سُورَةُ النازعات
Sura An-Naazi'aat
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 79:1١
Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu! [1]
Tanbihi
[1] Ninaapa kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuving'oa vitu kutokana na pahala pao kwa nguvu,
- 79:2٢
Na kwa wanao toa kwa upole! [2]
Tanbihi
[2] Na kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuvitoa vitu kwa utaratibu na ulaini,
- 79:3٣
Na wanao ogelea! [3]
Tanbihi
[3] Na kwa kila kilicho pewa mbio za kutekeleza kazi yake kwa sahala na wepesi.
- 79:4٤
Wakishindana mbio! [4]
Tanbihi
[4] Na kwa vinavyo shindania kutimiza waajibu ulio twikwa juu yao kushindania kwa juhudi,
- 79:5٥
Wakidabiri mambo. [5]
Tanbihi
[5] Na vinavyo dabiri, kupanga, mambo na kuyaendesha kwa mujibu wa vilivyo khusishwa,
- 79:6٦
Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka! [6]
Tanbihi
[6] Bila ya shaka Saa ya Kiyama itafika; hiyo siku ambayo mpulizo wa mwanzo wa barugumu utavitikisa viumbe vyote,
- 79:7٧
Kifuate cha kufuatia. [7]
Tanbihi
[7] Na mpulizo huo utafuatiwa na wa pili ambao ndio utakao kuwa wa kufufuliwa watu.
- 79:8٨
Siku hiyo nyoyo zitapiga piga! [8]
Tanbihi
[8] Siku hiyo nyoyo zitapapatika kwa khofu.
- 79:9٩
Macho yatainama chini! [9]
Tanbihi
[9] Macho ya watu yatakuwa na huzuni, manyonge.
- 79:10١٠
Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza? [10]
Tanbihi
[10] Watu hawa husema duniani kwa kukanya kufufuliwa: Ati tutarudishwa sisi baada ya kwisha kufa, tuumbwe tena kama tulivyo kuwa?
- 79:11١١
Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa? [11]
Tanbihi
[11] Tukisha kuwa mafupa yaliyo chakaa, ati tutarejeshwa tufufuliwe upya?
- 79:12١٢
Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara! [12]
Tanbihi
[12] Wanasema, kwa kukanya na kejeli: Kurejea huko kama kukitokea basi ni marejeo ya khasara, na sisi si watu wa kukhasiri.
- 79:13١٣
Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu, [13]
Tanbihi
[13] Msidhani kurejea huko ni kuzito. Kwani hayo ni ukelele mmoja tu,
- 79:14١٤
Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano! [14]
Tanbihi
[14] Mara maiti wote watahudhurishwa kwenye ardhi ya mkusanyiko!
- 79:15١٥
Je! Imekufikia hadithi ya Musa? [15]
Tanbihi
[15] Ewe Muhammad! Imekufikilia hadithi ya Musa,
- 79:16١٦
Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T'uwaa, akamwambia: [16]
Tanbihi
[16] Alipo mwita Mola wake Mlezi katika bonde lilio takaswa, linalo itwa "T'uwa"?
- 79:17١٧
Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri [17]
Tanbihi
[17] Akaambiwa: Nenda kwa Firauni aliye pindukia mpaka katika udhalimu.
- 79:18١٨
Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa? [18]
Tanbihi
[18] Umwambie: Je! Huelekei kut'ahirika?
- 79:19١٩
Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha. [19]
Tanbihi
[19] Na mimi nikuongoze upate kumjua Mola wako Mlezi, umwogope.
- 79:20٢٠
Basi alimwonyesha Ishara kubwa. [20]
Tanbihi
[20] Musa akamwonyesha Firauni miujiza mikubwa.
- 79:21٢١
Lakini aliikadhibisha na akaasi. [21]
Tanbihi
[21] Lakini Firauni alimkadhibisha Musa kwa aliyo kuja nayo, na akamuasi kwa aliyo mwitia.
- 79:22٢٢
Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi. [22]
Tanbihi
[22] Kisha akamgeuzia mgongo, akenda kujitahidi kumpinga.
- 79:23٢٣
Akakusanya watu akanadi. [23]
Tanbihi
[23] Akawakusanya wachawi, na akawaita watu,
- 79:24٢٤
Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa. [24]
Tanbihi
[24] Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa.
- 79:25٢٥
Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo. [25]
Tanbihi
[25] Mwenyezi Mungu akampa adhabu kwa kauli yake ya mwisho, nayo ni vile kusema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa. Na akampa adhabu kwa kauli yake ya mwanzo, nayo ni kumkadhibisha Musa a.s.
- 79:26٢٦
Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa. [26]
Tanbihi
[26] Hakika katika hadithi hiyo yapo mawaidha kwa mwenye kumkhofu Mwenyezi Mungu.
- 79:27٢٧
Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga! [27]
Tanbihi
[27] Enyi mnao kanya kufufuliwa! Kukuumbeni nyinyi ni taabu zaidi au kuziumba mbingu, kuzikusanya sehemu zake zilio tawanyika mbali mbali,
- 79:28٢٨
Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri. [28]
Tanbihi
[28] Na kunyanyua kimo chake, na zikakaa sawa hazina tafauti wala ila?
- 79:29٢٩
Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake [29]
Tanbihi
[29] Na akatia kiza katika usiku wake, na akautokeza mchana wake ukawa na mwangaza?
- 79:30٣٠
Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi. [30]
Tanbihi
[30] Na ardhi baada ya hayo akaikunjua, na akaisawazisha, ikasilihi kukaliwa na watu wake?
- 79:31٣١
Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake, [31]
Tanbihi
[31] Akatoa ndani yake maji yake yanayo tibuka katika chemchem zake, na ikamiminika mito yake, na ikawa na mimea yake ya chakula kwa ajili ya watu na wanyama;
- 79:32٣٢
Na milima akaisimamisha, [32]
Tanbihi
[32] Na milima akaithibitisha imara
- 79:33٣٣
Kwa nafuu yenu na mifugo yenu. [33]
Tanbihi
[33] Kwa ajili ya manufaa yenu na wanyama wenu mnao wafuga!
- 79:34٣٤
Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa, [34]
Tanbihi
[34] Kitakapo fika Kiyama ambacho vitisho vyake vitaenea kote,
- 79:35٣٥
Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya, [35]
Tanbihi
[35] Siku atakapo kumbuka mtu vitendo vyake vya kheri au shari,
- 79:36٣٦
Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona, [36]
Tanbihi
[36] Na Jahannamu ikadhihirishwa wazi, akaiona kila mwenye macho kuwa ndio malipo,
- 79:37٣٧
Basi ama yule aliye zidi ujeuri, [37]
Tanbihi
[37] Basi ama mwenye kupita mpaka kwa maasi yake,
- 79:38٣٨
Na akakhiari maisha ya dunia, [38]
Tanbihi
[38] Na akajichagulia nafsi yake maisha yanayo pita njia,
- 79:39٣٩
Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake! [39]
Tanbihi
[39] Basi Moto wa Jahannamu unao babua upepo wake ndio makaazi yake wala hana mengineyo.
- 79:40٤٠
Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, [40]
Tanbihi
[40] Na ama mwenye kukhofu ukubwa na utukufu wa Mola wake Mlezi, na akaizuia nafsi yake na matamanio ya kumpumbaza,
- 79:41٤١
Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake! [41]
Tanbihi
[41] Basi huyo nyumba ya neema ya Peponi ndio makaazi yake, wala hana penginepo.
- 79:42٤٢
Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini? [42]
Tanbihi
[42] Ewe Muhammad! Wanakuuliza, ati, khabari za Saa ya Kiyama, itakuwa lini?
- 79:43٤٣
Una nini wewe hata uitaje? [43]
Tanbihi
[43] Ujuzi wa hayo hauko kwako hata uwatajie.
- 79:44٤٤
Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake. [44]
Tanbihi
[44] Ujuzi wa hayo uko kwa Mola wako Mlezi tu, si kwa mwenginewe. (Nabii Isa a.s. ambaye Wakristo wanasema ni Mwana wa Mungu, au ndiye Mungu, pia anasimuliwa katika Biblia kuwa hakuijua Saa na Siku ya Kiyama. Injili ya Mathayo inanukulu maneno ya Yesu: "Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.")
- 79:45٤٥
Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu. [45]
Tanbihi
[45] Kwani waajibu wako ni kuwaonya wanao khofu si kuwatangazia wakati wake.
- 79:46٤٦
Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake. [46]
Tanbihi
[46] Na wao siku watakayo iona hiyo Saa ya Kiyama ni kama kwamba hawakuishi duniani zaidi kuliko jioni moja tu, au mchana wake.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย