سُورَةُ الإنشقاق
Sura Al-Inshiqaaq
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 84:1١
Itapo chanika mbingu! [1]
Tanbihi
[1] Mbingu itapo chanika, ikaamrishwa iondoke,
- 84:2٢
Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza! [2]
Tanbihi
[2] Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi na ikamt'ii, na ndio maelekeo yake isikie na kut'ii,
- 84:3٣
Na ardhi itakapo tanuliwa! [3]
Tanbihi
[3] Na ardhi ikazidi upana wake kwa kulazwa milima na kuondolewa kifusi chake,
- 84:4٤
Na kuvitoa vilivyo kuwa ndani yake, ikawa tupu! [4]
Tanbihi
[4] Na ardhi ikatoa nje maiti na khazina ziliyo kuwamo ndani yake, na ikaachana navyo vyote hivyo,
- 84:5٥
Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza! [5]
Tanbihi
[5] Na ikamwelekea Mola wake Mlezi kwa kuzidi kutanuka kwake na kutoa vilio kuwemo ndani yake na kuachana navyo, na hayo ni haki yake kuwa. Yakitokea yote hayo yaliyo tangulia kusimuliwa basi kila mtu atapata malipo ya vitendo vyake.
- 84:6٦
Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta. [6]
Tanbihi
[6] Ewe mtu! Hakika wewe unafanya juhudi katika vitendo vyako vikufikishie lengo lako. Basi utakuja kukutana na Mola wako Mlezi kwa a'mali yako, naye atakulipa kwayo.
- 84:7٧
Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia! [7]
Tanbihi
[7] Ama mwenye kupewa daftari la vitendo vyake kwa mkono wake wa kulia
- 84:8٨
Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi! [8]
Tanbihi
[8] Basi atahisabiwa kwa hisabu nyepesi,
- 84:9٩
Na arudi kwa ahali zake na furaha. [9]
Tanbihi
[9] Na atarejea kwa jamaa zake Waumini naye furahani.
- 84:10١٠
Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, [10]
Tanbihi
[10] Ama mwenye kupewa daftari lake kwa mkono wa kushoto wake nyuma ya mgongo wake kwa kudharauliwa shani yake,
- 84:11١١
Basi huyo ataomba kuteketea. [11]
Tanbihi
[11] Huyo atatamani ajiue,
- 84:12١٢
Na ataingia Motoni. [12]
Tanbihi
[12] Na ataingia Motoni aungulie mbali!
- 84:13١٣
Hakika alikuwa furahani kati ya jamaa zake. [13]
Tanbihi
[13] Kwani huyo hakika duniani alikuwa furahani kati ya jamaa zake akitanaamu na pumbao alilo kuwa nalo hata akapuuza a'mali ya kuitenda kwa mustakabali wake.
- 84:14١٤
Huyo hakika alidhani kuwa hatarejea tena. [14]
Tanbihi
[14] Hakika huyo alidhani kuwa kabisa hatorejea kwa Mwenyezi Mungu akamhisabu.
- 84:15١٥
Kwani? Hakika Mola wake Mlezi alikuwa akimwona! [15]
Tanbihi
[15] Bali atarejea, na atahisabiwa! Kwani Mola wake Mlezi alikuwa anamwona vyema yeye na vitendo vyake.
- 84:16١٦
Basi ninaapa kwa wekundu wa jua linapo kuchwa, [16]
Tanbihi
[16] Basi naapa kiapo cha mkazo kwa wekundu wa mbingu baada ya kuchwa jua!
- 84:17١٧
Na kwa usiku na unavyo vikusanya, [17]
Tanbihi
[17] Na kwa usiku na unavyo vikusanya vyote katika giza lake, wanaadamu, wanyama na vyenginevyo!
- 84:18١٨
Na kwa mwezi unapo pevuka, [18]
Tanbihi
[18] Na mwezi unapo kamilika kupevuka na kutimia nuru yake,
- 84:19١٩
Lazima mtapanda t'abaka kwa t'abaka! [19]
Tanbihi
[19] Hapana shaka yoyote mtakutana na hali baada ya hali, baadhi yake zina shida zaidi kuliko nyenginezo, za kufa na kufufuliwa na vitisho vya Kiyama.
- 84:20٢٠
Basi wana nini hawaamini? [20]
Tanbihi
[20] Wana nini hawa makafiri yanayo wazuia wasimuamini Mwenyezi Mungu na kufufuliwa baada ya kuwekwa wazi dalili zake zote za kuwajibika kwake?
- 84:21 ۩ Sijida٢١
Na wanapo somewa Qur'ani hawasujudu? [21]
Tanbihi
[21] Na pindi wakizisikia Aya za Qur'ani hawasujudu wakanyenyekea?
- 84:22٢٢
Bali walio kufuru wanakanusha tu. [22]
Tanbihi
[22] Bali watu hawa, kwa ukafiri wao, wanakanusha kwa inadi na kutakabari kuikataa Haki!
- 84:23٢٣
Na Mwenyezi Mungu anajua wanayo yadhamiria. [23]
Tanbihi
[23] Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kabisa hayo wanayo yadhamiria katika nyoyo zao.
- 84:24٢٤
Basi wabashirie adhabu chungu! [24]
Tanbihi
[24] Basi wabashirie, kwa kejeli, kuwa watapata adhabu ya kutia uchungu.
- 84:25٢٥
Isipo kuwa wale walio amini na wakatenda mema; hao watakuwa na ujira usio malizika. [25]
Tanbihi
[25] Lakini walio amini na wakatenda mema watapata, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ujira usio wakatikia na wala usio kuwa na hisabu juu yao.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย