سُورَةُ القيامة
Sura Al-Qiyaama
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 75:1١
Ninaapa kwa Siku ya Kiyama! [1]
Tanbihi
[1] Ninaapa na natilia mkazo kiapo hichi kwa Siku ya Kiyama, na hiyo ni kweli iliyo thibiti;
- 75:2٢
Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu! [2]
Tanbihi
[2] Na ninaapa na natilia mkazo kiapo hichi kwa nafsi inayo mlaumu mtu kwa dhambi zake na upungufu wake, ya kwamba bila ya shaka yoyote mtafufuliwa baada ya kukusanywa mafupa yenu yaliyo tawanyika.
- 75:3٣
Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake? [3]
Tanbihi
[3] Hivyo mtu anadhani baada ya kuwa Sisi tulimuumba naye hakuwa kitu chochote, tutakuja shindwa kuyakusanya mafupa yake yaliyooza na yakatapanyika?
- 75:4٤
Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake! [4]
Tanbihi
[4] Hasha! Sisi tuna uweza wa kuviweka sawa hata vifupa vya vidole vyake vilivyo vurugika, wachilia mbali mafupa yake makubwa makubwa ya mwili wake.
- 75:5٥
Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake. [5]
Tanbihi
[5] Hivyo mtu anakanya kufufuliwa? Anataka abakie katika uasi wake katika siku zote zilizo mbakilia katika umri wake ulio salia?
- 75:6٦
Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama? [6]
Tanbihi
[6] Anauliza kwa kuona haiwezi kutokea saa ya Kiyama: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?
- 75:7٧
Basi jicho litapo dawaa! [7]
Tanbihi
[7] Jicho litapo tahayari kwa kufazaika na kushtuka,
- 75:8٨
Na mwezi utapo patwa! [8]
Tanbihi
[8] Na mwangaza wa mwezi ukapotea,
- 75:9٩
Na likakusanywa jua na mwezi! [9]
Tanbihi
[9] Na jua likakusanyika na mwezi kuchomoza magharibi,
- 75:10١٠
Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio? [10]
Tanbihi
[10] Mtu hapo atasema: Yako wapi makimbilio kuikimbia hii adhabu?
- 75:11١١
La! Hapana pa kukimbilia! [11]
Tanbihi
[11] Huachi, ewe mtu, kutafuta makimbilio? Leo huna pa kukimbilia wewe,
- 75:12١٢
Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu. [12]
Tanbihi
[12] ila kwa Mola wako Mlezi peke yake, ndipo penye matulivu ya waja, Peponi au Motoni.
- 75:13١٣
Siku hiyo ataambiwa aliyo yatanguliza na aliyo yaakhirisha. [13]
Tanbihi
[13] Siku hiyo mtu ataambiwa vitendo vyake alivyo vitanguliza na alivyo viakhirisha.
- 75:14١٤
Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake. [14]
Tanbihi
[14] Bali mtu yeye mwenyewe ni hoja iliyo wazi juu ya nafsi yake inayo mkazania kwa anayo yatenda na anayo yaacha.
- 75:15١٥
Na ingawa atatoa chungu ya udhuru. [15]
Tanbihi
[15] Na ijapo kuwa atajitolea chungu nzima ya udhuru na akazieneza, hawezi kabisa kuepukana na hoja hizo.
- 75:16١٦
Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka. [16]
Tanbihi
[16] Usiuharikishe ulimi wako kwa kuisoma Qur'ani na kujaribu kuihifadhi kwa haraka pale unapo teremshiwa kwa Wahyi.
- 75:17١٧
Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. [17]
Tanbihi
[17] Hakika ni juu yetu Sisi kuikusanya hiyo katika kifua chako, na kuithibitisha katika ulimi wako.
- 75:18١٨
Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake. [18]
Tanbihi
[18] Akikusomea Mjumbe wetu (Jibril) basi nawe ifuatilize kama unavyo isikia.
- 75:19١٩
Kisha ni juu yetu kuubainisha. [19]
Tanbihi
[19] Kisha baada ya hayo ni juu yetu kuibainisha ikiingia tatizo lolote juu yako.
- 75:20٢٠
Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani, [20]
Tanbihi
[20] Wacheni kukanya kufufuliwa, na hilo ni jambo la kweli. Lakini nyinyi mnaipenda dunia na starehe zake,
- 75:21٢١
Na mnaacha maisha ya Akhera. [21]
Tanbihi
[21] Na mnaiacha Akhera na neema zake.
- 75:22٢٢
Zipo nyuso siku hiyo zitao ng'ara, [22]
Tanbihi
[22] Siku hiyo zitakuwapo nyuso nzuri, zenye kumwangalia Mola wao Mlezi bila ya kusema kwa sifa gani, wajihi gani, au masafa gani.
- 75:23٢٣
Zinamwangallia Mola wao Mlezi. [23]
Tanbihi
[23] Siku hiyo zitakuwapo nyuso nzuri, zenye kumwangalia Mola wao Mlezi bila ya kusema kwa sifa gani, wajihi gani, au masafa gani.
- 75:24٢٤
Na zipo nyuso siku hiyo zitakao kunjana. [24]
Tanbihi
[24] Na nyuso nyengine zitakuwapo zimenuna, zimekunjana mno, zinangojea zitendewe jambo ambalo kwa kitisho chake linavunja uti wa mgongo.
- 75:25٢٥
Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo. [25]
Tanbihi
[25] Zinangojea zitendewe jambo ambalo kwa kitisho chake linavunja uti wa mgongo.
- 75:26٢٦
La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo, [26]
Tanbihi
[26] Mna nini na kuipenda dunia ambayo mnaifariki roho inapo fika katika mafupa ya kooni,
- 75:27٢٧
Na pakasemwa: Nani wa kumganga? [27]
Tanbihi
[27] Na walio hudhuria wakasema: Yupo wa kumganga huyu kwa haya aliyo nayo?
- 75:28٢٨
Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki; [28]
Tanbihi
[28] Akayakinisha yule yaliyo mfika mauti kama lililo mshukia ni kuiacha dunia inayo pendwa, na imekwisha mfika shida yake kikomo cha mwisho.
- 75:29٢٩
Na utapo ambatishwa muundi kwa muundi, [29]
Tanbihi
[29] Na muundi wa mguu umekwisha ambatana na wa pili wakati wa kutoka roho.
- 75:30٣٠
Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi! [30]
Tanbihi
[30] Kwa Mola wako Mlezi tu siku hiyo ndio machungio ya waja, ama Peponi au Motoni.
- 75:31٣١
Kwa sababu hakusadiki, wala hakuswali. [31]
Tanbihi
[31] Binaadamu amekanya kufufuliwa, na kwa hivyo hakumsadiki Mtume wala Qur'ani. Wala hakumtimizia Mwenyezi Mungu faridha za Swala.
- 75:32٣٢
Bali alikanusha, na akageuka. [32]
Tanbihi
[32] Lakini aliikadhibisha Qur'ani, akaipuuza Imani,
- 75:33٣٣
Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao. [33]
Tanbihi
[33] Na akatoka kwenda kwa watu wake wa nyumbani kwa maringo na kujitapa.
- 75:34٣٤
Ole wako, ole wako! [34]
Tanbihi
[34] Ewe unaye kadhibisha, utaangamia!
- 75:35٣٥
Kisha Ole wako, ole wako! [35]
Tanbihi
[35] Tena utaangamia! Na tena utaangamia, na utaangamia!
- 75:36٣٦
Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure? [36]
Tanbihi
[36] Hivyo anadhani huyu mtu anaye kanya kufufuliwa kuwa ataachwa hivi hivi akiringa tu katika maisha yake, na akisha kufa iwe basi, wala asifufuliwe akahisabiwa kwa vitendo vyake?
- 75:37٣٧
Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa? [37]
Tanbihi
[37] Kwani yeye mtu hakuwa ni tone tu ya manii, ilio jaaliwa kuwemo katika tumbo la uzazi?
- 75:38٣٨
Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo. [38]
Tanbihi
[38] Kisha hiyo tone ikawa kipande cha damu iliyo ganda, na Mwenyezi Mungu akaiumba, akaisawazisha mpaka ikawa na umbo zuri?
- 75:39٣٩
Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke. [39]
Tanbihi
[39] Akajaalia namna mbili, mwanamume na mwanamke?
- 75:40٤٠
Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu? [40]
Tanbihi
[40] Je! Huyo Muumba wa mwanzo aliye fanya yote haya, basi si muweza wa kuwahuisha maiti baada ya kuyakusanya mafupa yao?
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย