سُورَةُ الليل
Sura Al-Lail
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 92:1١
Naapa kwa usiku unapo funika! [1]
Tanbihi
[1] Naapa kwa usiku kinapo enea kiza chake!
- 92:2٢
Na mchana unapo dhihiri! [2]
Tanbihi
[2] Na naapa kwa mchana unapo zagaa mwangaza wake!
- 92:3٣
Na kwa Aliye umba dume na jike! [3]
Tanbihi
[3] Na naapa kwa Mjuzi aliye umba viwili viwili, dume na jike, katika kila vinavyo zaliwa!
- 92:4٤
Hakika juhudi zenu bila ya shaka ni mbali mbali. [4]
Tanbihi
[4] Hakika juhudi zenu bila ya shaka zimekhitalifiana; kwani wapo wenye kubahatika katika juhudi zao, na wako wasio bahatika.
- 92:5٥
Ama mwenye kutoa na akamchamngu! [5]
Tanbihi
[5] Ama mwenye kutoa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na akamkhofu Mola wake Mlezi, na kwa hivyo akaepuka anayo yakataza,
- 92:6٦
Na akaliwafiki lilio jema! [6]
Tanbihi
[6] Na akayakinika kufuata fadhila njema, nayo ni Imani kumuamini Mwenyezi Mungu kwa kumjua,
- 92:7٧
Tutamsahilishia yawe mepesi. [7]
Tanbihi
[7] Basi Sisi tutamtengenezea awe katika khulka ya wepesi na raha kwa kumwongoza kwenye njia ya kheri.
- 92:8٨
Na ama mwenye kufanya ubakhili, na asiwe na haja ya wenzake! [8]
Tanbihi
[8] Ama mwenye kufanya ubakhili kwa mali yake asitoe haki ya Mwenyezi Mungu iliomo humo, na akawa hana haja na yatokayo kwa Mwenyezi Mungu,
- 92:9٩
Na akakanusha lilio jema! [9]
Tanbihi
[9] Na akakadhibisha khulka nzuri,
- 92:10١٠
Tutamsahilishia yawe mazito! [10]
Tanbihi
[10] Basi huyo tutamtengenezea khulka ambayo inapelekea uzito na mashaka ya milele.
- 92:11١١
Na mali yake yatamfaa nini atapo kuwa anadidimia? [11]
Tanbihi
[11] Na kitu gani katika adhabu ambacho hayo mali yake yataweza kumkinga nacho, atapo teketea yeye mwenyewe mzima?
- 92:12١٢
Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu. [12]
Tanbihi
[12] Hakika ni juu yetu, Sisi, kwa kufuatana na hikima yetu, ndio tuwabainishie viumbe njia ya uwongofu.
- 92:13١٣
Na hakika ni yetu Sisi Akhera na dunia. [13]
Tanbihi
[13] Na juu yetu Sisi peke yetu, bila ya shaka, hili jambo la kuendesha yaliomo duniani na Akhera.
- 92:14١٤
Basi nakuonyeni na Moto unao waka! [14]
Tanbihi
[14] Ndio maana tukakutieni khofu ya Moto unao waka na kuripuka!
- 92:15١٥
Hatauingia ila mwovu kabisa! [15]
Tanbihi
[15] Hawauingii kwa kudumu ila kafiri
- 92:16١٦
Anaye kadhibisha na kupa mgongo. [16]
Tanbihi
[16] Aliye ikadhibisha Haki na akazipuuza Ishara za Mola wake Mlezi.
- 92:17١٧
Na mchamngu ataepushwa nao, [17]
Tanbihi
[17] Na atakuwa mbali na huo Moto aliye mwingi wa kujikinga na ukafiri na maasi,
- 92:18١٨
Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa. [18]
Tanbihi
[18] Amabye hutoa mali yake wakati wa nafasi ili kujisafisha na uchafu wa ubakhili, na najsi ya uchoyo.
- 92:19١٩
Na wala si kwa kuwa yupo yeyote aliye mfanyia hisani ndio anamlipa. [19]
Tanbihi
[19] Na mtoaji huyu si kama anaye mtu yeyote ambaye ndio anamlipa kwa neema aliyo mfanyia zamani,
- 92:20٢٠
Ila ni kutaka radhi ya Mola wake Mlezi aliye juu kabisa. [20]
Tanbihi
[20] Bali anatoa hicho kwa kutafuta radhi ya Mola wake Mlezi Mtukufu tu.
- 92:21٢١
Naye atakuja ridhika! [21]
Tanbihi
[21] Na bila ya shaka atakuja pata kutoka kwa Mola wake Mlezi anacho kitaka kwa njia za ukamilifu kabisa, hata itimie radhi kwake.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย