۝٣٣

    Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangeli jua! [33]

    Tanbihi

    [33] Mfano wa kama hayo yaliyo yasibu hilo shamba ndio inakuwa adhabu yangu ninayo iteremsha duniani kwa anaye stahiki. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi lau kuwa watu wanajua hayo.

  66. 68:34
    ۝٣٤

    Hakika wachamngu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi. [34]

    Tanbihi

    [34] Hakika wachamngu watapata kwa Mola wao Mlezi Bustani za neema safi.

  67. 68:35
    ۝٣٥

    Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu? [35]

    Tanbihi

    [35] Je! Sisi tudhulumu katika hukumu yetu, tuwafanye Waislamu sawa na makafiri?

  68. 68:36
    ۝٣٦

    Mna nini? Mnahukumu vipi? [36]

    Tanbihi

    [36] Vipi mnahukumia mfano wa hukumu kama hii ya dhulma?

  69. 68:37
    ۝٣٧

    Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma? [37]

    Tanbihi

    [37] Kwani mnacho kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu mnacho kisoma,

  70. 68:38
    ۝٣٨

    Kuwa mtapata humo mnayo yapenda? [38]

    Tanbihi

    [38] Na humo yamo hayo mnayo yapenda?

  71. 68:39
    ۝٣٩

    Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayo jihukumia? [39]

    Tanbihi

    [39] Au kwani mnazo ahadi juu yetu zenye kutiliwa mkazo kwa viapo, zenye kubaki mpaka Siku ya Kiyama, kwamba mnayo haki ya hayo mnayo jihukumia?

  72. 68:40
    ۝٤٠

    Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya? [40]

    Tanbihi

    [40] Ewe Muhammad! Waulize washirikina: Ni nani dhamini wa hukumu hiyo?

  73. 68:41
    ۝٤١

    Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli. [41]

    Tanbihi

    [41] Kwani wanao wanao shirikiana nao, na wanao fuata mwendo wao katika kauli yao hii? Basi na wawalete hao washirika wao, ikiwa wao ni wasema kweli katika madai yao.

  74. 68:42
    ۝٤٢

    Siku utakapo wekwa wazi mundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza, [42]

    Tanbihi

    [42] Siku mambo yatapo shitadi na yakawa magumu, na wakatakiwa makafiri wasujudu kwa kuwaemea na kuwakejeli, na wasiweze, (Kuwekwa wazi mundi, ni kinaya ya kudhihirishwa kweli yote Siku ya kwima kondo, Siku ya Kiyama. Chambilecho Sayyid Abdulla bin Ali bin Nassir katika Al Inkishaf: Tafakari siku ya kwima kondo Ya kuaridhiwa kila kitendo Pindi madhulumu atapo ondo Achamba Ya Rabi namua naye)

  75. 68:43
    ۝٤٣

    Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima [43]

    Tanbihi

    [43] Macho yao yameinama chini, yamefunikwa na fedheha. Na duniani walikuwa wakitakiwa wasujudu walipo kuwa wakiweza na wakakataa kusujudu.

  76. 68:44
    ۝٤٤

    Basi niache na wanao kadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua. [44]

    Tanbihi

    [44] Ewe Muhammad! Nachilie na hao wanao ikadhibisha Qur'ani. Tutawajongeza kwenye adhabu kidogo kidogo kwa jiha wasio ijua kuwa adhabu itatokea huko.

  77. 68:45
    ۝٤٥

    Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara. [45]

    Tanbihi

    [45] Na nitawapa muhula kwa kuiakharisha adhabu. Hakika mipango yangu ni ya nguvu, na hawezi kuporonyoka yeyote akasalimika nayo.

  78. 68:46
    ۝٤٦

    Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo? [46]

    Tanbihi

    [46] Kwani wewe unawaomba ujira kwa kuufikisha Ujumbe wako, na kwa hivyo wao wanaona uzito kwa gharama hiyo unayo wakalifisha?

  79. 68:47
    ۝٤٧

    Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika? [47]

    Tanbihi

    [47] Au kwani wao wanajua yaliyo fichikana na wao wanayaandika na ndio wanahukumu kwa hayo?

  80. 68:48
    ۝٤٨

    Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, alipo nadi naye kazongwa. [48]

    Tanbihi

    [48] Basi wewe subiri kwa tunavyo wapa muhula na kukuakhirisha kukuletea manusura yetu juu yao. Wala usiwe kama Yunus, aliye mezwa na samaki, akawa na haraka na kuwaghadhibikia watu wake, alipo mnadia Mola wake Mlezi, naye kajaa hasira na ghadhabu, akitaka waadhibiwe kwa haraka.

  81. 68:49
    ۝٤٩

    Kama isingeli mfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa. [49]

    Tanbihi

    [49] Lau kuwa neema ya Mola wake Mlezi haikumdiriki kwa kukubali toba yake, angeli tupwa kutokana na tumbo la samaki ufukweni, naye akiteseka kwa kuteleza kwake.

  82. 68:50
    ۝٥٠

    Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema. [50]

    Tanbihi

    [50] Lakini Mola wake Mlezi kamteuwa kwa kuikubali toba yake, na akamjaalia miongoni mwa watu wema.

  83. 68:51
    ۝٥١

    Na walio kufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanapo sikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu. [51]

    Tanbihi

    [51] Na makafiri wangeli karibia kukutelezesha na pahala pako, kwa jicho lao wanalo kuangalia kwa uadui na chuki wanapo isikia Qur'ani, wakisema: Hakika huyu ni mwendawazimu.

  84. 68:52
    ۝٥٢

    Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. [52]

    Tanbihi

    [52] Na Qur'ani si chochote ila ni mawaidha, na hikima, na ukumbusho kwa walimwengu wote.

  85. Sura Al-Haaqqa

    سُورَةُ الحاقة
  86. 69:1
    ۝١

    Tukio la haki. [1]

    Tanbihi

    [1] Kiyama ni Tukio litakalo tukia kwa haki, yaani kwa kweli.

  87. 69:2
    ۝٢

    Nini hilo Tukio la haki? [2]

    Tanbihi

    [2] Nini hicho Kiyama kitacho tokea kweli?

  88. 69:3
    ۝٣

    Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki? [3]

    Tanbihi

    [3] Na kitu gani kitacho kujuvya ukweli wake, na kitacho kupa sura ya kitisho chake na shida zake?

  89. 69:4
    ۝٤

    Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha. [4]

    Tanbihi

    [4] Kina Thamudi na kina A'di walikanusha Kiyama kinacho wagutua walimwengu wote kwa kitisho chake na shida zake.

  90. 69:5
    ۝٥

    Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno. [5]

    Tanbihi

    [5] Ama Thamudi basi walihilikiwa kwa tukio lilio pindukia mipaka yote kwa ukali wake.

  91. 69:6
    ۝٦

    Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika. [6]

    Tanbihi

    [6] Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo ubaridi na mkali,

  92. 69:7
    ۝٧

    Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani. [7]

    Tanbihi

    [7] Mwenyezi Mungu aliwasalitisha nao muda wa masiku saba, na siku nane zilizo fuatana mfululizo, utaona walio patikana na upepo huo wamekuwa maiti kama magogo ya mitende yaliyo kuwa matupu ndani yake. ("Masiku" ni wingi wa "Usiku"; "Siku" wingi wake ni "Siku" vile vile.)

  93. 69:8
    ۝٨

    Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki? [8]

    Tanbihi

    [8] Je! Unamwona yeyote aliye bakia katika hao?

  94. 69:9
    ۝٩

    Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia. [9]

    Tanbihi

    [9] Akaja Firauni, na mataifa mengine yaliyo kufuru kabla yake, na wale jamaa walio acha mwendo wa haki na vitendo vya maumbile wakafanya vitendo vichafu kabisa hata miji yao ikapinduliwa juu chini.

  95. 69:10
    ۝١٠

    Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu. [10]

    Tanbihi

    [10] Kila umma katika hawa walimuasi Mtume wa Mola wao Mlezi. Naye Mwenyezi Mungu akawashika kwa kuwaadhibu kwa mshiko ulio zidi ukali.

  96. 69:11
    ۝١١

    Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina, [11]

    Tanbihi

    [11] Maji yalipo zidi ukomo wake, na yakapanda juu ya milima katika tukio la tofani ya Nuhu, Sisi tulikupandisheni, yaani kwa kuwapandisha wazee wenu wa asli, katika safina inayo kwenda baharini.

  97. 69:12
    ۝١٢

    Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi. [12]

    Tanbihi

    [12] Ili kulifanya tukio hilo la kuwaokoa Waumini na kuwazamisha makafiri liwe zingatio na mawaidha kwenu, na lihifadhiwe na kila sikio lenye kuhifadhi linalo sikia.

  98. 69:13
    ۝١٣

    . Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu, [13]

    Tanbihi

    [13] Litakapo pulizwa barugumu kwa mpulizo mmoja,

  99. 69:14
    ۝١٤

    Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja, [14]

    Tanbihi

    [14] Na ardhi na milima ikaondolewa pahala ilipo, na ikavunjwa mara moja,

  100. 69:15
    ۝١٥

    Siku hiyo ndio Tukio litatukia. [15]

    Tanbihi

    [15] Siku hiyo ndiyo kitashuka cha kushuka,

  101. 69:16
    ۝١٦

    Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa. [16]

    Tanbihi

    [16] Na mbingu zitapasuka kwa kuondoka hukumu zake na sharia zake, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu baada ya kuwa madhubuti zenye nguvu.

  102. 69:17
    ۝١٧

    Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi. [17]

    Tanbihi

    [17] Na Malaika pembezoni mwake, na wapo Malaika wanane siku hiyo watakao beba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi, juu ya Malaika hawa wengine.

  103. 69:18
    ۝١٨

    Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu. [18]

    Tanbihi

    [18] Siku hiyo ndio mtaletwa kwa ajili ya kuhisabiwa. Wala haifichikani siri yenu yoyote mliyo kuwa mkiificha.

  104. 69:19
    ۝١٩

    Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! [19]

    Tanbihi

    [19] Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema akiwatangazia furaha yake walio karibu naye: Chukueni msome kitabu changu!

  105. 69:20
    ۝٢٠

    Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu. [20]

    Tanbihi

    [20] Mimi nilikuwa na yakini tangu duniani kuwa nitapata hisabu yangu, basi nikajitayarisha nafsi yangu kwa mkutano huu.

  106. 69:21
    ۝٢١

    Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza, [21]

    Tanbihi

    [21] Basi huyo atakuwa katika maisha yaliyo enea kupendeza.

  107. 69:22
    ۝٢٢

    Katika Bustani ya juu, [22]

    Tanbihi

    [22] Katika Bustani ya pahali na daraja ya juu.

  108. 69:23
    ۝٢٣

    Matunda yake yakaribu. [23]

    Tanbihi

    [23] Matunda yake yakaribu kwa kuyachuma. (kuyatunda).

  109. 69:24
    ۝٢٤

    Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita. [24]

    Tanbihi

    [24] Kuleni na mnywe kwa kula na kunywa kusio na karaha, wala maudhi, kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kwisha vitanguliza katika siku za duniani zilizo pita.

  110. 69:25
    ۝٢٥

    Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu! [25]

    Tanbihi

    [25] Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto atasema kwa majuto na huzuni: Laiti kuwa sikupewa kitabu changu,

  111. 69:26
    ۝٢٦

    Wala nisingeli jua nini hisabu yangu. [26]

    Tanbihi

    [26] Wala sikuijua hisabu yangu!

  112. 69:27
    ۝٢٧

    Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa. [27]

    Tanbihi

    [27] Laiti kuwa kule kufa niliko kwisha kufa kungeli kuwa ndio kumalizika kwangu kwa mwisho, wala nisingeli fufuliwa tena!

  113. 69:28
    ۝٢٨

    Mali yangu hayakunifaa kitu. [28]

    Tanbihi

    [28] Hapana chochote nilicho kimiliki duniani kilicho nifaa.

  114. 69:29
    ۝٢٩

    Madaraka yangu yamenipotea. [29]

    Tanbihi

    [29] Uzima wangu umenipotea, na nguvu zangu zimenitoka.

  115. 69:30
    ۝٣٠

    (Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu! [30]

    Tanbihi

    [30] Wataambiwa walinzi wa Jahannamu: Mshikeni, na mfungeni mikono yake kwenye shingo yake.

  116. 69:31
    ۝٣١

    Kisha mtupeni Motoni! [31]

    Tanbihi

    [31] Kisha msimtie popote ila ndani ya Moto wa Jahannamu,

  117. 69:32
    ۝٣٢

    Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini! [32]

    Tanbihi

    [32] Kisha mfungeni kwenye mnyororo mrefu kabisa.

  118. 69:33
    ۝٣٣

    Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, [33]

    Tanbihi

    [33] Hakika huyo alikuwa hamsadiki Mwenyezi Mungu Mtukufu,

  119. 69:34
    ۝٣٤

    Wala hahimizi kulisha masikini. [34]

    Tanbihi

    [34] Wala hamhimizi yoyote kuwalisha masikini.

  120. 69:35
    ۝٣٥

    Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu, [35]

    Tanbihi

    [35] Basi hii leo huyu kafiri hana jamaa wa kumtetea,

  121. 69:36
    ۝٣٦

    Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni. [36]

    Tanbihi

    [36] Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni, ambao kwa hakika ni mchanganyiko wa damu na usaha.

  122. 69:37
    ۝٣٧

    Chakula hicho hawakili ila wakosefu. [37]

    Tanbihi

    [37] Hawakili chakula hicho ila wakosefu walio kusudia kufanya maasi yao, na wakakamia kuendelea nayo.

  123. 69:38
    ۝٣٨

    Basi naapa kwa mnavyo viona, [38]

    Tanbihi

    [38] Basi naapa kwa mnavyo viona katika vinavyo onekana,

  124. 69:39
    ۝٣٩

    Na msivyo viona, [39]

    Tanbihi

    [39] Basi naapa kwa mnavyo viona katika vinavyo onekana, na msivyo viona katika ulimwengu wa ghaibu,

  125. 69:40
    ۝٤٠

    Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima. [40]

    Tanbihi

    [40] Kwamba hakika Qur'ani bila ya shaka inatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ulimi wa Mjumbe mwenye cheo cha juu.

  126. 69:41
    ۝٤١

    Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini. [41]

    Tanbihi

    [41] Wala Qur'ani si maneno ya mtunga mashairi kama mnavyo dai. Ama nyinyi ni chache mno imani yenu ya kuwa Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu.

  127. 69:42
    ۝٤٢

    Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka. [42]

    Tanbihi

    [42] Wala Qur'ani haisemi kwa maneno ya kumunyia munyia kama wanenavyo makuhani mlio wazoea. Ni uchache mno kukumbuka kwenu na kuzingatia khitilafu zilioko baina ya Qur'ani na maneno ya makuhani.

  128. 69:43
    ۝٤٣

    Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [43]

    Tanbihi

    [43] Hii ni uteremsho unao toka kwa Mwenye kuwaangalia walimwengu wote kwa kuwaumba na kuwalea.

  129. 69:44
    ۝٤٤

    Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, [44]

    Tanbihi

    [44] Na lau kuwa angeli dai kitu chochote ambacho tusicho kisema

  130. 69:45
    ۝٤٥

    Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, [45]

    Tanbihi

    [45] Basi bila ya shaka tungeli mshika akitoe kama mtu anavyo mkamata mtu kwa mkono wa kulia akammaliza hapo hapo.

  131. 69:46
    ۝٤٦

    Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo! [46]

    Tanbihi

    [46] Kisha bila ya shaka tungeli mkata mshipa wake wa moyo, afe saa ile ile. (Biblia inasema katika Kumbukumbu la Torati 18.20 "Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.")

  132. 69:47
    ۝٤٧

    Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia. [47]

    Tanbihi

    [47] Na hapana yeyote katika nyinyi, hata ange kuwa na nguvu namna gani, angeli weza kuzuia adhabu yetu isimfikilie.

  133. 69:48
    ۝٤٨

    Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu. [48]

    Tanbihi

    [48] Na hakika Qur'ani ni mawaidha kwa wanao fuata amri za Mwenyezi Mungu, na wanaepuka makatazo yake.

  134. 69:49
    ۝٤٩

    Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha. [49]

    Tanbihi

    [49] Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba kati yenu wapo wanao ikanusha Qur'ani.

  135. 69:50
    ۝٥٠

    Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa. [50]

    Tanbihi

    [50] Na kwamba hakika hiyo bila ya shaka ni sababu ya majuto ya wanao ikataa, wakati watapo iona adhabu yao, na neema za wenye kusadiki.

  136. 69:51
    ۝٥١

    Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini. [51]

    Tanbihi

    [51] Na hakika Qur'ani bila ya shaka ni Haki iliyo thibiti, isiyo na shaka yoyote.

  137. 69:52
    ۝٥٢

    Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu. [52]

    Tanbihi

    [52] Basi mtakase Mola wako Mlezi, na dumisha kudhukuru jina lake.

  138. Sura Al-Ma'aarij

    سُورَةُ المعارج
  139. 70:1
    ۝١

    Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea! [1]

    Tanbihi

    [1] Ameita, mwenye kuita, kuhimiza kama kufanya kejeli, iletwe upesi adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo hapana shaka itawashukia makafiri.

  140. 70:2
    ۝٢

    Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia . [2]

    Tanbihi

    [2] Wala hapana chochote cha kuzuia adhabu hiyo,

  141. 70:3
    ۝٣

    Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja. [3]

    Tanbihi

    [3] Kwani hiyo inatoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu, ambako huko ndiko zinatoka nguvu zinazo simama, na hukumu inayo tekelezwa.

  142. 70:4
    ۝٤

    Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu! [4]

    Tanbihi

    [4] Malaika na Jibrili wanapanda kwenda kunako toka amri yake kwa siku ambayo urefu wake ni miaka khamsini elfu kwa mujibu wa hisabu ya miaka ya duniani.

  143. 70:5
    ۝٥

    Basi subiri kwa subira njema.Hakika wao wanaiona iko mbali! [5]

    Tanbihi

    [5] Basi, ewe Muhammad! Subiri uwastahamilie hizo kejeli zao, na kuhimiza kwao adhabu, kwa subira isiyo kuwa na mbabaiko ndani yake wala mashtaka.

  144. 70:6
    ۝٦

    Hakika wao wanaiona iko mbali! [6]

    Tanbihi

    [6] Hakika hao makafiri wanaiona hiyo Siku ya Kiyama ni kitu cha muhali kutokea.

  145. 70:7
    ۝٧

    Na Sisi tunaiona iko karibu. [7]

    Tanbihi

    [7] Na Sisi tunaona kuwa ni jambo jepesi katika uweza wetu, wala halina uzito wowote.

  146. 70:8
    ۝٨

    Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa. [8]

    Tanbihi

    [8] Siku mbingu itakapo kuwa kama fedha iliyo yayuka,

  147. 70:9
    ۝٩

    Na milima itakuwa kama sufi. [9]

    Tanbihi

    [9] Na milima itakapo kuwa kama sufi iliyo tiwa rangi na ikapigwa,

  148. 70:10
    ۝١٠

    Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake. [10]

    Tanbihi

    [10] Wala jamaa hamuulizi jamaa yake: Nini hali yako? Kwa sababu kila mmoja kajishughulikia nafsi yake!

  149. 70:11
    ۝١١

    Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe, [11]

    Tanbihi

    [11] Watakuwa wakijuulishana wao kwa wao mpaka wajuane baraabara, na ilhali hapana amuulizae mwenzie kitu. Kafiri atatamani lau ange pata kujikomboa nafsi yake na adhabu hiyo Siku ya Kiyama kwa kumtoa mwanawe awe ni fidia yake,

  150. 70:12
    ۝١٢

    Na mkewe, na nduguye, [12]

    Tanbihi

    [12] Au mkewe, au nduguye,

  151. 70:13
    ۝١٣

    Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu, [13]

    Tanbihi

    [13] Au jamaa zake aliyo khusiana nao,

  152. 70:14
    ۝١٤

    Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye. [14]

    Tanbihi

    [14] Na wote waliomo duniani, apate kuokoka yeye tu!

  153. 70:15
    ۝١٥

    La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa, [15]

    Tanbihi

    [15] Ewe mkosefu! Wacha hayo unayo yatamani ya kutaka kujikomboa kwa fidia! Hakika huo moto, unawaka kweli!

  154. 70:16
    ۝١٦

    Unao babua ngozi ya kichwa! [16]

    Tanbihi

    [16] Utakubabua mikono yako, na miguu yako, na viungo vyako vyote,

  155. 70:17
    ۝١٧

    Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka. [17]

    Tanbihi

    [17] Utanadi kwa jina la huyo aliye iacha Haki, na akaacha ut'iifu,

  156. 70:18
    ۝١٨

    Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi. [18]

    Tanbihi

    [18] Na akakusanya mali akayaweka katika mabweta yake, wala hakutoa haki ya Mwenyezi Mungu iliomo katika hayo mali!

  157. 70:19
    ۝١٩

    Hakika mtu ameumbwa na papara. [19]

    Tanbihi

    [19] Hakika tabia ya binaadamu ni papara, mwingi wa kupapatika,

  158. 70:20
    ۝٢٠

    Inapo mgusa shari hupapatika. [20]

    Tanbihi

    [20] Na kutoridhika akifikiwa na lolote la karaha na uzito,

  159. 70:21
    ۝٢١

    Na inapo mgusa kheri huizuilia. [21]

    Tanbihi

    [21] Na ni mwingi wa kuzuia na kunyima akipata kheri na neema.

  160. 70:22
    ۝٢٢

    Isipo kuwa wanao swali, [22]

    Tanbihi

    [22] Isipo kuwa wanao swali,

  161. 70:23
    ۝٢٣

    Ambao wanadumisha Sala zao, [23]

    Tanbihi

    [23] Ambao wanadumisha Swala zao, hawakikosi hata kipindi kimoja.

  162. 70:24
    ۝٢٤

    Na ambao katika mali yao iko haki maalumu [24]

    Tanbihi

    [24] Na wale ambao katika mali yao ipo haki iliyo ainiwa

  163. 70:25
    ۝٢٥

    Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba; [25]

    Tanbihi

    [25] iliyo wekwa kwa ajili ya masikini mwenye kuomba kutaka msaada, na anaye jizuilia kuomba pia. (Katika wanao zuilika kuomba wanaingia si wenye kustahi na kuona vibaya tu, bali pia wasio weza kuomba kama watoto wachanga, wagonjwa, na wanyama pia.)

  164. 70:26
    ۝٢٦

    Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo, [26]

    Tanbihi

    [26] Na wale wanao isadiki Siku ya Malipo, basi wanajitayarisha kwa ajili yake;

  165. 70:27
    ۝٢٧

    Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi. [27]

    Tanbihi

    [27] Na wale wanao iogopa adhabu ya Mola wao Mlezi basi wanajikinga nayo wala hawajitii katika jambo la kuwaletea adhabu hiyo.

  166. 70:28
    ۝٢٨

    Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo. [28]

    Tanbihi

    [28] Kwani hakika adhabu ya Mola wao Mlezi hapana hata mmoja anaye weza kuaminika nayo isimpate.

  167. 70:29
    ۝٢٩

    Na ambao wanahifadhi tupu zao. [29]

    Tanbihi

    [29] Na ambao wanazihifadhi tupu zao hata hawaemewi na matamanio yao.

  168. 70:30
    ۝٣٠

    Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi [30]

    Tanbihi

    [30] Lakini kwa wake zao na masuria wao hawazihifadhi; kwa sababu hapo hawalaumiwi kuifuata tabia ya maumbile.

  169. 70:31
    ۝٣١

    Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka. [31]

    Tanbihi

    [31] Basi mwenye kutafuta starehe ya maingiliano kwa wasio kuwa wake na masuria, basi hao tena ni wenye kuikiuka halali na kuingia katika haramu.

  170. 70:32
    ۝٣٢

    Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao, [32]

    Tanbihi

    [32] Na hao wenye kuzihifadhi amana za sharia na amana za waja wa Mwenyezi Mungu, na walio lazimika nayo kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu bila ya kukhuni wala kupunja,

  171. 70:33
    ۝٣٣

    Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao, [33]

    Tanbihi

    [33] Na ambao kwa shahada zao wamesimama sawa sawa kwa haki bila ya kuficha wanalo lijua,

  172. 70:34
    ۝٣٤

    Na ambao wanazihifadhi Sala zao. [34]

    Tanbihi

    [34] Na wanao hifadhi Swala zao wakizisali sawasawa kwa ukamilifu -

  173. 70:35
    ۝٣٥

    Hao ndio watakao hishimiwa Peponi. [35]

    Tanbihi

    [35] Watu wenye sifa kama hizo nzuri watakuwa ni wenye kuhishimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu huko Peponi.

  174. 70:36
    ۝٣٦

    Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu? [36]

    Tanbihi

    [36] Kitu gani kinawapelekea hao walio kufuru kukujia mbio mbio ?

  175. 70:37
    ۝٣٧

    Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto! [37]

    Tanbihi

    [37] Kutoka kuliani na kushotoni kwa makundi?

  176. 70:38
    ۝٣٨

    Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema? [38]

    Tanbihi

    [38] Je, kwani kila mmoja wao ana tamaa ya kuingia kwenye Pepo yenye neema, baada ya kusikia kuwa Mwenyezi Mungu amemuahidi Mtume wake na Waumini kuwatia Peponi?

  177. 70:39
    ۝٣٩

    La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua. [39]

    Tanbihi

    [39] Basi nawaache hiyo tamaa yao ya kuingia Peponi. Hakika Sisi tumewaumba wao kutokana na maji ya kudharauliwa.

  178. 70:40
    ۝٤٠

    Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza [40]

    Tanbihi

    [40] Naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote, na magharibi zote za siku, na sayari na hidaya, kwamba hakika bila ya shaka Sisi tuna uweza wa kuwaangamiza,

  179. 70:41
    ۝٤١

    Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi. [41]

    Tanbihi

    [41] Na kuwaleta walio wat'iifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko wao. Wala Sisi hatushindwi kubadilisha huko. Huenda ikawa inakusudiwa kwa "mashariki zote" na "magharibi zote" ni maeneo ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu yote ambayo hayana mpaka kama ilivyo ashiriwa katika Aya 137 ya Surat Al-A'araf: "Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki za nchi na magharibi zake ambayo tuliitia baraka", kuonyesha sehemu zote za hiyo nchi inayo tajwa. Na huenda ikawa makusudio yake ni mashariki za jua na mwezi na nyota zote na sayari, na magharibi zao, kwa ajili ya kuonyesha vile vile ufalme wa Mwenyezi Mungu wote. Na kwa hivyo inadhihirika kwetu kuwa vyombo vinavyo kwenda katika qubba la mbingu vinachomoza kwenye upeo wa mashariki na kuchwa kwenye upeo wa magharibi, au kwa uchache vinazunguka kutoka mashariki kwendea magharibi kuizunguka nyota ya Pole, katika sehemu ya kaskazini ya dunia. Kwani umbali wa Pole kwa nyota ni mdogo kuliko pahala unapo angalia, basi nyota hapo haichomozi wala haichwi, bali hupiga duru ndogo kuizunguka North Pole. Na kwa hiyo Aya inaashiria saa za usiku. Rejea kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: " Na alama na kwa nyota wao wanaongoka." Na kwa udhaahiri wa kuchomoza na kuchwa ipo ishara ya kuzunguka kwa dunia, na hiyo ni neema kubwa kabisa katika neema za Mwenyezi Mungu juu ya maisha katika sayari hii. Kwani bila ya kuzunguka kwa dunia juu ya msumari-kati wake nusu ya dunia ingeli pigwa na jua mfululizo muda wa nusu mwaka kaamili, na ingeli nyimwa mwangaza kabisa nusu nyengine. Kwa hivyo uhai kama tulivyo uzoea usinge kuwako. Na tukifanya hizo mashariki na hizo magharibi ni za jua peke yake, wachilia mbali nyota nyengine na sayari, basi itakuwa ishara ni kule kuchomoza jua kila siku pahala pengine na kuchwa pahala pengine kila siku, au hata katika kila dakika linapo pita juu ya dunia. Kwani jua kila dakika linakuchwa pahala na linachomoza pahala papili mfululizo. Na haya ni katika mipango ya Mwenyezi Mungu na miujiza ya uweza wake. Tazama pia maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 5 katika Surat Assaffat, na Aya 17 ya Surat Arrah'man.

  180. 70:42
    ۝٤٢

    Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa, [42]

    Tanbihi

    [42] Basi waachilie wakiporojoka katika upotovu wao, na wakicheza na dunia yao, mpaka wakutane na siku yao waliyo ahidiwa kupewa adhabu.

  181. 70:43
    ۝٤٣

    Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo, [43]

    Tanbihi

    [43] Siku watakapo tolewa makaburini mbio mbio kumwendea huyo ataye waita, kama kwamba wamemweka ufundo na wakimuabudu duniani walivyo kuwa wakimkimbilia badala ya Mwenyezi Mungu,

  182. 70:44
    ۝٤٤

    Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa. [44]

    Tanbihi

    [44] Macho yameinama chini, hawawezi kuyanyanyua, yamegubikwa na unyonge na udhalili. Hiyo ndiyo siku waliyo kuwa wakiahidiwa duniani na wao wakiikanusha.

  183. Sura Nooh

    سُورَةُ نوح
  184. 71:1
    ۝١

    Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake: Uwaonye kaumu yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu. [1]

    Tanbihi

    [1] Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake, na tukamwambia: Waonye watu wako kabla haijawajia adhabu yenye machungu makali.

  185. 71:2
    ۝٢

    Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji wa dhaahiri kwenu! [2]

    Tanbihi

    [2] Nuh'u akasema: Enyi watu wangu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu, nina risala kutoka kwa Mola wenu Mlezi kwa lugha mnayo ijua,

  186. 71:3
    ۝٣

    Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche Yeye, na mumt'ii. [3]

    Tanbihi

    [3] Ya kwamba mumt'ii Mwenyezi Mungu, na mumnyenyekee katika kutimiza waajibu zote; na mwogopeni Yeye kwa kuacha mnayo katazwa, na nit'iini mimi katika ninayo kunasihini.

  187. 71:4
    ۝٤

    Atakughufirieni madhambi yenu, na atakuakhirisheni mpaka muda ulio wekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapo fika haucheleweshwi. Laiti mngejua! [4]

    Tanbihi

    [4] Ndipo Mwenyezi Mungu atapo kusameheni madhambi yenu, na atakupeni umri mrefu mpaka ifike ajali iliyo wekwa mwisho wa umri wenu. Hakika mauti yakija hayaakhirishwi kabisa! Lau kuwa mngeli jua majuto mtakayo kuwa nayo utapo kwisha muda wenu mngeli amini.

  188. 71:5
    ۝٥

    Akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu wangu usiku na mchana! [5]

    Tanbihi

    [5] Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu wangu waamini usiku na mchana bila ya kuchoka,

  189. 71:6
    ۝٦

    Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia. [6]

    Tanbihi

    [6] Hawakuzidishwa na wito wangu ila kuukimbia ut'iifu wako.

  190. 71:7
    ۝٧

    Na hakika mimi kila nilipo waita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno! [7]

    Tanbihi

    [7] Na mimi kila nikiwataka wakuamini Wewe upate kuwasamehe, hubandika vidole vyao kwenye masikio yao ili wasisikie wito wangu, na hujifunika kwa maguo yao ili wasiuone uso wangu! Na wakasimama kidete juu ya ukafiri wao, na wakatakabari kutakabari kukubwa mno!

  191. 71:8
    ۝٨

    Tena niliwaita kwa uwazi! [8]

    Tanbihi

    [8] Kisha nikawaita waje kwako kwa sauti ya juu,

  192. 71:9
    ۝٩

    Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri. [9]

    Tanbihi

    [9] kisha nikaudhihirisha wito kwa namna moja, na nikawaita kisirisiri kwa namna nyengine, ili nijaribu kila njia.

  193. 71:10
    ۝١٠

    Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. [10]

    Tanbihi

    [10] Nikawambia watu wangu: Takeni kwa Mola wenu Mlezi maghfira kwa kufru zenu na maasi yenu. Kwani Yeye bado ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya mwenye kurejea kwake.

  194. 71:11
    ۝١١

    Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo. [11]

    Tanbihi

    [11] Atakuleteeni mawingu yatakayo miminika mvua kwa wingi,

  195. 71:12
    ۝١٢

    Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito. [12]

    Tanbihi

    [12] Na atakupeni mali na wana, na hayo ndiyo mapambo ya dunia, na atakupeni mashamba mtayo starehea kwa uzuri wake na matunda yake, na atakujaalieni mito ya kunyweshea mazao yenu na mifugo yenu.

  196. 71:13
    ۝١٣

    Mna nini hamweki heshima ya Mwenyezi Mungu? [13]

    Tanbihi

    [13] Mna nini nyinyi hata hamumtukuzi Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kutukuzwa, ili mtaraji akukirimuni kwa kukuokoeni na adhabu,

  197. 71:14
    ۝١٤

    Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja? [14]

    Tanbihi

    [14] Na hali Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa madaraja, tangu tone ya manii, kisha pande la damu, kisha pande la nyama, kisha mafupa na nyama?

  198. 71:15
    ۝١٥

    Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyo ziumba mbingu saba kwa matabaka? [15]

    Tanbihi

    [15] Kwani huoni vipi Mwenyezi Mungu alivyo ziumba mbingu saba, moja juu ya moja,

  199. 71:16
    ۝١٦

    Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya jua kuwa taa? [16]

    Tanbihi

    [16] Na akaufanya mwezi katika mbingu hizo unatoa nuru, na akalifanya jua ni taa ambayo kwayo watu wa duniani ndio wanaona kwa mwangaza wake yote wanayo hitajia kuyaona?

  200. 71:17
    ۝١٧

    Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi kama mimea. [17]

    Tanbihi

    [17] Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, akakuotesheni kama miema kwa njia ya ajabu,

  201. 71:18
    ۝١٨

    Kisha atakurudsheni humo na atakutoeni tena. [18]

    Tanbihi

    [18] Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, akakuotesheni kama miema kwa njia ya ajabu, kisha baada ya kufa atakurejesheni huko huko kwenye ardhi, na tena atakutoeni huko kwa hakika hapana hivi wala hivi.

  202. 71:19
    ۝١٩

    Na Mwenyezi Mungu amekukunjulieni ardhi kama busati. [19]

    Tanbihi

    [19] Na Mwenyezi Mungu ameifanya ardhi iliyo kunjuliwa ili mpate kwenda humo katika njia zenye wasaa.

  203. 71:20
    ۝٢٠

    Ili mtembee humo katika njia zilizo pana. [20]

    Tanbihi

    [20] Na Mwenyezi Mungu ameifanya ardhi iliyo kunjuliwa ili mpate kwenda humo katika njia zenye wasaa.

  204. 71:21
    ۝٢١

    Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika hao wameniasi, na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila khasara. [21]

    Tanbihi

    [21] Alisema Nuh'u: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikatalia mimi niliyo waamrisha ya kuamini na kutaka msamaha, na wakawafuata madhaifu miongoni mwao ambao mali yao na watoto wao hawawazidishii ila khasara tupu katika Akhera.

  205. 71:22
    ۝٢٢

    Na wakapanga vitimbi vikubwa. [22]

    Tanbihi

    [22] Na vitimbi vya hao wenye mali mengi, na wana wengi, kwa wanyonge wanao wafuata ni vitimbi vilivyo fika ukomo kwa ukubwa.

  206. 71:23
    ۝٢٣

    Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa' wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra. [23]

    Tanbihi

    [23] Na wao wakiwaambia: Msiache kuiabudu miungu yenu, wala msimwache Wadda, wala Suwaa' , wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra. Na hawa walikuwa miungu ya masanamu iliyo chongwa kwa sura ya wanyama namna mbali mbali.

  207. 71:24
    ۝٢٤

    Na hao walikwisha wapoteza wengi, wala usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea. [24]

    Tanbihi

    [24] Na miungu hii iliwapoteza watu wengi. Na wala huwazidishii wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na inda, ili kuzidi kubaidika na Haki.

  208. 71:25
    ۝٢٥

    Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakaingizwa Motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu. [25]

    Tanbihi

    [25] Kwa sababu ya madhambi yao wakazamishwa kwa tofani, na baada ya kuangamizwa kwao wakatiwa Motoni kwenye moto mkali wa kuwaka na kuteketeza, na wala wasipate yeyote baada ya kumkosa Mwenyezi Mungu, wa kuwanusuru na kuwakinga na adhabu!

  209. 71:26
    ۝٢٦

    Na Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Usimwache juu ya ardhi mkaazi wake yeyote katika makafiri! [26]

    Tanbihi

    [26] Na Nuh'u akasema baada ya kukata tamaa nao watu wake: Mola wangu Mlezi! Usimwache yeyote katika hao wanao kukataa Wewe akabaki akizunguka juu ya ardhi!

  210. 71:27
    ۝٢٧

    Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao hawatazaa ila waovu makafiri. [27]

    Tanbihi

    [27] Ewe Mola wangu Mlezi! Ukiwaacha hao bila ya kuwateketeza na kuwang'oa watawatia waja wako katika upotovu, na wao hawatozaa ila wenye kupotoka vile vile wakaiacha haki, na wakakithiri kukukanya na kukuasi.

  211. 71:28
    ۝٢٨

    Mola wangu Mlezi! Nighufirie mimi na wazazi wangu, na kila aliye ingia nyumbani mwangu kuwa ni mwenye kuamini, na Waumini wote wanaume, na Waumini wanawake. Na wala usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea. [28]

    Tanbihi

    [28] Mola wangu Mlezi! Nisamehe mimi na wazazi wangu ambao ndio walio kuwa ni sababu ya kuzaliwa mimi, na kila mwenye kuingia nyumbani kwangu kwa kukuamini Wewe, na uwasamehe Waumini wote wanaume na wanawake. Na usiwazidishie makafiri ila kuwaangamiza.

  212. Sura Al-Jinn

    سُورَةُ الجن
  213. 72:1
    ۝١

    Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu! [1]

    Tanbihi

    [1] Ewe Muhammad! Waambie watu wako: Nimepata wahyi kwamba kikundi cha majini kimesikia kusoma kwangu Qur'ani, nao wakawaambia wenzao: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya namna ya peke yake, hatujapata kusikia mfano wake kabla yake,

  214. 72:2
    ۝٢

    Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi. [2]

    Tanbihi

    [2] inaitia kwenye uwongofu na usawa. Kwa hivyo tumeiamini hiyo Qur'ani tuliyo isikia; na kabisa hatutamshirikisha Mola wetu Mlezi aliye tuumba na kutulea na chochote katika waja wake.

  215. 72:3
    ۝٣

    Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka kabisa; hana mke wala mwana. [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwamba hakika cheo na utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka; hana mke wala mwana.

  216. 72:4
    ۝٤

    Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu. [4]

    Tanbihi

    [4] Na hakika wajinga katika sisi walikuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu maneno yaliyo kuwa mbali kabisa na ukweli na kuwa sawa.

  217. 72:5
    ۝٥

    Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo Mwenyezi Mungu. [5]

    Tanbihi

    [5] Na hakika sisi tulikuwa tunadhani kuwa haiwi binaadamu au jini kumzulia Mwenyezi Mungu jambo ambalo si laiki naye kusifika nalo.

  218. 72:6
    ۝٦

    Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi. [6]

    Tanbihi

    [6] Na walikuwako wanaume katika wanaadamu wakitafuta ulinzi kwa wanaume wa kijini. Basi hao binaadamu hawakuwazidishia majini ila kuzidi uasi na ujinga na ujeuri.

  219. 72:7
    ۝٧

    Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume. [7]

    Tanbihi

    [7] Na hakika majini walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, enyi binaadamu, kwamba Mwenyezi Mungu hatamfufua yeyote baada ya kwisha kufa, wala hatowaletea watu Mtume yeyote wa kibinaadamu.

  220. 72:8
    ۝٨

    Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo. [8]

    Tanbihi

    [8] Na hakika sisi tulitaka kufikilia mbinguni, tukakuta kumejaa walinzi wa kimalaika wenye nguvu, na vimondo vinavyo unguza kutoka upande huo.

  221. 72:9
    ۝٩

    Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia! [9]

    Tanbihi

    [9] Na sisi kabla ya leo tulikuwa tukikaa pande za mbinguni kwenye makao kwa ajili ya kuchunguza khabari za mbinguni. Lakini sasa mwenye kutaka kusikiliza anakuta vimondo vinamngojea kumzuia na kumteketeza.

  222. 72:10
    ۝١٠

    Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu. [10]

    Tanbihi

    [10] Na hakika sisi hatujui imekusudiwa adhabu kwa walioko katika ardhi kwa huku kulindwa mbingu hata ikazuiliwa kusikilizwa, au Mola wao Mlezi anawatakia kheri na uwongofu?

  223. 72:11
    ۝١١

    Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali. [11]

    Tanbihi

    [11] Na hakika miongoni mwetu wapo walio wema wachamngu, na miongoni mwetu pia wapo walio kinyume na hivyo. Na hao ni walio wastani katika wema wao. Kwa hivyo sisi ni wa makundi mbali mbali.

  224. 72:12
    ۝١٢

    Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia. [12]

    Tanbihi

    [12] Na hakika sisi tumeyakinika kwamba hatutamshinda Mwenyezi Mungu popote tutapo kuwapo katika ardhi, wala hatutamshinda hata tukifanya tuikimbie hukumu yake kwendea mbinguni.

  225. 72:13
    ۝١٣

    Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa. [13]

    Tanbihi

    [13] Na hakika sisi tulipo isikia Qur'ani tuliiamini. Na mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi hachelei kupunguziwa chochote katika mema yake, wala kudhulumiwa kwa kuzidishiwa maovu yake.

  226. 72:14
    ۝١٤

    Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu. [14]

    Tanbihi

    [14] Na hakika kati yetu wapo Waislamu wenye kuikubali Haki, na miongoni mwetu wapo wenye kuiacha njia ya uwongofu. Basi wenye kusilimu hao wameifuata njia ya Haki, na ni wenye kufanya jitihada katika kuikhiari njia hiyo.

  227. 72:15
    ۝١٥

    Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu. [15]

    Tanbihi

    [15] Ama majeuri walio iacha njia ya Uislamu basi hao watakuwa ndio kuni za Jahannamu.

  228. 72:16
    ۝١٦

    Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia tungeli wanywesha maji kwa wingi, [16]

    Tanbihi

    [16] Na hakika lau kuwa watu na majini wakifuata Njia ya Uislamu, wala wasende upogo wakaiwacha, basi bila ya shaka tutawanywesha maji mengi yatakayo enea nyakati za haja.

  229. 72:17
    ۝١٧

    Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu. [17]

    Tanbihi

    [17] Ili tuwajaribu tuwaone vipi watavyo mshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema anazo waneemesha. Na mwenye kukengeuka na ibada ya Mola wake Mlezi atamtia katika adhabu ya mashaka asiyo yaweza kuyachukua.

  230. 72:18
    ۝١٨

    Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu. [18]

    Tanbihi

    [18] Na imefunuliwa kwangu kwamba kwa hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu peke yake. Basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.

  231. 72:19
    ۝١٩

    Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga! [19]

    Tanbihi

    [19] Na imefunuliwa kwangu kwamba alipo simama Mja wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, katika Swala yake akimuabudu Mwenyezi Mungu, majini walijikusanya makundi kwa makundi, wakistaajabu kwa waliyo kuwa wakiyaona na wakiyasikia.

  232. 72:20
    ۝٢٠

    Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote. [20]

    Tanbihi

    [20] Sema: Hakika mimi namuabudu Mola wangu Mlezi peke yake, wala simshirikishi na yeyote katika ibada.

  233. 72:21
    ۝٢١

    Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni. [21]

    Tanbihi

    [21] Sema: Mimi sina uweza wowote juu yenu wa kukuondoleeni madhara, wala kukuleteeni uwongofu na manufaa.

  234. 72:22
    ۝٢٢

    Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu. [22]

    Tanbihi

    [22] Sema: Hakika mimi hapana yeyote awezae kuniondolea adhabu nikimuasi Mwenyezi Mungu. Wala sipati pa kukimbilia, kuikimbia adhabu yake.

  235. 72:23
    ۝٢٣

    Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele. [23]

    Tanbihi

    [23] Lakini niliwezalo ni kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu na Risala zake alizo nituma nizifikishe. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipuuza Dini ya Mwenyezi Mungu, basi hakika mtu huyo atapata Moto wa Jahannamu abakie humo milele.

  236. 72:24
    ۝٢٤

    Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo jua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi. [24]

    Tanbihi

    [24] Hata watakapo iona adhabu waliyo ahidiwaa, hapo basi watajua wakati itapo shuka, nani mwenye msaidizi dhaifu asiye na nguvu, na yupi mchache wa idadi. Ni wao au Waumini?

  237. 72:25
    ۝٢٥

    Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu. [25]

    Tanbihi

    [25] Sema: Enyi makafiri! Sijui ni karibu hiyo adhabu mliyo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi ataifanya iwe mbali?

  238. 72:26
    ۝٢٦

    Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake, [26]

    Tanbihi

    [26] Yeye ndiye Mjuzi wa ghaibu, yaliyo siri. Hapana mmoja katika viumbe vyake anaye ijua siri yake,

  239. 72:27
    ۝٢٧

    Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake. [27]

    Tanbihi

    [27] ila Mtume aliye mridhia kumjuvya baadhi ya hiyo siri. Naye humwekea mbele ya huyo Mtume na nyuma yake Malaika wa kumkinga na wasiwasi.

  240. 72:28
    ۝٢٨

    Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu. [28]

    Tanbihi

    [28] Ili Mwenyezi Mungu ayajue hayo yametokea kwa kuwafikiana na alivyo kadiria, ya kwamba Manabii hakika wamefikisha Risala za Mola wao Mlezi. Na kwa hakika Yeye kesha jua kwa kufananua yote waliyo nayo, na anajua idadi ya viumbe vyote. Hapana kitu kinacho mpotea Yeye.

  241. Sura Al-Muzzammil

    سُورَةُ المزمل
  242. 73:1
    ۝١

    Ewe uliye jifunika! [1]

    Tanbihi

    [1] Ewe uliye jigubika kwa nguo zako!

  243. 73:2
    ۝٢

    Kesha usiku kucha, ila kidogo tu! [2]

    Tanbihi

    [2] Inuka kwa ajili ya Swala usiku kucha, ila kidogo tu!

  244. 73:3
    ۝٣

    Nusu yake, au ipunguze kidogo. [3]

    Tanbihi

    [3] Simama nusu ya usiku, au punguza kidogo katika hiyo nusu mpaka ifikie thuluthi,

  245. 73:4
    ۝٤

    Au izidishe - na soma Qur'ani kwa utaratibu na utungo. [4]

    Tanbihi

    [4] Au zidisha kwenye nusu mpaka ifikie thuluthi mbili. Na soma Qur'ani kwa pole pole ukibainisha harufi, na pa kusita usite, pasiwe na nuksani yoyote.

  246. 73:5
    ۝٥

    ka Hakika Sisi tutakuteremshia uli nzito. [5]

    Tanbihi

    [5] Ewe Mtume! Hakika Sisi tutakuteremshia Qur'ani yenye kukusanya amri, na makatazo, na takalifu nzito nzito.

  247. 73:6
    ۝٦

    Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo, na maneno yake yanatua zaidi. [6]

    Tanbihi

    [6] Hakika ibada zinazo fanywa usiku zinaganda zaidi katika moyo wa mtu, na zinabainika zaidi ulimini, na zinasibu vyema zaidi, kuliko visomo vya ibada za mchana.

  248. 73:7
    ۝٧

    Kwani hakika mchana una shughuli nyingi. [7]

    Tanbihi

    [7] Hakika mchana unakuwa na mambo mengi ya kukuhangaisha kutafuta maslaha ya maisha yako, na kushughulika na mambo ya kufikisha Ujumbe. Basi jiwekee nafsi yako faragha ya usiku kwa ajili ya kumuabudu Mola wako Mlezi.

  249. 73:8
    ۝٨

    Na lidhukuru jina la Mola wako Mlezi, na ujitolee kwake kwa ukamilifu. [8]

    Tanbihi

    [8] Na pitisha ulimini mwako kudhukuru jina la Mola aliye kuumba na kukulea, na mkhusishe Yeye tu kwa ibada kwa ukamilifu.

  250. 73:9
    ۝٩

    Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, hapana mungu isipo kuwa Yeye, basi mfanye kuwa Mtegemewa wako. [9]

    Tanbihi

    [9] Yeye ndiye Mwenye kumiliki mashariki na magharibi, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye. Basi mfanye Yeye tu ndiye wa kukutosha katika mambo yako yote, ndiye wa kutegemewa peke yake kama alivyo ahidi.

  251. 73:10
    ۝١٠

    Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kwa vizuri. [10]

    Tanbihi

    [10] Na vumilia upuuzi wanao usema, na jitenge nao kwa moyo wako, na nenda kinyume na vitendo vyao, pamoja na kuwapuuza, na kuacha kujilipizia.

  252. 73:11
    ۝١١

    Na niache Mimi na hao wanao kanusha, walio neemeka; na wape muhula kidogo! [11]

    Tanbihi

    [11] Niachilie Mimi hao wanao kadhibisha, wenye kuneemeshwa, na uwape muhula muda mfupi.

  253. 73:12
    ۝١٢

    Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unao waka kwa ukali kabisa! [12]

    Tanbihi

    [12] Huko Akhera tumewawekea wanao kadhibisha pingu nzito, na Moto wa kuunguza,

  254. 73:13
    ۝١٣

    Na chakula kinacho kwama kooni, na adhabu inayo umiza. [13]

    Tanbihi

    [13] Na chakula kinacho sakama kooni, hakimezeki, na adhabu yenye uchungu mkali usio stahamilika.

  255. 73:14
    ۝١٤

    Siku ambayo ardhi itatikiswa na milima pia, na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga. [14]

    Tanbihi

    [14] Siku itakapo tikisika ardhi na milima kwa mtikiso mkubwa mno, na milima ikawa mirundu ya mchanga ulio tapanyika, baada ya kuwa mawe magumu yaliyo shikamana.

  256. 73:15
    ۝١٥

    Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu, kama tulivyo mtuma Mtume kwa Firauni. [15]

    Tanbihi

    [15] Enyi watu wa Makka! Hakika Sisi tumekutumieni Muhammad kuwa ni Mtume wa kukushuhudilieni Siku ya Kiyama kwa kukubali na kukataa, kama tulivyo mtuma Musa kwa Firauni awe ni Mtume.

  257. 73:16
    ۝١٦

    Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamshika mshiko wa mateso. [16]

    Tanbihi

    [16] Firauni akamkataa huyo Mtume, basi tukamshika kwa mshiko wa nguvu!

  258. 73:17
    ۝١٧

    Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku ambayo itawafanya watoto wadogo waote mvi? [17]

    Tanbihi

    [17] Basi mkikufuru mtajikinga vipi na adhabu ya Siku ambayo kwa kitisho chake itawafanya vijana wawe vikongwe wasio na nguvu?

  259. 73:18
    ۝١٨

    Hapo mbingu zitapasuka! Ahadi yake itakuwa imetekelezwa. [18]

    Tanbihi

    [18] Mbingu juu ya nguvu zake na ukubwa wake, Siku hiyo zitapasukilia mbali kwa shida zake na vitisho vyake. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni lazima itokee, hapana hivi wala hivi.

  260. 73:19
    ۝١٩

    Kwa hakika hili ni kumbusho. Mwenye kutaka atashika njia ya kwendea kwa Mola wake Mlezi. [19]

    Tanbihi

    [19] Hakika Aya hizi zinazo taja ahadi ya Mwenyezi Mungu ni mawaidha. Kwa hivyo mwenye kutaka kunafiika kwazo ataishika njia ya kumwendea Mola wake Mlezi kwa kuchamngu na kunyenyekea.

  261. 73:20
    ۝٢٠

    Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe kadhaalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye ukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni. Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo, na mshike Swala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayo itanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [20]

    Tanbihi

    [20] Hakika Mola wako Mlezi anajua kwamba wewe, Muhammad, unakesha pengine akali kuliko thuluthi mbili za usiku, na mara nyengine unakesha nusu ya usiku, na pia wanakesha baadhi ya masahaba zako kama ukeshavyo wewe. Na hapana anaye weza kuukadiria urefu wa usiku na mchana, na kudhibiti saa zake, ila Mwenyezi Mungu. Yeye anajua kuwa hamwezi kuhisabu baraabara kila sehemu katika sehemu za usiku na mchana. Kwa hivyo amekukhafifishieni. Basi someni katika Swala kilicho chepesi katika Qur'ani. Yeye anajua kuwa watakuwepo kati yenu walio wagonjwa, ambao watapata taabu kukesha usiku; na wengine wamo safarini kwa ajili ya biashara na kazi, wakitafuta riziki ya Mwenyezi Mungu. Na wengine wanapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kulitukuza Neno lake. Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani, na zishikeni baraabara faridha za Swala, na toeni Zaka iliyo kuwajibikieni, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema, kwa kuwapa mafakiri kwa khiari juu ya hayo yaliyo kulazimuni. Na chochote cha kheri mnacho kitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu, mtakuta thawabu zake kwa Mwenyezi Mungu zimekuwa bora zaidi kuliko hicho mlicho kiacha na kukitoa, na malipo mema zaidi. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu kwa vitendo viovu na kwa upungufu katika vitendo vyema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya Waumini, na ni Mwenye kuwarehemu.

  262. Sura Al-Muddaththir

    سُورَةُ المدثر
  263. 74:1
    ۝١

    Ewe uliye jigubika!

  264. 74:2
    ۝٢

    Simama uonye!

  265. 74:3
    ۝٣

    Na Mola wako Mlezi mtukuze!

  266. 74:4
    ۝٤

    Na nguo zako, zisafishe.

  267. 74:5
    ۝٥

    Na yaliyo machafu yahame!

  268. 74:6
    ۝٦

    Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa.

  269. 74:7
    ۝٧

    Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri!

  270. 74:8
    ۝٨

    Basi litapo pulizwa barugumu,

  271. 74:9
    ۝٩

    Siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu.

  272. 74:10
    ۝١٠

    Kwa makafiri haitakuwa nyepesi.

  273. 74:11
    ۝١١

    Niache peke yangu na niliye muumba;

  274. 74:12
    ۝١٢

    Na nikamjaalia awe na mali mengi,

  275. 74:13
    ۝١٣

    Na wana wanao onekana,

  276. 74:14
    ۝١٤

    Na nikamtgenezea mambo vizuri kabisa.

  277. 74:15
    ۝١٥

    Kisha anatumai nimzidishie!

  278. 74:16
    ۝١٦

    Hasha! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia inadi Aya zetu!

  279. 74:17
    ۝١٧

    Nitamtesa kwa mateso yasio wezekana.

  280. 74:18
    ۝١٨

    Kwani hakika yeye alifikiri na akapima.

  281. 74:19
    ۝١٩

    Basi ameangamia! Vipi alivyo pima!

  282. 74:20
    ۝٢٠

    Tena ameangamia! Vipi alivyo pima!

  283. 74:21
    ۝٢١

    Kisha akatazama,

  284. 74:22
    ۝٢٢

    Kisha akakunja kipaji, na akanuna.

  285. 74:23
    ۝٢٣

    Kisha akaipa kisogo haki, na akatakabari.

  286. 74:24
    ۝٢٤

    Na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio nukuliwa.

  287. 74:25
    ۝٢٥

    Haya si chochote ila kauli ya binaadamu.

  288. 74:26
    ۝٢٦

    Nitakuja mtia kwenye Moto wa Saqar.

  289. 74:27
    ۝٢٧

    Na nini kitakujuulisha ni nini huo Moto wa Saqar?

  290. 74:28
    ۝٢٨

    Haubakishi wala hausazi.

  291. 74:29
    ۝٢٩

    Unababua ngozi iwe nyeusi.

  292. 74:30
    ۝٣٠

    Juu yake wapo kumi na tisa.

  293. 74:31
    ۝٣١

    Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, wala hatukuifanya idadi yao hiyo ila kuwatatanisha walio kufuru, wapate kuwa na yakini walio pewa Kitabu, na wazidi Imani wale walio amini, wala wasiwe na shaka walio pewa Kitabu na Waumini, na wapate kusema wenye maradhi katika nyoyo zao na makafiri: Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu? Ndio kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha apotee amtakaye, na humwongoa amtakaye. Na hapana yeyote anaye jua majeshi ya Mola wako Mlezi ila Yeye tu. Na haya si chochote ila ni ukumbusho kwa binaadamu.

  294. 74:32
    ۝٣٢

    Hasha! Naapa kwa mwezi!

  295. 74:33
    ۝٣٣

    Na kwa usiku unapo kucha!

  296. 74:34
    ۝٣٤

    Na kwa asubuhi inapo pambazuka!

  297. 74:35
    ۝٣٥

    Hakika huo Moto ni katika mambo yaliyo makubwa kabisa!

  298. 74:36
    ۝٣٦

    Ni onyo kwa binaadamu,

  299. 74:37
    ۝٣٧

    Kwa anaye taka miongoni mwenu kutangulia au kuchelewa.

  300. 74:38
    ۝٣٨

    Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyo yachuma.

  301. 74:39
    ۝٣٩

    Isipo kuwa watu wa kuliani.

  302. 74:40
    ۝٤٠

    Hao watakuwa katika Mabustani, wawe wanaulizana

  303. 74:41
    ۝٤١

    Khabari za wakosefu:

  304. 74:42
    ۝٤٢

    Ni nini kilicho kupelekeni Motoni?

  305. 74:43
    ۝٤٣

    Waseme: Hatukuwa miongoni walio kuwa wakiswali.

  306. 74:44
    ۝٤٤

    Wala hatukuwa tukiwalisha masikini.

  307. 74:45
    ۝٤٥

    Na tulikuwa tukizama pamoja na walio zama katika maovu.

  308. 74:46
    ۝٤٦

    Na tulikuwa tukiikanusha siku ya malipo.

  309. 74:47
    ۝٤٧

    Mpaka yakini ilipo tufikia.

  310. 74:48
    ۝٤٨

    Basi hautawafaa kitu uombezi wa waombezi.

  311. 74:49
    ۝٤٩

    Basi wana nini hata wanapuuza onyo hili?

  312. 74:50
    ۝٥٠

    Kama kwamba wao ni mapunda walio timuliwa,

  313. 74:51
    ۝٥١

    Wanao mkimbia simba!

  314. 74:52
    ۝٥٢

    Ati kila mmoja katika wao anataka apewe nyaraka zilizo funuliwa.

  315. 74:53
    ۝٥٣

    Hasha! Kwani wao hawaiogopi Akhera?

  316. 74:54
    ۝٥٤

    Hasha! Kwa hakika huu ni ukumbusho!

  317. 74:55
    ۝٥٥

    Basi anaye taka atakumbuka.

  318. 74:56
    ۝٥٦

    Na hawatakumbuka isipo kuwa Mwenyezi Mungu atake. Uchamngu ni kwake Yeye, na msamaha ni wake Yeye.

  319. Sura Al-Qiyaama

    سُورَةُ القيامة
  320. 75:1
    ۝١

    Ninaapa kwa Siku ya Kiyama! [1]

    Tanbihi

    [1] Ninaapa na natilia mkazo kiapo hichi kwa Siku ya Kiyama, na hiyo ni kweli iliyo thibiti;

  321. 75:2
    ۝٢

    Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu! [2]

    Tanbihi

    [2] Na ninaapa na natilia mkazo kiapo hichi kwa nafsi inayo mlaumu mtu kwa dhambi zake na upungufu wake, ya kwamba bila ya shaka yoyote mtafufuliwa baada ya kukusanywa mafupa yenu yaliyo tawanyika.

  322. 75:3
    ۝٣

    Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake? [3]

    Tanbihi

    [3] Hivyo mtu anadhani baada ya kuwa Sisi tulimuumba naye hakuwa kitu chochote, tutakuja shindwa kuyakusanya mafupa yake yaliyooza na yakatapanyika?

  323. 75:4
    ۝٤

    Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake! [4]

    Tanbihi

    [4] Hasha! Sisi tuna uweza wa kuviweka sawa hata vifupa vya vidole vyake vilivyo vurugika, wachilia mbali mafupa yake makubwa makubwa ya mwili wake.

  324. 75:5
    ۝٥

    Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake. [5]

    Tanbihi

    [5] Hivyo mtu anakanya kufufuliwa? Anataka abakie katika uasi wake katika siku zote zilizo mbakilia katika umri wake ulio salia?

  325. 75:6
    ۝٦

    Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama? [6]

    Tanbihi

    [6] Anauliza kwa kuona haiwezi kutokea saa ya Kiyama: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?

  326. 75:7
    ۝٧

    Basi jicho litapo dawaa! [7]

    Tanbihi

    [7] Jicho litapo tahayari kwa kufazaika na kushtuka,

  327. 75:8
    ۝٨

    Na mwezi utapo patwa! [8]

    Tanbihi

    [8] Na mwangaza wa mwezi ukapotea,

  328. 75:9
    ۝٩

    Na likakusanywa jua na mwezi! [9]

    Tanbihi

    [9] Na jua likakusanyika na mwezi kuchomoza magharibi,

  329. 75:10
    ۝١٠

    Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio? [10]

    Tanbihi

    [10] Mtu hapo atasema: Yako wapi makimbilio kuikimbia hii adhabu?

  330. 75:11
    ۝١١

    La! Hapana pa kukimbilia! [11]

    Tanbihi

    [11] Huachi, ewe mtu, kutafuta makimbilio? Leo huna pa kukimbilia wewe,

  331. 75:12
    ۝١٢

    Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu. [12]

    Tanbihi

    [12] ila kwa Mola wako Mlezi peke yake, ndipo penye matulivu ya waja, Peponi au Motoni.

  332. 75:13
    ۝١٣

    Siku hiyo ataambiwa aliyo yatanguliza na aliyo yaakhirisha. [13]

    Tanbihi

    [13] Siku hiyo mtu ataambiwa vitendo vyake alivyo vitanguliza na alivyo viakhirisha.

  333. 75:14
    ۝١٤

    Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake. [14]

    Tanbihi

    [14] Bali mtu yeye mwenyewe ni hoja iliyo wazi juu ya nafsi yake inayo mkazania kwa anayo yatenda na anayo yaacha.

  334. 75:15
    ۝١٥

    Na ingawa atatoa chungu ya udhuru. [15]

    Tanbihi

    [15] Na ijapo kuwa atajitolea chungu nzima ya udhuru na akazieneza, hawezi kabisa kuepukana na hoja hizo.

  335. 75:16
    ۝١٦

    Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka. [16]

    Tanbihi

    [16] Usiuharikishe ulimi wako kwa kuisoma Qur'ani na kujaribu kuihifadhi kwa haraka pale unapo teremshiwa kwa Wahyi.

  336. 75:17
    ۝١٧

    Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. [17]

    Tanbihi

    [17] Hakika ni juu yetu Sisi kuikusanya hiyo katika kifua chako, na kuithibitisha katika ulimi wako.

  337. 75:18
    ۝١٨

    Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake. [18]

    Tanbihi

    [18] Akikusomea Mjumbe wetu (Jibril) basi nawe ifuatilize kama unavyo isikia.

  338. 75:19
    ۝١٩

    Kisha ni juu yetu kuubainisha. [19]

    Tanbihi

    [19] Kisha baada ya hayo ni juu yetu kuibainisha ikiingia tatizo lolote juu yako.

  339. 75:20
    ۝٢٠

    Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani, [20]

    Tanbihi

    [20] Wacheni kukanya kufufuliwa, na hilo ni jambo la kweli. Lakini nyinyi mnaipenda dunia na starehe zake,

  340. 75:21
    ۝٢١

    Na mnaacha maisha ya Akhera. [21]

    Tanbihi

    [21] Na mnaiacha Akhera na neema zake.

  341. 75:22
    ۝٢٢

    Zipo nyuso siku hiyo zitao ng'ara, [22]

    Tanbihi

    [22] Siku hiyo zitakuwapo nyuso nzuri, zenye kumwangalia Mola wao Mlezi bila ya kusema kwa sifa gani, wajihi gani, au masafa gani.

  342. 75:23
    ۝٢٣

    Zinamwangallia Mola wao Mlezi. [23]

    Tanbihi

    [23] Siku hiyo zitakuwapo nyuso nzuri, zenye kumwangalia Mola wao Mlezi bila ya kusema kwa sifa gani, wajihi gani, au masafa gani.

  343. 75:24
    ۝٢٤

    Na zipo nyuso siku hiyo zitakao kunjana. [24]

    Tanbihi

    [24] Na nyuso nyengine zitakuwapo zimenuna, zimekunjana mno, zinangojea zitendewe jambo ambalo kwa kitisho chake linavunja uti wa mgongo.

  344. 75:25
    ۝٢٥

    Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo. [25]

    Tanbihi

    [25] Zinangojea zitendewe jambo ambalo kwa kitisho chake linavunja uti wa mgongo.

  345. 75:26
    ۝٢٦

    La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo, [26]

    Tanbihi

    [26] Mna nini na kuipenda dunia ambayo mnaifariki roho inapo fika katika mafupa ya kooni,

  346. 75:27
    ۝٢٧

    Na pakasemwa: Nani wa kumganga? [27]

    Tanbihi

    [27] Na walio hudhuria wakasema: Yupo wa kumganga huyu kwa haya aliyo nayo?

  347. 75:28
    ۝٢٨

    Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki; [28]

    Tanbihi

    [28] Akayakinisha yule yaliyo mfika mauti kama lililo mshukia ni kuiacha dunia inayo pendwa, na imekwisha mfika shida yake kikomo cha mwisho.

  348. 75:29
    ۝٢٩

    Na utapo ambatishwa muundi kwa muundi, [29]

    Tanbihi

    [29] Na muundi wa mguu umekwisha ambatana na wa pili wakati wa kutoka roho.

  349. 75:30
    ۝٣٠

    Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi! [30]

    Tanbihi

    [30] Kwa Mola wako Mlezi tu siku hiyo ndio machungio ya waja, ama Peponi au Motoni.

  350. 75:31
    ۝٣١

    Kwa sababu hakusadiki, wala hakuswali. [31]

    Tanbihi

    [31] Binaadamu amekanya kufufuliwa, na kwa hivyo hakumsadiki Mtume wala Qur'ani. Wala hakumtimizia Mwenyezi Mungu faridha za Swala.

  351. 75:32
    ۝٣٢

    Bali alikanusha, na akageuka. [32]

    Tanbihi

    [32] Lakini aliikadhibisha Qur'ani, akaipuuza Imani,

  352. 75:33
    ۝٣٣

    Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao. [33]

    Tanbihi

    [33] Na akatoka kwenda kwa watu wake wa nyumbani kwa maringo na kujitapa.

  353. 75:34
    ۝٣٤

    Ole wako, ole wako! [34]

    Tanbihi

    [34] Ewe unaye kadhibisha, utaangamia!

  354. 75:35
    ۝٣٥

    Kisha Ole wako, ole wako! [35]

    Tanbihi

    [35] Tena utaangamia! Na tena utaangamia, na utaangamia!

  355. 75:36
    ۝٣٦

    Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure? [36]

    Tanbihi

    [36] Hivyo anadhani huyu mtu anaye kanya kufufuliwa kuwa ataachwa hivi hivi akiringa tu katika maisha yake, na akisha kufa iwe basi, wala asifufuliwe akahisabiwa kwa vitendo vyake?

  356. 75:37
    ۝٣٧

    Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa? [37]

    Tanbihi

    [37] Kwani yeye mtu hakuwa ni tone tu ya manii, ilio jaaliwa kuwemo katika tumbo la uzazi?

  357. 75:38
    ۝٣٨

    Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo. [38]

    Tanbihi

    [38] Kisha hiyo tone ikawa kipande cha damu iliyo ganda, na Mwenyezi Mungu akaiumba, akaisawazisha mpaka ikawa na umbo zuri?

  358. 75:39
    ۝٣٩

    Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke. [39]

    Tanbihi

    [39] Akajaalia namna mbili, mwanamume na mwanamke?

  359. 75:40
    ۝٤٠

    Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu? [40]

    Tanbihi

    [40] Je! Huyo Muumba wa mwanzo aliye fanya yote haya, basi si muweza wa kuwahuisha maiti baada ya kuyakusanya mafupa yao?

  360. Sura Al-Insaan

    سُورَةُ الانسان
  361. 76:1
    ۝١

    Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa. [1]

    Tanbihi

    [1] Hakika kimempitia mwanaadamu kipindi cha zama kabla hajapuliziwa roho, naye hata bado hakuwa ni kitu cha kutajika kwa jina lake, wala hajuulikani nini atakuwa.

  362. 76:2
    ۝٢

    Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona. [2]

    Tanbihi

    [2] Hakika Sisi tumemuumba mwanaadamu naye ana sifa namna mbali mbali, kwa ajili ya kumtia mtihanini, majaribioni, baadaye. Kwa hivyo tukamjaalia awe anasikia na anaona, ili apate kuzisikia Aya na azione Ishara.

  363. 76:3
    ۝٣

    Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru. [3]

    Tanbihi

    [3] Hakika Sisi tumembainishia Njia ya Uwongofu, ama awe Muumini au awe kafiri.

  364. 76:4
    ۝٤

    Hakika HaSisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali. [4]

    Tanbihi

    [4] Hakika Sisi tumewawekea tayari makafiri minyororo kuwafungia miguu yao, pingu za kuwafungia mikono na shingo, na moto unao waka.

  365. 76:5
    ۝٥

    Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri! [5]

    Tanbihi

    [5] Hakika walio kuwa wakweli katika Imani yao watakunywa mvinyo iliyo changanywa na maji ya kafuri.

  366. 76:6
    ۝٦

    Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi. [6]

    Tanbihi

    [6] Hiyo ni chemchem wanayo inywa waja wa Mwenyezi Mungu, na wanaipitisha watakapo kwa sahala.

  367. 76:7
    ۝٧

    Wanatimiza ahadi,na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana, [7]

    Tanbihi

    [7] Wanatekeleza yaliyo wajibikia , na wanaikhofu Siku kubwa hiyo ambayo madhara yake yataenea kote kote,

  368. 76:8
    ۝٨

    Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa. [8]

    Tanbihi

    [8] Na huwalisha chakula mafakiri wasio weza kazi, na watoto walio fiwa na wazee wao, na wafungwa wasio miliki kitu, ijapo kuwa wao wenyewe hao watoaji wanakipenda hicho wanacho kitoa, na wanakihitajia.

  369. 76:9
    ۝٩

    Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. [9]

    Tanbihi

    [9] Na hujiambia nafsi zao: Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutaka thawa;bu za Mwenyezi Mungu. Sisi hatutaki kwenu malipo au zawadi, wala hatutaki kushukuriwa na kusifiwa.

  370. 76:10
    ۝١٠

    Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu. [10]

    Tanbihi

    [10] Hakika sisi tunakhofu kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku ya kumletea msiba atakaye kuwapo siku hiyo, na siku ya watu kukunja nyuso zao na vipaji vyao.

  371. 76:11
    ۝١١

    Basi Mwenyezi Mungu atwalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha. [11]

    Tanbihi

    [11] Basi Mwenyezi Mungu akawalinda na shida za siku hiyo, na badala ya mkunjo wa wenye maasi, akawapa nyuso za kupendeza, na ukunjufu na furaha katika nyoyo zao,

  372. 76:12
    ۝١٢

    Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri. [12]

    Tanbihi

    [12] Na akawajazi kwa ile subira yao Pepo imeenea furaha, na nguo zake ni hariri laini.

  373. 76:13
    ۝١٣

    Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali. [13]

    Tanbihi

    [13] Wakiegemea huko Peponi juu ya makochi, hawaoni joto la jua, wala shida ya baridi.

  374. 76:14
    ۝١٤

    Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning'inia mpaka chini. [14]

    Tanbihi

    [14] Na Pepo ambayo vivuli vya miti yake vimeenea kote kote, na matunda yake mepesi kuyachuma.

  375. 76:15
    ۝١٥

    Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae, [15]

    Tanbihi

    [15] Na wakiwazungukia watumishi wao kwa bilauri za kunywea zilio fanywa kwa fedha, lakini unaona kiliomo ndani kama kwamba ni kigae,

  376. 76:16
    ۝١٦

    Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo. [16]

    Tanbihi

    [16] Na vinapimwa vinywaji kwa kadiri wanavyo penda wanywaji.

  377. 76:17
    ۝١٧

    Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi. [17]

    Tanbihi

    [17] Na watu wema hupewa kunywa huko Peponi mvinyo inayo fanana na sharubati ya tangawizi kwa utamu.

  378. 76:18
    ۝١٨

    Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil. [18]

    Tanbihi

    [18] Hiyo ni kutokana na chemchem ya Peponi inayo itwa Salsabil, kwa sababu ya wepesi wa unywaji wake na uzuri wake.

  379. 76:19
    ۝١٩

    Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa. [19]

    Tanbihi

    [19] Na watakuwa wanawazunguka vijana ambao hawabadiliki hali yao, kwa furaha na sururi. Ukiwaona wanapo zunguka kwa wepesi na uchangamfu, utawadhania kwa uzuri wao na usafi wa rangi zao, kama lulu zilizo tandazwa mbele yako zinang'ara.

  380. 76:20
    ۝٢٠

    Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa. [20]

    Tanbihi

    [20] Na ukitazama popote katika hiyo Pepo utaona neema kubwa, na ufalme ulio tanda.

  381. 76:21
    ۝٢١

    Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at'ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji safi kabisa. [21]

    Tanbihi

    [21] Juu yao zipo nguo za hariri nyepesi za kijani, na nguo za hariri nzito. Na mapambo yao yaliomo mikononi mwao ni vikuku vya fedha. Na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji kingine kilio safi, hakina uchafu wala najisi.

  382. 76:22
    ۝٢٢

    Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa. [22]

    Tanbihi

    [22] Hakika neema hizi ameziandaa kwa kukulipeni kwa vitendo vyenu. Na hizo juhudi zenu duniani ni zenye kusifika kwa Mwenyezi Mungu, na zinampendeza, na zimekubaliwa.

  383. 76:23
    ۝٢٣

    Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani kidogo kidogo. [23]

    Tanbihi

    [23] Hakika Sisi, kwa rehema yetu na hikima yetu, tumekuteremshia wewe Qur'ani kwa njia ya kukutuza moyo wako, na uweze daima kuihifadhi, basi huto isahau kabisa.

  384. 76:24
    ۝٢٤

    Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt'ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru. [24]

    Tanbihi

    [24] Basi subiri, uivumilie hikima ya Mola wako Mlezi kwa kuakhirisha kushinda kwako kuwashinda maadui zako, na wewe ukapata mitihani kwa maudhi yao. Wala usiwat'ii washirikina, wingi wa madhambi, walio zama katika ukafiri.

  385. 76:25
    ۝٢٥

    Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni; [25]

    Tanbihi

    [25] Na dumisha kumkumbuka na kumtaja Mola wako Mlezi, na sali alfajiri mapema, na adhuhuri, na alasiri jioni,

  386. 76:26
    ۝٢٦

    Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu. [26]

    Tanbihi

    [26] Na usiku sali magharibi na isha. Na fanya ibada za usiku kwa muda mrefu.

  387. 76:27
    ۝٢٧

    Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyuma yao siku nzito. [27]

    Tanbihi

    [27] Hakika hawa makafiri wanaipenda dunia, na wanaifadhilisha kuliko Akhera. Na wanaiacha migongoni mwao siku yenye misiba mikubwa, na vitisho vikali. Wala wao hawajui nini cha kuwaokoa wao na hayo!

  388. 76:28
    ۝٢٨

    Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao. [28]

    Tanbihi

    [28] Sisi tumewaumba wao, na tumefanya kwa hikima kuumbwa kwao. Na tukitaka tutawateketeza wao na tutawaleta mfano ya wao badala yao, ambao hao watakuja kumt'ii Mwenyezi Mungu kinyume na wao.

  389. 76:29
    ۝٢٩

    Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi. [29]

    Tanbihi

    [29] Hakika Sura hii ni mawaidha kwa walimwengu wote. Basi mwenye kutaka atafuata njia ya Imani na uchamngu kwendea kwa Mola wake Mlezi imfikishe kwenye maghfira yake na Pepo yake.

  390. 76:30
    ۝٣٠

    Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima. [30]

    Tanbihi

    [30] Wala nyinyi hamwezi kutaka kitu chochote ila wakati anapo taka Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zenu, Mwenye hikima kwa anayo yataka na akayakhiari.

  391. 76:31
    ۝٣١

    Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu. [31]

    Tanbihi

    [31] Humuingiza amtakaye katika Pepo yake. Basi kuingia Peponi ni kwa fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu. Naye amewadhalilisha wenye kudhulumu, amewatengenezea adhabu iliyo chungu.

  392. Sura Al-Mursalaat

    سُورَةُ المرسلات
  393. 77:1
    ۝١

    Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole! [1]

    Tanbihi

    [1] Naapa kwa Aya zilizo tumwa kwa ulimi wa Jibrili kumpelekea Muhammad kwa upole wa kawaida na kheri,

  394. 77:2
    ۝٢

    Na zinazo vuma kwa kasi! [2]

    Tanbihi

    [2] Na kwa Aya zenye kuzitwaa kwa nguvu dini nyengine zote za uwongo zikizipeperushia mbali,

  395. 77:3
    ۝٣

    Na zikaeneza maeneo yote! [3]

    Tanbihi

    [3] Na kwa Aya zenye kueneza hikima na uwongofu katika nyoyo za walimwengu kwa uenezi mkubwa mno,

  396. 77:4
    ۝٤

    Na zinazo farikisha zikatawanya! [4]

    Tanbihi

    [4] Na zenye kufarikisha baina ya kweli na uwongo kwa mfarakano ulio wazi kabisa,

  397. 77:5
    ۝٥

    Na zinazo peleka mawaidha! [5]

    Tanbihi

    [5] Na zenye kuwapa watu mawaidha ya kuwanufaisha,

  398. 77:6
    ۝٦

    Kwa kuudhuru au kuonya, [6]

    Tanbihi

    [6] Ili iwe ni udhuru kwao na onyo wasiwe na hoja,

  399. 77:7
    ۝٧

    Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa! [7]

    Tanbihi

    [7] Hakika haya mliyo ahidiwa ya kuja Kiyama kwa yakini yatatimia tu bila ya shaka yoyote.

  400. 77:8
    ۝٨

    Wakati nyota zitakapo futwa, [8]

    Tanbihi

    [8] Basi nyota zitapo ondolewa kabisa,

  401. 77:9
    ۝٩

    Na mbingu zitakapo pasuliwa, [9]

    Tanbihi

    [9] Na mbingu zitapo pasuka,

  402. 77:10
    ۝١٠

    Na milima itakapo peperushwa, [10]

    Tanbihi

    [10] Na milima ikavurugwa na ikapeperushiwa mbali na upepo,

  403. 77:11
    ۝١١

    Na Mitume watakapo wekewa wakati wao, [11]

    Tanbihi

    [11] Na Mitume wakawekewa wakati maalumu wahudhurie kwa ajili ya kuwatolea ushahidi kaumu zao.

  404. 77:12
    ۝١٢

    Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo? [12]

    Tanbihi

    [12] Kwa ajili ya siku gani yametayarishwa mambo haya makubwa makubwa?

  405. 77:13
    ۝١٣

    Kwa siku ya kupambanua! [13]

    Tanbihi

    [13] Kwa ajili ya siku watakapo pambanuliwa baina ya viumbe.

  406. 77:14
    ۝١٤

    Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni nini? [14]

    Tanbihi

    [14] Na nini cha kukujuvya ina nini hiyo siku ya kupambanua?

  407. 77:15
    ۝١٥

    Ole wao, siku hiyo hao wanao kanusha! [15]

    Tanbihi

    [15] Ni maangamio ya milele siku hiyo kwa hao wanao kadhibisha walio waahidi Mitume!

  408. 77:16
    ۝١٦

    Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia? [16]

    Tanbihi

    [16] Kwani hatukuwaangamiza mataifa ya zamani yaliyo kadhibisha,

  409. 77:17
    ۝١٧

    Kisha tukawafuatilizia walio fuatia? [17]

    Tanbihi

    [17] Na kisha tukawafuatilizia hao wenginewe tukawateketeza hali kadhaalika,

  410. 77:18
    ۝١٨

    Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu! [18]

    Tanbihi

    [18] Kwa madhambi waliyo yafanya na walivyo mkataa Mwenyezi Mungu?

  411. 77:19
    ۝١٩

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [19]

    Tanbihi

    [19] Siku hiyo ni siku ya kuteketezwa walio kadhibisha, kama tulivyo waahidi.

  412. 77:20
    ۝٢٠

    Kwani hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa? [20]

    Tanbihi

    [20] Kwani hatukukuumbeni kutokana na maji yaliyo dhalili, nayo ni manii,

  413. 77:21
    ۝٢١

    Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti? [21]

    Tanbihi

    [21] Na tukayaweka maji haya katika pahala patulivu,

  414. 77:22
    ۝٢٢

    Mpaka muda maalumu? [22]

    Tanbihi

    [22] Mpaka kutimilia kuumbwa kwake na kutengenezwa kwake kwa muda anao ujua Mwenyezi Mungu.

  415. 77:23
    ۝٢٣

    Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria. [23]

    Tanbihi

    [23] Nasi tukaweka vipimo katika kuumbwa kwake, na kutengenezwa kwake, na kutoka kwake. Basi wabora wa kupima na kukadiria ni Sisi.

  416. 77:24
    ۝٢٤

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [24]

    Tanbihi

    [24] Ole wao hao wanao kadhibisha neema za kuumba na kukadiria.

  417. 77:25
    ۝٢٥

    Kwani hatukuifanya ardhi yenye kukusanya [25]

    Tanbihi

    [25] Kwani hatukuifanya ardhi kuwa imekusanya juu ya mgongo wake

  418. 77:26
    ۝٢٦

    Walio hai na maiti? [26]

    Tanbihi

    [26] Viumbe vilivyo hai visio hisabika, na vilio kufa visio kadirika,

  419. 77:27
    ۝٢٧

    Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu? [27]

    Tanbihi

    [27] Na tukaweka milima iliyo thibiti imara mirefu, na tukakunywesheni maji matamu?

  420. 77:28
    ۝٢٨

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [28]

    Tanbihi

    [28] Wataangamia siku hiyo hao wanao kadhibisha neema hizi!

  421. 77:29
    ۝٢٩

    Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha! [29]

    Tanbihi

    [29] Siku ya kupambanua wataambiwa makafiri: Nendeni huko Motoni mliko kuwa mkikukanusha.

  422. 77:30
    ۝٣٠

    Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu! [30]

    Tanbihi

    [30] Nendeni kwenye joto la moshi wa Jahannamu ulio gawika kwa ukubwa wake mapande matatu.

  423. 77:31
    ۝٣١

    Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako. [31]

    Tanbihi

    [31] Hapana cha kujikinga na joto la siku hiyo, wala kivuli hicho hakipunguzi joto la mwako hata kidogo.

  424. 77:32
    ۝٣٢

    Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba! [32]

    Tanbihi

    [32] Moto huo hutupa macheche yenye ukubwa kama majumba,

  425. 77:33
    ۝٣٣

    Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano! [33]

    Tanbihi

    [33] Au utaona hayo macheche kama ngamia weusi wenye kuingia rangi ya manjano.

  426. 77:34
    ۝٣٤

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [34]

    Tanbihi

    [34] Wataangamia siku hiyo wanao kanusha kwamba hizi ndizo sifa za Moto.

  427. 77:35
    ۝٣٥

    Hii ni siku ambayo hawatatamka kitu, [35]

    Tanbihi

    [35] Haya uliyo simuliwa yatatokea katika siku ambayo hawatatamka kitu cha kuwanufaisha,

  428. 77:36
    ۝٣٦

    Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru. [36]

    Tanbihi

    [36] Wala hawatakuwa na idhini ya kutamka, wala hawatatoa udhuru, kwani hawana udhuru.

  429. 77:37
    ۝٣٧

    Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! [37]

    Tanbihi

    [37] Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha siku hii.

  430. 77:38
    ۝٣٨

    Hii ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia. [38]

    Tanbihi

    [38] Hii ndiyo siku ya kufafanua baina ya mwenye ukweli, na mwenye uwongo, kwa kuwa kila mmoja atalipwa kwa mujibu wa anavyo stahiki. Enyi mnao mkadhibisha Muhammad! Tumekujaalieni nyinyi na walio kutangulieni walio kadhibisha mfano wenu,

  431. 77:39
    ۝٣٩

    kiwa mnayo hila, nifanyieni hila Mimi! [39]

    Tanbihi

    [39] Kama mnayo hila ya kujikinga na adhabu basi fanyeni hila hiyo. Basi njooni muepukane na adhabu yangu.

  432. 77:40
    ۝٤٠

    Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! [40]

    Tanbihi

    [40] Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha ahadi ya Mwenyezi Mungu.

  433. 77:41
    ۝٤١

    Hakika wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem, [41]

    Tanbihi

    [41] Hakika wachamngu wenye kujikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu watakuwa katika kivuli kikubwa, na chemchem zinazo miminika,

  434. 77:42
    ۝٤٢

    Na matunda wanayo yapenda, [42]

    Tanbihi

    [42] Na matunda wanayo yaonea ladha, na wanayo yapenda,

  435. 77:43
    ۝٤٣

    Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda. [43]

    Tanbihi

    [43] Wataambiwa kwa kuamkiwa na kukirimiwa: Kuleni na mnywe chakula na vinywaji kwa starehe kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kuwa mkivitenda duniani.

  436. 77:44
    ۝٤٤

    Hakika ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema. [44]

    Tanbihi

    [44] Hakika Sisi huwalipa mfano wa malipo hayo matukufu watu wema.

  437. 77:45
    ۝٤٥

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [45]

    Tanbihi

    [45] Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha Pepo.

  438. 77:46
    ۝٤٦

    Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu! [46]

    Tanbihi

    [46] Na makafiri wataambiwa: Kuleni na mjistareheshe kwa starehe isiyo baki muda mrefu, kwani hakika nyinyi ni wakosefu kwa kumshirikisha kwenu Mwenyezi Mungu.

  439. 77:47
    ۝٤٧

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [47]

    Tanbihi

    [47] Wataangamia siku hiyo wanao ikadhibisha neema.

  440. 77:48
    ۝٤٨

    Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami. [48]

    Tanbihi

    [48] Na wakiambiwa: Swalini kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na mnyenyekeeni Yeye, hawanyenyekei wala hawaswali; bali hushikilia kiburi chao!

  441. 77:49
    ۝٤٩

    Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! [49]

    Tanbihi

    [49] Wataangamia siku wanao kadhibisha amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake.

  442. 77:50
    ۝٥٠

    Basi maneno gani baada ya haya watayaamini? [50]

    Tanbihi

    [50] Basi maneno gani hawa watayaamini ikiwa hawaiamini Qur'ani, na hali hii ni muujiza ulio toka mbinguni?

Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani