سُورَةُ الواقعة
Sura Al-Waaqia
Sikiliza sura nzima
Msomaji: Mishary Rashid Alafasy- 56:1١
Litakapo tukia hilo Tukio . [1]
Tanbihi
[1] Kitakapo tukia Kiyama
- 56:2٢
Hapana cha kukanusha kutukia kwake. [2]
Tanbihi
[2] Haitotokea nafsi yoyote ya kukadhibisha.
- 56:3٣
Literemshalo linyanyualo! [3]
Tanbihi
[3] Kiyama hicho kitawateremsha chini walio waovu, na kitawanyanyua juu walio wema.
- 56:4٤
Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso! [4]
Tanbihi
[4] Ardhi itakapo tikiswa, na ikatetemeshwa kwa nguvu.
- 56:5٥
Na milima itapo sagwasagwa! [5]
Tanbihi
[5] Na milima ikavurugwa teketeke,
- 56:6٦
Iwe mavumbi yanayo peperushwa! [6]
Tanbihi
[6] Ikawa vumbi la kupeperushwa, Aya hizi tukufu zinaeleza hadi gani vitakuwa vitisho vitavyo uteremkia ulimwengu kitapo fika Kiyama. Na katika vitisho hivyo ni hayo masaibu ya dunia yatakayo athiri ardhi na mat'abaka yake. Kwani hii ardhi tunayo ishi juu ya mgongo wake si yenye kutulia na kukaa sawa kwa utimilivu. Kwani hiyo imeundwa kwa mat'abaka ya majabali yaliyo ingiliana ovyo. Huenda baadhi yao yakateremka yakaachana na mengineyo yaliyo jirani nayo. Na huwa hiyo inayo itwa kupasuka kwa mat'abaka ya ardhi, Geological cleavage kama inavyo tokea katika maeneo kadhaa wa kadhaa. Mpasuko huu ulikuwa na ungali kuwa ndio asili ya chini kabisa ya zilzala, mitetemeko, mikubwa kwa kuathirika na nguvu za kudidimiza na kuvuta zinazo fuatana na mat'abaka ya ardhi yanapo vunjika. Basi mizani ya utulivu ya nguvu hizi inapo geuka kwa kuathirika na mambo mengineyo ya nje huenda zikafunguka nguvu za mtikiso mkubwa ndio ikatokea mitetemeko na mitikisiko ya ardhi, ambayo hubomoa kila kitu kiliopo juu ya ardhi karibu na ilipo anzia hiyo zilzala. Na hapo tena hutokea uharibifu mkubwa mno. Na hayo maelezo ya kisayansi hayageuzi kitu, wala hayako mbali na nadhari ya kidini. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huenda akajaalia sababu za maumbile za kawaida zikajumuika kwa njia tusiyo izoea sisi ili zikiingiliana kwa njia ya kutisha ndio sababu ya kuharibika dunia. Hapo maelezo ya kisayansi yanafuatana na Aya zenye kuonya kwa vitisho hivyo vikuu. Na yote hayo yanatokana kwa Mwenyezi Mungu. Na hutokea kwa idhini yake Mwenyezi Mungu kutimiza hukumu yake katika dunia yetu.
- 56:7٧
Na nyinyi mtakuwa namna tatu: . [7]
Tanbihi
[7] Na mkawa nyote siku hiyo namna tatu kwa mujibu wa vitendo vyenu;
- 56:8٨
Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani? [8]
Tanbihi
[8] Basi watu wa mkono wa kulia, watu wa cheo kilio bora, utukufu ulioje huo wa hali yao!
- 56:9٩
Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni? [9]
Tanbihi
[9] Na watu wa kushotoni, hao ni watu wa cheo duni, uovu ulioje wa hali yao!
- 56:10١٠
Na wa mbele watakuwa mbele. [10]
Tanbihi
[10] Na walio tangulia mbele katika mambo ya kheri duniani ndio watakuwa mbele katika vyeo vya Akhera.
- 56:11١١
Hao ndio watakao karibishwa [11]
Tanbihi
[11] Hao ndio walio karibishwa mbele kwa Mwenyezi Mungu. Mola wao Mlezi atawatia katika Bustani zenye neema.
- 56:12١٢
Katika Bustani zenye neema. [12]
Tanbihi
[12] Mola wao Mlezi atawatia katika Bustani zenye neema.
- 56:13١٣
Fungu kubwa katika wa mwanzo, [13]
Tanbihi
[13] Hawa walio karibishwa mbele ni kundi la wengi katika mataifa yaliyo tangulia na Manabii wao,
- 56:14١٤
Na wachache katika wa mwisho. [14]
Tanbihi
[14] Na wachache katika umma wa Muhammad ukiwalinganisha na hao.
- 56:15١٥
Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa. [15]
Tanbihi
[15] Juu ya viti au vitanda vilivyo nakishiwa kwa nakshi za vito vya thamani,
- 56:16١٦
Wakiviegemea wakielekeana. [16]
Tanbihi
[16] wakivitegemea kwa raha na utulivu huku wakielekezana nyuso kwa ziada ya mahaba.
- 56:17١٧
Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele, [17]
Tanbihi
[17] Wakiwazungukia kwa kuwakhudumia vijana watakao baki milele hivyo hivyo,
- 56:18١٨
Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi. [18]
Tanbihi
[18] Nao wamechukua vikombe na mabirika yaliyo jaa vinywaji vya Peponi, na bilauri zenye mvinyo kutoka chemchem zinazo miminika,
- 56:19١٩
Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa. [19]
Tanbihi
[19] Vinywaji hivyo haviwaletei kuumwa kichwa wala kutokwa akili kwa ulevi.
- 56:20٢٠
Na matunda wayapendayo, [20]
Tanbihi
[20] Na matunda ya kila namna wanayo yapenda na wanayo yaona;
- 56:21٢١
Na nyama za ndege kama wanavyo tamani. [21]
Tanbihi
[21] Na nyama za ndege kama zinavyo tamani nafsi zao.
- 56:22٢٢
Na Mahurulaini, [22]
Tanbihi
[22] Na wanawake wenye macho ya vikombe,
- 56:23٢٣
Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa. [23]
Tanbihi
[23] Kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa katika chaza, kwa usafi wao na urembo wao.
- 56:24٢٤
Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda. [24]
Tanbihi
[24] Watapewa haya kuwa ni malipo kwa mambo mema waliyo kuwa wakiyatenda duniani.
- 56:25٢٥
Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi, [25]
Tanbihi
[25] Huko Peponi hawatasikia maneno yasiyo kuwa na maana, wala masimulizi ya kumtia dhambini mwenye kuyasikia.
- 56:26٢٦
Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama. [26]
Tanbihi
[26] Ila watalo sikia ni kauli ya wao kwa wao: Tunakusalimuni kwa Salama.
- 56:27٢٧
Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani? [27]
Tanbihi
[27] Na watu wa mkono wa kulia, hapana ajuaye nini malipo ya watu wa kuliani.
- 56:28٢٨
Katika mikunazi isiyo na miba, [28]
Tanbihi
[28] Katika miti ya mikunazi iliyo katwa miba yake,
- 56:29٢٩
Na migomba iliyo pangiliwa, [29]
Tanbihi
[29] Na migomba iliyo pangika na ndizi zake zimepandana juu ya mikungu,
- 56:30٣٠
Na kivuli kilicho tanda, [30]
Tanbihi
[30] Na kivuli kilicho enea wala hakiondoki,
- 56:31٣١
Na maji yanayo miminika, [31]
Tanbihi
[31] Na maji yanayo miminika karibu yao popote wayatakapo,
- 56:32٣٢
Na matunda mengi, [32]
Tanbihi
[32] Na matunda ya namna nyingi na kabila nyingi yasiyo tindikia wakati wowote,
- 56:33٣٣
Hayatindikii wala hayakatazwi, [33]
Tanbihi
[33] Wala hazuiwiliwi ayatakayo,
- 56:34٣٤
Na matandiko yaliyo nyanyuliwa. [34]
Tanbihi
[34] Na matandiko yaliyo nyanyuliwa ya starehe.
- 56:35٣٥
Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya, [35]
Tanbihi
[35] Hakika Sisi tulianza kuwaumba Mahurulaini mwanzo,
- 56:36٣٦
Na tutawafanya vijana, [36]
Tanbihi
[36] Na tukawafanya kuwa ni vijana,
- 56:37٣٧
Wanapendana na waume zao, hirimu moja. [37]
Tanbihi
[37] Wenye kupendwa na waume zao, wenye umri ulio karibiana,
- 56:38٣٨
Kwa ajili ya watu wa kuliani. [38]
Tanbihi
[38] Wa tayari kwa neema ya watu wa kuliani.
- 56:39٣٩
Fungu kubwa katika wa mwanzo, [39]
Tanbihi
[39] Watu wa kulia ni wengi katika mataifu yaliyo kwisha tangulia,
- 56:40٤٠
Na fungu kubwa katika wa mwisho. [40]
Tanbihi
[40] Na kikundi kikubwa katika umma wa Muhammad.
- 56:41٤١
Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni? [41]
Tanbihi
[41] Na watu wa kushoto, hapana anaye jua nini adhabu ya watu wa kushoto.
- 56:42٤٢
Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka, [42]
Tanbihi
[42] Watakuwa kwenye upepo umoto utakao wazunguka, unao penya katika tundu za mwili, na maji yaliyo chemshwa motoni wayanywe na wamiminiwe vichwani,
- 56:43٤٣
Na kivuli cha moshi mweusi, [43]
Tanbihi
[43] Na katika kivuli cha kiza cheusi cha moshi umoto,
- 56:44٤٤
Si cha kuburudisha wala kustarehesha. [44]
Tanbihi
[44] Hapana ubaridi wa kupunguza joto la hewa, wala huruma ya kuwaletea nafuu wanapo vuta pumzi.
- 56:45٤٥
Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa. [45]
Tanbihi
[45] Hakika hao kabla ya haya walikuwa wamepita kiasi katika kustarehea neema za duniani, wamepumbaa hawataki kumt'ii Mwenyezi Mungu Mtukufu.
- 56:46٤٦
Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa, [46]
Tanbihi
[46] Na walikuwa wameshikilia daima kufanya dhambi kubwa kabisa, kwani waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba kabisa Mwenyezi Mungu hatamfufua aliye kufa.
- 56:47٤٧
Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa? [47]
Tanbihi
[47] Na walikuwa wakisema kwa kukanusha kurejea tena: Ati tutafufuliwa baada ya kwisha kufa, na baadhi ya miili yetu ikisha kuwa udongo na mengine mifupa iliyo chakaa? Ati sisi tutarudishwa tuwe hai mara ya pili?
- 56:48٤٨
Au baba zetu wa zamani? [48]
Tanbihi
[48] Ati tutafufuliwa sisi na baba zetu wa zamani walio kwisha kuwa udongo ulio tapanyika na umepotea katika ardhi?
- 56:49٤٩
Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho [49]
Tanbihi
[49] Waambie kwa kuwajibu kukanusha kwao: Hakika wa zamani na wa mwisho, ambao nyinyi ni katika jumla ya hao,
- 56:50٥٠
Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu. [50]
Tanbihi
[50] Nyote mtakusanywa katika wakati wa siku malumu, na wala hamtoipita.
- 56:51٥١
Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha, [51]
Tanbihi
[51] Kisha nyinyi, enyi mnao ipinga Njia ya Uwongofu, mnao kanusha kufufuliwa,
- 56:52٥٢
Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu. [52]
Tanbihi
[52] Bila ya shaka mtakula mti wa Zaqqumu katika Jahannamu, na mtayajaza matumbo yenu kwa shida ya njaa.
- 56:53٥٣
Na kwa mti huo mtajaza matumbo. [53]
Tanbihi
[53] Na mtayajaza matumbo yenu kwa shida ya njaa.
- 56:54٥٤
Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka. [54]
Tanbihi
[54] Mtakunywa juu ya mlicho kila maji yenye kutokota, yasiyo ondoa kiu,
- 56:55٥٥
Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu. [55]
Tanbihi
[55] Na mtakunywa kwa wingi na pupa kama anavyo kunywa ngamia mwenye kiu kisicho katika kiu chake kwa maji.
- 56:56٥٦
Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo. [56]
Tanbihi
[56] Hayo yaliyo tajwa ya mateso mbali mbali ndio karamu yao waliyo andaliwa kwa siku ya malipo.
- 56:57٥٧
Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki? [57]
Tanbihi
[57] Sisi tulianza kukuumbeni mlipo kuwa si chochote, basi hebu hamkiri uweza wetu wa kukurejesheni tena baada ya kukufufueni?
- 56:58٥٨
Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza? [58]
Tanbihi
[58] Hamuangalii manii mnayo itia katika tumbo la uzazi?
- 56:59٥٩
Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji? [59]
Tanbihi
[59] Ni nyinyi ndio mwenye uweza juu yake na kuilea mpaka ikawa mtu, au ni Sisi ndio twenye makadara hayo?
- 56:60٦٠
Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi [60]
Tanbihi
[60] Sisi tumekuhukumieni mauti, na tumeweka wakati makhsuri wa kufa kwenu. Na wala Sisi si wenye kushindwa kukubadilisheni sura zenu,
- 56:61٦١
Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua. [61]
Tanbihi
[61] Na wala Sisi si wenye kushindwa kukubadilisheni sura zenu, na kuzileta nyengine, na tukakuumbeni katika umbo jengine na sura nyengine msiyo ijua.
- 56:62٦٢
Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki? [62]
Tanbihi
[62] Bila ya shaka mmekwisha yakinika kuwa Mwenyezi Mungu alikuumbeni mara ya kwanza, basi je, hamkumbuki kwamba Mwenye kuweza hayo ni Mweza zaidi wa kufanya tena.
- 56:63٦٣
Je! Mnaona makulima mnayo yapanda? [63]
Tanbihi
[63] Je! Hamuangalii mbegu mnayo ipanda katika ardhi?
- 56:64٦٤
Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha? [64]
Tanbihi
[64] Ni nyinyi mnao ifanya imee au ni Sisi peke yetu ndio tunaifanya imee?
- 56:65٦٥
Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu, [65]
Tanbihi
[65] Tungeli taka tungeli ifanya mimea hiyo iwe mabua na mapepe yaliyo katika katika kabla haijapevuka, mkawa mkistaajabu tu kwa uovu ulio isibu,
- 56:66٦٦
Mkisema: Hakika sisi tumegharimika; [66]
Tanbihi
[66] Huku mkisema: Hakika sisi tumepata khasara baada ya juhudi yetu.
- 56:67٦٧
Bali sisi tumenyimwa. [67]
Tanbihi
[67] Bali sisi hatuna bahati, tumenyimwa riziki.
- 56:68٦٨
Je! Mnayaona maji mnayo yanywa? [68]
Tanbihi
[68] Je! Hamyaoni maji matamu mnayo yanywa?
- 56:69٦٩
Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha? [69]
Tanbihi
[69] Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni, au ni Sisi ndio Wenye kuyateremsha kuwa ni rehema juu yenu? Katika Kiarabu limetajwa neno Almuzni. Maana yake ni mawingu yanayo leta mvua. Na kitendo cha kunyesha mvua kinahitajia mambo yaliyo khusiana na hali ya hewa maalumu ambayo mwanaadamu hana mamlaka nayo, au kuyaleta kwa juhudi zake. Kwa mfano zinahitajiwa pepo zinazo kwenda kwa mkondo zilizo baridi juu ya nyengine zilizo za joto, au hali za kuondoka utulivu katika anga. Na watu wamejaribu kuinyesha mvua kwa mawingu yanayo pita kwa njia ya ufundi, lakini juhudi hizo mpaka sasa ni majaribio, na lilio thibiti katika sayansi ni kufuzu kwa majaribio hayo ni kudogo mno, na hata hivyo kunalazimu ziwepo hali maalumu za maumbile zinazo saidia.
- 56:70٧٠
Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru? [70]
Tanbihi
[70] Lau tungeli taka tungeli yafanya hayo maji yakawa ya chumvi yasiyo nyweka. Basi mbona hamumshukuru Mwenyezi Mungu aliye yajaalia matamu yenye kunyweka?
- 56:71٧١
Je! Mnauona moto mnao uwasha? [71]
Tanbihi
[71] Je! Hamuuoni moto huo mnao uasha?
- 56:72٧٢
Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji? [72]
Tanbihi
[72] Ni nyinyi ndio mlio uotesha mti wake, na mkautia ndani ya huo mti moto, au ni Sisi ndio tulio uumbia hivyo, kadhaalika?
- 56:73٧٣
Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani. [73]
Tanbihi
[73] Sisi tumeufanya huu moto uwe ni ukumbusho wa Moto wa Jahannamu mtapo uona, na uwe ni manufaa kwa wasafiri wa msitu na nyika, wakinafiika kwa kupikia chakula chao na kuotea moto wakati wa baridi.
- 56:74٧٤
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu. [74]
Tanbihi
[74] Basi dumisha kusabihi, kutakasa, kwa kulidhukuru jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa, kwa kumtakasa na kumshukuru kwa neema hizi nzuri.
- 56:75٧٥
Basi naapa kwa maanguko ya nyota, [75]
Tanbihi
[75] Basi ninaapa kweli kwa maangukio ya nyota pale zinapo tua mwisho wa usiku wakati wa Tahajudi, ibada za usiku, na kustaghafiru.
- 56:76٧٦
Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua! [76]
Tanbihi
[76] Na hakika bila ya shaka hicho ni kiapo kikubwa chenye maana ya kufikia mbali, lau kuwa mnafikiri makusudio yake. Aya mbili hizi zinabainisha hadi ya umuhimu wa kiapo hichi kikubwa. Kwani nyota ni vitu vyenye kutoa mwangaza wenyewe, na nyota ya karibu mno kwetu sisi, nayo ni jua, ni kiasi ya masafa ya miaka 500 ya mwangaza. Na nyota ifuatayo kwa ukaribu iko mbali nasi kwa kiasi cha miaka 4 ya mwangaza takriban. Basi nguvu tunazo zitumia kutokana na jua ndizo zinazo tuwezesha kuishi. Lau kuwa umbali wa jua kutokana na ardhi ni duni ya hivyo au zaidi ya hivyo basi hapana shaka kuwa maisha yangeli kuwa taabu, bali ni muhali. Kadhaalika ukubwa wa nyota unakhitalifiana. Zipo nyota kubwa mno hata ukubwa wake unaweza kukusanya hii ardhi na jua juu ya umbali wao. Vipo vikundi vya nyota vinavyo itwa A'naqiid vinaogelea angani zikivuka Njia ya Maziwa The Milky Way mara kwa mara. Wakati wa kupita kwake zikasadifiana kukutana na kikundi cha jua na zikagongana basi hakika hapo itakuwa ndio maangamizo na kumalizika kwa kweli. Hata ikikaribia nyota moja katika nyota zitokazo kwenye jua basi hayo pia yataleta kuharibika mizani na kupelekea maangamizo na kumalizika ulimwengu. Kwa hivyo basi hakika Ishara za mazingatio na uweza wa Mwenyezi Mungu zinaonekana katika ulimwengu huu alio uumba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala na akaupanga.
- 56:77٧٧
Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu, [77]
Tanbihi
[77] Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani yenye manufaa mengi,
- 56:78٧٨
Katika Kitabu kilicho hifadhiwa. [78]
Tanbihi
[78] Imo katika ubao ulio hifadhiwa Al-lauhu-lmahfudh, usio karibiwa na yeyote ila Malaika walio karibishwa kwa Mwenyezi Mungu. (Kwa watumiaji Computer wanaweza kukisia kuwa hiyo Al-lauhu-lmahfudh ni kama Disk iliyomo ndani ya Computer na haigusi mtu, na Misahafu tunayo iona, na kuisoma, ni kama yapigwayo chapa kutoka hiyo Disk.)
- 56:79٧٩
Hapana akigusaye ila walio takaswa. [79]
Tanbihi
[79] Hawaigusi Qur'ani Tukufu ila walio t'ahirika na najisi na hadathi, vitengua udhu;
- 56:80٨٠
Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [80]
Tanbihi
[80] imeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote.
- 56:81٨١
Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza? [81]
Tanbihi
[81] Je! Mnapuuza? Ni Qur'ani hii tukufu ndio nyinyi mnaidharau?
- 56:82٨٢
Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha? [82]
Tanbihi
[82] Na badala ya kuishukuru riziki yenu ndio mna ikadhibisha?
- 56:83٨٣
Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo, [83]
Tanbihi
[83] Basi je! Ikifika roho ya mmoja wenu kwenye mapitio ya pumzi,
- 56:84٨٤
Na nyinyi wakati huo mnatazama! [84]
Tanbihi
[84] Na nyinyi inapo fika roho kwenye koo nanyi mnamwangalia huyo anaye kufa,
- 56:85٨٥
Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi. [85]
Tanbihi
[85] Na Sisi tuko karibu zaidi kwa huyo aliye kabiliwa na mauti na tunaijua zaidi hali yake kuliko nyinyi, lakini nyinyi hamjui hayo wala hamhisi.
- 56:86٨٦
Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu, [86]
Tanbihi
[86] Basi je! Ikiwa nyinyi si wenye kunyenyekea kwa Ungu wetu,
- 56:87٨٧
Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli? [87]
Tanbihi
[87] Mrudishieni roho yake huyo aliye kabiliwa na mauti ikiwa nyinyi mwasema kweli kwamba nyinyi mnazo nguvu na hamshindwi.
- 56:88٨٨
Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, [88]
Tanbihi
[88] Ama akiwa huyo aliye kabiliwa na mauti ni katika walio tangulia walio karibishwa ,
- 56:89٨٩
Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema. [89]
Tanbihi
[89] Basi mwisho wake ni raha, na rehema, na riziki njema, na Pepo yenye neema.
- 56:90٩٠
Na akiwa katika watu wa upande wa kulia, [90]
Tanbihi
[90] Ama akiwa katika watu wa mkono wa kulia,
- 56:91٩١
Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia. [91]
Tanbihi
[91] Basi ataambiwa kwa maamkio na takrima: Unapewa salamu kutokana na watu wa kuliani.
- 56:92٩٢
Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu, [92]
Tanbihi
[92] Na ama akiwa ni katika wa kushoto, wanao kanusha, walio wapotovu,
- 56:93٩٣
Basi karamu yake ni maji yanayo chemka, [93]
Tanbihi
[93] Basi atakirimiwa maji ya moto hadi ya kuchemka,
- 56:94٩٤
Na kutiwa Motoni. [94]
Tanbihi
[94] Na kubabuliwa na moto wa mwisho wa ukali.
- 56:95٩٥
Hakika hii ndiyo haki yenye yakini. [95]
Tanbihi
[95] Hakika haya yaliyo tajwa katika Sura hii tukufu bila ya shaka ni kiini cha yakini iliyo thibiti, isiyo ingiliwa na shaka.
- 56:96٩٦
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa. [96]
Tanbihi
[96] Tanguliza tasbihi kwa kumdhukuru Mola wako Mlezi aliye Mkubwa, kwa kumtakasa na kumshukuru kwa neema zake.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani
Soma kwa lugha nyingine
EnglishالعربيةবাংলাاردوBahasa IndonesiaTürkçeFrançaisBahasa MelayuفارسیNederlandsHausaРусский中文Shqipไทย