Quran Touch

Juzuu 19

Al-Furqaan 25:21 – An-Naml 27:55 · 339 aya

Aa
Neno kwa neno

  1. 25:21
    ۝٢١

    NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno! [21]

    Tanbihi

    [21] Na wakasema wanao kataa kufufuliwa na wala hawatumai kuwa yapo malipo kwa vitendo vyao: Kwa nini hatuteremshiwi Malaika wa kukuunga mkono, au Mwenyezi Mungu akajionyesha kwetu na akatwambia kwamba kweli Yeye kakutuma? Kiburi kimewajaa katika nafsi zao, na wamepita mpaka katika udhalimu na ujabari!

  2. 25:22
    ۝٢٢

    Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali! [22]

    Tanbihi

    [22] Siku ya Kiyama watawaona Malaika kama walivyo tamani, na hayo yatakuwa ni sababu ya kitisho kwao wala si jambo la kuwafurahisha. Watatafuta kujilinda nao, kama walivyo kuwa wakitafuta kujilinda na vinavyo watisha duniani.

  3. 25:23
    ۝٢٣

    Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika. [23]

    Tanbihi

    [23] Na Siku ya Kiyama tutawaletea waliyo yatenda katika mambo ya kuonyesha wema kwa dhaahiri na hisani katika dunia, na Sisi tutayafanya yaondokee patupu, na tutawaharimisha thawabu zake, kwa kuwa yamekosa Imani ambayo ni dharura ipatikane ili vitendo vitiwe maanani.

  4. 25:24
    ۝٢٤

    Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri. [24]

    Tanbihi

    [24] Watu wa Peponi Siku ya Kiyama ndio watao kuwa na utulivu bora, na mashukio mazuri, na makaazi ya starehe, kwa sababu hii ni Pepo walio andaliwa Waumini, si Moto walio andaliwa makafiri.

  5. 25:25
    ۝٢٥

    Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi, [25]

    Tanbihi

    [25] Ewe Nabii! Itaje Siku itapo pasuka mbingu na ikafunguka, na yakadhihiri kati yake mawingu, na Malaika wakashuka khasa kwa yakini.

  6. 25:26
    ۝٢٦

    Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri. [26]

    Tanbihi

    [26] Katika siku hii mali ya watu wenye mali yataharibika, madai yao wanao jidai yatakatika, na Ufalme wote utabaki ni wa Arrahmani , Mwingi wa Rehema, peke yake. Na itakuwa siku ya shida ngumu mno kwa makafiri.

  7. 25:27
    ۝٢٧

    Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! [27]

    Tanbihi

    [27] Siku ya Kiyama mwenye kujidhulumu nafsi yake atajiuma mikono yake kwa hasira na majuto kwa ukafiri wake na kumwendea kinyume Mtume, na kwa kutamani atasema: Laiti lau ningeli mfuata Mtume, nikaifuata njia ya kwendea Peponi, na nikaiepuka njia ya kwendea Motoni!

  8. 25:28
    ۝٢٨

    Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki! [28]

    Tanbihi

    [28] Na atasema kwa kujuta kuwafuata walio mpoteza: Laiti ningeli kuwa sikumsadiki fulani, ambaye nimemwachia aniongoze.

  9. 25:29
    ۝٢٩

    Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet'ani ni khaini kwa mwanaadamu. [29]

    Tanbihi

    [29] Rafiki huyu amenibaidisha na Ukumbusho, Dhikr, kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuikumbuka Qur'ani baada ya kwisha kuwa ni nyepesi kwangu. Ndio hivi Shetani anavyo mkhini binaadamu, na kumtokomeza kwenye hilaki yake.

  10. 25:30
    ۝٣٠

    Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur'ani ni kihame. [30]

    Tanbihi

    [30] Na Mtume alisema akimshitakia Mwenyezi Mungu kwa taabu anazo zipata kwa watu wake: Hakika hawa wameiacha Qur'ani na wameihama, na wameshikilia katika kuipuuza, na kuifanyia inda na uadui.

  11. 25:31
    ۝٣١

    Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru. [31]

    Tanbihi

    [31] Kama tulivyo wajaalia watu wako, ewe Muhammad, wanavyo kufanyia uadui na kukukadhibisha, basi kadhaalika tulimjaalia kila Nabii ana maadui miongoni mwa wakosefu, wanao mfanyia uadui na wanaupinga wito wake. Na Mwenyezi Mungu atakunusuru, na atakuongoa mpaka uwashinde. Na Yeye anakutosha kwa uwongofu na kukunusuru.

  12. 25:32
    ۝٣٢

    Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu. [32]

    Tanbihi

    [32] Na makafiri kutaka kuikebehi Qur'ani walisema: Kwa nini haikuteremshwa kwa mara moja? Na Sisi hakika tumeiteremsha kwa mapande mapande ili moyo wako uthibiti kwayo kwa raha yako na ili uihifadhi. Na tumeisoma, yaani tumeigawa kwa Aya, au tumeisoma kwa ulimi wa Jibril, kidogo kidogo kwa utulivu na upole.

  13. 25:33
    ۝٣٣

    Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora. [33]

    Tanbihi

    [33] Na wala hawakujii na upinzani dhaifu, ila nasi tunakuletea Haki ya kubainisha, na bora ya maelezo.

  14. 25:34
    ۝٣٤

    Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia. [34]

    Tanbihi

    [34] Na walio ukataa Ujumbe wako watabururwa kupelekwa Motoni kifudifudi na madhalili. Hao ndio watu wa chini kabisa kwa cheo, na ndio walio zama mno katika upotovu.

  15. 25:35
    ۝٣٥

    Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri. [35]

    Tanbihi

    [35] Na Mtume s.a.w. anapozwa kwa yaliyo wapata Mitume wa kabla yake. Hakika Sisi tulimteremshia Musa Taurati, na tukamkalifisha afikishe Ujumbe wetu, na tukamuunga mkono kwa ndugu yake Harun, awe waziri wake na msaidizi katika kazi yake.

  16. 25:36
    ۝٣٦

    . Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa. [36]

    Tanbihi

    [36] Tukasema: Nenda wewe na nduguyo kwa Firauni na watu wake. Tukamuunga mkono kwa miujiza inayo onyesha ukweli wake. Hawakumuamini, wakamkadhibisha. Mwisho wao ukawa tukawateketeza na tukawafutilia mbali!

  17. 25:37
    ۝٣٧

    Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu chungu. [37]

    Tanbihi

    [37] Hali kadhaalika kabla ya Musa tuliwafanyia kaumu ya Nuhu walipo mkadhibisha, na aliye mkanusha Mtume mmoja basi amewakanusha Mitume wote. Nao tukawazamisha katika tufani, na tukawafanya wawe ni zingatio kwa watu. Na tukawajaalia hao na kila mshirikina kupata adhabu chungu Akhera.

  18. 25:38
    ۝٣٨

    Na tuliwaangamiza kina A'di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao. [38]

    Tanbihi

    [38] Na kadhaalika tuliwahiliki A'di na Thamudi na watu wa Rass walipo wakanusha Mitume wao. Na tuliziangamiza kaumu nyingi baina ya kaumu ya Nuhu na baina ya A'di, yakawapata malipo ya wenye kudhulumu. Rass, kama ilivyo elezwa katika Mufradaat ya Raaghib Al-As'fahani, ni bonde, na akatolea ushahidi ubeti wa shairi: (Nao ni bonde la Rass, kama mkono kwa mdomo.) Hao watu wa Rass, kama ilivyo kuja katika Aya tukufu, ni watu walio kuwa wakiabudu masanamu. Mwenyezi Mungu aliwatumia Shuaib. Basi hao ndio walio pelekewa Mtume Shuaib a.s. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika amewaeleza hao kaumu ya Shuaib kuwa ni Watu wa Vichakani (Al-Aykat), napo ni pahali penye miti mingi panasifika kwa neema, na mara nyengine wanaitwa Watu wa Rass, nalo ni bonde lenye kheri kubwa, kuonesha neema alizo waneemesha Mwenyezi Mungu. Nao wakazikufuru neema za Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu.

  19. 25:39
    ۝٣٩

    Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa. [39]

    Tanbihi

    [39] Na Sisi tumezionya kaumu zote hizi. Tukawakumbusha mawaidha, na mifano ya kweli yenye manufaa. Lakini hawakuwaidhika. Tukawashika wote kwa kuwaadhibu, tukawahiliki, na tukayabomoa majumba yao mpaka kifusi.

  20. 25:40
    ۝٤٠

    Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa. [40]

    Tanbihi

    [40] Na hawa Makureshi katika safari zao za kwenda Sham wanapita kwenye mji wa kaumu Lut'i, tulio unyeshea mvua ya shari na ovu kabisa, nayo ni mawe ya Motoni. Je! Hawauoni mji huo wakawaidhika kwa yaliyo wafika watu wake? Hakika wao wanauona huo, lakini si kwa macho ya kuwaidhika na kuzingatia. Kwani hawaamini ahadi (za Mwenyezi Mungu) wala kufufuliwa. Wala hawataraji kuwa ipo siku watakuja fufuliwa kwa ajili ya hisabu.

  21. 25:41
    ۝٤١

    Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume? [41]

    Tanbihi

    [41] Na wakikuona watu hawa hawakuchukulii ila kukufanyia kejeli na maskhara. Na huambiana wao kwa wao: Ndiye huyu aliye mtuma kwetu Mwenyezi Mungu awe ni Mtume, na sisi tumfuate twende nyuma yake?

  22. 25:42
    ۝٤٢

    Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia. [42]

    Tanbihi

    [42] Mtu huyu hakika kajaaliwa kuwa na ufasihi mzuri, na hoja za kuvutia kwa wanao msikia. Na hapana shaka ameweza kuchota katika imani zetu hata alikaribia kututoa kwa miungu yetu tumfuate mungu wake. Lakini sisi tumesimama imara juu miungu yetu na dini yetu. (Mwenyezi Mungu anasema:) Tutakuja wabainishia ukweli wa mambo watapo kuja iona adhabu Siku ya Kiyama, na watajua nani huyo aliye thibiti katika upotovu na makosa.

  23. 25:43
    ۝٤٣

    Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake? [43]

    Tanbihi

    [43] Ewe Mtume! Umeona upotovu wa mwenye kufuata matamanio yake na pumbao lake hata akawa anaabudu mawe ambayo hayadhuru wala hayanafiishi? Na wewe umetumwa uwe mwonyaji na mbashiri, wala hukuwakilishwa kwa imani yao na uwongofu wao.

  24. 25:44
    ۝٤٤

    Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia. [44]

    Tanbihi

    [44] Na hivyo unadhani kuwa wengi wao wanasikia kwa sikio la kufahamu au wanaongoka kwa akili zao? Wamesha tupilia mbali kama walivyo amrishwa na ndoto zao. Wamekuwa kama wanyama wa kufuga, hawanalo linalo washughulisha ila kula, na kunywa, na kustarehe na maisha ya dunia. Wala hawana fikra yoyote baada ya hayo. Bali hali yao ni ovu zaidi kuliko ya wanyama, kwani wanyama huwafuata bwana zao katika yenye kheri nao, na wanayaepuka ya kuwadhuru. Lakini watu hawa wanajitokomeza wenyewe kwenye mambo ya kuwahiliki.

  25. 25:45
    ۝٤٥

    Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake. [45]

    Tanbihi

    [45] Tumesimamisha dalili za Tawhidi, Upweke wa Mwenyezi Mungu, za kuwaongoa wenye akili. Hebu kiangalie kivuli. Mwenyezi Mungu amekitandaza na akakifanya kimetulia mwanzo wa mchana. Kisha tukalipeleka jua likaondoa pahala pake kwa mwako wake. Likawa jua ni kama ndio linaongoza kivuli. Bila ya jua, kivuli kisingeli juulikana. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu ange penda angeli kifanya kivuli kitulie vile vile kimewang'ang'ania watu, na yakawaharibikia maslaha yao na mambo yao. " Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake." Aya hii inadhihirisha hima ya Muumba na uwezo wake. Kwani kutandaza kivuli kunaonyesha mzunguko wa dunia na kuinama kwa msumari-kati (axis) wake. Na lau kuwa ardhi, yaani dunia, ingeli tulia tu, haitaharaki kulizunguka jua, na pia ikawa haizunguki wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake, basi kivuli kingeli tulia, na mwako wa jua ungeli piga juu ya nusu ya dunia, na nusu ya pili ikabaki ni usiku, moja kwa moja. Hayo yangeli leta khitilafu kubwa za baridi na joto, na ingeli pelekea kutoweka uhai kabisa katika dunia. Na kadhaalika ingeli kuwa hii ni hali ya dunia basi kivuli kingeli tulia. Na haya pia yange tokea ikiwa muda wa kuzunguka ardhi juu ya msumari-kati wake ndio muda ule ule muda wa kuzunguka kwake kulizunguka jua, yaani siku moja ikawa sawa na mwaka mzima. Lakini hapana awezaye kufanya hayo isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Haya licha ya kuwa kivuli nafsi yake ni neema miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu aliviumba vitu vyote vyapenyeza mwangaza (transparent) kisingeli kuwapo kivuli, na vitu visingeli pata fursa ya kuwepo ambavyo vinahitajia vivuli.

  26. 25:46
    ۝٤٦

    Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo. [46]

    Tanbihi

    [46] Na kukiondoa kwetu kivuli ni kwa utaratibu, kwa kipimo. Hakukuwa kwa mara moja. Na katika hayo yapo manufaa kwa watu.

  27. 25:47
    ۝٤٧

    Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka. [47]

    Tanbihi

    [47] Na katika Ishara za Tawhidi ni kuwa tumeufanya usiku ni sitara kwa kiza chake, ndani yake wanaingia viumbe ukawazunguka kama inavyo wazunguka nguo kwa mwenye kuivaa. Na tukawatengenezea malazi, ikawa ni mapumziko kupumzika na machofu, na kwa mwangaza wa jua wanazinduliwa watu watafute maisha yao na riziki zao.

  28. 25:48
    ۝٤٨

    Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi. [48]

    Tanbihi

    [48] Na Yeye ndiye aliye zifanya pepo zimtumikie, zikasukuma mawingu, nayo yakawabashiria watu itakuja mvua, ambayo ni rehema itokayo kwake kuwaendea wao. Na hakika Sisi tunateremsha kutoka mbinguni maji safi yanayo safisha kuondoa najisi na uchafu. "Na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi." Katika Aya hii tukufu Mwenyezi Mungu anawasimbulia watu kwa kuwateremshia maji yaliyo safi kutoka mbinguni. Na Aya hii inafahamisha kuwa maji ya mvua katika asli ya kuumbwa kwake ni maji safi kabisa. Na juu ya kuwa baada yake yanabeba takataka nyingi katika anga, lakini bado yamo katika daraja ya usafi.

  29. 25:49
    ۝٤٩

    Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba. [49]

    Tanbihi

    [49] Tunaiteremsha mvua kwa sababu makulima yapate kumea na kukua, na ardhi ipate kufufuka baada ya kufa kwake, na wanyweshwe watu na wanyama walio umbwa.

  30. 25:50
    ۝٥٠

    Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru. [50]

    Tanbihi

    [50] Na hii Qur'ani tumeibainisha na tumeisarifu, tumeifanya, ili watu wamkumbuke Mola wao Mlezi, na wawaidhike, na watende kwa mujibu wake. Lakini wengi wa watu wanakataa isipo kuwa ukafiri na inda tu.

  31. 25:51
    ۝٥١

    Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji. [51]

    Tanbihi

    [51] Na lau kuwa tumetaka basi tungeli mpeleka mwonyaji kwenye kila mji. Basi jitahidi na wito wako; na wacha maneno ya makafiri; na tupilia mbali wanayo yaleta.

  32. 25:52
    ۝٥٢

    Basi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa. [52]

    Tanbihi

    [52] Na endelea na kulingania kwako kwa Haki, na kufikisha Ujumbe wa Mola wako Mlezi. Na wao wakiupinga wito wako, na wakawavamia Waumini basi wapige vita, na kwa hayo pigana Jihadi kubwa.

  33. 25:53
    ۝٥٣

    Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho. [53]

    Tanbihi

    [53] Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziendesha bahari mbili, bahari ya maji matamu na bahari ya maji ya chumvi. Na akafanya njia ya kila moja inakaribiana na nyengine. Na juu ya hivyo maji yao hayachanganyikani. Hiyo ni neema na rehema kwa watu. "Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho." Yamkini Aya hii inaashiria neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwa kuto changanyika maji ya chumvi yanayo penya kutoka baharini kwenye miamba ya karibu na mwambao, na maji matamu yanayo penya kutoka bara, yasichanganyike kwa ukamilifu na hali nayo yanakutana. Matamu yanakuwa yako juu ya maji chumvi kama kwamba baina yao pana kinga kinacho zuia haya yasiingiane na haya, na kizuizi kizuiacho, yaani kizuizi chembamba tusicho weza kukiona. Na haya si tu, bali ipo kanuni madhubuti inayo hukumu makhusiano haya, na inayo yahukumu kwa maslaha ya wanaadamu wanao kaa katika maeneo hayo, na maisha yao yanategemea kuwepo hayo maji matamu. Kwani imethibiti kuwa t'abaka ya maji matamu yalioko juu huzidi unene wake kwa mujibu wa kuzidi usawa (level) wa bahari kwa mpango maalumu. Hata inakuwa yawezekana kuhisabu kina cha mwisho cha maji matamu ambayo yamkinika kuyapata. Kwani hiyo ni sawa sawa na kadri ya khitilafu baina ya usawa (level) wa ardhi na usawa wa bahari mara arubaini.

  34. 25:54
    ۝٥٤

    Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza. [54]

    Tanbihi

    [54] Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba kutokana na manii hawa watu, na akawajaalia wanaume na wanawake walio khusiana kwa nasaba ya kuzaana na kwa ushemeji wa kuoana. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza kwa atakayo, kwani kwa hiyo hiyo manii ameumba namna mbili mbali mbali.

  35. 25:55
    ۝٥٥

    Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi. [55]

    Tanbihi

    [55] Na baada ya Ishara hizi zenye kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye stahiki kuabudiwa, na kwamba hapana mungu isipo kuwa Yeye, wanatoka kikundi cha watu kuabudu masanamu yasiyo wafaa wala kuwadhuru. Na hawa kwa kujua kwao haya wanamsaidia Shetani, na yeye anawapoteza. Basi hao inakuwa wanasaidiana katika kuipinga Haki ambayo Mwenyezi Mungu anawaitia.

  36. 25:56
    ۝٥٦

    Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji. [56]

    Tanbihi

    [56] Na ewe Nabii! Huna jukumu ila kufikisha hayo ulio tumwa basi, na kuwabashiria Pepo Waumini, na kuwakhofisha makafiri kwa haya watayo yakuta. Baada ya hayo huna jengine unalo takiwa.

  37. 25:57
    ۝٥٧

    Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi. [57]

    Tanbihi

    [57] Na waambie: Hakika mimi sitafuti kwa huku kukuiteni muufuate Uislamu ujira wowote wala malipo. Ila nilitakalo ni mwongoke na muifuate Njia ya Haki mrejee kwa Mola wenu Mlezi.

  38. 25:58
    ۝٥٨

    Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake. [58]

    Tanbihi

    [58] Na katika mambo yako mtegemee Mwenyezi Mungu Aliye Hai, ambaye hayumkini kufa. Na mtakase na mtukuze kwa kuzisifu neema zake. Na waachilie mbali walio toka kwenye Njia. Kwani Mwenyezi Mungu anawajua vyema, na atawalipa kwa dhambi zao.

  39. 25:59
    ۝٥٩

    . Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye. [59]

    Tanbihi

    [59] Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao kwa siku sita. Naye ametawala juu ya A'rshi, Kiti cha Enzi, cha Ufalme wote, na madaraka yake yameenea kila kitu. Na Yeye ndiye Mwingi wa Rehema, Arrahman. Na ukitaka lolote katika sifa zake muulize ajuae atakujibu. Naye ni Mwenyezi Mungu Mwenye hikima. "Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Ulize khabari zake kwa wamjuaye." Hizo Siku Sita ni usemi wa Mwenyezi Mungu, Mtukufu Aliye tukuka, kueleza wakati. Na Yeye Mtukufu ndiye Mwenye kujua zaidi kipimo cha hiyo Siku. Na kwa upande wa kiilimu za sayansi kazi ya kuumba ulimwengu unahitaji kupita vipindi na viwango mbali mbali. Na "Mbingu na ardhi na viliomo ndani yake" ni ishara ya vyombo vyote vya mbinguni, nyota, majua, sayari, miezi, mavumbi, gesi za namna mbali mbali, na nishat'i, Energy , na vyote hivyo vinavyo fanya ndio ulimwengu wa duniani na angani. Na kwa kuupanga ulimwengu wote, yaani uumbaji wote, kwa tafsili ya ukamilifu inayo kusanya kila kitu, ndio inaweka wazi, Utawala wa Mwenyezi Mungu, Subhanahu juu ya ulimwengu kwa jumla na kwa tafsili. "Uliza khabari zake kwa ajuaye". Katika kifungu hichi cha Aya hii tukufu pana uwongozi wa kisayansi kutokana na Mwenyezi Mungu kuonyesha dharura ya uchunguzi na utafiti wa mambo yanayo onekana ya uumbaji na mipango yake tuyaangalie ya ndani, ili tujue siri za uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuanzisha huu ulimwengu.

  40. 25:60 ۩ Sijida
    ۝٦٠

    Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki. [60]

    Tanbihi

    [60] Na wakiambiwa hawa makafiri: Mnyenyekeeni Arrahmani, Mwingi wa Rehema, na mumuabdu, wao husema: Nani huyo Arrahmani? Sisi hatumjui, hata tumsujudie. Basi tukufuate amri yako tu? Na wanazidi kuwa mbali na kutengeka na Imani.

  41. 25:61
    ۝٦١

    Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara. [61]

    Tanbihi

    [61] Ametukuka Arrahman, Mwingi wa Rehema, na zimezidi fadhila zake. Ameziumba sayari mbinguni na akazijaalia na vituo vyake vya kupitia, na katika hizo akaumba jua kuwa ni taa yenye mwangaza, na mwezi wenye nuru. "Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara." Aya hii tukufu inaashiria maana za ki-ilimu za sayansi zenye kukusanywa katika mpango wa ulimwengu alio uumba Mwenyezi Mungu, Aliye takasika, Aliye tukuka, na zikazidi fadhila zake. Na sisi tunashuhudia nyota za mbinguni kwa sura ya makundi ambayo takriban hayageuki sura na yangapitiliwa na karne, na Buruuj nayo ndio hayo makundi ya nyota, ni yale yale yanayo pitiwa mbele yake na jua katika mzunguko wake unavyo dhihiri kuizunguka ardhi. Hizo Buruuj ni kama vituo vya jua katika mzunguko wake katika mwaka. Na kila tatu katika hizo huwa ni musimu katika misimu ya mwaka. Nazo kwa kuzitaja moja moja kuanzia msimu wa Rabii' (Spring) unao kuja baina ya siku za baridi na joto, ni kama ifuatavyo kwa majina ya Kiarabu na Kizungu: Alh'aml (Aries, or Ram), Ath-thawr (Taurus), Aljawzaa' (Gemini), Assarat'aan (Cancer), Al Asad (Leo), Assunbulah (Spica), Al Miizaan (Libra), Al-A'qrab (Scorpion), Al Jadyu (Capricorn), Addalwu (Aquarius), Alh'uut (Pisces). Na jua ni moja katika nyota zenye nguvu za kati na kati. Nalo kama nyota zilizo baki lina mwangaza wake mwenyewe wa dhati kwa vituko vya kichembechembe (atomic reaction) vinavyo tokea ndani yake. Basi miale ya jua inayo toka kwenye nguvu hizo huangukia juu ya sayari, na ardhi, na miezi, na vyombo vilio baki vya mbinguni ambavyo havina mwanga wa nafsi yao. Kwa hivyo navyo hutoa nuru. Basi jua ndio Taa inayo waka kwa nafsi yake. Ama mwezi unarudisha nuru ya mwanga wa jua kutokana na uso wake, kama kiyoo. Hakika kwa kusifiwa Jua kuwa ni Taa, na ukasifiwa mwezi kuwa unatoa nuru, ni ishara ya kuwa Jua ndio chanzo cha nguvu, nishati, (T'aaqah, Energy) za joto.

  42. 25:62
    ۝٦٢

    Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru. [62]

    Tanbihi

    [62] Mwingi wa Rehema ndiye aliye ufanya usiku na mchana kufuatana, mmoja nyuma ya mwenzie. Na tumeyapanga haya ili mwenye kutaka akumbuke mpango huu, na ajue hikima ya Mwenyezi Mungu na uweza wake; au apate kushukuru kwa neema hii njema.

  43. 25:63
    ۝٦٣

    Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama! [63]

    Tanbihi

    [63] Na waja wa Mwenyezi Mungu ni wale wanao nyenyekea duniani. Wakitembea katika ardhi wanatembea kwa utulivu na staha. Hali kadhaalika katika mambo yao yote. Na masafihi katika washirikina wakiwasubu (wakiwatukana) wanawaachilia mbali na shani yao, na wanawaambia: Hatuna shani nanyi. Letu sisi ni Assalamu Alaikum!

  44. 25:64
    ۝٦٤

    Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama. [64]

    Tanbihi

    [64] Na wale ambao wanakesha katika ibada na Sala, wakimdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi.

  45. 25:65
    ۝٦٥

    Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi. [65]

    Tanbihi

    [65] Na wale ambao khofu yao inashinda matarajio - nao ndio mwendo wa wachamngu. Basi wanaikhofu adhabu ya Akhera, na hawaachi kumwomba Mwenyezi Mungu awaepusha na adhabu ya Jahannamu. Kwani adhabu yake ikimteremkia mkosefu inamganda, wala haimwachi.

  46. 25:66
    ۝٦٦

    Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya. [66]

    Tanbihi

    [66] Na hakika Jahannamu ni kituo kiovu mno kwa mwenye kutua, na makao maovu kwa mwenye kukaa ndani yake.

  47. 25:67
    ۝٦٧

    Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo. [67]

    Tanbihi

    [67] Na katika alama za waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wana kiasi katika kutumia kwao mali, kwa ajili ya nafsi zao na jamaa zao. Wao hawafanyi ubadhirifu, wala hawabanii matumizi bila ya kiasi. Bali kutoa kwao ni kati kati baina ya hayo.

  48. 25:68
    ۝٦٨

    Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara, [68]

    Tanbihi

    [68] Na katika sifa zao hao waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wameisafia niya Tawhid, na wakatupilia mbali kila athari ya ushirikina katika kumuabudu Mola wao Mlezi. Na wakajizuia kuuwa nafsi aliyo kataza Mwenyezi Mungu kuuliwa, ila ikiwa imefanya uadui basi huuliwa kwa haki. Nao hujitenga mbali na uzinzi, na katika mambo ya starehe hawatendi ila lilio halali tu, ili waepukane na adhabu ya mambo yanayo angamiza. Kwani anaye tenda katika mambo hayo atakuta shari na adhabu.

  49. 25:69
    ۝٦٩

    Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka. [69]

    Tanbihi

    [69] Na Siku ya Kiyama atapata adhabu mardufu kuliko hiyo, na atadumu Motoni kwa udhalili na unyonge.

  50. 25:70
    ۝٧٠

    Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [70]

    Tanbihi

    [70] Lakini mwenye kutubu na madhambi haya na akawa mkweli katika Imani yake, na akafuatiliza hayo kwa ut'iifu na vitendo vyema, hao atawasamehe kwa rehema yake, na atawajaalia bora ya thawabu badala ya maovu yaliyo kwisha tangulia. Na hakika shani ya Mwenyezi Mungu ni kurehemu na kusamehe.

  51. 25:71
    ۝٧١

    Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu. [71]

    Tanbihi

    [71] Na hivyo ndio mambo yetu yendavyo, yaani kuwa mwenye kutubu madhambi, na akaonyesha matokeo yake katika kukubali ut'iifu na kuepuka maasi, basi huyo Mwenyezi Mungu huikubalia toba yake. Na kwa hivyo hurejea kwa Mola wake Mlezi baada ya kumwacha kwake.

  52. 25:72
    ۝٧٢

    Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao. [72]

    Tanbihi

    [72] Na katika khulka za waja wa Mwingi wa Rehema ni kuwa wanajiepusha na kutoa ushahidi wa uwongo, na wakisadifu kukutana na mtu asiye kuwa na kauli au kitendo chema hawashirikiani naye katika hayo, na huacha kufuatana naye.

  53. 25:73
    ۝٧٣

    Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu. [73]

    Tanbihi

    [73] Na katika sifa zao ni kuwa mwenye kuwaidhi akiwapa mawaidha, na akawasomea Aya za Mwenyezi Mungu, humwelekea kumsikiliza, na nyoyo zao zikawaidhika, na macho yao hufunuka. Wala hawawi kama wale ambao wanatapatapa wanapo yasikia, wanapuuza, masikio yao hayapenyi kitu, wala macho yao hayafumbuki.

  54. 25:74
    ۝٧٤

    Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu. [74]

    Tanbihi

    [74] Na wao humwomba Mola wao Mlezi awajaalie wake zao na watoto wao wawe wa kuwapoza moyo kwa vitendo vya kheri, na awajaalie wawe ni waongozi katika kheri ili watu wema wawafuate.

  55. 25:75
    ۝٧٥

    Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu. [75]

    Tanbihi

    [75] Hawa wenye kusifiwa kwa sifa hizi tulizo zitaja ndio waja wa Mwenyezi Mungu wa kweli. Na malipo yao ni makao ya Peponi ya juu, kuwa ni jazaa ya kusubiri kwao juu ya ut'iifu. Na huko Peponi watakuta maamkio, na kusalimiwa.

  56. 25:76
    ۝٧٦

    Wadumu humo - kituo na makao mazuri kabisa. [76]

    Tanbihi

    [76] Na neema zao za Peponi ni za daima, hazikatiki. Pepo ndio kituo na makao mema kabisa.

  57. 25:77
    ۝٧٧

    Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe. [77]

    Tanbihi

    [77] Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu hakutakini nyinyi ila mumuabudu Yeye, na mumwombe Yeye katika mambo yenu, wala msimwombe yeyote mwenginewe. Na kwa hayo ndio kakuumbeni. Lakini makafiri katika nyinyi wameyakanusha waliyo kuja nayo Mitume. Basi adhabu yao itawaganda hao, wala hapana wa kuwaokoa nayo.

  58. Sura Ash-Shu'araa

    سُورَةُ الشعراء
  59. 26:1
    ۝١

    T'aa Siin Miim. (T'.S.M.) . [1]

    Tanbihi

    [1] Harufi hizi na mfano wa hizi ndizo zikakusanyika kuifanya Qur'ani kuwa ni muujiza ulio washinda watu kuiga mfano wake, ijapo kuwa hizo harufi ndizo wanazo zitamka. Basi mwenye kuitilia shaka hii Qur'ani kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu au la, basi na alete mfano wake. Na hatoweza.

  60. 26:2
    ۝٢

    Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. [2]

    Tanbihi

    [2] Maneno haya niliyo kufunulia ni Aya za Kitabu chenye kuweka wazi hukumu zote ziliomo ndani yake.

  61. 26:3
    ۝٣

    Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini. [3]

    Tanbihi

    [3] Ewe Nabii! Hebu jionee huruma nafsi yako. Usijikere kwa kuhuzunukia inadi ya watu wako, na kuto amini kwao.

  62. 26:4
    ۝٤

    Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao. [4]

    Tanbihi

    [4] Sisi tunaweza kuwaletea muujiza wa kuwalazimisha Imani, wat'ii kwa unyenyekevu amri yake, na yatimie unayo yatarajia. Lakini hatuwaletei, kwa sababu mwendo wetu ni kuwaongoza watu waamini bila ya kuwalazimisha, ili isikosekane hikima ya kujaribiwa kwa mitihani, na yanayo kuja baada yake ya thawabu na adhabu.

  63. 26:5
    ۝٥

    Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao. [5]

    Tanbihi

    [5] Wala Mwenyezi Mungu hawaletei watu wako kwa ufunuo wake ya kuwakumbusha Dini ya Haki kuwa ni rehema kwao, ila wao huzua upya upinzani na ukafiri kuukataa. Kwani njia ya uwongofu imekwisha zibwa mbele yao.

  64. 26:6
    ۝٦

    Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. [6]

    Tanbihi

    [6] Hawa hakika wamekadhibisha Haki uliyo ileta, na wakaifanyia maskhara. Lakini wewe wasubirie. Wataona matokeo ya maskhara yao ya kuangamiza.

  65. 26:7
    ۝٧

    Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri? [7]

    Tanbihi

    [7] Hivyo hao wanatenda watendavyo katika ukafiri wao na kukadhibisha kwao wala hawaangalii baadhi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu katika hii hii ardhi? Lau kuwa wanaangalia kwa kuzingatia wangeli ongoka. Hebu wazingatie hii mimea ya kila namna yenye manufaa tunayo itoa Sisi kwenye ardhi, na wala hawezi hayo isipo kuwa Mungu Mmoja Muweza.

  66. 26:8
    ۝٨

    Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. [8]

    Tanbihi

    [8] Hakika katika kutoka kwa hii mimea ni dalili kubwa ya kuwepo Muumba Muweza. Lakini wengi wa watu si wenye kuamini.

  67. 26:9
    ۝٩

    Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [9]

    Tanbihi

    [9] Hakika Mwenye kumiliki mambo yako, na Mwenye kukulinda, ndiye atakaye waadhibu hao wanao kadhibisha, na ndiye Mwenye kuwafadhili Waumini kwa rehema.

  68. 26:10
    ۝١٠

    Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu, [10]

    Tanbihi

    [10] Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha Musa pale Mola wako Mlezi alipo mwita: Ewe Musa! Nenda kwa Utume kwa watu walio dhulumu nafsi zao kwa ukafiri, na wakawadhulumu Wana wa Israili kwa kuwafanya watumwa na kuwauwa watoto wao wanaume.

  69. 26:11
    ۝١١

    Watu wa Firauni. Hawaogopi? [11]

    Tanbihi

    [11] Nenda kwa kaumu ya Firauni; kwani hao wamepita mipaka katika dhulma yao. Ama ajabu ya watu hawa! Hawaogopi nini litalo wafika kwa vitendo vyao hivi, wakatahadhari?

  70. 26:12
    ۝١٢

    Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe. [12]

    Tanbihi

    [12] Musa akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nina khofu wasije kuukataa ujumbe wangu kwa kiburi na inda.

  71. 26:13
    ۝١٣

    Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun. [13]

    Tanbihi

    [13] Na mimi nimejaa dhiki kwa kuwa wataniambia mwongo, na ulimi wangu si mkunjufu wa kuweza kuhojiana nao kama ninavyo penda. Basi mtume Jibril ende kwa ndugu yangu aje kuniunga mkono katika hii kazi yangu.

  72. 26:14
    ۝١٤

    Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa. [14]

    Tanbihi

    [14] Na watu hawa wana kisasi juu yangu. Kwani mimi nilimuuwa mtu katika wao. Basi nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi kabla sijatimiza kazi yangu. Hayo yananizidisha khofu.

  73. 26:15
    ۝١٥

    Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza. [15]

    Tanbihi

    [15] Mwenyezi Mungu akamwambia: Hawatokuuwa. Na kwa mintarafu ya Haruni nimekukubalia ombi lako. Basi nendeni nanyi mmejizatiti na miujiza yetu. Mimi niko pamoja nanyi kwa ulinzi. Nayasikia yanayo jiri baina yenu na Firauni. Nyinyi mtapata ushindi, na kuungwa mkono.

  74. 26:16
    ۝١٦

    Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [16]

    Tanbihi

    [16] Muelekeeni Firauni na mwambieni: Sisi ni Watume wawili tumetumwa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  75. 26:17
    ۝١٧

    Waachilie Wana wa Israili wende nasi. [17]

    Tanbihi

    [17] Anakwambia Mola Mlezi wa walimwengu wote: Waachilie huru Wana wa Israili, wende nasi.

  76. 26:18
    ۝١٨

    (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? [18]

    Tanbihi

    [18] Firauni akamwambia Musa kwa kumsimbulia, naye alimtambua walipo ingia na wakakadimisha Ujumbe wao, kwani alilelewa mle mle katika kasri lake: Hatukukulea sisi ulipo kuwa mtoto? Na ukaishi chini ya ulezi wetu kwa miaka mingi katika umri wako?

  77. 26:19
    ۝١٩

    Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani? [19]

    Tanbihi

    [19] Na ukatenda makosa yako ya jinaya maovu kumuuwa mtu katika kaumu yangu, na ukazikanusha neema zangu nilizo kufanyia, hukuwahifadhi raia zangu, ukaushambulia ungu wetu kwa kudai kuwa wewe ati ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  78. 26:20
    ۝٢٠

    (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea. [20]

    Tanbihi

    [20] Musa akasema: Niliyafanya uliyo yataja kwa kutojua yanayo faa kutambulikana kwa akili nayo ni jambo la kuuwa. Basi hapana masimbulizi juu yangu.

  79. 26:21
    ۝٢١

    Basi nilikukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi, akanitunukia hukumu, na akanijaali niwe miongoni mwa Mitume. [21]

    Tanbihi

    [21] Nikakukimbieni nilipo khofu kuwa mtakuja niuwa kwa jinaya hii ambayo sikuukusudia. Mola wangu Mlezi akanitunukia fahamu na ilimu, kwa fadhila zake na neema zake, na akanifanya mmoja katika Mitume.

  80. 26:22
    ۝٢٢

    Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili? [22]

    Tanbihi

    [22] Musa akaashiria sifa katika sifa ovu kabisa za Firauni, nayo ni kuwa kawafanya watumwa Wana wa Israili, na akiwauwa watoto wao wanaume. Na akakataa kukuita kule kulelewa kwake katika jumba la Firauni kuwa ni neema, kwani yaliyo sabibisha hayo ni yale aliyo kwisha yataja, ndio yeye alitupwa mtoni aokoke asiuliwe. Akaishia kwenye jumba la Firauni. Na lau kuwa si hivyo basi angeli lelewa na wazazi wake.

  81. 26:23
    ۝٢٣

    Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote? [23]

    Tanbihi

    [23] Firauni akasema: Na nini hizo sifa za Mola Mlezi wa walimwengu wote ambaye unakithiri kumtaja, na wewe unadai kuwa ni Mtume wake, na hali sisi hatujui lolote khabari zake?

  82. 26:24
    ۝٢٤

    Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini. [24]

    Tanbihi

    [24] Musa akasema: Yeye huyo ndiye Mwenye kuzimiliki mbingu na ardhi na kila kilio baina yao. Ikiwa nyinyi mna yakini ya ukweli wa jawabu hii basi mtanafiika, na mtaongoka, na mtajua kuwa ufalme wa Firauni wa kujidai haufui dafu mbele ya Ufalme wake Mwenyezi Mungu. Kwani ufalme wa Firauni haupindukii hata eneo moja katika hii dunia.

  83. 26:25
    ۝٢٥

    (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi? [25]

    Tanbihi

    [25] Firauni kuonyesha mastaajabu kwa wale walio mzunguka kwa kuwa Musa katika jawabu yake alipo mtaja Mola wake Mlezi na akadhukuru Ufalme wake hakuugusia hata kidogo ufalme wa Firauni, alisema: Mwayasikiaje maneno ya Musa?

  84. 26:26
    ۝٢٦

    (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza. [26]

    Tanbihi

    [26] Musa akiendelea na usemi wake bila ya kujali hasira za Firauni na uchafu wa maneno yake, akasema: Ndiye huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote, aliye kuumbeni nyinyi na baba zenu walio tangulia. Na miongoni mwa hao walikuwako walio dai ungu kama unavyo dai wewe. Na wao wameteketea. Na wewe utateketea, na hayo unayo yadai yatapotelea mbali. Kwani Mungu wa kweli hafi.

  85. 26:27
    ۝٢٧

    (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu. [27]

    Tanbihi

    [27] Firauni akwaambia watu wake yale yanayo mtibuwa roho na kumghadhibisha, akautaja Utume wa Musa ni kwao wao, wala si kwake yeye, na akambandikiza wazimu, kwa kuwa ati akiulizwa kitu hujibu kingine, na anamsifu Mola Mlezi kwa sifa za kiajabu ajabu. Na kwa hivyo Firauni anawahimiza wamkadhibishe.

  86. 26:28
    ۝٢٨

    . (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini. [28]

    Tanbihi

    [28] Musa akasema: Ikiwa nyinyi mna akili, basi uaminini Ujumbe wangu. Kwani kuchomoza jua na kuchwa kwake kwa mpango madhubuti ni dalili wazi ya Mwenye kuumba. Kwa hivyo basi ni nyinyi ndio mnastahiki kuambiwa wendawazimu.

  87. 26:29
    ۝٢٩

    (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani. [29]

    Tanbihi

    [29] Firauni akamwambia Musa: Ukimfuata mungu yeyote badala yangu mimi, utakuwa mmoja katika wanao ijua hali yao mbaya katika magereza yangu. Na yeye Firauni kaangukia kitisho hichi baada ya kushindwa kuondoa athari za kazi za Muumbaji.

  88. 26:30
    ۝٣٠

    Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi? [30]

    Tanbihi

    [30] Musa akasema kwa upole kwa kutumai asaa akaamini: Utanitia gerezani hata nikikuletea ushahidi mkubwa wa ukweli wa haya niyasemayo?

  89. 26:31
    ۝٣١

    Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli. [31]

    Tanbihi

    [31] Firauni akasema: Ulete ushahidi utao onyesha Unabii wako kama wewe kweli unasema kweli katika wito wako. Kasema hayo kwa tamaa ya kuwa huenda akapata kipengee cha udhaifu katika hoja zake.

  90. 26:32
    ۝٣٢

    Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. [32]

    Tanbihi

    [32] Musa akaitupa fimbo yake mbele yao. Ikageuka nyoka kweli kweli, si kitu cha uwongo cha uchawi kinacho fanana na nyoka.

  91. 26:33
    ۝٣٣

    Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao. [33]

    Tanbihi

    [33] Musa akautoa mkono wake kutoka mfukoni mwake. Hiyo ni Ishara ya pili. Nao ukawa mweupe, bila ya maradhi, hata wakashangaa watazamaji kwa kumetuka kwake.

  92. 26:34
    ۝٣٤

    (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu. [34]

    Tanbihi

    [34] Firauni akawaambia watu wake: Hakika Musa ni mchawi bingwa katika uchawi wake. Kasema hayo kwa kuchelea watu wake wasiifuate Haki waliyo iona kwa Musa.

  93. 26:35
    ۝٣٥

    Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani? [35]

    Tanbihi

    [35] Tena Firauni akasema: Mchawi huyu anataka kunifanyia kahari apate kukutoeni katika hii nchi yenu. Na haya ni uchochezi dhidi ya Musa, kwani katika la dhiki mno katika hayo yaliyo dhiki ni mtu kuiacha nchi yake, na khasa ikiwa kwa kahari. Naye akataka mawazo ya wale walio kuwa wanamuabudu. Kasahau ungu wake kwa nguvu za Ishara za Musa.

  94. 26:36
    ۝٣٦

    Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo. [36]

    Tanbihi

    [36] Watu wake wakamwambia: Akhirisha kukata shauri yao hawa, na uwatume askari wende wawakusanye wachawi katika raia zako. Kwani uchawi hupingwa kwa uchawi.

  95. 26:37
    ۝٣٧

    Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu. [37]

    Tanbihi

    [37] Watakuletea wengi, na wote wamebobea kwa uchawi, na wamemshinda Musa kwa ufundi na ustadi. Wamekusudia kwa haya kumpunguzia dukuduku lake Firauni.

  96. 26:38
    ۝٣٨

    Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu. [38]

    Tanbihi

    [38] Wakakusanywa wachawi kutoka kila upande wa nchi. Wakawekewa wakati wa mchana siku ya Sikukuu kukutana na Musa.

  97. 26:39
    ۝٣٩

    Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika? [39]

    Tanbihi

    [39] Na watu wakahimizana kuhudhuria siku hiyo waone ramsa wakiambizana: Mtakusanyika? Yaani ndio: Mkusanyike!

  98. 26:40
    ۝٤٠

    Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda. [40]

    Tanbihi

    [40] Wakatangaza matarajio yao ya kushinda wachawi, ili wapate kuthibiti katika dini yao, na pia ndio kampeni ya nguvu na juhudi apate kushindwa Musa.

  99. 26:41
    ۝٤١

    Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda? [41]

    Tanbihi

    [41] Walipo kuja wachawi kwa Firauni walimwambia: Je! Tutapata kwako ujira mkubwa pindi tukishinda?

  100. 26:42
    ۝٤٢

    Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele. [42]

    Tanbihi

    [42] Firauni akasema: Naam, mtapata mnacho kisema. Na juu ya huo ujira mkubwa mtakuwa watu wa karibu kwangu, watu wa cheo na madaraka.

  101. 26:43
    ۝٤٣

    Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa. [43]

    Tanbihi

    [43] Ulipo fika wakati ulio wekwa katika siku iliyo pangwa Musa aliwaambia wachawi: Tupeni huo uchawi mnao taka kuutupa.

  102. 26:44
    ۝٤٤

    Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda. [44]

    Tanbihi

    [44] Wakazitupa kamba zao na fimbo zao, na watu wakazugwa wakaona kama ni nyoka wanakwenda. Wakaapa kwa utukufu wa Firauni na nguvu zake hapana shaka hawa leo watashinda

  103. 26:45
    ۝٤٥

    Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua. [45]

    Tanbihi

    [45] Musa tena akatupa fimbo yake. Mara ikawa joka kubwa likaingia kuvimeza vile walivyo vizua kwa uchawi, navyo ni kamba na fimbo, wakidanganya kuwa ni nyoka wanao kwenda.

  104. 26:46
    ۝٤٦

    Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. [46]

    Tanbihi

    [46] Wachawi wakaanguka wakasujudu kumsujudia Mwenyezi Mungu, walipo yakinika kuwa mambo ya Musa si uchawi.

  105. 26:47
    ۝٤٧

    Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote. [47]

    Tanbihi

    [47] Wakasema ili kutia mkazo kule kusujudu kwao kwa kauli yao: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  106. 26:48
    ۝٤٨

    Mola Mlezi wa Musa na Harun. [48]

    Tanbihi

    [48] Na wakabainisha kuwa hakika Mola Mlezi wa walimwengu wote walio muamini ndiye: Mola Mlezi wa Musa na Harun.

  107. 26:49
    ۝٤٩

    (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote. [49]

    Tanbihi

    [49] Firauni kwa kukasarika kuwa wale wachawi wamemuamini Musa bila ya yeye kuwapa ruhusa, aliwatishia ya kwamba yeye ndiye mwalimu wao aliye wafunza fani za uchawi, na watakuja jua adhabu itakayo wateremkia. Akawaambia: Nitakata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, nitakata wa kulia huu kwa wa kushoto huu, na kinyume cha hayo. Na nyote nitakutundikeni juu ya misalaba.

  108. 26:50
    ۝٥٠

    Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. [50]

    Tanbihi

    [50] Wachawi wakasema: Hapana la kutudhuru sisi kwa adhabu unazo tutishia, kwani sisi ni wenye kurejea kwenye malipo ya Mola wetu Mlezi. Na Yeye ndiye mbora wa kulipa na mbora wa kuadhibu.

  109. 26:51
    ۝٥١

    Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini. [51]

    Tanbihi

    [51] Hakika sisi tunataraji Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu tuliyo yafanya zamani, kwa kuwa sisi ndio wa mwanzo wa Waumini katika kaumu yako.

  110. 26:52
    ۝٥٢

    Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa. [52]

    Tanbihi

    [52] Na Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Musa a.s. atoke usiku usiku pamoja na Waumini miongoni mwa Wana wa Israili, ilipo kuwa tena haiwi kumsubirisha Musa. Mpango ukawa wa makundi mawili kwamba atangulie Musa na kaumu yake, na Firauni afuatie na kaumu yake, mpaka waingie katika maingilio ya njia ya baharini, na Mwenyezi Mungu awateketeze.

  111. 26:53
    ۝٥٣

    Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo. [53]

    Tanbihi

    [53] Firauni akawatuma askari wake katika miji ya mamlaka yake, wawakusanye wenye maguvu katika kaumu yake, alipo jua kuwa Musa kesha toka na Wana wa Israili, ili awazuie lile walilo kusudia.

  112. 26:54
    ۝٥٤

    (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo. [54]

    Tanbihi

    [54] Firauni akasema: Hakika hawa Wana wa Israili walio kimbia na Musa ni taifa dogo kwa nguvu zao. Idadi yao ni chache. Anasema hayo kutia mori katika nyoyo za askari wake.

  113. 26:55
    ۝٥٥

    Nao wanatuudhi. [55]

    Tanbihi

    [55] Na wao juu ya hivyo, wanatutibua roho kwa kuvunja amri yetu na kutoka bila ya idhini yetu.

  114. 26:56
    ۝٥٦

    Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari. [56]

    Tanbihi

    [56] Na sisi ni wengi. Miongoni mwa ada zetu ni kuchukua hadhari, na kuwa macho, na kupania.

  115. 26:57
    ۝٥٧

    Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, [57]

    Tanbihi

    [57] Tukawatoa Firauni na askari wake kwenye nchi yao iliyo fanana na mabustani yapitiwayo na mito kati yao, wakaangamia kwa kujitenga kwao na Haki, na kuchochewa kutaka kumfuatia Musa, kama ilivyo kuja katika Aya tatu zilizo tangulia.

  116. 26:58
    ۝٥٨

    Na makhazina, na vyeo vya hishima, [58]

    Tanbihi

    [58] Tukawatoa, kadhaalika, kwenye khazina za dhahabu na fedha, na majumba waliyo kuwa wakiyakalia, wakineemeka kwa uzuri wake na ubora wa starehe zake.

  117. 26:59
    ۝٥٩

    Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili. [59]

    Tanbihi

    [59] Ni kutoka kama huku kwa ajabu tulivyo kueleza ndivyo tulivyo watoa, na tukawapa ufalme huo na kila namna ya neema zilizo kuwamo Wana wa Israili, baada ya kuwa masikini hawana mbele wala nyuma.

  118. 26:60
    ۝٦٠

    Basi wakawafuata lilipo chomoza jua. [60]

    Tanbihi

    [60] Firauni na watu wake wakakaza mwendo ili wapate kuwawahi Wana wa Israili. Wakawakuta wakati wa kuchomoza jua.

  119. 26:61
    ۝٦١

    Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! [61]

    Tanbihi

    [61] Walipo onana makundi mawili, watu wa Musa walisema: Hakika Firauni na watu wake watatupata. Basi tutaangamia.

  120. 26:62
    ۝٦٢

    (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa! [62]

    Tanbihi

    [62] Musa akasema: Hakika mimi ninao uangalizi wa Mwenyezi Mungu unao nifuata kwa kunihifadhi. Na Yeye ataniongoza kwenye Njia ya uwokovu. Amesema hayo ili awatuze kuwa watasalimika, na iwe mbali na mawazo yao fikra ya kutisha kwamba takuja patikana. .

  121. 26:63
    ۝٦٣

    Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa. [63]

    Tanbihi

    [63] Tukamuamrisha Musa kwa wahyi, ufunuo, aipige bahari kwa fimbo yake. Ikapasuka bahari njia kumi na mbili kwa mujibu wa idadi ya mataifa ya Wana wa Israili. Kila njia katika hizo njia ilikuwa na kizuizi cha maji yaliyo nyanyuka kama mlima ulio simama imara.

  122. 26:64
    ۝٦٤

    Na tukawajongeza hapo wale wengine. [64]

    Tanbihi

    [64] Tukawajongeza Firauni na kaumu yake mpaka wakaingia kwenye zile njia nyuma ya Musa na kaumu yake.

  123. 26:65
    ۝٦٥

    Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote. [65]

    Tanbihi

    [65] Tukamwokoa Musa na walio kuwa pamoja naye kwa hifadhi ya bahari nayo imeshikamana, mpaka wakamalizika kuvuka.

  124. 26:66
    ۝٦٦

    Kisha tukawazamisha hao wengine. [66]

    Tanbihi

    [66] Kisha tukamzamisha Firauni pamoja na walio kuwa pamoja naye kwa kuwafudikiza kwa maji pale walipo wafuata.

  125. 26:67
    ۝٦٧

    Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini. [67]

    Tanbihi

    [67] Hakika katika vituko hivi vya ajabu vya kiungu pana funzo la kuzingatia kwa atakaye kunafiika. Lakini watu wengi si wenye kusadiki.

  126. 26:68
    ۝٦٨

    Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [68]

    Tanbihi

    [68] Hakika Muumba wako na Mlezi wako ndiye huyo Mwenye nguvu katika kuwaadhibu wanao kanusha, Mwenye kuwaneemesha kwa rehema Waumini.

  127. 26:69
    ۝٦٩

    Na wasomee khabari za Ibrahim. [69]

    Tanbihi

    [69] Ewe Mtume! Na wasomee makafiri hadithi ya Ibrahim , Alayhi Ssalaam.

  128. 26:70
    ۝٧٠

    Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini? [70]

    Tanbihi

    [70] Alipo mwambia baba yake: Mnaabudu kitu gani hichi, ambacho hakifai kuabudiwa? Anakusudia kwa hayo kuyakebehi masanamu.

  129. 26:71
    ۝٧١

    Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea. [71]

    Tanbihi

    [71] Wakasema kujibu kwa njia ya kujitapa: Tunaabudu masanamu, nasi tunadumu daima dawamu tukiyaabudu, kwa kuyaadhimisha na kuyatukuza!

  130. 26:72
    ۝٧٢

    Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? [72]

    Tanbihi

    [72] Ibrahim akasema: Kwani yanasikia madua yenu? Au yanakuitikieni mnapo yaomba? Kwa hayo anakusudia kuwanabihisha upotovu wa mwendo wao.

  131. 26:73
    ۝٧٣

    Au yanakufaeni, au yanakudhuruni? [73]

    Tanbihi

    [73] Au yanakuleteeni manufaa mnapo yat'ii? Au yanakupatilizeni kwa madhara mkiyaasi?

  132. 26:74
    ۝٧٤

    Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo. [74]

    Tanbihi

    [74] Wakasema: Hawafanyi lolote katika hayo. Lakini sisi tumewakuta baba zetu wakiyaabudu mfano wa ibada yetu. Basi sisi tukawafwata kwa waliyo kuwa wakiyafanya.

  133. 26:75
    ۝٧٥

    Je! Mmewaona hawa mnao waabudu- [75]

    Tanbihi

    [75] Ibrahim akasema kwa kuwasusuika: Je! Mlifikiri hata mkalijua jambo lolote lilio kupelekeeni kudumu na kuyaabudu hayo masanamu?

  134. 26:76
    ۝٧٦

    Nyinyi na baba zenu wa zamani? [76]

    Tanbihi

    [76] Nyinyi na baba zenu wa zamani - ati haya yanastahiki kuabudiwa au la? Lau mngeli zingatia mngeli jua kuwa hakika nyinyi mko katika upotovu ulio wazi.

  135. 26:77
    ۝٧٧

    Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [77]

    Tanbihi

    [77] Kwani hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maaadui kwangu mimi na kwenu. Basi mimi siwaabudu hao. Lakini ninaye muabudu na najijongeza kwake ni Muumba wa walimwengu wote, na Mwenye kumiliki mambo yao, na Mwenye kuwalinda.

  136. 26:78
    ۝٧٨

    Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa, [78]

    Tanbihi

    [78] Ambae ndiye aliye nizua kabla sijawa chochote akaniumba kwa bora ya umbo, na akanitunukia uwongofu wa kunifikishia kwenye mafanikio yangu ya duniani na Akhera.

  137. 26:79
    ۝٧٩

    Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. [79]

    Tanbihi

    [79] Na Yeye ndiye aliye nineemesha kwa vyakula na vinywaji, na akaniwezesha kuvipata na kunafiika kwavyo, ili kuhifadhi uhai wangu.

  138. 26:80
    ۝٨٠

    Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha. [80]

    Tanbihi

    [80] Na yakinishukia maradhi ni Yeye ndiye anaye niponesha, kwa kunisahilishia sababu za kupona na kuniwezesha kuzipata.

  139. 26:81
    ۝٨١

    Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha. [81]

    Tanbihi

    [81] Na Yeye ndiye atanifisha ikifika ajali yangu, na tena atanihuisha mara nyengine kwa ajili ya hisabu na malipo.

  140. 26:82
    ۝٨٢

    Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo. [82]

    Tanbihi

    [82] Na Yeye ndiye ninaye mtumai kunighufiria na kuyasemehe makosa yangu madogo madogo ya kujikwaa duniani, utapo fika wakati wa hisabu.

  141. 26:83
    ۝٨٣

    Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema. [83]

    Tanbihi

    [83] Ibrahim a.s. akasema kwa kuomba: Mola wangu Mlezi! Nitunukie ukamilifu wa ilimu na vitendo, ili nipate kustahili kuubeba Ujumbe wako na hukummu kwa waja wako, na niwezeshe niungane pamoja na kundi la watendao wema.

  142. 26:84
    ۝٨٤

    Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye. [84]

    Tanbihi

    [84] Na nijaalie nipate sifa nzuri na kumbusho jema kwa kaumu zitazo kuja baada yangu, mabaki yake yasalie mpaka Siku ya Kiyama.

  143. 26:85
    ۝٨٥

    Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema. [85]

    Tanbihi

    [85] Na nijaalie katika waja wako ulio watunukia neema za Peponi, kuwa ni malipo kwa sababu ya Imani yao kukuamini Wewe, na ibada yao kukuabudu Wewe.

  144. 26:86
    ۝٨٦

    Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu. [86]

    Tanbihi

    [86] Na mjaalie baba yangu astahili msamaha kwa kumwezesha kuwa Muislamu. Na yeye alikuwa kamuahidi kusilimu siku alio achana naye, kwani yeye huyo baba alikuwa ameitupa kando njia ya uwongofu na uwongozi.

  145. 26:87
    ۝٨٧

    Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa. [87]

    Tanbihi

    [87] Wala usinitie aibu au hizaya mbele ya watu, Siku watapo tolewa makaburini kwa ajili ya hisabu na malipo.

  146. 26:88
    ۝٨٨

    Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana. [88]

    Tanbihi

    [88] Siku ambayo hapana mtu ataye nafiika kwa mali ayatoe, au kwa wana wamsaidie.

  147. 26:89
    ۝٨٩

    Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi. [89]

    Tanbihi

    [89] Isipo kuwa aliye kuwa Muumini, na akamkabili Mwenyezi Mungu na moyo ulio mzima, hauna maradhi ya ukafiri, na unaafiki, na riya (kujionesha).

  148. 26:90
    ۝٩٠

    Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu. [90]

    Tanbihi

    [90] Na Pepo itajongezwa, na itakaribishwa pahala pa watu wema. Basi wataiendea wale walio jikinga na ukafiri na maasi, na wakaikubali Imani na ut'iifu duniani.

  149. 26:91
    ۝٩١

    Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu. [91]

    Tanbihi

    [91] Na Moto utaletwa mbele ya walio iacha Dini ya Haki, mpaka ndimi zake zikaribie kuwanyakua, nao watakuwa majutoni.

  150. 26:92
    ۝٩٢

    Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu [92]

    Tanbihi

    [92] Wakaambiwa kwa kuwatahayarisha: Iko wapi hiyo miungu yenu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu?

  151. 26:93
    ۝٩٣

    Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe? [93]

    Tanbihi

    [93] Badala ya Mwenyezi Mungu, na mnadai kuwa ati ndio itakuombeeni hii leo? Je! Inakufaeni kitu kwa kukunusuruni, au hata inajifaa wenyewe kujisaidia? Hapana lolote. Kwani wao na miungu yao ni kuni za Moto.

  152. 26:94
    ۝٩٤

    Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu, [94]

    Tanbihi

    [94] Watatumbukizwa katika Jahannamu kifudifudi, wakipinduliwa pinduliwa mpaka waishie ndani kabisa shimoni, wao na walio wapoteza na wakawatia katika madhambi na upotovu.

  153. 26:95
    ۝٩٥

    Na majeshi ya Ibilisi yote. [95]

    Tanbihi

    [95] Na pamoja nao watakuwapo wasaidizi wa Ibilisi walio kuwa wakiwapambia shari na madhambi, au wale watu na majini walio wakiwafuata katika maasi.

  154. 26:96
    ۝٩٦

    Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo: [96]

    Tanbihi

    [96] Watasema huku wakiungama makosa yao, na huku wanagombana na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu:

  155. 26:97
    ۝٩٧

    Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri, [97]

    Tanbihi

    [97] Wallahi! Hakika sisi tulikuwa katika dunia yetu tumepotea kweli, na wajinga wa kutupwa, na tumeiacha Haki ambayo haina kificho ndani yake.

  156. 26:98
    ۝٩٨

    Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. [98]

    Tanbihi

    [98] Pale tulipo kufanyeni nyinyi tulio kuabuduni badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ati ni sawa sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote katika kustahiki kuabudiwa, juu ya kuwa hamjiwezi wala hamfai kwa lolote.

  157. 26:99
    ۝٩٩

    Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. [99]

    Tanbihi

    [99] Wala hapana walio tutia katika hilaki hii ila wakosefu walio tupotoa tukaiwacha Njia Iliyo Nyooka.

  158. 26:100
    ۝١٠٠

    Basi hatuna waombezi. [100]

    Tanbihi

    [100] Basi hapana wa kuombwa akaja kutuvua na adhabu hii kama tulivyo dhania pale kwanza.

  159. 26:101
    ۝١٠١

    Wala rafiki wa dhati. [101]

    Tanbihi

    [101] Wala hapana rafiki wa kuwaonea uchungu kwa hali yao, licha ya kuwaokoa.

  160. 26:102
    ۝١٠٢

    Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini. [102]

    Tanbihi

    [102] Basi hapo ndio wanajitamania nafsi zao lau wangeli rejea duniani wapate kuwa Waumini ili waokoke.

  161. 26:103
    ۝١٠٣

    Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. [103]

    Tanbihi

    [103] Na hakika katika khabari za Ibrahim zilizo tajwa yapo mawaidha na mazingatio kwa mwenye kutaka mawaidha na akazingatia. Na wala si wengi katika watu wako wanao somewa khabari hizi wenye kuitikia wito wako.

  162. 26:104
    ۝١٠٤

    Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [104]

    Tanbihi

    [104] Na hakika hapana shaka Mola wako Mlezi ni Muweza wa kuwaadhibu wanao kadhibisha, naye ni Mfadhili wa watu wema kwa neema nyingi.

  163. 26:105
    ۝١٠٥

    Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume. [105]

    Tanbihi

    [105] Na Mwenyezi Mungu ametaja khabari za Nuhu kwa kauli yake: Kaumu ya Nuhu iliukanusha Utume wake, wakamrudishia mwenyewe. Kwa kitendo hicho ikawa wamewakadhibisha Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wito wao ni mmoja katika asli yake na lengo lake.

  164. 26:106
    ۝١٠٦

    Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?. [106]

    Tanbihi

    [106] Waliukanusha Utume huu pale alipo waambia ndugu yao Nuhu - ndugu kwa makhusiano ya nasaba si kwa Dini - akiwahadharisha: Hamumchi Mwenyezi Mungu, mkaacha kuabudu wenginewe?

  165. 26:107
    ۝١٠٧

    Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. [107]

    Tanbihi

    [107] Hakika mimi ni Mtume, nimetumwa kwenu nikuongoeni kwenye Njia ya wongofu, na ni muaminifu wa kufikisha huu Ujumbe.

  166. 26:108
    ۝١٠٨

    Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [108]

    Tanbihi

    [108] Basi mkhofuni Mwenyezi Mungu, na fuateni amri yangu katika hayo ninayo kuitieni kwayo ya kumuamini Mwenyezi Mungu wa pekee na kumt'ii.

  167. 26:109
    ۝١٠٩

    Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [109]

    Tanbihi

    [109] Na wala sitaki kwenu ujira kwa ajili ya ninayo kupeni ya nasaha na wito. Na sina malipo ila kwa Mwenye kuwaumba viumbe wote, Aliye miliki mambo yao.

  168. 26:110
    ۝١١٠

    Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [110]

    Tanbihi

    [110] Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na fuateni ninayo kuamrisheni.

  169. 26:111
    ۝١١١

    Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?. [111]

    Tanbihi

    [111] Watu wa Nuhu, huku wakiukataa wito wake, walisema: Hatutokuwa na imani nawe maadamu wanakufuata watu duni kabisa, wasio kuwa na hadhi wala mali.

  170. 26:112
    ۝١١٢

    Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?. [112]

    Tanbihi

    [112] Nuhu akasema: Kitu gani cha kunijuvya uchache wa hadhi yao na mali yao? Nikitakacho mimi kwao ni Imani yao bila ya kutafuta kuzijua kazi zao.

  171. 26:113
    ۝١١٣

    Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!. [113]

    Tanbihi

    [113] Hapana wa kuwalipa kwa vitendo vyao na kazi zao ila Mola wangu Mlezi; kwani Yeye ndiye anaye yajua vyema ya undani wao. Kama nyinyi ni watu watambuzi mngeli tambua hayo.

  172. 26:114
    ۝١١٤

    Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini. [114]

    Tanbihi

    [114] Wala mimi siye wa kuwafukuza watu wanao uamini wito wangu vyovyote itavyo kuwa hali yao ya ufakiri au utajiri, kwa sababu ati ya kukubalieni nyinyi kwa mtakalo ili ndio mpate kuniamini.

  173. 26:115
    ۝١١٥

    Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri. [115]

    Tanbihi

    [115] Mimi si chochote ila ni Mtume niliye toka kwa Mwenyezi Mungu kuwaonya walio wajibikiwa kwa onyo lilio wazi, kwa ushahidi wa kutenganisha baina ya kweli na uwongo, bila ya farka yoyote baina ya mtukufu na mnyonge. Basi vipi itanifalia mimi kuwafukuza Waumini kwa sababu ya ufakiri wao?

  174. 26:116
    ۝١١٦

    Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe. [116]

    Tanbihi

    [116] Wakasema: Ewe Nuhu! Ikiwa hutoacha huu wito wako basi jua yakini tutakupopoa mawe. Yaani wanakusudia kwa haya kumtishia kumuuwa.

  175. 26:117
    ۝١١٧

    Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha. [117]

    Tanbihi

    [117] Nuhu kuonyesha kushikilia watu wake kuukadhibisha wito wake, alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha! Kuthibitisha kuwa wanastahiki maapizo yake.

  176. 26:118
    ۝١١٨

    Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini. [118]

    Tanbihi

    [118] Basi tuhukumie baina yangu na wao, kwa hukumu ya kuwaangamiza wanao pinga Upweke wako, na wakamkadhibisha Mtume wako! Na niokoe mimi na Waumini walio pamoja nami na adhabu ya uasi wao.

  177. 26:119
    ۝١١٩

    Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni. [119]

    Tanbihi

    [119] Ndio hivyo tukamwokoa yeye pamoja na walio amini katika safina iliyo pakia pomoni wao hao pamoja na mahitaji yao, kwa kuitikia dua yake.

  178. 26:120
    ۝١٢٠

    Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia. [120]

    Tanbihi

    [120] Baada ya kuokoka kwa Nuhu na walio amini, Mwenyezi Mungu aliwazamisha walio baki katika kaumu ya Nuhu walio kuwa hawakuamini.

  179. 26:121
    ۝١٢١

    Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [121]

    Tanbihi

    [121] Hakika katika yaliyo simuliwa na Qur'ani juu ya khabari za Nuhu ni hoja ya kuthibitisha ukweli wa Mitume na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na katika watu walio somewa hadithi hizi si wengi walio amini.

  180. 26:122
    ۝١٢٢

    Kina A'd waliwakanusha Mitume. [122]

    Tanbihi

    [122] Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu za kumuadhibu kila jabari mwenye inda, Mwenye kuwaneemesha wachamngu kwa kila namna ya fadhila.

  181. 26:123
    ۝١٢٣

    Kina A'd waliwakanusha Mitume. [123]

    Tanbihi

    [123] Kabila ya A'di ilimkanusha Mtume wao Hud a.s. Na kwa hivyo wakawa ndio wamewakadhibisha Mitume wote, kwa kuwa wito wao ni mmoja katika asli yake na lengo lake.

  182. 26:124
    ۝١٢٤

    Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu? [124]

    Tanbihi

    [124] Alipo waambia ndugu yao Hud: Hamumwogopi Mwenyezi Mungu, mkamsafia ibada?

  183. 26:125
    ۝١٢٥

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [125]

    Tanbihi

    [125] Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili nikuongoeni mfuate uwongozi, na ni mwenye kuulinda ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Naufikisha ujumbe huo kama alivyo niamrisha Mola wangu Mlezi.

  184. 26:126
    ۝١٢٦

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. [126]

    Tanbihi

    [126] Basi ifuateni amri ya Mwenyezi Mungu. Na ikhofuni adhabu yake. Na t'iini ninayo kuamrisheni yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu.

  185. 26:127
    ۝١٢٧

    Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [127]

    Tanbihi

    [127] Wala kwa hii nasaha yangu na uwongozi wangu sitaki kwenu ujira. Sina malipo isipo kuwa kwa Muumba wa viumbe vyote.

  186. 26:128
    ۝١٢٨

    Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi? [128]

    Tanbihi

    [128] Je! Mnasimamisha juu ya kila pahala palipo nyanyuka katika nchi jengo refu kwa ajili ya kujifakhirisha, na mnakutana humo kwa mambo ya upuuzi na fisadi? Mwenyezi Mungu Subhanahu anataka kwa haya kuwazindua watende yatakayo wanufaisha, na anawatahayarisha kwa kuacha kwao Imani na vitendo vyema.

  187. 26:129
    ۝١٢٩

    Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! [129]

    Tanbihi

    [129] Na mnajenga majumba ya fakhari na imara, na mahodhi ya maji, kwa kutaraji kuishi milele katika dunia hii, kama kwamba hamtakufa.

  188. 26:130
    ۝١٣٠

    Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. [130]

    Tanbihi

    [130] Na mnapo ingia kutesa, mnapita kiasi katika uasi na uvamizi wa jeuri, mnauwa, na mnapiga kwa chuki bila ya huruma.

  189. 26:131
    ۝١٣١

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. [131]

    Tanbihi

    [131] Mwogopeni Mwenyezi Mungu katika kutumia nguvu, Na fuateni amri yangu katika ninayo kuitieni. Kwani hayo hakika ndiyo yatakayo kukufaeni na ndiyo yatakayo dumu zaidi.

  190. 26:132
    ۝١٣٢

    Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua. [132]

    Tanbihi

    [132] Na tahadharini na ghadhabu za Mwenyezi Mungu aliye kukunjulieni neema zake, kwa mnayo yajua yaliyo mbele yenu ya vipawa vyake vya namna mbali mbali.

  191. 26:133
    ۝١٣٣

    Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. [133]

    Tanbihi

    [133] Kama alivyo kupeni mifugo kama ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi, na wana wenye nguvu, wakukulindieni mifugo yenu, na kukusaidieni katika shida za maisha.

  192. 26:134
    ۝١٣٤

    Na mabustani na chemchem. [134]

    Tanbihi

    [134] Na mabustani yenye matunda, na chemchem zenye kutiririka maji mnayo yahitajia.

  193. 26:135
    ۝١٣٥

    Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa. [135]

    Tanbihi

    [135] Mimi nina khofu asije Mwenyezi Mungu akakuteremshieni adhabu kali hapa duniani, na Akhera akakutieni katika Moto wa Jahannamu kwa sababu ya ujabari wenu na starehe alizo kustarehesheni Mwenyezi Mungu.

  194. 26:136
    ۝١٣٦

    Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha. [136]

    Tanbihi

    [136] Wakasema kwa kumkejeli: Ni sawa kwetu, ukitupa waadhi na kutuonya au ukawa si katika wenye kutoa waadhi.

  195. 26:137
    ۝١٣٧

    Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani. [137]

    Tanbihi

    [137] Haya uliyo tuletea si lolote ila ni uwongo na upotovu wa watu wa zamani. Wao wamezoea kuzua kama hivyo. Kwa hivyo sisi hatutaacha tuliyo kuwa nayo.

  196. 26:138
    ۝١٣٨

    Wala sisi hatutaadhibiwa. [138]

    Tanbihi

    [138] Wala sisi hatutaadhibiwa kwa vitendo tuvitendavyo.

  197. 26:139
    ۝١٣٩

    Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [139]

    Tanbihi

    [139] Basi wakaendelea kushikilia kumkanusha. Mwenyezi Mungu akawafanyia haraka kuwateketeza. Hakika katika hayo aliyo wateremshia Mwenyezi Mungu kina A'di kwa kuwa ni malipo kwa ukanushi wao, ni hoja inayo juulisha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na si wengi katika wanao somewa khabari za A'adi walio Waumini.

  198. 26:140
    ۝١٤٠

    Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [140]

    Tanbihi

    [140] Na Mola wako Mlezi ndiye Mtenda nguvu wa kuwashinda hao majabari, Mwenye kuwarehemu Waumini.

  199. 26:141
    ۝١٤١

    Kina Thamud waliwakanusha Mitume. [141]

    Tanbihi

    [141] Kabila ya Thamud ilimkanusha Swaleh katika Ujumbe wake na wito wake, na kwa hivyo ikawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa asli ya Ujumbe ni moja, na lengo ni moja.

  200. 26:142
    ۝١٤٢

    Alipo waambia ndugu yao Swaleh: Je! Hamumchimngu? [142]

    Tanbihi

    [142] Ewe Mtume! Watajie watu wako, wakati ule kina Thamud walipo ambiwa na ndugu yao kwa uzao na uwananchi, si kwa dini, Swaleh: Hamumwogopi Mwenyezi Mungu, mkamuaabudu Yeye tu?

  201. 26:143
    ۝١٤٣

    Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. [143]

    Tanbihi

    [143] Hakika mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu kwenu kwa mambo yenye kheri yenu na mafanikio yenu. Na mimi ni mwenye kuuhifadhi Ujumbe huu kama nilivyo upokea kwa Mwenyezi Mungu.

  202. 26:144
    ۝١٤٤

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. [144]

    Tanbihi

    [144] Kwa hivyo tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nifuateni kwa haya ninayo kuitieni kwayo kutokana na amri zake.

  203. 26:145
    ۝١٤٥

    Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [145]

    Tanbihi

    [145] Wala sitaki kwenu ujira wowote kwa hii nasaha yangu na uwongozi wangu. Ujira wangu uko kwa Mwenye kumiliki walimwengu wote.

  204. 26:146
    ۝١٤٦

    Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa? [146]

    Tanbihi

    [146] Lilio wazuia ni kule kuamini kwao kwamba ati wataselelea katika zile starehe, watasalimika na adhabu, na kutoweka, na mauti,

  205. 26:147
    ۝١٤٧

    Katika mabustani, na chemchem? [147]

    Tanbihi

    [147] Katika mabustani ya matunda, na chemchem zenye kutoa maji matamu,

  206. 26:148
    ۝١٤٨

    Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva. [148]

    Tanbihi

    [148] Na konde zilizo wiva, na mitende ambayo mazao yake yamedhihiri mapevu na laini.

  207. 26:149
    ۝١٤٩

    Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi. [149]

    Tanbihi

    [149] Na mnachonga milimani majumba kwa ufundi na ustadi katika hayo mnayo yaunda.

  208. 26:150
    ۝١٥٠

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [150]

    Tanbihi

    [150] Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuto mshukuru kwenu kwa neema zake; na pokeeni nasiha yangu na muitende.

  209. 26:151
    ۝١٥١

    Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka,. [151]

    Tanbihi

    [151] Wala msiit'ii amri ya walio pindukia mipaka kwa ushirikina na kufuata pumbao na matamanio.

  210. 26:152
    ۝١٥٢

    Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi. [152]

    Tanbihi

    [152] Ambao wanapitisha maisha yao katika ardhi kwa uharibifu, wala hawafanyi ya maslaha ya kutengeneza nchi.

  211. 26:153
    ۝١٥٣

    Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa. [153]

    Tanbihi

    [153] Wakasema: Wewe si chochote isipo kuwa miongoni mwa walio rogwa kikweli mpaka zikapotea akili zao. Na katika jawabu hii mna ukali na usafihi.

  212. 26:154
    ۝١٥٤

    Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. [154]

    Tanbihi

    [154] Wewe si chochote ila ni mmoja unaye fanana na sisi kwa ubinaadamu, basi yawaje uwe bora kuliko sisi kwa Unabii na Utume? Na ukiwa wewe ni mkweli katika madai yako basi lete muujiza wa kuonyesha uthibitisho wa Utume wako.

  213. 26:155
    ۝١٥٥

    Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu. [155]

    Tanbihi

    [155] Saleh akawaambia - alipo pewa na Mwenyezi Mungu ngamia jike kuwa ni muujiza wake: Huyu hapa ngamia jike wa Mwenyezi Mungu, amekutoleeni kuwa ni Ishara. Yeye ana sehemu yake ya maji katika siku moja; siku hiyo msinywe nyinyi. Na nyinyi mna sehemu yenu siku nyengine. Kunyweni siku hiyo.

  214. 26:156
    ۝١٥٦

    Wala ms!imguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa. [156]

    Tanbihi

    [156] Wala msimletee madhara yoyote huyu ngamia, msije mkahiliki kwa adhabu kubwa.

  215. 26:157
    ۝١٥٧

    Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta. [157]

    Tanbihi

    [157] Wakamchinja ngamia, kinyume na walivyo wafikiana na Swaleh. Kwa hivyo wakastahiki kuwashukia adhabu, wakawa ni wenye kujuta kwa kitendo chao hicho.

  216. 26:158
    ۝١٥٨

    Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [158]

    Tanbihi

    [158] Basi ikawateketeza adhabu aliyo waahidi Swaleh, wala majuto hayakuwakinga na adhabu ya ukosefu wao. Hakika katika kusimulia kisa chao pana dalili ya kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kuwateketeza makafiri na kuwaokoa Waumini. Na si wengi katika watu wako wenye kuamini.

  217. 26:159
    ۝١٥٩

    Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [159]

    Tanbihi

    [159] Na hakika bila ya shaka aliye kuumba ndiye Yeye Muweza wa kuwateketeza wapinzani, na Mfadhili wa kuwaokoa wachamngu.

  218. 26:160
    ۝١٦٠

    Watu wa Luut'i waliwakanusha Mitume. [160]

    Tanbihi

    [160] Alipo waita Luut'i watu wake wamuabudu Mwenyezi Mungu pekee, na waache ushirikina, waliwakanusha Mitume wote.

  219. 26:161
    ۝١٦١

    Alipo waambia ndugu yao, Luut'i: Je! Hamumchimngu?. [161]

    Tanbihi

    [161] Ewe Mtume! Watajie watu wako pale Lut'i alipo waambia watu wake, naye ni ndugu yao na shemeji yao:

  220. 26:162
    ۝١٦٢

    Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu. [162]

    Tanbihi

    [162] Hakika mimi nimetumwa kwenu na Mwenyezi Mungu nikuleteeni Dini ya Haki. Nami ni muaminifu wa kuifikisha Dini hii.

  221. 26:163
    ۝١٦٣

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi. [163]

    Tanbihi

    [163] Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ifuateni amri yangu kwa ninayo kuitieni.

  222. 26:164
    ۝١٦٤

    Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [164]

    Tanbihi

    [164] Wala mimi sitaki kwenu ujira kwa uwongofu na uwongozi ninao kuitieni. Sina ujira ila kwa Mwenye kumiliki viumbe vyote na Mlezi wao.

  223. 26:165
    ۝١٦٥

    Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?. [165]

    Tanbihi

    [165] Lut'i alisema: Nyinyi mnastarehea kuwaingilia wanaume mkaacha wanawake? Kwa hayo anakusudia kuyakanya yale waliyo yazoea ya vitendo vichafu. "Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?" Yaani kazi ya liwat'i, ambayo tangu asli yake ni ukosefu muovu, unao chusha hata kuusikia, kinyume na maumbile, unao mteremsha mwanaadamu chini kabisa. Na lau kuwa unaenea basi huharibu sunna ya kuoa, nayo ni sunna ya maumbile, hata uzazi ukatike na ulimwengu usite kuendelea. Na kwa liwat'i huenea maradhi kama yanavyo enea kwa uzinzi kama tego, kisonono, donda ndugu, maradhi ya ngozi kama ukurutu, na hutokea ishara za kudhoofika nyama za nyuma hata ikawa mtu hawezi kujizuia kutokwa na choo ovyo. Na nyuma kwake mtu huchanua kukawa kama mdomo wa tarumbeta. Na huko nyuma hujaa vijidudu vya maradhi na hivyo humuambukiza mwenye kumuingilia na yeye hivyo vijidudu vikenda mletea maradhi mengine ya njia za mkojo. Na huenda huyo mwenye kufanywa mambo hayo akawa mpumbavu hafai kitu, ikiwa kaanza tangu utotoni. Na huenda akajidai kuonesha ujanadume mwingi kuliko kiasi kwa kutaka kuficha upungufu wake wa uume. (Karibuni imedhihiri kuwa maradhi ya khatari kabisa ya AIDS [Ukimwi] yameenea zaidi sana kwa watendao kitendo hichi na watumiao madawa ya ulevi, ijapo kuwa na wazinzi nao hupata!). Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameukemea ukosefu huu katika Aya kadhaa wa kadhaa, na akabainisha hikima ya Mwenye kuhukumu kwa kuharimisha huku, kwa kusema: " Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume? Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!"

  224. 26:166
    ۝١٦٦

    Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!. [166]

    Tanbihi

    [166] Na mnaacha aliyo kuumbieni Mwenyezi Mungu ya kustarehe na wake zenu walio halali yenu? Ama hakika nyinyi ni watu mlio pindukia mipaka ya udhalimu katika kufanya maasi.

  225. 26:167
    ۝١٦٧

    Wakasema: Ewe Luut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!. [167]

    Tanbihi

    [167] Walikasirika kwa kule kuwakataza na kuwakemea kwa sababu ya jambo ovu na wakasema: Kama hukuacha kutukebehi tutakutoa mji kwa izara kubwa.

  226. 26:168
    ۝١٦٨

    Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu. [168]

    Tanbihi

    [168] Lut'i akasema: Hakika mimi nakichukia mno hichi kitendo chenu, wala sitoacha kabisa kukipinga na kukikebehi.

  227. 26:169
    ۝١٦٩

    Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo. [169]

    Tanbihi

    [169] Na akamwomba Mola wake Mlezi amwokoe yeye na ahali zake na wayatendayo wale wajinga, baada ya kwisha kata tamaa kuwa hawamsikilizi.

  228. 26:170
    ۝١٧٠

    Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,. [170]

    Tanbihi

    [170] Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi lake, akamwokoa yeye na wale walio fuata wito wake, kwa kuwatoa wote majumbani mwao wakati wa kuteremka adhabu kuwashukia wenye kukanusha.

  229. 26:171
    ۝١٧١

    Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma. [171]

    Tanbihi

    [171] Ila mkewe kizee aliye baki, na hakutoka nao. Yeye akaangamia kwa kufuru zake na ukhaini wake, kwa kuwaunga mkono wakosefu.

  230. 26:172
    ۝١٧٢

    Kisha tukawaangamiza wale wengine. [172]

    Tanbihi

    [172] Kisha Mwenyezi Mungu akawahiliki makafiri watendao uovu kwa hilaki kali na mbaya.

  231. 26:173
    ۝١٧٣

    Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa. [173]

    Tanbihi

    [173] Na Mwenyezi Mungu aliwateremshia wale watu wapotovu mawe kutoka mbinguni, yakawateketeza. Na ilikuwa mvua ya kutisha kwa wingi wake na namna yake. Basi mvua ovu ya walio kwisha onywa ni mvua hiyo, kwani iliteremka kwa uangamizi mkubwa mno!

  232. 26:174
    ۝١٧٤

    Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [174]

    Tanbihi

    [174] Hakika adhabu ile iliyo wateremkia watu wale hapana shaka ni hoja yenye kuonyesha utimilivu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Wala si wengi katika watu wako wenye kusadiki hayo.

  233. 26:175
    ۝١٧٥

    Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. [175]

    Tanbihi

    [175] Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kusifika kwa rehema iliyo kamilika. Huwapa adhabu watendao dhambi, na huwalipa wema Waumini.

  234. 26:176
    ۝١٧٦

    Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume. [176]

    Tanbihi

    [176] Hichi kisa cha Shuaibu pamoja na Watu wa Al Aykat, Machakani, nao ni msitu wenye miti mizuri, karibu na Madian. Kikundi cha watu waliteremkia hapo na wakakaa. Mwenyezi Mungu akawapelekea Shuaibu kama alivyo wapelekea watu wa Madian. Wakamkadhibisha katika wito wake. Na kwa hivi wakawa wamekanusha risala za Mitume wote.

  235. 26:177
    ۝١٧٧

    Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?. [177]

    Tanbihi

    [177] Ewe Muhammad! Watajie watu wako pale Shuaibu alipo waambia watu wa Machakani: Je! Hamumkhofu Mwenyezi Mungu mkamuamini? Wakaingia kumkadhibisha.

  236. 26:178
    ۝١٧٨

    Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. [178]

    Tanbihi

    [178] Hakika mimi nimetumwa na Mola Mlezi wa walimwengu wote nikuongoeni na nikuongozeni. Nami ni muaminifu wa kuufikisha ujumbe wake kwenu.

  237. 26:179
    ۝١٧٩

    Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [179]

    Tanbihi

    [179] Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na nit'iini kwa kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na kuziokoa nafsi zenu na madhambi.

  238. 26:180
    ۝١٨٠

    Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [180]

    Tanbihi

    [180] Na mimi kwa hivi kukuongozeni na kukufunzeni sikutakini ujira wowote. Mimi sina malipo kaamili kwa sababu ya kazi yangu ila kutokana na Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  239. 26:181
    ۝١٨١

    Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja. [181]

    Tanbihi

    [181] Shuaibu akawaamrisha kutimiza vipimo kwa ukamilifu wanapo pima, kwani ilikuwa ada yao kupunguza kwa pishi na mizani, kupunguza haki za watu kwa kuwapunja na kuwapimia kasoro.

  240. 26:182
    ۝١٨٢

    Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;. [182]

    Tanbihi

    [182] Na wapimieni watu kwa mizani ya sawa sawa, ili wachukue haki yao kwa uadilifu ulio nyooka.

  241. 26:183
    ۝١٨٣

    Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi. [183]

    Tanbihi

    [183] Wala msiwapunguzie watu haki zao, wala msipite katika nchi mkifisidi kwa kuuwa, na uharamia, na kufanya madhambi, na kufuata pumbao.

  242. 26:184
    ۝١٨٤

    Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia. [184]

    Tanbihi

    [184] Na tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni, na akaumba kaumu zenye nguvu na takaburi zilizo tangulia.

  243. 26:185
    ۝١٨٥

    Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa. [185]

    Tanbihi

    [185] Wakasema: Wewe si chochote ila ni mtu aliye sibiwa na uchawi mkali na ikapotea akili yake.

  244. 26:186
    ۝١٨٦

    Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo. [186]

    Tanbihi

    [186] Na wewe si chochote ila ni mmoja wetu sawa na sisi kwa utu. Basi vipi ujipe ubora kuliko sisi kwa Utume? Nasi tunaamini kuwa wewe ni mwongo wa kubobea.

  245. 26:187
    ۝١٨٧

    Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. [187]

    Tanbihi

    [187] Basi hebu tuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni ikiwa ni katika wasemao kweli kwa huu ujumbe wako! Na chini ya shauri hii kwa hakika pana kila namna ya ubishi.

  246. 26:188
    ۝١٨٨

    Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda. [188]

    Tanbihi

    [188] Shuaibu akasema: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi, upeo wa kujua, wa maasi yote myatendayo, na adhabu mnayo stahiki. Yeye atakuteremshieni hayo kwa wakati wake alio ukadiria. Na huu ndio hadi ya mwisho wa kumwachilia Mwenyezi Mungu kila kitu, na kuwatisha hao makafiri.

  247. 26:189
    ۝١٨٩

    Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa. [189]

    Tanbihi

    [189] Lakini wao waliendelea kumkadhibisha. Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa adhabu ya joto kuu mno. Wakawa wanatapa tapa hawana pa kukimbilia. Walipo pata kiwingu cha kuwapa kivuli kukinga mwako wa jua walijikusanya chini yake. Mwenyezi Mungu akawateremshia moto, ukawateketeza wote katika siku ya kitisho kikubwa mno.

  248. 26:190
    ۝١٩٠

    Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [190]

    Tanbihi

    [190] Hakika adhabu iliyo wateremkia watu wa Machakani kuwa ni malipo ya uasi wao, ni dalili ya ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na hawakuwa wengi wa watu wako wenye kusadiki.

  249. 26:191
    ۝١٩١

    Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [191]

    Tanbihi

    [191] Na hakika Mola wako Mlezi hapana shaka ndiye Yeye aliye tengeka kwa Nguvu na Ushindi, Mwenye kuwaneemesha Waumini kwa rehema nyingi.

  250. 26:192
    ۝١٩٢

    Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [192]

    Tanbihi

    [192] Na hakika hii Qur'ani iliyo tajwa ndani yake visa vya kweli imeteremshwa kutoka kwa Mwenye kuumba walimwengu wote, Mwenye kumiliki mambo yao, na Mlezi wao. Basi khabari zake ni za kweli. Na hukumu yake inatimizwa mpaka Siku ya Kiyama.

  251. 26:193
    ۝١٩٣

    Ameuteremsha Roho muaminifu,. [193]

    Tanbihi

    [193] Ameiteremsha Roho muaminifu, naye ni Jibril a.s.,

  252. 26:194
    ۝١٩٤

    Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,. [194]

    Tanbihi

    [194] Juu ya moyo wako ulio tulia kuihifadhi na kuifahamu, na idhibitike katika moyo wako iwe madhubuti isisahaulike, ili upate kuwaonya wakhalifu kwa adhabu ziliomo ndani yake.

  253. 26:195
    ۝١٩٥

    Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi. [195]

    Tanbihi

    [195] Jibril amekuteremshia kwa lugha ya Kiarabu, yenye maana wazi, yenye hoja zilizo dhaahiri kwa wanayo hitajia ya kutengeneza mambo yao ya dunia na Dini.

  254. 26:196
    ۝١٩٦

    Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale. [196]

    Tanbihi

    [196] Na hakika kuitaja Qur'ani na kueleza kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu kumteremshia Muhammad s.a.w. yametajwa katika Vitabu vya Manabii walio tangulia.

  255. 26:197
    ۝١٩٧

    Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?. [197]

    Tanbihi

    [197] Je! Hawa wenye inda wanaikataa Qur'ani na hali wao wanayo hoja inayo onyesha ukweli wa Muhammad s.a.w., nayo ni ilimu ya wanazuoni wa Wana wa Issraili juu ya Qur'ani kama ilivyo katika vitabu vyao?

  256. 26:198
    ۝١٩٨

    Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,. [198]

    Tanbihi

    [198] Na lau tungeli mteremshia mtu asiye kuwa Mwaarabu, anaye weza kusema Kiarabu lakini si kwa ufasihi, wasingeli waza kumtuhumu kuwa kaizua.

  257. 26:199
    ۝١٩٩

    Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini. [199]

    Tanbihi

    [199] Na angeli wasomea baraabara kinyume na ada bado wangeli mkanusha, na wakapatia kisababu kwa ukafiri wao.

  258. 26:200
    ۝٢٠٠

    Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu. [200]

    Tanbihi

    [200] Sisi tumekutia huko kukanusha katika nyoyo za wakosefu; na tumekuthibitisha kama tulivyo kuthibitisha katika nyoyo za wenye sifa kama zao.

  259. 26:201
    ۝٢٠١

    Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. [201]

    Tanbihi

    [201] Basi hapana njia ya wao kuacha tabia yao ya ukafiri mpaka wateseke kwa hiyo adhabu kali walio ahidiwa.

  260. 26:202
    ۝٢٠٢

    Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari. [202]

    Tanbihi

    [202] Itawateremkia adhabu kwa ghafla bila ya kuitaraji, wala wao hawajui kama inakuja.

  261. 26:203
    ۝٢٠٣

    Na watasema: Je, tutapewa muhula?. [203]

    Tanbihi

    [203] Watasema itapo teremka hiyo adhabu: Je, tutapewa muhula? Haya ni kwa majuto kwa kupitiwa na Imani na kutaka waakhirishiwe adhabu. Lakini hawajibiwi.

  262. 26:204
    ۝٢٠٤

    Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?. [204]

    Tanbihi

    [204] Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Watu wa Makka wameghurika na kuchelewesha kwangu kuwaadhibu, basi ndio wanaihimiza? Anakusudia Subhanahu Aliye takasika kuzisafihi akili zao kwa sababu ya kuhimiza kwao adhabu juu ya kuwaonya na kuwatisha.

  263. 26:205
    ۝٢٠٥

    Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,. [205]

    Tanbihi

    [205] Je, umefikiri ukajua, kama Sisi tuliwastarehesha kwa uhai kwa muda wa miaka mingi pamoja na maisha mema?

  264. 26:206
    ۝٢٠٦

    Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,. [206]

    Tanbihi

    [206] Kisha ikawateremkia adhabu iliyo ahidiwa.

  265. 26:207
    ۝٢٠٧

    Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?. [207]

    Tanbihi

    [207] Kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mema hakutowakinga hata chembe na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuja tu, kama si leo kesho. Wala hapana kheri katika neema ambayo khatima yake ni adhabu.

  266. 26:208
    ۝٢٠٨

    Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji. [208]

    Tanbihi

    [208] Na mwendo wetu kwa kaumu zote ni kuwa hatuuteketezi umma ila baada ya kuwatumia Mitume wa kuwaonya kwa kufuata hoja,

  267. 26:209
    ۝٢٠٩

    Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu. [209]

    Tanbihi

    [209] Wakumbuke na wazingatie. Wala si shani yetu kudhulumu hata tuuadhibu umma kabla ya kuwaletea Mtume.

  268. 26:210
    ۝٢١٠

    Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo, [210]

    Tanbihi

    [210] Qur'ani inakataa waliyo yasema makafiri wa Makka ya kwamba Muhammad anafuata majini, nao ndio wanampa Qur'ani. Qur'ani inasema: Mashetani hawakuiteremsha hii Qur'ani.

  269. 26:211
    ۝٢١١

    Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi. [211]

    Tanbihi

    [211] Wala haiwafalii wao kuiteremsha, na hawawezi kufanya hivyo.

  270. 26:212
    ۝٢١٢

    Hakika hao wametengwa na kusikia. [212]

    Tanbihi

    [212] Kwani hao hakika wanazuiwa wasiisikie Qur'ani pale inapo funuliwa kwa Muhammad s.a.w.

  271. 26:213
    ۝٢١٣

    Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa. [213]

    Tanbihi

    [213] Basi wewe muelekee Mwenyezi Mungu ukiendelea na usafi wako wa ibada, wala usishughulike na fisadi za madai ya washirikina na mwendo wao muovu. Na hivi kutakiwa Mtume s.a.w. awe na ikhlasi ya namna hii ni wito kwa jamii ya watu waliomo katika umma wake.

  272. 26:214
    ۝٢١٤

    Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe. [214]

    Tanbihi

    [214] Watie khofu ya adhabu ya shirki na maasi walio karibu nawe katika jamaa zako.

  273. 26:215
    ۝٢١٥

    Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini. [215]

    Tanbihi

    [215] Na kuwa mpole kwa wanao itikia wito wako wa Imani.

  274. 26:216
    ۝٢١٦

    Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda. [216]

    Tanbihi

    [216] Pindi wakikuasi na wasikufuate basi jitenge nao, na jitenge na vitendo vyao vya ushirikina na maasi yote.

  275. 26:217
    ۝٢١٧

    Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [217]

    Tanbihi

    [217] Na tegemeza mambo yako kwa Mwenye nguvu, Mwenye uweza wa kuwatenda nguvu adui zako kwa utukufu wake, na kukunusuru wewe na kumnusuru kila mwenye kufanya a'mali yake kwa usafi wa niya.

  276. 26:218
    ۝٢١٨

    Ambaye anakuona unapo simama, [218]

    Tanbihi

    [218] Ambaye anakuona pale unapo simama kwa ibada za usiku na vitendo vyote vya kheri.

  277. 26:219
    ۝٢١٩

    Na mageuko yako kati ya wanao sujudu. [219]

    Tanbihi

    [219] Na anaona mwendo wako kati ya wanao sali, kwa kusimama, na kukaa, na kurukuu na kusujudu, pale unapo waongoza katika Swala.

  278. 26:220
    ۝٢٢٠

    Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. [220]

    Tanbihi

    [220] Hakika Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kusikia dua zako na dhikri zako, ndiye Mjuzi wa kujua niya yako na vitendo vyako. Ni kama kwamba Subhanahu anamwambia: Usichukue taklifu kubwa bila ya kiasi katika mashaka ya ibada, kwani uyatendayo yote nayaona na nayasikia Mimi.

  279. 26:221
    ۝٢٢١

    Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani? [221]

    Tanbihi

    [221] Washirikina walisema: Mashetani ndio wanamsomea Qur'ani Muhammad. Qur'ani ikawajibu: Nikupeni khabari watu gani Mashetani ndio wanawateremkia, na wakawashawishi?

  280. 26:222
    ۝٢٢٢

    Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi. [222]

    Tanbihi

    [222] Wanamteremkia kila mwenye kubeba dhambi za namna mbaya kabisa za uwongo, na madhambi ya kuchusha kabisa. Nao ni hao makohani mafisadi ambao tabia zao na tabia za Mashetani ni jinsi moja na zimewafikiana.

  281. 26:223
    ۝٢٢٣

    Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo. [223]

    Tanbihi

    [223] Hao hutega masikio yao kwa Mashetani, na kwao wakapata mambo ya dhana dhana tu. Na wengi wao ni waongo, na huzidisha tena juu ya kauli walizo zipata kwa Mashetani.

  282. 26:224
    ۝٢٢٤

    Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata. [224]

    Tanbihi

    [224] Makafiri wanasema: Hii Qur'ani ni mashairi, na Muhammad ni mtungaji mashairi. Mwenyezi Mungu ameyavunja haya kwa kuthibitisha kuwa hakika Qur'ani imejaa hikima na hukumu. Mpango wake unapingana na mpango wa mashairi ambao unategemea juu ya kweli na uwongo. Na amebainisha kwamba hali ya Muhammad s.a.w. inapingana na hali ya watungaji mashairi. Yeye anasema kwa hikima, wao wanasema kwa udanganyifu. Na hii ndiyo hali ya wengi katika watungaji mashairi.

  283. 26:225
    ۝٢٢٥

    Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde? [225]

    Tanbihi

    [225] Kwani huwaoni vile wanavyo tangatanga katika mabonde ya maneno wala hawaongoki kwenye Haki?

  284. 26:226
    ۝٢٢٦

    Na kwamba wao husema wasiyo yatenda? [226]

    Tanbihi

    [226] Na kwamba wao husema kwa ndimi zao wasio yaambatisha na vitendo vyao?

  285. 26:227
    ۝٢٢٧

    Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka. [227]

    Tanbihi

    [227] Lakini walio hidika kwa hidaya ya Mwenyezi Mungu, na wakatenda mema mpaka zikatua katika nafsi zao sifa bora, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi mpaka ikathibiti khofu katika nyoyo zao, hawa basi huyafanya mashairi kama dawa ilio sibu kwa ugonjwa wake. Na hupambana kwa ajili ya kuiwania Dini yao na kusimamisha Haki, inapo kuwa Haki inafanyiwa jeuri. Na walio dhulumu nafsi zao kwa shirki na kumkejeli Mtume kwa mashairi, watatafuta wapi pa kuikimbia shari na hilaki wanayo iendea.

  286. Sura An-Naml

    سُورَةُ النمل
  287. 27:1
    ۝١

    T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu kinacho bainisha; . [1]

    Tanbihi

    [1] T'aa Siin, (T' na S) harufi mbili za kutamkwa, ni harufi za alifbete, ndizo zimeanzia Sura hii, ili kunabihisha siri ya muujiza wa Qur'ani pamoja na kuashiria kuwa imeundwa kwa jinsi ya harufi hizi hizi mnazo zitumia katika kusema, na pia kuzindua akili ziisikilize hii Qur'ani inapo somwa. Hizi Aya zilizo teremka kwa kusomwa, na ni Kitabu chenye kubainisha mambo yaliyo kuja ndani yake.

  288. 27:2
    ۝٢

    Uwongofu na bishara kwa Waumini! [2]

    Tanbihi

    [2] Na hii Qur'ani ni Uwongofu wa kuwaahidi Waumini waifuate njia ya kheri, na kufuzu duniani na Akhera, na inawabashiria kuwa watapata malipo mazuri.

  289. 27:3
    ۝٣

    Ambao wanashika Swala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo. [3]

    Tanbihi

    [3] Waumini hao ndio wanao ishika Swala kwa unyenyekevu na kutimiliza nguzo, na wanatoa Zaka kwa nyakati zake, nao wana yakini ya maisha ya baadaye Akhera, na yatayo kuwa huko ya adhabu na thawabu.

  290. 27:4
    ۝٤

    Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo. [4]

    Tanbihi

    [4] Hakika wale ambao hawaiamini Akhera, Sisi tumewapambia vitendo vyao kwa kuwaumbia matamanio ndani yake. Kwa hivyo wao wanababaika humo katika upotovu wao.

  291. 27:5
    ۝٥

    Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika Akhera ndio watapata khasara zaidi. [5]

    Tanbihi

    [5] Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na Akhera ndio watakuwa khasarani kushinda wote.

  292. 27:6
    ۝٦

    Na hakika wewe unafundishwa Qur'ani inayo tokana kwake Mwenye hikima Mwenye kujua. [6]

    Tanbihi

    [6] Ewe Nabii! Wewe unapokea Qur'ani hii unayo teremshiwa kutokana na Yeye ambaye hapana anaye mkaribia kwa hikima yake, naye anajua kila kitu.

  293. 27:7
    ۝٧

    (Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili mpate kuota moto. [7]

    Tanbihi

    [7] Kumbuka pale Musa alipo mwambia mkewe na walio pamoja naye na yeye ndio anarejea Misri: Mimi nimeona moto. Nitakwenda kuleteeni khabari ya njia, au nitapata kijinga cha moto, kitacho kufaeni kwa kuota moto kwa hii baridi.

  294. 27:8
    ۝٨

    Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. [8]

    Tanbihi

    [8] Alipo fika huko paliitwa: Wamebarikiwa waliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake, yaani karibu yake. Nao ni Malaika na Musa. Na Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote ametakasika na kila kisicho kuwa laiki naye.

  295. 27:9
    ۝٩

    Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima. [9]

    Tanbihi

    [9] Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kuweka kila kitu pahala pake.

  296. 27:10
    ۝١٠

    Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu Mitume. [10]

    Tanbihi

    [10] Na katika njia ya kufikisha wito wako, tupa fimbo yako na utaiona inatikisika kama kijoka jepesi kinakwenda mbio. Yeye akarudi nyuma, wala hakurejea baada ya kurudi nyuma. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtuza kwa kauli yake: Usiogope. Mbele yangu hawaogopi. Mitume ninapo sema nao. Kisa cha Musa kimetajwa zaidi ya mara moja katika Qur'ani. Pengine hutolewa yasiyo tajwa penginepo. Na kila sehemu ina mnasaba wake. Katika sehemu hii makusudio ni kuondoa yale mastaajabu ya kuwa Nabii Muhammad s.a.w. kapata Ufunuoa (Wahyi) vile vile.

  297. 27:11
    ۝١١

    Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [11]

    Tanbihi

    [11] Lakini mwenye kutenda asicho ruhusiwa, na kisha akaleta wema baada ya kuteleza kwake, basi Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mkubwa wa kurehemu.

  298. 27:12
    ۝١٢

    Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe bila ya maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu waovu. [12]

    Tanbihi

    [12] Na utie mkono wako katika mfuko wa nguo zako, utatoka mweupe wala si kwa balanga. Hayo ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu, ni makafiri. Hizo Ishara tisa ni:- Kupasuka bahari, T'ufani (Kimbunga), Nzige, Chawa, Vyura, Damu, Ukame, Fimbo, Kutoka mkono mweupe bila ya maradhi.

  299. 27:13
    ۝١٣

    Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri. [13]

    Tanbihi

    [13] Ilipo kuja miujiza hii kwa uwazi na dhaahiri wakasema: Huu ni uchawi wazi!

  300. 27:14
    ۝١٤

    Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi! [14]

    Tanbihi

    [14] Wakaikadhibisha miujiza wakikataa kuwa inaonyesha dalili ya Utume. Na hakika yakini ilikwisha waingia katika nyoyo zao, lakini hawakusalimu amri kwa kuwa walikwisha tangaza kufuata upotovu na kushika uasi. Basi ewe Nabii! Hebu angalia vipi yalikuwa matokeo ya walio shikilia ufisadi, wakaikanya miujiza nayo iko wazi.

  301. 27:15
    ۝١٥

    Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye tufadhilisha kuliko wengi katika waja wake Waumini. [15]

    Tanbihi

    [15] Hizo ndizo jeuri za Firauni kwa sababu ya ufalme wake. Hebu sasa angalia utawala muadilifu, utawala wa hukumu, utawala wa unabii wa Daudi na mwanawe, Sulaiman, Mwenyezi Mungu awape amani. Sisi tuliwapa ilimu nyingi za sharia na mazoezi ya kuhukumu. Wakasimamisha uadilifu, na wakamhimidi Mwenyezi Mungu aliye wapa fadhila kushinda wengi katika waja wake wenye kusadiki, na kuifuata Haki.

  302. 27:16
    ۝١٦

    Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri. [16]

    Tanbihi

    [16] Ufalme na hukumu ukatoka kwa Daudi ukenda kwa mwanawe, Sulaiman; naye akasema: Enyi watu! Sisi tumefunzwa lugha ya ndege, na tumepewa mengi tunayo yahitajia katika utawala wetu. Hakika neema hizi ni fadhila iliyo wazi aliyo tukhusisha sisi Mwenyezi Mungu, "Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri." Sulaiman a.s. ni mwana wa Daudi, naye ni Nabii na Mfalme kama yeye. Aliishi mnamo mwaka 974 mpaka 937 K.K. (yaani Kabla ya Kuzaliwa Nabii Isa). Mwenyezi Mungu alimjaalia kumjuvya kufahamu maneno ya ndege. Uchunguzi wa kisasa umeonyesha kwamba kila namna ya ndege wana njia zao za kufahamiana wao kwa wao. Katika njia hizo ni kwa kugusa, na sauti, na ishara.

  303. 27:17
    ۝١٧

    Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu. [17]

    Tanbihi

    [17] Na Sulaiman alikusanya majeshi yake ya majini, watu, na ndege, kwenye uwanja mmoja. Na wao wakawa jeshi moja lenye nidhamu kwa vile kudhibitiwa wa mwanzo mpaka mwisho.

  304. 27:18
    ۝١٨

    Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua. [18]

    Tanbihi

    [18] Hata walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, mdudu chungu mmoja akasema: Enyi wadudu chungu! Ingieni vishimoni mwenu, asije Sulaiman na askari wake wakakuuweni na wao wala hawahisi kuwa nyinyi mpo. "Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua." Inafahamikana wazi katika Aya hii kuwa wadudu chungu wanaishi kwa makundi, yaani wana umoja, na moja katika sifa zao ni kuwa macho na kutahadhari. Na inajuulikana tangu zamani kuwa wadudu chungu wana sifa kadhaa wa kadhaa makhsusi ambazo zinaonyesha kuwa wana umoja wenye nidhamu madhubuti katika hukumu, na wana kiasi kikubwa cha akili, na werevu, na nguvu za kukumbuka, na kupenda kazi na kukakamia, na juhudi isiyo jua kunyong'onyea wala kukata tamaa. Kama wanavyo juulikana kuwa wana wingi wa hila za kuendesha kazi zao. Na dalili ya hayo ni kuwa jamaa wa wadudu chungu ni peke yao baada ya binaadamu ndio wanao zika maiti wao. Na makundi mbali mbali yao yanashughulikia kukutana pahala pamoja kwa nyakati maalumu. Kwa ajili ya hayo zimewekwa siku makhsusi za kusimamisha soko wanapo kusanyika makundi yote kwa kubadilishana bidhaa na kujuana. Na makundi haya yanapo kutana hutokea mazungumzo kwa hima kubwa, na huulizana masuala yaliyo khusiana na mambo yao. Katika yanayo onekana yaliyo fungamana na mikusanyiko hiyo ni kuzuka mashauri yaliyo khusu umma wao, kama kutengeneza barabara ndefu, kwa subira na kukakamia kunako staajabisha. Wala makundi haya hayatosheki na kufanya kazi mchana tu, bali huendeleza kazi zao katika masiku ya mbaamwezi; ama masiku ya kiza hubaki mwahala mwao. Na jamaa wa makundi haya wana njia za pekee za kukusanya na kubeba na kuhifadhi vifaa vyao vya kula. Akishindwa mdudu kuchukua chakula alicho kikusanya kwa mdomo wake hukisukuma kwa miguu yake ya nyuma, na akakinyanyua kwa mikono yake. Na katika mtindo wao ni kuzing'ong'ona mbegu, na kuzipasua baadhi ya nafaka kabla ya kuzirindika ili zisije kuchipua. Na mbegu kubwa kubwa huzigawa vipande vipande ili iwe wepesi kuziingiza katika ghala zao. Na pindi zikiroana kwa mvua huzitoa zipate upepo na jua zikauke.

  305. 27:19
    ۝١٩

    Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema. [19]

    Tanbihi

    [19] Sulaiman akatabasamu akicheka kwa ile kauli ya mdudu chungu yenye kushughulikia maslaha yao, na akahisi neema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo juu yake. Akasema: Ewe Uliye niumba! Nijaalie niwe na shukrani kwako kwa neema ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na niwezeshe nitende vitendo vyema unavyo viridhia, na unitie kwenye rehema yako iliyo timia.

  306. 27:20
    ۝٢٠

    Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu? [20]

    Tanbihi

    [20] Akalikagua jeshi lake la ndege asimwone Hud-hud. Akastaajabu, akasema: Mbona simwoni Hud-hud! Yupo hapa na mimi simwoni, au ameghibu hayupo miongoni mwetu?

  307. 27:21
    ۝٢١

    Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee hoja ya kutosha. [21]

    Tanbihi

    [21] Wallahi! Nitampatisha adhabu kali ya kumshikisha adabu, au nitamchinja ikiwa kosa lake ni kubwa! Ila aniletee hoja madhubuti ya kumtoa makosani kwa kuto kuwepo mbele yangu.

  308. 27:22
    ۝٢٢

    Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini. [22]

    Tanbihi

    [22] Na Hud-hud alikuwa kakaa si pahala mbali kwa muda usio kuwa mrefu. Kisha akamjia Sulaiman, akamwambia: Nimejua jambo ulilo kuwa wewe hujalijua, na nimekujia kutoka nchi ya Sabai na khabari muhimu sana, nayo ni ya kweli kwa yakini. "Basi hakukaa mbali, na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka." Hizi ndizo Aya khasa zilizo khusu Ufalme wa Sabai. Na hii Sabai ni moja katika falme za kusini ya Arabuni, inayo itwa Yaman, na ambayo zamani ilikuwa ni maarufu kwa jina la "Arabia Iliyo Neemeka". Na jina hili la mwisho linaonyesha maendeleo yake na utajiri wake. Kwani kwa hakika ilikuwa nchi hiyo ina ustaarabu wa juu tangu miaka elfu mbili kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. Ikitegemea makulima, kwa sababu ya rutuba ya ardhi yake, na uzuri wa hali yake ya hewa. Na pia ikitegemea biashara kwa kuwa ipo kati baina ya Bara Hindi, na Uhabeshi, na Somalia, na Sham, na Iraq. Na kwa hakika mahodhi yaliyo jengwa kuwekea maji na kuyatumia, na maarufu yao yote ni Hodhi Maa'rib (Tazama Aya 16 Surat Sabai) na miji iliyo jengewa ngome, na makasri, na mahekalu, yanashuhudia mpaka hii leo maendeleo ya kijamii ya utajiri ulio kuwako katika nchi hii. Na hakika nakshi walizo zinakishi watawala wao, na baina ya nakshi hizo zipo kanuni za kuendesha mambo ya ujenzi na mengineyo, yanaonyesha kwa kila dalili ukomo wa ustaarabu ulio nawiri walio ufikilia. Na huu ufalme wa Sabai ambao ulifikilia kilele cha kustawi kwake katika siku za Sulaiman a.s. kiasi ya karne kumi kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. ulikuwa ni ufalme kama wa kabla yake, yaani watoto wakiwarithi baba zao. Na kwa hivyo alikuwa akihukumu wakati wa Sulaiman a.s. Malkia. Wataalamu wa taarikhi wamekhitalifiana juu ya jina la Malkia huyo. Waarabu wakimwita Balqiis; akisaidiwa na wazee wahishimiwa kama ni Baraza la Mashauri lake. (Tazama Aya 28-33 katika Surat An-naml.) Wala haikuthibitisha taarikh (historia) kuwa Ufalme wa Sabai ulikuwa dola ya kuteka nchi, bali ulikuwa ufalme wa biashara, na misafara. Katika mabaki yake hatuoni kutajwa vita au kuteka nchi isipo kuwa kwa uchache. Na haya ni kuwa umuhimu wa majeshi yake ulikuwa ni kuhifadhi ngome zake na kuzihami, na kulinda misafara yake kwa aghlabu. Na wananchi wa Sabai walikuwa ni mapagani, makafiri, wakiliabudu jua, kama ilivyo kuja katika Aya tukufu nambari 24 katika Sura hii. Pia wakiabudu mwezi. Na hao ndio miungu yao muhimu kabisa. Na walikuwa wakiwatolea sadaka na wakifukiza ubani katika mahekalu yao.

  309. 27:23
    ۝٢٣

    Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa. [23]

    Tanbihi

    [23] Hakika mimi nimewaona watu wa Sabai wanatawaliwa na mwanamke, na amepewa kila kheri za kidunia, naye ana kiti cha enzi kikubwa kinacho onyesha dalili ya utukufu wa ufalme na nguvu za madaraka yake.

  310. 27:24
    ۝٢٤

    Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka [24]

    Tanbihi

    [24] Nimemwona yeye na watu wake wanaabudu jua, wala hawamuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani amewazainishia vitendo vyao na wenyewe wakaviona ni vizuri na hali ni viovu. Kwa hivyo amewapoteza Njia ya Haki, basi hawakuongoka.

  311. 27:25
    ۝٢٥

    Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza. [25]

    Tanbihi

    [25] Hawamsujudii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye anayafichua yaliyo fichika katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo fanya kwa siri na kwa dhaahiri.

  312. 27:26 ۩ Sijida
    ۝٢٦

    Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi tukufu [26]

    Tanbihi

    [26] Mwenyezi Mungu, ambaye hapana wa kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye, ndiye Mwenye madaraka makuu yasio na ukomo juu ya kila kiumbe.

  313. 27:27
    ۝٢٧

    Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo. [27]

    Tanbihi

    [27] Sulaiman akasema kumwambia Hud-hud: Tutaichungua khabari yako hii tujue kwamba umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.

  314. 27:28
    ۝٢٨

    Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini. [28]

    Tanbihi

    [28] Nenda na barua yangu hii umfikishie yeye na kaumu yake. Kisha jitenge nao ujifiche pahali karibu, uangalie wanarejesheana maneno gani.

  315. 27:29
    ۝٢٩

    (Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa barua tukufu. [29]

    Tanbihi

    [29] Barua ikamfikia yule Malkia, naye basi akawakusanya wahishimiwa wa kaumu yake, na halmashauri wake. Naye akasema: Enyi wahishimiwa! Mimi hakika imenifikilia barua yenye shani kuu.

  316. 27:30
    ۝٣٠

    Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. [30]

    Tanbihi

    [30] Kisha akawasomea hiyo barua, nayo imeanzia kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na neema zote, ambaye daima anawamiminia waja wake rehema zake.

  317. 27:31
    ۝٣١

    Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye kusalimu amri. [31]

    Tanbihi

    [31] Msifanye kiburi juu yangu, na nijieni nanyi mmet'ii na wanyenyekevu.

  318. 27:32
    ۝٣٢

    Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie. [32]

    Tanbihi

    [32] Akaiambia baraza ya washauri wake: Nibainishieni lifaalo katika haya mambo muhimu nilio wekewa mbele yangu. Kwani mimi sikati shauri juu ya jambo lolote mpaka muwe nyinyi mmehudhuria.

  319. 27:33
    ۝٣٣

    Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha. [33]

    Tanbihi

    [33] Wakamwambia nao wametua: Sisi ni watu wenye nguvu za mwili, na tuna moyo na mashujaa. Hatuogopi vita. Basi angalia wewe jambo unalo taka kutuamrisha nasi ni wenye kut'ii.

  320. 27:34
    ۝٣٤

    Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo. [34]

    Tanbihi

    [34] Akasema kwa taratibu na kupendelea salama: Hakika watawala wakiingia katika miji mikubwa pamoja na majeshi yao huifisidi, wakaondoa matengenezo yake, wakateketeza makulima na roho, na wakawafanya walio watukufu katika watu wa hiyo miji kuwa ndio madhalili, na huo ndio mtindo wao daima.

  321. 27:35
    ۝٣٥

    Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi nayo wajumbe. [35]

    Tanbihi

    [35] Na mimi kwa kupendelea salama na uzima nitampelekea zawadi Sulaiman na kaumu yake, na nitatazama wajumbe watarejea na nini - wataikubali zawadi au watairudisha?

  322. 27:36
    ۝٣٦

    Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu. [36]

    Tanbihi

    [36] Wajumbe walifika kwa Sayyidina Sulaiman na zawadi zao. Huku anazijua neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu zilio juu yake, Akawaambia naye ndio anamsemeza huyo Malkia na watu wake katika mkabala na wajumbe: Hivyo ndio mnanipa mimi mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ya Unabii, na ufalme, na neema, ni makubwa zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Bali nyinyi kwa hizi zawadi zenu na wingi wa mali yenu mnafurahi, sio kama mimi. Kwa sababu nyinyi hamjui ila yaliyo shikamana na dunia hii tu.

  323. 27:37
    ۝٣٧

    Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge. [37]

    Tanbihi

    [37] Akasema, akimsemeza yule msemaji kwa jina lao: Ewe mjumbe! Rejea kwao. Wallahi! tutawatokea kwa majeshi wasio yaweza kupambana nayo na kuyakabili. Na tutawatoa kwenye nchi ya Sabai nao wamepoteza utukufu wao, wamefanywa watumwa.

  324. 27:38
    ۝٣٨

    Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri. [38]

    Tanbihi

    [38] Sulaiman akawaelekea binaadamu na majini aliyo dhalilishiwa na Mwenyezi Mungu kumtumikia, akawashitua kwa jambo geni. Akasema: Ni nani katika nyinyi anaweza kuniletea kiti chake cha enzi kikubwa kabla hawajanijia nao wamekwisha nyenyekea wanat'ii.

  325. 27:39
    ۝٣٩

    Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu. [39]

    Tanbihi

    [39] Mmoja pandikizi la kijini lilisema: Mimi nitakuletea, na wewe umekaa katika baraza yako hii, kabla hujaondoka. Na mimi hakika naweza hayo, na muaminifu katika maneno yangu na vitendo vyangu.

  326. 27:40
    ۝٤٠

    Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu. [40]

    Tanbihi

    [40] Akasema aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kiti cha enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza aliyo yasema. Sulaiman alipo kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya mtingisiko, alisema: Haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba na akanipa kheri zake ili anifanyie mtihani, nitashukuru kwa neema hizi au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi huyo hakika amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na mwenye kuacha kushukuru kwa neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si mwenye kuhitajia shukrani. Naye ni Karimu wa kuneemesha.

  327. 27:41
    ۝٤١

    Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone ataongoka, au atakuwa miongoni mwa wasio ongoka. [41]

    Tanbihi

    [41] Sulaiman akawaambia watu wake: Kigeuzeni geuzeni hichi kiti cha enzi kwa baadhi ya mabadiliko ya nje, tupate kuona atakijua kwa kukiendea au hato kijua na kwa hivyo hato kiendea.

  328. 27:42
    ۝٤٢

    Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake wakasema): Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu. [42]

    Tanbihi

    [42] Alipo fika jicho lake lilipiga kwenye kiti chake cha enzi. Akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni mfano wa hiki? Akasema kwa vile kilivyo kamilika kufanana: Kama kwamba ndicho hichi. Na Sulaiman na walio pamoja naye wakasema: Sisi tulisha pewa ujuzi kumjua Mwenyezi Mungu na uwezo wake na ukweli wa yaliyo kuja kutoka kwake kama anavyo jua mwanamke huyu. Na sisi tangu hapo ni watu tulio mfuata Mwenyezi Mungu na tunamsafia Yeye ibada.

  329. 27:43
    ۝٤٣

    Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri. [43]

    Tanbihi

    [43] Na zile ibada za jua na mfano wake zilimzuia yule Malkia kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwani yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.

  330. 27:44
    ۝٤٤

    Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo liona alidhani ni maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman) akasema: Hakika hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja na Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. [44]

    Tanbihi

    [44] Baada ya hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja wake wa ndani ulikuwa umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki wakiogelea humo. Kupandisha nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa alidhania ni maji. Sulaiman akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri yale madhaahiri ya kilimwengu, na akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman. Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu kwa kughurika na ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea pamoja na Sulaiman kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu wote na kuwalea na kuwasimamia.

  331. 27:45
    ۝٤٥

    . Na kwa kina Thamud tulimtuma ndugu yao Swaleh kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayo gombana. [45]

    Tanbihi

    [45] Na tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh kuwafunza wamuamini Mwenyezi Mungu pekee. Wao wakakimbilia kugombana na kukhitalifiana. Wakawa makundi mawili. Moja lenye kuamini, na moja la kikafiri.

  332. 27:46
    ۝٤٦

    Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe? [46]

    Tanbihi

    [46] Swaleh akasema nao kuwanasihi: Enyi watu! Mbona mnaihimiza adhabu mlio ahidiwa kabla ya kutubu? Kwa nini hamwombi msamaha kwa Mola wenu Mlezi, mkamuamini Yeye kwa kutaraji akurehemuni?

  333. 27:47
    ۝٤٧

    Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni watu mnao jaribiwa. [47]

    Tanbihi

    [47] Wakasema: Sisi tunakuona wewe na hao walio nawe ni wakorofi, ndio tukapatilizwa na ukame. Yeye akasema: Sababu za kheri na shari zinazo kuteremkieni bila ya shaka yoyote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi ni watu mnao pewa mitihani ya neema na nakama, ili mpate kuamini.

  334. 27:48
    ۝٤٨

    Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha. [48]

    Tanbihi

    [48] Na waongozi wa shari kati yao walikuwa ni tisa, kazi yao ni kufisidi katika nchi kwa maoni yao na madai yao. Wala haukuwa mtindo wao kutenda jema lolote.

  335. 27:49
    ۝٤٩

    Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli. [49]

    Tanbihi

    [49] Wale washirikina wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Apishaneni kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwamba kwa yakini tutamshambulia yeye na ahali zake, na tutawauwa. Kisha tutamwambia jamaa yao wa damu kwamba sisi hatukayaona mauwaji yake wala ya ahali zake. Na hakika sisi ni wasema kweli kwa haya tuliyo yataja.

  336. 27:50
    ۝٥٠

    Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu, na wao hawatambui. [50]

    Tanbihi

    [50] Walipanga kumuuwa Swaleh na ahali zake, na Mwenyezi Mungu nyuma yao kapanga kumwokoa Nabii wake na ahali zake, na kuwateketeza wao, na hali wao hata hawatambui.

  337. 27:51
    ۝٥١

    Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote. [51]

    Tanbihi

    [51] Ewe Nabii! Hebu tazama vipi yalikuwa matokeo ya mipango yao na mipango yetu. Sisi tuliwaangamiza wote hao wao na kaumu yao.

  338. 27:52
    ۝٥٢

    Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua. [52]

    Tanbihi

    [52] Na hebu yatazame mabaki yao. Utakuta nyumba zao zimeanguka, zimevurugika, kwa sababu ya udhalimu wao na kufru zao, na kumtakia shari Nabii wao. Hakika kwa walio fanyiwa kina Thamud ipo Ishara kwa watu wanao ujua uwezo wetu na wakawaidhika.

  339. 27:53
    ۝٥٣

    Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa wanamchamngu. [53]

    Tanbihi

    [53] Na Sisi tukakiokoa kikundi kilicho muamini Saleh kutokana na hilaki hii, na wakawa wanao gopa kuziacha amri zake.

  340. 27:54
    ۝٥٤

    Na Luut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya uchafu nanyi mnaona? [54]

    Tanbihi

    [54] Ewe Nabii! Mtaje Luut'i na khabari zake pamoja na kaumu ya watendao uchafu, pale alipo waambia: Je! Mnafanya dhambi hizi ambazo zimepita hadi ya uchafu na kinyume na maumbile, na hali nyinyi mnaona na mnaangalia uovu wa haya mliyo yashikilia?

  341. 27:55
    ۝٥٥

    Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio badala ya wanawake? Hakika nyinyi ni watu mnao fanya ujinga kabisa! [55]

    Tanbihi

    [55] Hivyo inaelekea katika nadhari ya akili zenu na maumbile kuwaingilia wanaume kwa matamanio yenu, na mkwawacha wanawake? Ama kweli nyinyi mmesibiwa na upumbavu na ujinga wa kufudikiza, hata imekuwa hamwezi tena kuteuwa baina ya kiovu na chema.

Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani