Quran Touch

Juzuu 18

Al-Muminoon 23:1 – Al-Furqaan 25:20 · 202 aya

Aa
Neno kwa neno

  1. Sura Al-Muminoon

    سُورَةُ المؤمنون
  2. 23:1
    ۝١

    HAKIKA wamefanikiwa Waumini! [1]

    Tanbihi

    [1] Kumethibiti kufanikiwa kwa Waumini wanao muamini Mwenyezi Mungu na waliyo kuja nayo Mitume; na wamefuzu kwa wayatakayo.

  3. 23:2
    ۝٢

    Ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao! [2]

    Tanbihi

    [2] Hao ambao wameambatisha juu ya Imani yao vitendo vyema. Basi hao katika Swala zao humuelekea Mwenyezi Mungu kwa nyoyo zenye kumkhofu na kumnyenyekea, wanahisi unyenyekevu wa mwisho kwake Yeye .

  4. 23:3
    ۝٣

    Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi! [3]

    Tanbihi

    [3] Hao wanashughulikia mambo ya maana, wanapuuza vitendo na maneno yasiyo na kheri ndani yake.

  5. 23:4
    ۝٤

    Na ambao wanatoa Zaka! [4]

    Tanbihi

    [4] Nao wanashikilia kutoa Zaka kuwapa wanao stahiki. Kwa hivyo wanakusanya ibada ya mwili na ibada ya mali, na baina ya kujisafisha nafsi na kuyasafisha mali. "Na ambao wanatoa Zaka,": Huu waajibu wa kutoa Zaka unapelekea kujenga mashikamano ya umoja baina ya Waislamu, na kutia katika moyo wa kila mtu kuwa ana jukumu kwa nduguye, anahisi kama anavyo hisi yeye, na anaungulika kama anavyo ungulika yeye. Kwa hivyo ni waajibu wake kufanya awezavyo kumkinga na balaa za kilimwengu, na machungu ya ukosefu. Kwa hivyo fakiri au masikini hatomchukia tajiri, bali wote watahisi kama ni ukoo mmoja unao saidiana na wenye kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu. Wala mwenye deni hakati tamaa kuweza kulipa deni lake lilio bakia ikiwa hana cha kumalizia hilo deni. Wala haianguki chini azma ya mujaahidi anaye pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuinusuru Dini yake na kukomboa nchi yake kwa sababu ya kukosa mali ya kutimizia makusudio yake. Wala msafiri au mgeni mhitaji aliye mbali na mali yake hakosi wa kumkidhia haja zake kwa kumsaidia mpaka afike kwake. Na juu ya haya Zaka ilikuwa ni njia moja katika njia kubwa ulio chukua Uislamu kukombolea mateka na wafungwa na kuondoa utumwa. Na Uislamu umeongeza kutimiza malengo yake ya kijamii kwa ulimwengu mzima ikatupilia mbali chuki zinazo chusha za kidini, na ikatoa ruhusa Zaka wapewe makafiri ikihitajia haja kuwakopesha. Hali kadhaalika hupewa wale wanao itumikia Zaka, kama kuikusanya na kuigawa. Pia waandishi, na wasafiri, na wanao khasiri kwa ajili ya kupatanisha wenye kugombana, na wanao wasaidia Waislamu katika vita. Ama makusudio ya kiuchumi ya Zaka ni kuondoa ufakiri popote ulipo, na kumsaidia kila mwenye haja kama ilivyo kwisha tangulia.

  6. 23:5
    ۝٥

    Na ambao wanazilinda tupu zao! [5]

    Tanbihi

    [5] Nao wanajihifadhi nafsi zao wasiingiane na wanawake. "Na ambao wanazilinda tupu zao, isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka." Aya hizi zinaambatana na Aya nyengine ziliomo katika Suratun Nur zilio anzia: "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja wao bakora mia." Hakika Aya hizi tukufu zilizo tajwa zinaashiria maovu ya katika umma yanayo tokea kwa uzinzi. Ama katika umma ni kuvurugika nasaba ya watoto isijuulikane, ama katika siha ni sehemu mbili. KWANZA ni katika mwili, mfano wa kisonono, tego, AIDS n.k. Kisonono huweza kuzalisha maradhi ya urithi kwa watoto hata huweza kuleta upofu. Ama tego (Syphilis) huenea katika mishipa ya damu na ya hisiya na huweza kuishia wazimu, na pia huenea mpaka kwa vizazi, na huenda mtoto akafa tumboni au akatoka na kilema. Ama maradhi ya AIDS (Ukimwi) hayo ni maafa yasiyo semeka, Mwenyezi Mungu atulinde nayo. PILI ni kuathirika mishipa ya hisiya na akili, kwani uzinzi huweza kuathiri dhamiri ya mtu, na kuadhibika nayo, na hata mwishoe huweza kuingia wazimu.

  7. 23:6
    ۝٦

    Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. [6]

    Tanbihi

    [6] Isipo kuwa kwa njia ya ndoa ya kisharia, au wenye kumiliki masuria. Hao hawalaumiwi. Zamani utumwa ulikuwa ni jambo la kawaida, na ilikuwa mtu akiweza kuchukua katika wajakazi wake akawafanya kuwa ni wakeze. Na Uislamu ulihalalisha utumwa wa mateka katika vita vilivyo fuata sharia ikiwa maadui nao wanakamata watumwa, basi ilikuwa ni halali kuwatendea wao hali kadhaalika. Ikiwa maadui hawawafanyi mateka kuwa ni watumwa basi ilikuwa haiwafalii Waislamu kuwafanya mateka kuwa ni watumwa.

  8. 23:7
    ۝٧

    Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka. [7]

    Tanbihi

    [7] Mwenye kutaka kuingiliana na mwanamke bila ya kupitia njia hizi mbili, basi huyo amevuka mipaka ya sharia hadi ya kuvuka. Na (hao Waumini) wawe ni wenye kuhifadhi kila walicho pewa kuwa ni amana, ikiwa mali au neno au kitendo au chenginecho, na watimize kila ahadi iliyo baina yao na Mwenyezi Mungu au na watu. Wasikhuni amana, wala wasivunje ahadi.

  9. 23:8
    ۝٨

    Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao! [8]

    Tanbihi

    [8] Na (hao Waumini) wawe ni wenye kuhifadhi kila walicho pewa kuwa ni amana, ikiwa mali au neno au kitendo au chenginecho, na watimize kila ahadi iliyo baina yao na Mwenyezi Mungu au na watu. Wasikhuni amana, wala wasivunje ahadi.

  10. 23:9
    ۝٩

    Na ambao Swala zao wanazihifadhi . [9]

    Tanbihi

    [9] Na wawe wenye kudumisha kutimiza Swala kwa nyakati zake, na kuzitekeleza kwa nguzo zake na unyenyekevu wake, mpaka yapatikane makusudio yake. Nayo ni kuachisha uchafu na maovu.

  11. 23:10
    ۝١٠

    Hao ndio warithi, [10]

    Tanbihi

    [10] Hawa wenye kusifiwa hivi ndio watakao rithi kheri yote na wataipata Siku ya Kiyama. Hawa ndio Mwenyezi Mungu atawafadhili kwa kuwapa Firdausi, ndio pahala pa juu kabisa huko Peponi, wastarehe humo peke yao.

  12. 23:11
    ۝١١

    Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo. [11]

    Tanbihi

    [11] Hawa ndio Mwenyezi Mungu atawafadhili kwa kuwapa Firdausi, ndio pahala pa juu kabisa huko Peponi, wastarehe humo peke yao.

  13. 23:12
    ۝١٢

    Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo. [12]

    Tanbihi

    [12] Yawapasa watu waangalie asli ya kuumbwa kwao; kwani hiyo ni dalili za kuonyesha uwezo wetu zenye kupelekea kumuamini Mwenyezi Mungu, na kuamini kufufuliwa. Kwani Sisi tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.

  14. 23:13
    ۝١٣

    Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti. [13]

    Tanbihi

    [13] Kisha tukaumba vizazi vyake, navyo ni kuwa tulimfanya mtu kwanza tone ya mbegu ya uzazi - yaani maji yenye kila sifa ya uhai wa mwanzo. Tukaiweka kwenye tumbo la uzazi, napo ni pahala pa utulivu palipo lindwa.

  15. 23:14
    ۝١٤

    Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji. [14]

    Tanbihi

    [14] Kisha tukaifanya hii mbegu ya manii baada ya kuipandisha na yai la mwanamke kuwa damu. Kisha damu tukaigeuza kuwa kipande cha nyama, kisha tukafanya mafupa, na mafupa tukayavika nyama. Kisha tukatimiza uumbaji wake mwishoe baada ya kuipulizia roho kuwa kiumbe kingine mbali ili kuanza kumjenga. Shani ya Mwenyezi Mungu imetukuka kwa utukufu wake na uwezo wake. Yeye hana mshabaha wake na yeyote katika kuumba kwake na kutengeza kwake na kuanzisha kwake. Kisha hakika nyinyi wanaadamu baada ya haya mambo yenu tuliyo yataja ni wenye kuyaendea mauti bila ya shaka yoyote.

  16. 23:15
    ۝١٥

    Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa. [15]

    Tanbihi

    [15] Kisha hakika nyinyi wanaadamu baada ya haya mambo yenu tuliyo yataja ni wenye kuyaendea mauti bila ya shaka yoyote.

  17. 23:16
    ۝١٦

    Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa. [16]

    Tanbihi

    [16] Na kisha nyinyi mtafufuliwa Siku ya Kiyama kwa ajili ya kuhisabiwa na kulipwa jaza yenu.

  18. 23:17
    ۝١٧

    Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe. [17]

    Tanbihi

    [17] Na hakika Sisi tumeziumba mbingu saba zilizo nyanyuka juu yenu. Ndani yake vipo viumbe ambavyo hatukughafilika navyo. Tunavihifadhi na tunaviendesha. Na Sisi kabisa hatughafiliki na viumbe vyetu vyote. Bali tunavilinda visipotee na kuharibika, na tunavipangia mambo yao yote kwa hikima. "Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe." Hizo njia saba zilizo tajwa katika hiyo Aya maana yake ni mbingu saba, na kwamba hizo si mbingu moja, na Mwenyezi Mungu haghafiliki na mbingu hizo na viumbe viliomo ndani yake.

  19. 23:18
    ۝١٨

    Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa. [18]

    Tanbihi

    [18] Na Sisi tumeteremsha kutoka mbinguni mvua kwa hikima na kipimo katika umbo lake na kuteremka kwake. Na kusahilisha kwa ajili ya manufaa tumeijaalia ikae juu ya uso wa ardhi na ndani yake chini. Na Sisi hakika ni wenye kuweza kuiondoa wasipate kunafiika nayo. Lakini hatukufanya hayo kwa kukuoneeni huruma. Basi muaminini Mwenye kuiumba na mumshukuru. "Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa." Aya hii tukufu inaashiria maana ya kisayansi yenye kukhusu mzunguko wa maji katika ardhi. Yajuulikana kuwa mvuke unao paa kutoka baharini hupelekea kufanyika mawingu ambayo ndiyo huteremsha mvua. Na hivyo ndio chanzo cha maji matamu juu ya uso wa ardhi, na ndio chombo cha msingi cha uhai wa ardhini. Kutokana na mvua ndio huzuka mito inayo zua uhai katika sehemu kamwe zisio pitikiwa na mvua. Kisha hiyo mito inamiminika baharini, na khulka inarejea tena kutoka baharini kwenda angani na kwendea nchi kavu, na kisha kuingia baharini mara ya pili. Isipo kuwa baadhi ya hayo maji ya mvua yanatulia na yanazama kuhifadhika katika mahodhi ya chini ya ardhi, yakawekeka kwa muda mrefu. Mfano wa hayo ni hayo maji yanayo patikana chini ya Jangwa la Magharibi katika Libya, ambayo yamegunduliwa na watafiti hivi karibuni kutokana na asli yake ya kale. Na huenda maji kama haya yalio hifadhika chini yakapatwa na mabadiliko ya joto wanayo yaita wataalamu wa ilimu ya t'abaka za ardhi (Geology) kuwa ni Mikondo ya Jiolojia, ikenda hiyo na maji mpaka pahala pengine pakavu, ikaleta uhai baada ya kuwa ni maiti. Na Aya hii inaonyesha hikima kubwa ya uenezaji wa maji kwa kipimo, yaani kipimo cha haki na hikima, kwa ajili ya kuleta manufaa na kupinga madhara. Na tena maana nyengine ya Aya tukufu ni kufahamisha apendavyo Mwenye Kuumba, Aliye tukuka, navyo ni kujaalia yawepo maji ya kiasi maalumu katika bahari za ulimwengu kutosha kuwepo mizani ya joto la kufaa katika sayari hii, na ili isiwepo khitilafu kubwa mno baina ya joto la siku za joto, na baridi ya siku za baridi, hata ikawa ni muhali kubakia uhai, kama ilivyo katika sayari nyengine na katika mwezi. Kadhaalika maji ya ardhi yanateremka kwa kiasi maalumu, hayazidi yakafunika ardhi yote, wala hayatindikii sana hata yasipatikane hata kidogo kunyweshea baadhi ya nchi kavu.

  20. 23:19
    ۝١٩

    Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula; [19]

    Tanbihi

    [19] Kwa haya maji tukakuumbieni mabustani ya mitende na mizabibu yenye matunda mengi kwa ajili yenu, na katika hayo nyinyi mnakula.

  21. 23:20
    ۝٢٠

    Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao. [20]

    Tanbihi

    [20] Na tumekuumbieni mti wa zaituni unao ota katika jimbo la Mlima wa Sinai. Katika matunda yake yanapatikana mafuta yanayo kufaeni. Na hizo zaituni ni kitoweo cha chakula kwa wanao kula. "Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao." Aya hii tukufu inathibitisha kuwa mti wa zaituni ni miongoni mwa neema alizo mneemesha Mwenyezi Mungu binaadamu na ambazo baadhi yake zimetajwa katika Aya zilizo tangulia. Na la kuongeza kwenye Aya hii ni kuwa mzaituni ni miongoni mwa miti ya mbao inayo ishi muda mrefu sana, zaidi ya mamia ya miaka. Kwa hivyo hauhitajii juhudi kubwa kwa mtu, bali huendelea kuzaa wenyewe mfululizo. Kadhaalika una sifa ya kuwa daima kijani, unapendeza kuutazama. Uchunguzi wa kisayansi unaonyesha kwamba zaituni ni katika chakula kizuri. Kwani ndani yake imo Protein nyingi. Vile vile zimo chumvi za Calcium, chuma na Phospohorous. Na hivi ni muhimu na vya kutegemewa katika chakula cha binaadamu. Na juu ya hivyo zaituni inayo Vitamin A na Vitamin B. Na kutokana na tunda lake hutolewa mafuta ya zaituni, ambayo ni mafuta bora ya mafuta mepesi. Mafuta haya hutumiwa katika chakula. Uchunguzi wa kitabibu unaongeza kusema kuwa zipo faida nyengine katika mafuta ya zaituni, nazo ni kuwa zinasaidia kwa jumla katika viungo vya usagaji wa chakula, na khasa maini. Nayo yanashinda ubora mafuta yote yanayo tokana na mimea na wanyama, kwa kuwa hayasabibishi maradhi ya mishipa ya damu kama mafuta mengineyo, na kadhaalika yanalainisha ngozi. Na mafuta ya zaituni yana matumizi mengine mengi katika sanaa (ufundi), kwani yanatumiwa katika kufanya sabuni nzuri kabisa, na vitu vinginevyo katika ufanyaji wa vyakula na vitu vya sanaa.

  22. 23:21
    ۝٢١

    Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa - tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika hao manufaa mengi, na pia mnawala. [21]

    Tanbihi

    [21] Na nyinyi mnapata kutokana na nyama hoa, nyama wa kufuga, nao ni ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, mambo yanayo onyesha uwezo wetu na fadhila zetu juu yenu kwa kukuneemesheni. Tunakunywesheni kutoka matumboni mwao maziwa safi, matamu, mepesi kwa wenye kuyanywa. Na mbali ya maziwa mnapata manufaa mengine kama nyama, na sufi, na manyoya. Na kutokana na hao nyinyi mnaishi na mnaruzukiwa.

  23. 23:22
    ۝٢٢

    Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa. [22]

    Tanbihi

    [22] Na juu ya hawa wanyama wa kufuga na marikebu nyinyi mnapanda, na mnapakia mizigo. Basi Sisi tumekuumbieni njia za usafirishaji na upakizi nchi kavu na baharini. Na kwa hizo mnapata kuwasiliana nyinyi kwa nyinyi.

  24. 23:23
    ۝٢٣

    Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye. Basi je! Hamwogopi? [23]

    Tanbihi

    [23] Na katika visa vya watu wa kale pana mazingatio kwa ajili yenu mpate kuamini. Basi Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, naye akawaambia: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu pekee. Kwani nyinyi hamna anaye stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Hamwogopi adhabu yake, na kuondoka neema zake mkimuasi?

  25. 23:24
    ۝٢٤

    Walisema wale wakuu walio kufuru katika watu wake: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani. [24]

    Tanbihi

    [24] Wakubwa wa kaumu yake walio kufuru wakiukanya wito wake na wakizuia watu wasimfuate, walisema: Hapana khitilafu yoyote baina ya Nuhu na nyinyi. Kwani yeye ni mtu kama nyinyi, lakini anataka kujipa ubora juu yenu kwa huu wito wake. Na lau kuwa wapo Mitume wanao toka kwa Mwenyezi Mungu kama anavyo dai yeye, basi ange waletea Malaika. Sisi hatukupata kusikia wito huu katika taarikhi za baba zetu walio tangulia, wala kutumwa binaadamu kuwa ni Mtume.

  26. 23:25
    ۝٢٥

    Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa muda. [25]

    Tanbihi

    [25] Huyu si chochote ila ni mtu mwenye wazimu. Na kwa hivyo wakasema: Ngojeni, na mstahamilieni mpaka ukashifike wazimu wake, au kufike kuangamia kwake.

  27. 23:26
    ۝٢٦

    Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa wamenikanusha. [26]

    Tanbihi

    [26] Nuhu akamwomba Mola wake Mlezi baada ya kukata tamaa kuamini kwao, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru nao, na watie adabu kwa sababu ya kuukadhibisha kwao wito wangu!

  28. 23:27
    ۝٢٧

    Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. [27]

    Tanbihi

    [27] Tukamwambia kwa njia ya ufunuo (wahyi): Unda jahazi, nawe utalindwa na uangalizi wetu. Shari yao haitokupata, nasi tutakuongoza katika kazi yako. Na ikifikilia miadi ya kuwaadhibu, na ukaona tanuri inafoka maji kwa amri yetu, basi waingize katika jahazi katika kila namna ya viumbe vilivyo hai dume na jike. Na waingize ahali zako, isipo kuwa walio kwisha thibitika adhabu yao kwa kukosa kwao Imani. Wala usiniombe kuwaokoa wale walio dhulumu nafsi zao na wakawadhulumu na wengineo kwa ukafiri na uasi. Kwani Mimi nimewahukumia kuwazamisha kwa sababu ya dhulma yao ya ushirikina na uasi. "Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa." Hakika haya maelezo ya Tofani lilio tokea ijapo kuwa ni kwa mukhtasari tu katika hizi Aya tukufu, kwa mwenye akili ya kuzingatia yana maana na mambo ya hakika mengi ya ki-ilimu ambayo yanawapitia watu wengi. Na "tanuri" kwa lugha ni jiko la kuchomea mikate, au pia ni uso wa ardhi na kila chenye kutimbuka maji, na kila penye mkusanyiko wa maji. Na si wepesi kusema kwa yakini taarikhi ya hiyo Tofani, kwani zilitokea tofani nyingi zama za kale, kama katika Babilonia, Bara Hindi na Amerika. Na zipo baadhi ya hadithi za kienyeji mbali mbali zinazo taja khabari ya Tofani. Lakini haielekei kuwa hadithi hizo ndio zimekhusu hii Tofani kubwa au Tofani ya Nuhu. Uchunguzi umethibitisha na pia zimeonekana tofani nyingi ulimwenguni. Na tofani ya mwisho ya ulimwengu mzima ilikuwa sababu yake ni kumalizika kipindi cha barafu cha mwisho, na kuyayuka barafu nyingi ya kaskazini kabisa na kusini kabisa kwa dunia. Na sisi hatujui kwa yakini lini mizani iligeuka na tanuri ikafurika - yaani uso wa ardhi - kwa kupanda kwa ghafla kwa hivyo kuyayuka barafu, hata yakapanda juu maji ya bahari na ya kamwagika maji. Yafaa kutaja kuwa kuyayuka barafu ya zama za barafu za mwisho kulileta hali ya hewa yenye mvua nyingi sana katika sehemu za dunia zilio mbali na huko kaskazini na kusini kabisa kwa ulimwengu, kama vile katika Bahari ya Kati (Mediterenian). Vyo vyote vile ilivyo inakubalika kuwa hatuna ushahidi wa kuweza kusema lini khasa zilikuwa hizo zama za Nuhu na kaumu yake. Yaliyo dhaahiri kuwa yote hayo ni muujiza wa Mwenyezi Mungu. Na katika miujiza ni kuwa Nuhu aliwanasihi watu wake na akawaonya na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu akafunua kuwa atawazamisha ikiwa hawakutengenea. Na tena akamfunulia aunde marikebu. Kisha ikaja amri ya Mwenyezi Mungu, na mizani ikapinduka, na tanuri ikafurika, ikamiminika mvua kuthibitisha aliyo yasema Mwenyezi Mungu kumwambia Nuhu ya kwamba Mwenyezi Mungu anajua kuwa hatoamini mtu katika kaumu yake baada ya wale walio kwisha amini.

  29. 23:28
    ۝٢٨

    Basi utakapo tulia wewe na walio pamoja nawe humo marikebuni, sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliye tuokoa na watu madhaalimu! [28]

    Tanbihi

    [28] Na ukisha panda na ukatua wewe na walio pamoja nawe katika jahazi hiyo basi sema kwa kumshukuru Mola wako Mlezi: Alhamdulillahi! Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye tuokoa na shari ya watu makafiri walio asi.

  30. 23:29
    ۝٢٩

    Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji. [29]

    Tanbihi

    [29] Na useme: Ewe Mola Mlezi! Nijaalie nishuke mashukio yenye baraka, pahala pazuri pa kukaa wakati wa kuteremka nchi kavu. Na unitunukie amani hapo. Kwani ni Wewe tu peke yako unaye weza kututeremsha pahala pa kheri na amani na salama.

  31. 23:30
    ۝٣٠

    Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini Sisi ni wenye kuwafanyia mtihani. [30]

    Tanbihi

    [30] Hakika katika kisa hichi yapo mazingatio na mawaidha mengi. Na hakika Sisi tunawajaribu (tunawapa mitihani) waja wetu kwa kheri na shari. Na ndani ya nafsi zao wana utayarisho wa yote hayo.

  32. 23:31
    ۝٣١

    Kisha baada yao, tukanzisha kizazi kingine. [31]

    Tanbihi

    [31] Tena baada ya kaumu ya Nuhu tukaumba namna ya watu wengine, na wao ni A'adi.

  33. 23:32
    ۝٣٢

    Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu! Hamna mungu asiye kuwa Yeye. Jee, hamwogopi? [32]

    Tanbihi

    [32] Tukawapelekea Huud. Naye ni katika wao. Tukawaambia kwa ulimi wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi hamna Mungu anaye stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Ni Yeye peke yake anaye faa mumwogope. Basi, jee mmeikhofu adhabu yake mkimuasi?

  34. 23:33
    ۝٣٣

    Na wakubwa katika watu wake walioukufuru, na wakakanusha mkutano wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe, katika maisha ya dunia, walisem: Huyu si chochote ila ni mwanadamu kama nyinyi, anakula mlacho, na anakunywa mnywacho. [33]

    Tanbihi

    [33] Na wakubwa katika kaumu yake walio kufuru na kukadhibisha kukutana na Mwenyezi Mungu na mambo ya Akheria ya hisabu na malipo, na tukawapa sehemu kubwa ya starehe na neema, wakasema kwa kukanusha wito wake, na kuwazuia watu wasimfuate: Hapana khitilafu yo yote baina ya Huud na nyinyi. Anakula chakula hicho hicho mnacho kila nyinyi. Na anakunywa vinywaji hivyo hivyo mnavyo vinywa nyinyi. Mfano wa huyu hawezi kuwa Mtume, kwa sababu hana sifa msizo kuwa nazo nyinyi.

  35. 23:34
    ۝٣٤

    Na nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa khasarani. [34]

    Tanbihi

    [34] Na wakawahadharisha kwa nguvu na mkazo, wakiwaambia: Mkimt'ii mtu aliye kama nyinyi kwa utu wake, basi nyinyi hakika mtakuwa mmekhasiri kwa kuwa hamtapata manufaa yo yote mkimfuata.

  36. 23:35
    ۝٣٥

    Hivyo anakuahidini ati ya kwamba mtakapo kufa na mkawa udongo na mifupa kuwa mtatolewa? [35]

    Tanbihi

    [35] Wakawaambia pia katika kukanya kufufuliwa: Hivyo Huud anakuahidini kuwa mtafufuliwa kutoka makaburini kwenu baada ya kwisha kufa kwenu, na mkawa udongo na mafupa yasiyo kuwa na nyama na mishipa?

  37. 23:36
    ۝٣٦

    Hayawi! Hayawi hayo mnayo ahidiwa. [36]

    Tanbihi

    [36] Hayo anayo kuahidini ni ya mbali mno, wala hayatakuwa abadan.

  38. 23:37
    ۝٣٧

    Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na kuishi basi. Wala sisi hatutafufuliwa. [37]

    Tanbihi

    [37] Hapana uhai ila mmoja tu. Nao ndio huu uhai wa duniani, ambao tunauona una mauti na uhai unao tupitia. Kinacho zaliwa kinazaliwa, na kilicho hai kinakufa. Wala hatutofufuliwa baada ya kwisha kufa kabisa.

  39. 23:38
    ۝٣٨

    Huyu si lolote ila ni mtu anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, wala sisi sio wa kumuamini. [38]

    Tanbihi

    [38] Huyu si chochote ila ni mtu aliye mzulia Mwenyezi Mungu, na akadai kwamba Mwenyezi Mungu kamtuma yeye. Na amesema uwongo katika hayo anayo tuitia. Wala hatutomsadiki abadan. *

  40. 23:39
    ۝٣٩

    Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa sababu wananikanusha. [39]

    Tanbihi

    [39] Huud akasema baada ya kwisha kata tamaa kuamini kwao: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na uwatie adabu, kwa sababu ya kuukadhibisha wito wangu.

  41. 23:40
    ۝٤٠

    (Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache watakuwa wenye kujuta. [40]

    Tanbihi

    [40] Mwenyezi Mungu akamwambia Huud kuzidi kutilia nguvu ahadi yake: Baada ya muda mchache watakuja juta, kwa waliyo yafanya, itapo wateremkia adhabu.

  42. 23:41
    ۝٤١

    Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kama takataka zinazo elea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu! [41]

    Tanbihi

    [41] Ukawachukua ukelele mkali ulio wahilikisha kama walivyo stahiki. Tukawafanya kwa udhalili na udhaifu kama vijiti na majani ya miti yanayo chukuliwa na maji ya mvua. Na huko ni kuteketea na kupotelea mbali na rehema kwa madhaalimu kwa ukafiri wao na uasi wao.

  43. 23:42
    ۝٤٢

    Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine. [42]

    Tanbihi

    [42] Kisha baada yao tukawaumba kaumu nyengine wasio kuwa wao, kama kaumu ya Swaleh na ya Luut'i na ya Shuaib.

  44. 23:43
    ۝٤٣

    Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza. [43]

    Tanbihi

    [43] Kila umma una zama zake maalumu, hazitangulii wala hazikawii.

  45. 23:44
    ۝٤٤

    Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipo wafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya hawa, na tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Wakapotelea mbali watu wasio amini. [44]

    Tanbihi

    [44] Kisha tukawatuma Mitume wetu wakifuatana, kila mmoja kwa kaumu yake. Kila akija Mtume kwa kaumu yake waliukadhibisha wito wake. Nasi tukawateketeza mfululizo, na tukazifanya khabari zao ni hadithi za watu kusimuliana na kuzistaajabia. Basi hao kaumu wasio isadiki Haki wala hawaifuati wametengeka mbali na rehema, na wamehiliki.

  46. 23:45
    ۝٤٥

    Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na ishara zetu na hoja zilizo wazi. [45]

    Tanbihi

    [45] Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, tukawapa dalili za kukata kuthibitisha ukweli wa ujumbe wao, na hoja wazi yenye kudhihirisha kuwa wao ni kweli wametumwa kutoka kwangu.

  47. 23:46
    ۝٤٦

    Kumwendea Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna, nao walikuwa watu majeuri. [46]

    Tanbihi

    [46] Tuliwatuma wawili hao kwa Firauni na kaumu yake. Wakakataa kuamini kwa ajili ya takaburi, na wao ni watu walio kuwa wakisifika kwa kiburi, na majivuno, na ujeuri.

  48. 23:47
    ۝٤٧

    Wakasema: Je, tuwaamini wanaadamu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu? [47]

    Tanbihi

    [47] Wakasema kwa mastaajabu na kukanya: Je, tuuamini wito wa watu wawili walio ni wanaadamu kama sisi, na tena watu wao hawa Wana wa Israili ni wenye kutunyenyekea sisi na kutut'ii kama ni watumwa?

  49. 23:48
    ۝٤٨

    Basi wakawakanusha, na wakawa miongoni mwa walio angamizwa. [48]

    Tanbihi

    [48] Basi waliwafanya waongo katika huo wito wao, na wakawa wenye kuhiliki kwa kuzamishwa.

  50. 23:49
    ۝٤٩

    Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka. [49]

    Tanbihi

    [49] Na hakika tulimfunulia Musa Taurati apate kuwaongoa watu wake kwa yaliyomo ndani yake ya uwongozi kwendea hukumu na njia za mafanikio.

  51. 23:50
    ۝٥٠

    Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni Ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipo inuka penye utulivu na chemchem za maji. [50]

    Tanbihi

    [50] Na tumemjaalia Isa bin Maryamu na mama yake, kwa vile kuchukua mimba bila ya kuingiliwa na mtu, na kuzaliwa yeye Isa bila ya baba, kuwa dalili ya kukata ya uwezo wetu wenye kushinda. Na tukamweka Maryamu pahala pa kukaa penye ardhi iliyo nyanyuka na kukunjuka panapo faa kukaa, na pana maji mengi. Na hayo ndiyo yanayo wezesha maisha ya starehe.

  52. 23:51
    ۝٥١

    Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda. [51]

    Tanbihi

    [51] Tumewaambia Mitume wawafikishie watu wao: Kuleni vyakula vya kila namna vya halali na vizuri, na stareheni na ishukuruni neema yangu kwa vitendo vyema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa myatendayo na nitakulipeni kwayo.

  53. 23:52
    ۝٥٢

    Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi. [52]

    Tanbihi

    [52] Na tukawaambia wawafikishie watu wao: Hakika hii Dini niliyo kutumeni muifikishe ni Dini moja kwa mintarafu ya Imani na misingi ya sharia. Na hakika nyinyi ni umma mmoja katika vizazi vyote. Miongoni mwao wapo walio ongoka, na wapo walio potoka. Na Mimi ndiye Mola wenu Mlezi niliye kuamrisheni muifuate, basi iogopeni adhabu yangu pindi mkiasi.

  54. 23:53
    ۝٥٣

    Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali. Kila kundi likifurahia kwa waliyo nayo. [53]

    Tanbihi

    [53] Lakini watu walilikata kata hili jambo la Dini yao. Wapo kati yao walio ongoka, na wapo walio potoka ambao wakafuata matamanio yao, wakafarikiana kwa sababu hiyo wakawa makundi mbali mbali yenye kufanyiana uadui. Kila kikundi kinafurahi kwa walio nayo, kwa kudhania kuwa wao tu ndio walio sibu.

  55. 23:54
    ۝٥٤

    Basi waache katika ghafla yao kwa muda. [54]

    Tanbihi

    [54] Basi, ewe Muhammad, waachilie mbali makafiri na ujinga wao na kughafilika kwao, maadamu wewe umekwisha wanasihi, mpaka Mwenyezi Mungu awahukumie adhabu baadae.

  56. 23:55
    ۝٥٥

    Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyo wapa mali na watoto [55]

    Tanbihi

    [55] Hivyo hawa maasi wanadhani ya kwamba pale Sisi tunapo wawacha wakistarehe na mali na watoto tulio wapa

  57. 23:56
    ۝٥٦

    Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe hawatambui. [56]

    Tanbihi

    [56] Ndio basi Sisi tumekuwa radhi nao, na kheri zikawamiminikia mbio mbio na kwa wingi? Hao ni kama wanyama, hawatambui, kwa kuwa hawazitumii akili zao. Mimi si radhi nao. Na hizi neema ni kuwapururia tu, kuwapa muda.

  58. 23:57
    ۝٥٧

    Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea, [57]

    Tanbihi

    [57] Hakika wale ambao humkhofu Mwenyezi Mungu na humwogopa, na zimejaa ndani yao khofu ya Mwenyewe Subhanahu,

  59. 23:58
    ۝٥٨

    Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini, [58]

    Tanbihi

    [58] Na wale ambao wanaziamini Ishara za Mola wao Mlezi ziliomo ulimwenguni na zinazo somwa katika Kitabu kilicho teremshwa,

  60. 23:59
    ۝٥٩

    Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi, [59]

    Tanbihi

    [59] Na wale ambao hawamshirikishi Mwenyezi Mungu na yeyote,

  61. 23:60
    ۝٦٠

    Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi, [60]

    Tanbihi

    [60] Na wale ambao wanatoa katika vile anavyo waruzuku Mwenyezi Mungu, na wanafanya a'mali yao na hali wao wana khofu wasifanye taksiri, kwa sababu bila ya shaka wao ni wenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kufufuliwa na watahisabiwa,

  62. 23:61
    ۝٦١

    Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia. [61]

    Tanbihi

    [61] Hao wote hukimbilia na a'mali zao kuendea kupata kheri, na wao ni wenye kuwatangulia wengineo katika kupata huko.

  63. 23:62
    ۝٦٢

    Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa. [62]

    Tanbihi

    [62] Na Sisi hatumlazimishi mtu yeyote ila kwa analo liweza kulifanya, kwa sababu limo ndani ya makdara yake. Na kila a'mali katika a'mali za waja zimesajiliwa kwetu katika kitabu, na tutawapa khabari zake kama zilivyo. Na wao hawatadhulumiwa kwa kuongezewa adhabu wala kupunguziwa thawabu.

  64. 23:63
    ۝٦٣

    Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo vinginevyo wanavyo vifanya. [63]

    Tanbihi

    [63] Lakini makafiri kwa sababu ya inadi yao na chuki zao ni wenye kughafilika na kufanya kheri, na kujikalifu kufanya liwezekanalo, na kwamba kuna hisabu ya kuchungua kila kitu. Na mbali na hayo bado wanavyo vitendo vingine viovu wanavyo dumu navyo.

  65. 23:64
    ۝٦٤

    Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio dekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapo yayatika. [64]

    Tanbihi

    [64] Na Sisi tunapo wapatiliza adhabu matajiri wenye kudeka katika starehe zao hupiga makelele na wakayayatika kuomba msaada.

  66. 23:65
    ۝٦٥

    Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi. [65]

    Tanbihi

    [65] Basi tunawaambia: Msiyayatike, wala msiombe msaada hivi sasa. Hamtatoka ndani ya adhabu yangu, wala kuyayatika kwenu hakufai kitu.

  67. 23:66
    ۝٦٦

    Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu, [66]

    Tanbihi

    [66] Hamna udhuru. Kwani Aya zangu zenye kuteremshwa kwa wahyi zilikuwa mkisomewa, nanyi mkizipuuza kwa mapuuza yenye kugeuza hali zenu, na wala hamkuzisadiki, wala hamkuzifuata kwa vitendo.

  68. 23:67
    ۝٦٧

    Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa dharau. [67]

    Tanbihi

    [67] Na nyinyi katika mapuuza yenu mlikuwa mnatakabari na mnafanyia maskhara, mkiutaja huu Wahyi kwa sifa mbaya mnapo kutana katika taanusi zenu za usiku.

  69. 23:68
    ۝٦٨

    Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo wafikia baba zao wa zamani? [68]

    Tanbihi

    [68] Je! Hawa wenye kupuuza wamekuwa wajinga hata hawakuizingatia Qur'ani wakaijua kwamba hii hakika ni Haki? Au huu wito wa Muhammad kwao umekuwa ni namna mbali kuliko walio kuja nayo Mitume wengine kwa kaumu zilizo kwisha tangulia walio ambao baba zao waliwawahi?

  70. 23:69
    ۝٦٩

    Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa? [69]

    Tanbihi

    [69] Au hawamjui Mtume wao Muhammad aliye kulia kati yao katika tabia zake tukufu ambazo hazijapata kuwa na uwongo, na wao hivi sasa wanaukataa wito wake kwa dhulma na husda.

  71. 23:70
    ۝٧٠

    Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na wengi wao wanaichukia Haki. [70]

    Tanbihi

    [70] Au wanasema kuwa huyu ni mwendawazimu? Hasha! Huyu hakika kawaletea Dini ya Haki, na wengi wao wanaichukia haki, kwani hiyo ni kinyume na matamanio yao na mapenzi yao, basi kwa hivyo hawamuamini.

  72. 23:71
    ۝٧١

    Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao. [71]

    Tanbihi

    [71] Ingeli kuwa Haki inafuata matamanio yao ufisadi ungeli enea ulimwenguni, na hawa za nafsi zingeli pambana wenyewe kwa wenyewe. Lakini Sisi tumewapelekea Qur'ani ambayo inawakumbusha haki ambayo inapasa wote wajumuike juu yake. Na juu ya hivyo wao wanayapuuza hayo. "Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao." Hilo neno "Haki" ni tamko lenye maana kadhaa. Huweza kuwa maana yake ni "Mwenyezi Mungu" Subhanahu wa Taa'la , mfano wa kauli yake Mtukufu: "Ametukuka Mwenyezi Mungu wa Haki". Pengine huwa maana yake ni "Qur'ani" , kwa mfano :"Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki". Na huenda kukusudiwa "Dini yote", yaani miongoni mwake ni Qur'ani na Sunna (Hadithi) Sahihi, mfano wa kauli yake: "Na sema: Imekuja Haki na uwongo umetoweka". Na iliyo dhaahiri katika tamko la Haki hapa ni kuwa makusudio yake ni ile maana ya kwanza, yaani "Mwenyezi Mungu" Aliye takasika na kutukuka. Na kwa hivyo maana iliyo kusudiwa na Aya ni: Lau kuwa mwenendo wa Mwenyezi Mungu unafuatana na watakayo na wanayo yapendekeza makafiri mpango usingeli bakia katika hali iliyo simamia shani ya mpango wa mbingu na ardhi na wa viumbe viliomo ndani yake. Lakini Mwenyezi Mungu Mwenye hikima kuu na uwezo wa kutenda na ujuzi wake ulio enea kwa viumbe vyake na hikima yake ikadhamini kwa mpango madhubuti, na Qur'ani kusema kwa uwazi ya kwamba mbingu zina viumbe, anatuelekeza tufahamu: Kwanza kuwa Kuamini hayo kwa jumla ni yakini, tuache tafsili yake mpaka apendavyo Mwenyezi Mungu Subhanahu kuidhihirisha kwa kuambatana na kauli yake: "Tutawaonyesha Ishara zetu angani na katika nafsi zao." Pili: Anatuelekeza kwenye utafiti wa kisayansi kama tunaweza "kwani kufikilia hakika hii inatutilia nguvu Imani yetu. Na Imani ndiyo lengo muhimu katika kuelekea kwetu kwenye Ishara hizo."

  73. 23:72
    ۝٧٢

    Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanao ruzuku. [72]

    Tanbihi

    [72] Kwani, ewe Nabii! Unawataka ujira kwa huku kufikisha kwako ujumbe? Hayakuwa hayo! Kwa kuwa ujira hakika ujira wa Mola wako Mlezi ni bora zaidi kuliko walio nao wao; na Yeye ndiye Mbora wa kutoa.

  74. 23:73
    ۝٧٣

    Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka. [73]

    Tanbihi

    [73] Na hakika wewe, ewe Muhammad, hapana shaka yoyote unawaitia Dini ambayo ndiyo Njia Iliyo Nyooka yenye kupelekea Uwokovu.

  75. 23:74
    ۝٧٤

    Na hakika wale wasio iamini Akhera wanajitenga na Njia hiyo. [74]

    Tanbihi

    [74] Na hakika hao wasio iamini Akhera na yalioko huko ya Pepo au Moto wanaiacha Njia Iliyo Nyooka inayo mhifadhi mpitaji wakaishika njia ya ubabaishi na misukosuko na ufisadi.

  76. 23:75
    ۝٧٥

    Na lau tungeli warehemu na tukawaondolea shida waliyo nayo bila ya shaka wangeli endelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga. [75]

    Tanbihi

    [75] Na lau tungeli warehemu, na tukawaondolea madhara yalio wateremkia katika miili yao, na ukame katika mali yao, na mfano wa hayo, basi hapana shaka yoyote wangeli zidi ukafiri, na wakaendelea katika maasi na jeuri.

  77. 23:76
    ۝٧٦

    Na hakika tuliwatia adhabu kali; lakini hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala hawakunyenyekea. [76]

    Tanbihi

    [76] Na Sisi kwa hakika tuliwapa adhabu kama kwa kuwauwa au kuwaletea njaa. Na wala hawakumnyenyekea Mola wao Mlezi, bali waliendelea na jeuri zao na kiburi chao kiasi ya kuondoka tu hiyo adhabu.

  78. 23:77
    ۝٧٧

    Mpaka tulipo wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa. [77]

    Tanbihi

    [77] Wanashikilia kupuuza kwao mpaka pale tunapo wapatiliza kwa adhabu kali ya njaa au mauwaji hapa duniani huwa tena wanababaika na kukata tamaa, hawaioni njia ya kuvuka.

  79. 23:78
    ۝٧٨

    Na Yeye ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu. [78]

    Tanbihi

    [78] Na yawaje mkamkufuri Mwenyezi Mungu na hali ni Yeye ndiye aliye kuumbieni usikizi mkaisikia Haki, aliye kupena uwezo wa kuona mkauona ulimwengu na viliomo ndani yake, na akakupeni akili mzingatie kwayo utukufu wake mpate kuamini? Hakika nyinyi hamumshukuru Mwenye kuumba vyote hivyo kwa Imani na ut'iifu ila kwa uchache tu, nao ni uchache mno!

  80. 23:79
    ۝٧٩

    Na Yeye ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye mtakusanywa. [79]

    Tanbihi

    [79] Na Yeye ndiye aliye kuumbeni duniani, na kwake Yeye peke yake ndio mtarejeshwa Siku ya Kiyama kwa ajili ya malipo.

  81. 23:80
    ۝٨٠

    Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu? [80]

    Tanbihi

    [80] Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na kwa amri yake na sharia zake ndio usiku na mchana zinapitishana. Na kukhitalifiana kwazo kwa urefu na ufupi, hamzingatii hiyo kuwa ni dalili ya uwezo wake na kupasa kumuamini Yeye na kuamini kufufuliwa? "Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?" Aya zenye kutaja usiku na mchana zimekuja mwahala mwingi katika Qur'ani tukufu, na haya yanaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu wa Haki, Aliye takasika na kutukuka, anawakumbusha waja wake kwa Ishara hii ya uumbaji; na kwa kuwa yamo maana ya ndani inawapelekea wenye kufikiri wazidi kuzingatia na kuchungua. Na kukhitalifiana usiku na mchana kunatokana na pande mbili kubwa: Kwanza: Kukhitalifiana kwa wakati, urefu na ufupi. Na Pili: Kukhitalifiana kwa dhaahiri ya tabia na isiyo onekana. Kwanza - Khitilafu kwa nyakati: Mchana ni kipindi cha wakati baina ya kudhihiri ncha ya jua na inapo potea upeo wa macho, pale linapoonekana kwa jicho kama linagusa uso wa ardhi. Na ilivyo kuwa kwa hakika pale pahali pake pa kuzama jua sipo hapo upeo wa macho, bali tunaona tu hivyo kwa kuwa miale inayo tokana na jua inapinda inapo pita katika matabaka ya anga mpaka inapo fikilia kwenye jicho la mtazamaji, na yeye akaliona jua kama lipo huko upeo wa macho. Lilio kweli ni kuwa kuzama huku kuko chini kuliko upeo wa macho kwa kadri ya dakika 35 kwa kipimo cha mduara. Na Usiku ni kipindi cha kutimiliza wakati wa mchana mpaka kitimilie kipindi cha mzunguko wa ardhi juu ya nafsi yake kutoka magharibi kwendea mashariki. Na baina ya Usiku na Mchana vipo vipindi viwili, navyo vya magharibi na mapambazuko. Na kipindi cha mchana kinakhitalifiana kwa mujibu wa hali ya uwazi wa pahala na musimu wa mwaka. Hali kadhaalika kipindi cha usiku kinakhitalifiana hivyo hivyo kwa kufuatana haya. Na nyakati za Swala na Saumu zinawekwa kufuatana na matulio ya jua huko upeo wa macho. Pili - Khitilafu katika yanayo dhihiri katika tabia: Na madhaahiri haya ni ya namna nyingi, na yanazalikana kutokana na michanganyiko ya miale ya jua, inayo onekana na isiyo onekana, na vitu vilio beba nguvu za umeme pamoja na vifuniko vya anga na nyuso za bahari na majangwa n.k. Kadhaalika yapo mambo ya kuonekana kama kupatwa kwa jua na mwezi, na nyota zenye kufanya mikia, nyota za dasturi na nyota ziendazo na mawingu meupe, na nyota zinazo anguka, na ambazo hufumbwa na ukali wa anga la jua kuonekana mchana, ilhali usiku huonekana wazi. Na muhimu kabisa katika yanayo onekana kuwa ni khitilafu baina ya usiku na mchana ni huu mwangaza wa mchana. Na sababu yake ni kuwa miale inayo toka kwenye jua inapo piga juu ya funiko la anga, ambalo kwa hakika ni sehemu ndogo ndogo zenye chembe chembe ndogo mno za vumbi, hizo hurejesha mwangaza na kuutawanya pande mbali mbali. Ikiwa hali ya anga ni safi, na vile vichembe chembe vya vumbi ni vidogo sana, na jua liko upeo wa macho, basi rangi inayo enea zaidi na inayo onekana kwa macho zaidi, inakuwa ya kibuluu. Ama wakati wa kuchomoza jua au kuchwa basi mbingu huonekana na rangi ya machungwa yenye kupiga wekundu, na mwangu wa kibuluu unatawanyika. Nz kwa hivyo mbingu utosini huelekea kuwa kibuluu khafifu. Na wakati wa kuchwa jua tunaona rangi ya kijani kiasi ya nukta moja hivi au akali pembezoni mwake. Huu huitwa mmetuko wa kijani, na aghlabu yake huonekana unapo kuwa baharini, au nyuma ya kilele cha mlima, au hata kwenye kuta za majumba. Na asli ya kuonekana hivi ni kwa ajili ya kugeuka na kutawanyika miale ya jua hata ikatoa rangi mbali mbali katika hizo kijani. Mukhtasari wa haya ni kuwa miale ya jua ina rangi zinazo onekana na zisizo onekana. Na zinakhitalifiana kwa urefu wa mawimbi yake na kufuata kwake sifa hiyo. Kwa hivyo ndio tunaona kwa migongano hiyo mwangaza wa mchana, mazigazi (sarabi), upinde wa mvua, na rangi za aina mbali mbali zinazo zunguka jua, na mengineyo katika Ishara za mbinguni za ulimwengu tuuonao. Na linapo potea jua jioni mbingu inaonekana kwa rangi mbali mbali kwa sababu ya kuparaganyika mwangaza katika matabaka ya anga la juu. Na kila jua likiteremka unapungua mwangaza wa jioni, na zinapungua zile rangi zake za tabia, mpaka likifikilia daraja ya duara 18.5 mbingu inakuwa kiza. Na wataalamu wa nyakati wameweka kuwa huu ndio wakati wa kuambiwa kuwa usiku umekuwa giza na kwa hivyo ndio wakati wa kuadhinia Sala ya Isha. Na wakati huo khasa ndio huanza mwangaza wa nyota kama sura ya mnara wa sukari na tako lake liko upeo wa magharibi. Na hivyo huendelea katika masiku safi ya siku za baridi mpaka kilele cha ile "cone" au "makhruut'" yaani sura ya mnara wa sukari kifikie utosini. Na kati kati ya usiku hudhihiri rangi za kuchomoza jua kidogo kidogo wakati wa mapambazuko kwanza kama kilele cha ile "cone" au "makhruut'" . Kilele chake hicho huzidi kupanda , na tako lake hutanuka kwenye upeo wa mashariki mpaka inapo dhihiri alfajiri, yaani linapo kuwa jua liko chini ya upeo wa macho wa mashariki kwa kadri ya daraja 18.5 za duara. Na hapo ndio wakati wa kuadhiniwa Swala ya Alfajiri. Na rangi za mapambazuko huanza kudhihiri kwa taratibu kinyume na zile za kuchwea jua magharibi. Na imedhihiri karibuni kuwa jua lina kifuniko chembamba kimetanda angani takriban kimekaribia kufunika anga lote la ardhi. Kifuniko hichi chembemba ndicho kinacho sabibisha kuleta rangi mbali mbali za katika anga. Mambo haya mbali mbali ambayo tumeyataja kama ni mifano isiyo na ukomo imetuonyesha vipi mbingu inavyo kuwa pindi ikiwa hapana mawingu wala hapana pepo za mchanga. Kwani hapo tena huwa ni kiza. Na ikiwa mawingu yamebeba matone ya maji ya mvua basi hayo hupambana na miale ya jua, na hufanyika kama huo upinde wa mvua katika hali maalumu. Na ikiwa mawingu yenyewe ni ya namna fulani ambayo yanabeba maji yaliyo ganda (crystals) "kristali" zenye pande sita, basi maji hayo huingiana na miale ya jua na hiyo miale huvunjika ndani ya hayo maji (kama mwaangaza upitavyo katika kigae cha thuraya, "prism") kisha mwangaza huo ukatoka nje kwa rangi mbali mbali. Na katika hali fulani fulani ndio hutokea rangi nzuri nzuri kulizunguka jua. Na wakati wa weusi wa usiku utaziona nyota kama kwamba zipo karibu nasi na kwa hakika hizo ziko mbali kwa masafa makubwa sana ya kukisiwa kwa miaka na miaka ya mwendo wa mwanga. Vile vile tunaona katika anga hili nyota na sayari na nyota mkia na vimondo kama kwamba zipo karibu, utadhani kuwa khitilafu ya masafa imeondoka kabisa. Na haya ndiyo yanayo tupelekea tutambue maana iliyo fichikana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tumeifanya mbingu kama dari iliyo hifadhiwa; nao wamezipuuza Ishara zetu." Kama tulivyo kwisha eleza kuwa juu ya miale inayo tokana na jua kuna miale inayo tokana na vitu vingine vya eneo la jua vyenye nishat'i ya nguvu, na vyenye kubeba nguvu za umeme. Kadhaalika inatokana na hizo miale iliyo juu ya zambarau Ultra Violet Rays. Vitu hivi na miale hii inapambana na matabaka ya anga la juu, na huathirika kwa mvuto wa smaku kuizunguka dunia. Kwa hivyo hulitibua anga la kaskazini na kusini, na huleta kiza katika mbingu ya kaskaazini kama kwamba ni pazia kuzuia mianga yenye rangi nzuri nzuri za kijani zenye kumili kwenye wekundu na kibuluu. Sura hizi hubaki pengine muda wa saa kadhaa katika mbingu ya kaskazini, na zaidi waweza kuziona masiku kadhaa wa kadhaa linapo kuwa jua linashitadi. Mapazia haya si kama unayaona kaskazini tu, bali hata pia katika kati kati ya dunia. Na katika mbingu vipo vibebaji nguvu za umeme katika mawingu na anga ambavyo huzalikana kutokana navyo radi na mimetuko katika anga la juu. Mambo yote haya yanayo onekana ambayo tunayashuhudia yanatupelekea tufahama maana ya ndani ya kauli yake Subhanahu wa Taa'la: "Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi na kukhitalifana usiku na mchana pana Ishara kwa wenye akili." Kutokana na yaliyo pita kwa mambo ya dhaahiri ya maumbile inabainikana kwamba haya yanakuwa kwa sababu ambazo hayumkini mwanaadamu kuingilia ndani yake. Na hakika ni Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka shani yake, ndiye mwenye kuleta hizo khitilafu za usiku na mchana, wala hawezi binaadamu kabisa siku yoyote kuweza kugeuza usiku wala mchana. Na Yeye Mwenyezi Mungu Aliye tukuka shani yake ndiye anaye zifuatanisha usiku na mchana kwa mizani madhubuti na vipimo baraabara, na anaendesha siku zote mwaka ingia mwaka toka.

  82. 23:81
    ۝٨١

    Bali wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza. [81]

    Tanbihi

    [81] Hawakuzingatia hayo, bali waliwafuata wakanushaji walio kwisha tangulia, wakasema kama walivyo sema hao.

  83. 23:82
    ۝٨٢

    Walisema: Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa? [82]

    Tanbihi

    [82] Katika kukanusha kwao kufufuliwa, walisema: Hivyo sisi tutafufuliwa baada ya kwisha geuka mchanga na mifupa?

  84. 23:83
    ۝٨٣

    Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni visa vya uwongo vya watu wa zamani. [83]

    Tanbihi

    [83] Sisi tuliahidiwa haya, na pia baba zetu waliahidiwa hayo hayo hapo zamani. Haya si chochote ila ni ahadi za uwongo walizo buni watu wa zamani.

  85. 23:84
    ۝٨٤

    Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama nyinyi mnajua? [84]

    Tanbihi

    [84] Ewe Muhammad! Waambie: Ni nani aliye imiliki ardhi na viliomo ndani yake, tangu watu mpaka viumbe vyote? Kama nyinyi mna ujuzi nijibuni.

  86. 23:85
    ۝٨٥

    Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je, hamkumbuki? [85]

    Tanbihi

    [85] Watakiri kuwa ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Basi hapo tena waambie: Hamkumbuki kuwa Mwenye kumiliki hayo ndiye anaye faa kuabudiwa peke yake?

  87. 23:86
    ۝٨٦

    Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi Kuu? [86]

    Tanbihi

    [86] Waambie tena: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi Kuu? (Kiti Kikuu cha Enzi)

  88. 23:87
    ۝٨٧

    Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, hamwogopi? [87]

    Tanbihi

    [87] Watakiri kuwa huyo ni Mwenyezi Mungu. Basi waambie: Je! Hamwogopi matokeo ya ushirikina wenu na ukafiri wenu na kumuasi kwenu Mwenye uumbaji huu wote mkubwa?

  89. 23:88
    ۝٨٨

    Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua? [88]

    Tanbihi

    [88] Waambie vile vile: Nani mwenye ufalme wa kila kitu mkononi mwake, na mwenye madaraka yasio na ukomo katika kila kitu, na ambaye ndiye kwa uwezo wake analinda kila kitu, wala hayamkiniki yeyote kumlinda yeyote na adhabu yake? Kama nyinyi mnaijua jawabu, basi nijibuni.

  90. 23:89
    ۝٨٩

    Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi vipi mnadanganyika? [89]

    Tanbihi

    [89] Watakiri kuwa hakika huyo ni Mwenyezi Mungu. Waambie: Basi huwaje mkadanganyika kwa pumbao na kuchochewa na mashetani, na mkaacha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu?

  91. 23:90
    ۝٩٠

    Bali tumewaletea Haki, na kwa yakini hao ni waongo. [90]

    Tanbihi

    [90] Hakika Sisi tumewabainishia Haki kwa ndimi za Mitume, na wao ni waongo katika kila jambo linalo khitalifu na Haki hii.

  92. 23:91
    ۝٩١

    Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hanaye mungu mwengine. Inge kuwa hivyo basi kila mungu angeli chukua alivyo umba, na baadhi yao wangeli washinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazo msifu. [91]

    Tanbihi

    [91] Mwenyezi Mungu hakumchukua yeyote kuwa ni mwanawe. Yeye ametakasikia na hayo. Wala hana mshirika. Angeli kuwa na mshirika basi kila mmoja wao angejipa madaraka ya pekee kwa alivyo viumba, na vikawa ndio milki yake, na wangeli gombana wenyewe kwa wenyewe kama wanavyo onekana wafalme wanavyo fanya. Na ulimwengu ungeli fisidika kwa mizozano hiyo. Basi Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wayasemayo washirikina yanayo kwenda kinyume na Haki.

  93. 23:92
    ۝٩٢

    Mjuzi wa siri na dhaahiri, na ametukuka juu ya hayo wanayo mshirikisha nayo. [92]

    Tanbihi

    [92] Na Yeye amevizunguka vitu vyote kwa kuvijua. Anajua tusiyo yaona na tunayo yaona. Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mnasibisha nayo makafiri kuwa ati ana washirika.

  94. 23:93
    ۝٩٣

    Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha adhabu waliyo ahidiwa, [93]

    Tanbihi

    [93] Ewe Nabii! Sema: Ukiwateremshia adhabu ulio waahidi hapa duniani nami nipo pamoja nao,

  95. 23:94
    ۝٩٤

    Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu madhaalimu hao. [94]

    Tanbihi

    [94] Basi nakuomba usinifanye mwenye kuadhibiwa pamoja na makafiri waasi.

  96. 23:95
    ۝٩٥

    Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyeshsa tuliyo waahidi. [95]

    Tanbihi

    [95] Na Sisi tunaweza kwa utimilivu kukuonyesha adhabu tulio waahidi ikiwateremkia. Basi wewe tuwa ujue kuwa tutashinda.

  97. 23:96
    ۝٩٦

    Kinga maovu kwa kutenda yaliyo mema zaidi. Sisi tunajua wayasemayo. [96]

    Tanbihi

    [96] Wewe endelea na wito wako, na ukabili uovu wao kwa vitendo vilivyo vizuri kama kusamehe au vyenginevyo. Na Sisi tunajua vyema wanakutaja vipi wewe, na wanavyo usema kwa ubaya huo wito wako kwa uwovu na uzushi. Na Sisi tutawalipa kwa hayo.

  98. 23:97
    ۝٩٧

    Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi wa mashet'ani. [97]

    Tanbihi

    [97] Nawe sema: Ewe Mola Mlezi! Najilinda kwako na wasiwasi wa mashetani wasiniingilie katika nafsi yangu kwa vitendo visio kupendeza.

  99. 23:98
    ۝٩٨

    Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie. [98]

    Tanbihi

    [98] Na ewe Mola Mlezi! Najilinda kwako wasiwe nami katika kitendo chochote ili kitendo hicho kiwe kimetakasika, safi, kwa ajili ya ridhaa yako tukufu.

  100. 23:99
    ۝٩٩

    Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe. [99]

    Tanbihi

    [99] Wanaendelea kuwakanusha mpaka utapo fika wakati wa kufa mmoja wao hujuta na akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nirudishe duniani.

  101. 23:100
    ۝١٠٠

    Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa. [100]

    Tanbihi

    [100] Ili nipate kufanya a'mali njema katika mali au wakati nilio acha. Wala ombi lake halitokubaliwa. Kwani haya ni maneno anayasema bila ya faida, hayakubaliwi. Na pindi akikubaliwa hatotenda kitu. Na juu ya yote hatorudi kabisa! Kwani mauti ni kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani mpaka Mwenyezi Mungu atapo wafufua.

  102. 23:101
    ۝١٠١

    Basi litapo pulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana. [101]

    Tanbihi

    [101] Ukifika wakati wa kufufuliwa tutawafufua kutoka makaburini kwao. Na hayo ni kwa mfano wa kupulizwa tarumbeta watafufuka nao wamefarikiana. Hapana mtu utaomfaa ujamaa wake na fulani. (Ujamaa Kiswahili maana yake makhusiano ya nasaba, sio usoshalisti.) Wala hapana mtu atae muomba mtu kitu cha kumfaa. Kwani kila mmoja wao siku hiyo atakuwa kashughulika na lake.

  103. 23:102
    ۝١٠٢

    Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa. [102]

    Tanbihi

    [102] A'mali (Vitendo) ndio mizani ya kupimia. Mwenye Imani nzuri na vitendo vyema atakuwa na uzito katika mizani ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio walio fuzu.

  104. 23:103
    ۝١٠٣

    Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu. [103]

    Tanbihi

    [103] Na asiye kuwa na thawabu au vitendo vyenye uzito mbele ya Mwenyezi Mungu, hao ndio walio zikhasiri nafsi zao kwa kuziuza kwa Shetani. Nao wataadhibiwa Motoni, wadumu humo.

  105. 23:104
    ۝١٠٤

    Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizo kunjana. [104]

    Tanbihi

    [104] Moto utawababua nyuso zao, nazo zitakuwa zimekunjana kwa uwovu wa mwisho wao.

  106. 23:105
    ۝١٠٥

    Je! Hazikuwa Aya zangu mkisomewa, na nyinyi mkizikanusha?. [105]

    Tanbihi

    [105] Mwenyezi Mungu anawakemea na anawaambia: Aya zangu zilizo kuwa zinateremshwa zilikuwa mkisomewa duniani, nanyi mkizikadhibisha.

  107. 23:106
    ۝١٠٦

    Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio potea. [106]

    Tanbihi

    [106] Watasema nao wanakiri makosa yao : Ewe Mola wetu Mlezi! Maasi yetu yalikuwa mengi, ndio yakatupatia mashaka, na tukawa wenye kupotea tukaiacha njia ya sawa.

  108. 23:107
    ۝١٠٧

    Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli sisi ni wenye kudhulumu. [107]

    Tanbihi

    [107] Na watasema: Mola wetu Mlezi! Tutoe Motoni na uturejeshe duniani. Basi tukirudi tena kwenye ukafiri na uasi basi tutakuwa kweli ni twenye kujidhulumu nafsi zetu.

  109. 23:108
    ۝١٠٨

    Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeze. [108]

    Tanbihi

    [108] Na Mwenyezi Mungu atawaambia kwa kuwadharau na kuwabeza: Kaeni humo kwa madhila na unyonge, wala msiseme nami kabisa!

  110. 23:109
    ۝١٠٩

    Bila ya shaka lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanao rehemu. [109]

    Tanbihi

    [109] Mimi sikukudhulumuni, bali nyinyi mmejidhulumu wenyewe. Kwani Waumini wema katika waja wangu walikuwa wakisema duniani: Ewe Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe ndiwe Mbora wa wanao rehemu.

  111. 23:110
    ۝١١٠

    Lakini nyinyi mliwakejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka. [110]

    Tanbihi

    [110] Na nyinyi daima mlikuwa mkiwafanyia maskhara, mpaka maskhara yenu yakakusahaulisheni kunikumbuka Mimi na kuniabudu Mimi. Basi hamkuamini wala hamkut'ii. Nanyi mlikuwa mkiwacheka kwa kejeli.

  112. 23:111
    ۝١١١

    Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyo subiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu. [111]

    Tanbihi

    [111] Hakika Mimi hii leo nimewalipa wao kwa mafanikio, kwa kuwa waliyavumilia maskhara yenu na maudhi yenu.

  113. 23:112
    ۝١١٢

    Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka?. [112]

    Tanbihi

    [112] Mwenyezi Mungu atawaambia makafiri: Mliishi miaka mingapi huko duniani?

  114. 23:113
    ۝١١٣

    Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu. [113]

    Tanbihi

    [113] Watasema kwa kuyaona mafupi maisha yao kwa adhabu wanayo ikuta: Tuliishi muda wa siku moja au baadhi ya siku hivi. Basi waulize wanao weza kuhisabu, sisi tumeshughulishwa na hii adhabu.

  115. 23:114
    ۝١١٤

    Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua. [114]

    Tanbihi

    [114] Basi Mwenyezi Mungu atawaambia: Hamkuishi duniani ila muda mchache tu. Na lau ingeli kuwa mnajua malipo ya ukafiri na uasi na kwamba starehe ya duniani ni chache mngeli amini na mkat'ii.

  116. 23:115
    ۝١١٥

    Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?. [115]

    Tanbihi

    [115] Je? Mlidhani kuwa tuliwaumbeni bila ya hikma, ndio mukafanya ufisadi katika ardhi, na mkadhani kuwa hamtafufuliwa mpate kulipwa.

  117. 23:116
    ۝١١٦

    Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu. [116]

    Tanbihi

    [116] Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Na Yeye ndiye Mwenye kumiliki ufalme wote. Hapana Mwenye kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye. Na Yeye ndiye Mwenye A'rshi Tukufu.

  118. 23:117
    ۝١١٧

    Na anaye muomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi. [117]

    Tanbihi

    [117] Na mwenye kumuabudu mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu hana ushahidi wa kumfanya huyo astahiki kuabudiwa. Hakika Mwenyezi Mungu atampa adhabu kwa ushirikina wake bila ya shaka yoyote. Hakika makafiri hawaongokewi. Bali watao ongokewa ni Waumini.

  119. 23:118
    ۝١١٨

    Nawe sema: Mola wangu Mlezi! Samehe na urehemu nawe ni Mbora wa wanao rehemu. [118]

    Tanbihi

    [118] Na sema, ewe Nabii, ukimlingania Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea: Ewe Mola wangu Mlezi! Nisamehe dhambi zangu, na nirehemu. Kwani Wewe ni Mbora wa wanao rehemu, kwa sababu rehema yako imeenea na ipo karibu kwa watendao mema.

  120. Sura An-Noor

    سُورَةُ النور
  121. 24:1
    ۝١

    HII NI SURA Tuliyo iteremsha na tukailazimisha; tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke. [1]

    Tanbihi

    [1] Sura hii tumeifunua na tumewajibisha hukumu zake, na tumeteremsha ndani yake dalili zilizo wazi za kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na upweke wake, na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwake, ili mpate kuwaidhika.

  122. 24:2
    ۝٢

    Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini. [2]

    Tanbihi

    [2] Na miongoni mwa hukumu hizo ni hukumu ya mwanamke na mwanamume wenye kuzini. Basi kila mmoja wao mpigeni fimbo mia. Wala huruma kwao isikuzuieni kutimiza hukumu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Kwani yanayo takikana na Imani ni kukhiari kumridhi Mwenyezi Mungu kuliko kuwaridhi watu. Na wahudhurie baadhi ya jamaa Waumini waone hiyo adhabu inavyo tekelezwa, ili adhabu hiyo iwatishe wenginewe wasitende hivyo.

  123. 24:3
    ۝٣

    Mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo ya. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke meharimishwa kwa Waumini. [3]

    Tanbihi

    [3] Mwanamume muovu aliye zoea uzinifu hapendi kumwoa ila mchafu anaye zini au mshirikina. Na mwanamke mchafu ambaye kazi yake ni uzinifu hapendelei kuolewa ila na mchafu anaye zini;au mshirikina. Na ndoa namna hii haiwaelekei Waumini, kwa kuwa imeshabihi fiski na kupelekea kutuhumiwa. Haya ikiwa haikupita toba. Na tafsiri ya haya ni kuwa inabainishwa tabia za washirikina au wazinifu kuwa wao hawapendi ila mambo ya ufisadi tu. Na kwa mujibu wa maoni ya Hambali na Ahli-Dhaahir (na pia Ibadhi) haisihi ndoa ya mwanamume mzinifu au mwanamke mzinifu kabla ya toba.

  124. 24:4
    ۝٤

    Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu . [4]

    Tanbihi

    [4] Na wanao watuhumu wanawake wenye hishima zao wasio na makosa kwa tuhuma ya uzinzi bila ya kuleta mashahidi wane wa kuthibitisha tuhuma yao, waadhibuni kwa kuwapiga fimbo thamanini, na wala ushahidi wao usikubaliwe tena kwa jambo lolote muda wa uhai wao. Basi hawa ndio wanao faa kuitwa kwa jina la walio toka vibaya kwenye mipaka ya Dini. Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 2-4 " Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini. Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu." Makosa katika Sharia ya Kiislamu ni mambo yaliyo harimishwa na Mwenyezi Mungu akayakemea kwa kuyawekea adhabu au izara ya kufedhehesha. Na maharimishwa hayo ama ni kutenda kilicho katazwa kukitenda, au kuacha kutenda kilicho amrishwa na Sharia kutendwa. Na sababu ya kuharimishwa haya yaliyo katazwa ni kuwa hayo ni kupiga vita moja katika maslaha yanayo kubaliwa katika Uislamu. Na maslaha hayo yanayo kubaliwa ni matano, nayo ni: 1. Kuhifadhi nafsi. 2. Kuhifadhi Dini. 3. Kuhifadhi akili. 4. Kuhifadhi mali 5. Kuhifadhi hishima. Kuuwa kwa mfano ni kuipiga vita nafsi. Na kurtadi, kutoka katika Uislamu, ni kuipiga vita Dini. Na kutumia vinavyo levya ni kuipiga vita akili. Na wizi ni kuyapiga vita mali. Na uzinzi ni kuipiga vita hishima. Na wanazuoni wa ilimu ya Fiqhi (Sharia) wameyagawa makosa sehemu mbali mbali. Lakini sisi yatutosha kwa sababu ya kueleza Aya hizi kugawa kwa mujibu wa uzito wa adhabu zake, na namna ya kiasi chake. Nayo yamegawika mafungu matatu: 1. H'udud, yaani Adhabu. 2. Kisasi au Diya 3. Izara, au Fedheha. Ama H'udud, au Adhabu, ni makosa ambayo yanaonekana kuwa yanaingilia kuvunja Haki ya Mwenyezi Mungu, au kuwa Haki ya Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi ndani yake kuliko haki ya binaadamu. Na kwa hivyo ndio Mwenyezi Mungu akaiwekea MIPAKA ndio maana khasa ya H'udud. Kaiwekea mipaka adhabu yake katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume s.a.w. Ama makosa ya Kisasi na Diya ni makosa ambayo baadhi kubwa yake yamewakhusu wenyewe waja. Mwenyezi Mungu amewekea adhabu za baadhi yake katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume s.a.w., na amewaachilia mengine wapime wenyewe wenye madaraka. Mfano wa hayo makosa ya kumwaga damu, kama kuuwa na kukata viungo, na kujuruhu. Ama makosa ya Izara, Uislamu umejitosheleza kwa kutaja mwisho wa ukali na mwisho wa upole katika adhabu zao, na kuachia yaliyo baki wenye kutawala wahukumie kwa kila kosa kwa mujibu wa hali na zama yanapo tokea makosa. Makosa ya H'udud ni saba: 1. Uzinzi. 2. Kuzulia wanawake mahashumu wasio na makosa. 3. Udhalimu. 4. Wizi. 5. Uharamia. 6.Ulevi. 7. Kurtadi. (Kutoka katika Uislamu). Mwenyezi Mungu ameyawekea mipaka yote makosa hayo na ameyaleta kwa hisabu yake katika Qur'ani, kama alivyo wekea adhabu zake katika Qur'ani vile vile, isipo kuwa adhabu ya mwenye kuzini naye amewahi kuoa, yaani Zaani Muh's'an, ambaye hupigwa mawe, na mlevi na adhabu yake ni fimbo thamanini, na adhabu ya mwenye kurtadi ambaye jaza yake ni kuuwawa. Hayo yamekuja katika Sunna. Na zimezoea hizi kanuni za kuundwa na watu katika kupinga makosa ya uzinzi kwa adhabu khafifu kama vile kifungo, hata ndio uchafu ukaenea kati ya watu, na fiski na ukahaba ukazagaa, na hishima zikapotea, na maradhi yakakithiri, na nasaba za ukoo zikachanganyika. Katika jambo la ajabu ni kuwa hizi kanuni za kisasa za nchi zinazo ambiwa za kistaarabu ndio zinazo yalinda makosa haya. Katika kanuni za adhabu za Kifaransa, kwa mfano, wazinzi wasio oa wala kuolewa hawapati adhabu yoyote maadamu wao wakiwa wamekwisha fikilia utu uzima. Kwa kuwa ati uhuru wao wa binafsi unataka waachiliwe wajifanyie wenyewe watakalo. Ama mzinzi mwanamume aliye na mke, au mwanamke mwenye mume, basi huyo adhabu yake ni kifungo. Lakini mwana sharia wa serikali haingii kuchunguza ila akipata mashtaka kutokana na mume au mke. Na inaonyesha kuwa ni haki ya mume tu kuwa hilo kosa limetokea au la, kwani ikiwa yeye ndiye aliye fikisha mashtaka, basi yeye anaweza kuyafuta pia, na uchunguzi utasita. Na yeye anaweza kumsamehe mkewe akatoka gerezani kabla ya kutimiza muda wa kifungo chake ijapo kuwa hukumu ilikuwa ni juu yake huyo mwanamke mwishoni. Na wapo baadhi ambao ati wanaushutumu Uislamu kwa ukali wake kushadidia kwake kuadhibiwa wazinifu. Yaliyo elekea zaidi ni kuwa lau wangeli zingatia kuwa kama ilivyo kuwa adhabu ni kali, hali kadhaalika umeshadidiwa ushahidi kwa jambo hili. Kwani ijapo kuwa katika kosa la mauwaji yatosha ushahidi wa mashahidi wawili waadilifu, katika uzinzi ni lazima wapatikane mashahidi wane waadilifu walio ona kitendo hicho kwa macho yao, au aungame mkosa! Hayo, na tunaona kuwa Qur'ani Tukufu imelazimisha kuwa kupigwa hizo fimo kuwe jahara ili mkosa ajuulikane, na iwe ni onyo kuwakhofisha wenginewe.

  125. 24:5
    ۝٥

    Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu. [5]

    Tanbihi

    [5] Lakini mwenye kutubu katika wao akajuta kwa maasi yake, na akaazimia kuwa mt'iifu na kuonyesha ukweli wa toba yake kwa kwenda kwake mwendo mwema, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe kumuadhibu.

  126. 24:6
    ۝٦

    Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli. [6]

    Tanbihi

    [6] Na hao wanao watuhumu wake zao kuwa wamezini na hawana mashahidi wanao takikana kushuhudia ukweli wa tuhuma yao, basi anatakikana mmoja wa hao kama anataka isimpate adhabu, ashuhudie kwa Mwenyezi Mungu mara nne kuwa yeye ni mkweli katika hiyo tuhuma yake.

  127. 24:7
    ۝٧

    Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo. [7]

    Tanbihi

    [7] Na mara ya tano aseme kuwa yeye anastahiki kutengwa na rehema ya Mwenyezi Mungu akiwa ni mwenye kusema uwongo kwa hayo.

  128. 24:8
    ۝٨

    Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo. [8]

    Tanbihi

    [8] Baada ya haya mwanamke akinyamaza kimya itampasa kupata adhabu ya uzinzi. Ili kujikinga na adhabu yampasa ashuhudie kwa Mwenyezi Mungu mara nne kwamba mumewe ni mwongo kumtuhumu yeye kwa uzinzi.

  129. 24:9
    ۝٩

    Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama mumewe yu miongoni mwa wanao sema kweli. [9]

    Tanbihi

    [9] Na ataje katika mara ya tano kuwa yeye mwanamke anastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu imshukie ikiwa mumewe ni mwenye kusema kweli katika tuhuma yake.

  130. 24:10
    ۝١٠

    Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba. [10]

    Tanbihi

    [10] Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni fadhila na akakurehemuni, na kuwa Yeye ni Mwingi wa kukubali toba za waja wake, na Mwenye hikima katika vitendo vyake vyote, asingeli kufanyieni sharia za hukumu hizi, na angeli fanya haraka kukuadhibuni duniani kwa maasia.

  131. 24:11
    ۝١١

    Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa. [11]

    Tanbihi

    [11] Hakika hao walio zua uwongo ulio potoka na kila uwongofu kumzulia Aisha, mke wa Nabii s.a.w. walipo mtangazia uzushi, ni kikundi wanao ishi pamoja nanyi. Msidhani kituko hichi ni shari kwenu, bali ndiyo kheri yenu; kwa sababu kimewapambanua baina ya wanaafiki na Waumini wa kweli. Na ukadhihiri ukarimu wa walio wema na wenye kuingiwa na uchungu. Na kila mtu katika hawa walio tuhumu watapata malipo yao kwa mujibu wa kadri alivyo shiriki katika uzushi huu. Na mkuu wa kikundi hichi ndiye ataye pata adhabu kubwa kwa ukubwa wa makosa yake.

  132. 24:12
    ۝١٢

    Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri? [12]

    Tanbihi

    [12] Ilikuwa inavyo takikana kwa Imani ni kuwa wakati wa kusikia huu uzushi, ni Waumini wanaume na wanawake wajidhanie nafsi zao kheri ya usafi na unadhifu, na waseme kwa kupinga: Huu ni uwongo ulio wazi umezuliwa, kwa kuwa haya yamemkhusu bora ya Mitume na bora ya wanawake walio wa kweli.

  133. 24:13
    ۝١٣

    Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo. [13]

    Tanbihi

    [13] Je! Hao wazushi walileta mashahidi wane wa kushuhudia hayo waliyo yasema? Hawakufanya hayo...Na ikiwa hawakufanya basi hao kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu ni waongo.

  134. 24:14
    ۝١٤

    Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo jiingiza. [14]

    Tanbihi

    [14] Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni fadhila kwa kubainisha hukumu, na hakukurehemuni duniani kwa kuacha kuleta adhabu kwa haraka, na Akhera kwa kukusameheni, angeli kuteremshieni adhabu kubwa kwa sababu ya kujiingiza kwenu katika uzushi huu.

  135. 24:15
    ۝١٥

    Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa. [15]

    Tanbihi

    [15] Mmezichukua khabari hizo kwa ndimi zenu na mkazieneza kati yenu. Wala nyinyi hamkujua kuwa hizo ni khabari za kweli, na mkaona jambo hili ni dogo si la kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu, au sana adhabu yake ni ndogo; na ilhali ni jambo kubwa kweli la kuadhibiwa adhabu kali na Mwenyezi Mungu.

  136. 24:16
    ۝١٦

    Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa! [16]

    Tanbihi

    [16] Yanayo faa ni kuwa baada ya kusikia maneno haya ya uwongo ni kuambizana msiyazungumze, kwa sababu si laiki yenu, na mustaajabie kuzuliwa uwongo muovu wa namna hii wa khatari.

  137. 24:17
    ۝١٧

    Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini! [17]

    Tanbihi

    [17] Na hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni msirudie tena kufanya maasi namna hii kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini wa kweli. Kwani sifa za Imani zinapingana na mwendo huu.

  138. 24:18
    ۝١٨

    Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. [18]

    Tanbihi

    [18] Na Mwenyezi Mungu anakuteremshieni Aya zenye kuonyesha hukumu kwa uwazi dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa Ujuzi, hapana asicho kijua katika vitendo vyenu. Naye ni Mwenye hikima kwa kila anacho kitungia sharia na kukiumba. Kwani kila sharia zake na uumbaji wake ni kwa mujibu wa hikima.

  139. 24:19
    ۝١٩

    Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui. [19]

    Tanbihi

    [19] Hakika hao wanao penda kutangaza machafu, wakayatangaza baina ya Waumini watapata adhabu yenye kutia uchungu duniani kwa mateso yaliyo kwisha pasishwa, na Akhera watatiwa Motoni ikiwa hawato tubu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote, za dhaahiri na zilizo fichikana. Na nyinyi hamjui anayo yajua Yeye.

  140. 24:20
    ۝٢٠

    Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu. [20]

    Tanbihi

    [20] Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake kwenu, na kuwa Yeye ni Mwingi wa upole, Mkunjufu wa rehema, asingeli kubainishieni hukumu, na angeli kuleteeni mateso kwa haraka hapa duniani kwa maasi yenu.

  141. 24:21
    ۝٢١

    Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. [21]

    Tanbihi

    [21] Enyi mlio amini! Hifadhini nafsi zenu kwa Imani. Wala msimfuate Shetani anaye kuvutieni kwenda tangaza uchafu na maasi baina yenu. Na mwenye kumfuata Shetani basi huyo amekwisha a'si, kwani Shetani anaamrisha madhambi makubwa makubwa na maasi mabaya. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake kwenu kwa kubainisha hukumu na kukubali toba ya wenye kuasi asinget'ahirika hata mmoja wenu na uchafu wa maasi. Lakini Mwenyezi Mungu anamsafisha mwenye kumuelekea Yeye kwa kumwezesha kuwa mbali na maasi, au kwa kumsamehe kwa kutubu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia kila kauli, Mwenye kujua kila kitu, na atakulipeni kwayo.

  142. 24:22
    ۝٢٢

    Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [22]

    Tanbihi

    [22] Wala wasiape wema wenu wenye nafasi kuwa watazuia kuwafanyia hisani jamaa zao na masikini na walio hama makwao katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wengineo kwa sababu za kibinafsi, kama vile kuwa wamewatendea uovu fulani. Lakini inatakikana wawasamehe na wayaachilie mbali makosa yao. Na ikiwa mnapenda Mwenyezi Mungu akusameheni maovu yenu basi wafanyieni wanao kufanyieni mabaya mfano wa anavyo kufanyieni nyinyi Mola wenu Mlezi. Na fuateni mwendo wake kwani Yeye ni Mkunjufu wa kusamehe na kurehemu. Aya hii imeteremka pale Abu Bakar r.a. alipo apa kumkatia msaada jamaa yake Mist'ah bin Uthaathah hapo alipo ingia Mist'ah katika uzushi alio zuliwa bibi Aisha r.a.

  143. 24:23
    ۝٢٣

    Hakika wanao wasingizia wanawake, wanao jihishimu, walio ghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu kubwa. [23]

    Tanbihi

    [23] Hakika hao wanao wasingizia wanawake wema walio safi, ambao hawadhaniwi hayo, bali wao kwa kumshughulikia Mwenyezi Mungu hata wameghafilika na hayo wanayo singiziwa, Mwenyezi Mungu atawatenga mbali na rehema yake katika dunia na Akhera, na watapata adhabu kubwa ikiwa hawatotubu.

  144. 24:24
    ۝٢٤

    Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyatenda. [24]

    Tanbihi

    [24] Adhabu hiyo itakuwa Siku ya Kiyama ambapo itakuwa hapana njia ya kuikataa. Bali waliyo yatenda yatathibiti juu yao, kwa kuwa zitawashuhudia ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao, kwa madhambi yote waliyo yatenda. Na hayo ni kwa kudhihiri athari ya vitendo vyao juu ya viungo hivyo, au kwa kutamkishwa na Mwenyezi Mungu ambaye anatamkisha kila kitu.

  145. 24:25
    ۝٢٥

    Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi. [25]

    Tanbihi

    [25] Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iliyo kwisha hukumiwa wapewe kwa ukamilifu wake bila ya upungufu. Na hapo wataujua kwa ujuzi wa yakini Ungu wa Mwenyezi Mungu na hukumu za Sharia yake, na ukweli wa ahadi yake na kitisho chake. Kwani yote hayo yatakuwa wazi hayana kificho.

  146. 24:26
    ۝٢٦

    Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu. [26]

    Tanbihi

    [26] Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na kadhaalika wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Basi yamkini vipi kuwepo uwovu katika wema ulio hifadhiwa nao ni mke wa mwema muaminifu Mtume Mtukufu s.a.w.? Na wema hawa wamehifadhika na tuhuma wanazo wasingizia hao waovu. Na wao wana maghfira ya Mwenyezi Mungu kwa vijidhambi vidogo vidogo ambavyo mwanaadamu hakosekani kuwa navyo. Na watapata ukarimu mkubwa wa kupata neema za Peponi.

  147. 24:27
    ۝٢٧

    Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka. [27]

    Tanbihi

    [27] Enyi mlio amini! Msiingie katika nyumba zisio kuwa zenu ila baada ya kutaka idhini kwa wakaazi wake na mkaruhusiwa kuingia, na baada ya kuwatolea salamu wakaazi wake - na salamu ni bora kwenu kuliko kuingia tu bila ya kutoa salamu. Na Mwenyezi Mungu amekuwekeeni sharia hii ili mpate kunasihika na muifuate.

  148. 24:28
    ۝٢٨

    Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda. [28]

    Tanbihi

    [28] Na ikiwa katika hizo nyumba hamkumkuta mtu wa kukupeni idhini basi msiingie mpaka aje wa kukuruhusuni. Na ikiwa hakukuruhusuni na akakutakeni mrudi nyuma, basi rudini; wala msishikilie kutaka ruhusa ya kuingia. Kwani kurejea nyuma ni hishima zaidi na usafi zaidi kwa nafsi zenu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote na atakulipeni, basi msende kinyume na uwongozi wake.

  149. 24:29
    ۝٢٩

    Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisio kaliwa ambazo ndani yake yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yadhihirisha na mnayo yaficha. [29]

    Tanbihi

    [29] Na mkitaka kuingia nyumba za umma zisio kaliwa na watu makhsusi na ndani yake zipo haja zenu, kama vile maduka, mahoteli, nyumba za ibada, hapana ubaya kuingia bila ya kutaka ruhusa. Na Mwenyezi Mungu anajua kwa ujuzi wa timamu kabisa vitendo vyenu vyote vya dhaahiri na vilivyo fichikana. Basi tahadharini na kwenda kinyume naye.

  150. 24:30
    ۝٣٠

    Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayo yafanya. [30]

    Tanbihi

    [30] Ewe Nabii! Waambie Waumini katika yanayo pelekea zina na kutilisha shaka, wasitazame yanayo harimishwa kutazama, nayo ni tupu za wanawake na sehemu za uzuri wao, na wanaume wahifadhi tupu zao kwa kuzisitiri na kuto zitumilia kwa njia isiyo ruhusiwa na Sharia. Adabu hiyo ndio ina hishima zaidi na safi zaidi kwao wasiingie katika maasi na tuhuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara yote wayatendayo, na atakuja walipa kwayo.

  151. 24:31
    ۝٣١

    Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa. [31]

    Tanbihi

    [31] Vile vile ewe Nabii, waambie wanawake Waumini, wanaamrishwa waache kutazama yaliyo harimishwa, na wazihifadhi tupu zao kwa kuzisitiri na kutoingiliwa ila kwa njia ya Kisharia. Na wasiwaonyeshe wanaume ya kuwavutia katika uzuri wa umbo lao na mapambo, kama kifua, mabega, vidani, isipo kuwa yale tangu hapo yamedhihiri, kama uso na mikono. Na ewe Nabii! Watake hao wanawake wajisitiri mwahali zilipo funuka nguo, kama shingo na kifua. Na hayo kwa kuteremshia vitambaa vya kichwani. Na wasiachilie kuonekana uzuri wao ila kwa waume zao, na jamaa ambao ni haramu kuoana nao milele, kama baba zao, au baba za waume wao, au watoto wao, au watoto wa waume zao kwa wake wengine, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao. Na mfano wa hawa ni wanawake wenzao, sawa sawa wakiwa waungwana au wajakazi, na wanaume wanao ishi nao na hawana tena haja ya wanawake kwa ukongwe. Na kadhaalika watoto wadogo ambao hawajafikilia miaka ya kutamani. Na pia watake wanawake wasifanye vituko vya kutaka kuwavutia wanaume kama kugonga miguu chini ili isikilizane milio ya mitali na kugesi iliyo fichikana ndani ya nguo. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, kwa mlivyo iacha amri ya Mwenyezi Mungu. Na shikamaneni na adabu za Dini mpate kuongokewa katika dunia na Akhera yenu.

  152. 24:32
    ۝٣٢

    Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua. [32]

    Tanbihi

    [32] Na saidieni katika kujitenga na zina na yanayo pelekea zina, kwa kuwaoza ambao bado hawajaoana miongoni mwa wanaume wenu na wanawake wenu, na walio kuwa wanafaa kwa hayo katika watumwa wenu. Na wala umasikini usiwe sababu ya kuzuilia kuoa. Kwani Mwenyezi Mungu atasahilisha njia za maisha mazuri kwa mwenye kutaka kuishi maisha safi. Na fadhila za Mwenyezi Mungu ni kunjufu, na Yeye anajua kabisa niya za watu, na kila lipitalo katika ulimwengu.

  153. 24:33
    ۝٣٣

    Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [33]

    Tanbihi

    [33] Na ambao hawakupata uwezo wa fedha za kuolea basi wafuate mojapo wa njia nyengine kama saumu na riyadha na kazi za kutumia akili . Kwa hayo hujikurupusha mpaka Mwenyezi Mungu akawafungulia kwa fadhila zake zitakazo wawezesha kuoa. Na watumwa ambao wanataka kuandikiana nanyi ili wapate uhuru wao ni waajibu juu yenu kuwakubalia walitakalo, mkijua kuwa watatimiza kutekeleza na wanaweza. Na juu yenu kuwasaidia waweze kutimiza walio andikiana nanyi, na hayo ama ni kwa kuwapunguzia shuruti mlizo andikiana nao, au kwa kuwapa mali katika mali aliyo kuneemesheni Mwenyezi Mungu, mkawapa katika Zaka au Sadaka. Na ni haramu juu yenu kuwafanya vijakazi vyenu njia ya pato la duniani rakhisi kwa kuwafanya makahaba, na mkawalazimisha kwa hayo. Na vipi mnakwenda kumlazimisha uchafu anaye taka kuwa safi? Na mwenye kuwalazimisha, basi Mwenyezi Mungu humsamehe mwenye kulazimisha pindi akitubu kwa dhambi zake za kulazimisha. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema. Haya yanaelezwa na kauli ya Mtume s.a.w.: "Enyi vijana! mwenye kuweza kuwoa na aoe kwani hivyo linalindwa jicho, unahifadhiwa utupu. Asiye weza na afunge, kwani hivyo ni kinga yake."

  154. 24:34
    ۝٣٤

    Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na mifano kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu. [34]

    Tanbihi

    [34] Na Sisi tumekuteremshieni katika Sura hii na nyenginezo Aya zilizo wazi zenye kubainisha hukumu. Na tumekuteremshieni mifano ya hali mbali mbali za walio tangulia, na uwongozi, na mawaidha ambayo kwayo watapata faida wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu.

  155. 24:35
    ۝٣٥

    Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. [35]

    Tanbihi

    [35] Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha Nuru ya katika mbingu na ardhi. Yeye ndiye Mwenye kunawirisha vyote hivyo kwa nuru yote tunayo iona na tukenda ndani yake, na ya maana, kama Nuru ya Haki na uadilifu, na ilimu, na fadhila, na uwongofu, na Imani, na kwa ushahidi na athari kama alivyo waahidi viumbe vyake, na kwa vyote vinavyo onyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, na vikalingania Imani kumuamini Yeye Subhanahu. Na mfano wa Nuru yake Tukufu na dalili zake zilizo zagaa kwa uwazi ni kama mfano wa Nuru ya taa yenye kung'aa kwa ukali kabisa, iliyo wekwa kwenye shubaka la ukutani ili kuukusanya mwangaza wake na kuzidi kuupa nguvu. Na taa hiyo imevikwa tungi la kigae safi linameremeta kama inavyo meremeta nyota. Na taa ile inawaka kwa mafuta ya mti wenye baraka nyingi, ulio pandwa kwenye udongo mzuri na pahali pazuri. Mti huu ni mzaituni unao mea pahala pa kati na kati. Basi huo si wa mashariki ukakosa joto la jua wakati wa alasiri, wala si wa magharibi ukakosa joto la jua wakati wa asubuhi. Bali huo uko juu ya kilele cha mlima, au katika uwazi wa ardhi unao patisha jua mchana kutwa. Mafuta ya mti huu yanakaribia kutoa mwanga kwa ubora wa usafi wake hata ikiwa hayajaguswa na moto wa taa. Mambo haya yote yanazidisha mwangaza wa hiyo taa juu ya mwangaza wake, na Nuru juu ya Nuru. Na namna hii ndio zinakuwa dalili zilizo enea katika ulimwengu, za kuonekana na kupimika kwa akili; ni Ishara zilizo wazi hazitaki kutiliwa shaka yoyote kwa kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwajibikia Imani kumuamini Yeye, na Risala za Mitume aliyo waleta. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kufikia Imani amtakaye kwa njia ya dalili hizi ikiwa huyo mtu atajaribu kunafiika na nuru ya akili yake. Na Mwenyezi Mungu ameleta mifano ya kuweza kuhisiwa na kuonekana ili iwe wepesi kuelewa mambo ya kiakili. Na Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, anawajua wenye kuangalia Ishara zake na wenye kuzipuuza na wakapanda kiburi. Naye atawalipa kwa hayo.

  156. 24:36
    ۝٣٦

    Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni [36]

    Tanbihi

    [36] Hakika wapo watu wanao mtakasa Mwenyezi Mungu na wanamuabudu misikitini ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha ijengwe na iamirishwe kwa kudhukuriwa Mwenyezi Mungu, nao wameshughulikia hayo asubuhi na jioni.

  157. 24:37
    ۝٣٧

    Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka. [37]

    Tanbihi

    [37] Dunia na yaliomo duniani ya kuuza na kununua hayawashughulishi wakaacha kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumzingatia. Wao wanashika Swala, na wanatoa Zaka, na huku wakiikhofu Siku ya Kiyama ambapo nyoyo zitakuwa hazina utulivu kwa sababu ya wasiwasi na hamu, na kungojea matokeo, na macho yatadahadari kwa mhangaiko na kushtuka kwa vituko vigeni wanavyo viona, na wingi wa vitisho.

  158. 24:38
    ۝٣٨

    Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo yatenda, na awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu. [38]

    Tanbihi

    [38] Na malipo ya vitendo vyao ni kulipwa sawa sawa kwa ubora wa malipo kwa vitendo vyao vyema, na watapata fadhila kwa kupewa zaidi kuliko wanavyo stahiki. Kwani Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa fadhila, humpa amtakaye katika waja wake wema kipao kikubwa, asichoweza mtu kukihisabu wala wenye kuhisabu hawawezi kukisia.

  159. 24:39
    ۝٣٩

    Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. [39]

    Tanbihi

    [39] Na hao walio pinga na wakakanya wanadhani wenyewe kuwa wamefanya vizuri, na kwamba vitendo vyao vizuri vitawaletea faida Siku ya Kiyama. Lakini hao wamekosea katika dhana yao hiyo. Kwani mfano wa vitendo vyao katika upotovu wake na kukosa maana ni kama mmetuko unao tokea unapo angukia mwako wa jua wakati wa adhuhuri juu ya ardhi tambarare jangwani. Mwenye kiu hudhania kuwa ni maji. Hata akiyafikia asikute chochote chenye manufaa kama alivyo dhania. Hali kadhaalika vitendo vya makafiri siku ya malipo vitakuwa vumbi lilio tawanyika. Na kafiri ataikuta adhabu ya Mwenyezi Mungu inamngojea kwa utimilivu wake bila ya nuksani. Hakika hisabu ya Mwenyezi Mungu hapana shaka inakuja. Na Yeye, Aliye takasika, ni Mwepesi katika kuhisabu kwake, hachelewi wala hakosei.

  160. 24:40
    ۝٤٠

    Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru. [40]

    Tanbihi

    [40] Na huu mfano mwengine wa vitendo vya makafiri. Mfano wake ni mfano wa giza la bahari kubwa iliyo tanda yenye kina kirefu. Mawimbi yake yanapigana na kusukumana wenyewe kwa wenyewe. Nayo yamefunikwa na mawingu mazito meusi hayapitishi mwangaza. Katika giza hili lililo rundikana msafiri wa baharini hawezi kuuona mkono wake hata akiukurubisha machoni. Basi anabaki ameduwaa amebabaika hajijui. Na vipi ataona kitu atokane na butaa hili bila ya kupata Nuru ya kumwongoa katika mwendo wake, na kumwokoa na kugongana na kuhiliki. Na basi kama hali hiyo hiyo makafiri hawapati faida katika vitendo vyao, wala hawatoki katika upofu wao na upotovu wao, wala hawajiokoi nafsi zao, ila kwa Nuru ya Imani. Kwani hana Nuru ya kumwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. Basi atakuwa katika walio teketea. "Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu." Sarabi si chochote ila mandhari ya mwangaza yanayo sabibishwa na marejeo (reflection) ya miale inayo toka kwenye vitu vyenye kutoa mwanga. Na hiyo hurejeshwa tena kutokana na ardhi pana tupu, yaani uwanda, na kupanda kidogo kidogo mkabala na uso wa ardhi, na joto linapo panda wakati wa mchana, basi miale hiyo inayo rejea ikifika kwa jicho la mwenye kuangalia huona vile vitu vimegeuka juu chini kama kwamba kwenye kiyoo kikubwa kilicho tanda. Na kadhaalika mbingu safi ya rangi ya kibuluu huonekana kama kwamba ni ziwa la maji juu ya uso wa ardhi. Na vile vitu vingine kama miti miti na mitende iliyo onekana juu chini inazidi kuonyesha kama kwamba ni vivuli kwenye maji. Na hii Sarabi huzidi kudhihiri kwa uwazi kabisa inapo kuwa khitilafu ni kubwa baina ya joto la uso wa ardhi na angani katika hewa. Na hayo huonekana zaidi majangwani na nyandani na kwenye barabara za jangwani za lami zilio nyooka. Kwa maelezo hayo inaonekana kuwa Sarabi ni kiini macho tu. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 40: " Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru." Aya hii tukufu imekusanya yaliyo muhimu kabisa katika midharuba ya baharini. Ni maarufu kuwa midharuba ya bahari kuu huwa na mawimbi yanayo khitalifiana urefu wao na ukubwa wao au mnyanyuko wao, hata inaonekana kama kwamba hayo mawimbi yanapandana moja juu ya mwenzie, na kwa hivyo yakaziba mwangaza wa jua kwa vile hiyo midharuba inasabibisha kurundika kwa mawingu mazito ambayo nayo huuziba mwangaza wa jua, na kwa hivyo husabibisha giza mtu asiweze kuona kitu juu ya kuwa macho yake mazima. Na ilivyo kuwa Mtume s.a.w. kazaliwa na kakulia jangwani, kuja maelezo kama haya ya undani ya ki-ilimu kwa ulimi wake kuwa ni ufunuo ulio tokana na Mwenyezi Mungu, ni ushahidi kuwa Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na kuwa ni muujiza wa Mtume huyu mtukufu.

  161. 24:41
    ۝٤١

    Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua wayatendayo. [41]

    Tanbihi

    [41] Ewe Nabii! Hujui kwa yakini kwamba kwa Mwenyezi Mungu hunyenyekea kila kiliomo mbinguni na duniani? Na wanamnyenyekea ndege vile vile, nao wamekunjua mbawa zao? Basi viumbe vyote hivi vinanyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu na mipango yake. Vinamtakasa na washirika na kila lisio na laiki naye. Na kila kimojawapo kinajua kwa kujaaliwa na Mwenyezi Mungu yaliyo kiwajibikia katika unyenyekevu na kutakasa na kutimiza wadhifa wa maisha. Na Mwenyezi Mungu nyuma yao anajua kwa utimilivu wa kujua Swala ya kila mwenye kusali, na kusabihi kwa mwenye kusabihi, na yote wayafanyayo waja. Basi huwaje makafiri wakawa hawaamini?

  162. 24:42
    ۝٤٢

    Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya wote. [42]

    Tanbihi

    [42] Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, na ndiye Mwenye madaraka juu yao, na wote watarejea kwake Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo.

  163. 24:43
    ۝٤٣

    Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho. [43]

    Tanbihi

    [43] Ewe Nabii! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyavuta mawingu, kisha huyakusanya na kuyarindika moja juu ya moja. Utaona mvua inatoka kwenye mawingu. Na Mwenyezi Mungu huteremsha kutokana na mawingu yaliyo rindikana yanayo shabihi milima kwa ukubwa wake, vipande vya barafu kama changarawe, vikawaangukia watu vikawaletea manufaa au madhara, kufuatana na kanuni zake na matakwa yake, wala asiwateremshie wenginewe kwa mujibu apendavyo Yeye Subhanahu, Mtendaji, Mwenye kukhitari. Mwangaza wa umeme unao tokea kwa kugongana mawingu hukaribia kutia upofu kwa ukali wake. Na mambo kama haya ya kuonekana ni dalili za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu ambao unao wajibisha kuleta Imani ya kumuamini Yeye. Hajui kushabihiana baina ya mawingu na milima ila mwenye kupanda ndege (eropleni) inayo ruka juu ya mawingu, akayaona kutoka huko juu kama ni milima na vilima. Ilivyo kuwa ndege hizo hazijawa bado zama za Mtume s.a.w. basi hii inakuwa ni dalili kuwa maneno haya yanatokana na Mwenyezi Mungu anaye jua ya juu na chini. "Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho." Aya hii tukufu imeutangulia msafara wa sayansi. Kwani hii yaeleza daraja za kuundika mawingu yanayo rindikana, na sifa zake, na yaliyo juulikana hivi karibuni ki-sayansi ya kwamba mawingu ya mvua huanzia kwa sura ya moja moja kisha yakajumuika yakawa kikundi, ndiyo hayo mawingu yaliyo rindikana, yaani mawingu yanayo endelea kukua kwa kuelekea utosini. Hayo hukua kimo chake hata kufikia urefu wa kilomita 15 au 20, na hapo huonekana kama ni milima mikubwa iliyo nyanyuka. Na yajuulikanayo ki-sayansi ni kuwa mawingu yaliyo rindika yanapitia daraja tatu, nazo: Daraja ya kukusanyika na kukua. Daraja ya kunyesha. Na mwisho daraja ya kumalizikia. Kama ilivyo kuwa mawingu hayo - nayo ni peke yao - yenye mvua ya mawe na inabeba nguvu za umeme (electricity, Kahrabaa) , huweza kuwa yakashika mfululizo wa umeme na radi, hata huweza ikawa ni miripuko karibu 40 kwa dakika moja, hata mtu anaye tazama akawa hawezi tena kuona kwa ukali wa mwanga wake. Na haya ndiyo khasa yanayo wapata marubani wa meli na ndege wakati wa midharuba ya radi.

  164. 24:44
    ۝٤٤

    Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye kuona. [44]

    Tanbihi

    [44] Mwenyezi Mungu huzigeuza hali za usiku na mchana kwa urefu na ufupi, na kwa kuanzia na kumalizikia, kwa mizunguko ya falaki. Hakika katika hayo pana mazingatio kwa wenye akili zilio nzima zenye busara, na kwa njia hiyo wakamuamini Mwenyezi Mungu.

  165. 24:45
    ۝٤٥

    Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. [45]

    Tanbihi

    [45] Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na ndiye aliye anzisha kila kitu kwa kupenda kwake. Na akaumba kila kilicho hai kutokana na asili moja ya shirika, nayo ni maji. Na kwa hivyo kila kihai hakiachi kuwa na maji. Kisha zinawakhitalifisha khitilafu nyengine kwa namna, na uwezo, na sura, na kadhaalika. Katika wanyama wapo wanao tambaa kwa matumbo yao, kama samaki, na nyoka. Na wapo wanao kwenda kwa miguu miwili kama wanaadamu na ndege. Na wapo wanao kwenda kwa miguu mine kama mahayawani wengi wa kufugwa na wa mwituni. Mwenyezi Mungu huumba apendavyo kwa njia mbali mbali, kuonyesha uwezo wake na ujuzi wake. Kwani ni Mwenye kutaka atakacho, na Mwenye kukhitari apendacho. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. "Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu." Maji katika Aya hii tukufu ni maji ya uzazi, yaani vinyama vinavyo toa manii. Na Aya hii si kama imetangulia msafara wa sayansi katika kubainisha kuzalikana mtu kutokana na tone la manii, kama ilivyo kuja katika kauli yake Aliye tukuka: "Hebu naajitazame mtu, ameummbwa kwa kitu gani? Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa." (Sura Att'ariq 5,6), bali imetangulia pia katika kubainisha kwamba kila kinyama kinacho kwenda kwenye ardhi kimeumbwa kwa njia ya kuzalikana na vinyama vya manii, na vinga khitalifiana hivyo vinyama vya manii na sifa zao katika kila namna mnamo hizo namna za vinyama. Katika maana za kisayansi ambazo zaweza kuwa nazo hii Aya ni kuwa maji ni msingi wa kila kiumbe kilicho hai. Kwa mfano mwili wa mtu umekusanya 70% ya uzito wake kuwa ni maji. Yaani mtu mwenye uzito wa kilo 70, kiasi kilo 50 ni maji. Na kabla ya kuteremka Qur'ani haya hayakuwa yakijuulikana kabisa ya kuwa mtu ana sehemu hii kubwa ya mwili wake kuwa ni maji. Na maji ndio chakula cha dharura kabisa kwa mwanaadamu. Kwani hali mtu yamkini aishi siku 60 bila ya kula chakula chochote, hawezi kuishi bila ya maji kwa zaidi kuliko siku 3 mpaka 10 mwisho wake. Na maji ndio msingi wa kufanyika damu, na maji ya limfo, na ya katika ubongo wa mifupa, vimwagavyo na mwili, kama mkojo, na jasho, na machozi, na mate, na nyongo, na maziwa, na maji yanayo patikana katika viungo, na ambayo ndiyo sababu ya ulaini wa mwili. Na yakikosekana 20% ya maji yake basi mwanaadamu hukabiliwa na mauti. Na maji huyayusha vyakula vikasahilika kufyonzeka. Na kadhaalika huyayusha makombo yenye asili ya vilivyo hai au maadini katika mkojo na jasho. Na kwa namna hii maji yana sehemu kubwa zaidi na muhimu kabisa katika kuumbwa kwa mwili. Na kwa hivyo yamkini kusema kwamba kila kiumbe kilicho hai kimeumbwa kutokana na maji.

  166. 24:46
    ۝٤٦

    Kwa yakini tumeteremsha Ishara zinazo bainisha. Na Mwenyezi Mungu hummwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka. [46]

    Tanbihi

    [46] Na hakika Sisi tumeteremsha kwa wahyi Aya zilizo wazi za kubainisha hukumu na mawaidha, na zinazo piga mifano. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kwenye kheri ampendaye katika waja wake ambao wapo tayari kuziangalia na kufaidika nazo.

  167. 24:47
    ۝٤٧

    Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tumet'ii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini. [47]

    Tanbihi

    [47] Na wanaafiki husema kwa ndimi zao: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tunazifuata amri zao. Na wanapo tiwa mtihanini kikundi kati yao hukataa kushirikiana na Waislamu katika kazi ya kheri, kama Jihadi na nyenginezo, baada ya kauli yao hii. Na watu hawa si Waumini wa kweli, wala hawastahiki kutumiliwa jina la Waumini kwao.

  168. 24:48
    ۝٤٨

    Na wanapo itwa kumuendea Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa. [48]

    Tanbihi

    [48] Na katika hali zao ni kuwa wakitakiwa kuhukumiwa mbele ya Mtume kwa jambo alilo literemsha Mwenyezi Mungu, unaafiki wa baadhi yao hudhihiri, na wao hukataa kuhukumiwa wakijua kuwa haki ni ya wale makhasimu zao.

  169. 24:49
    ۝٤٩

    Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kut'ii. [49]

    Tanbihi

    [49] Ama wakijua kuwa haki iko upande wao basi humjia Mtume mbio mbio ili awahukumu baina yao na makhasimu zao.

  170. 24:50
    ۝٥٠

    Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au wanaogopa ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali hao ndio madhaalimu. [50]

    Tanbihi

    [50] Na kwa nini wanasimama msimamo huu katika kushitakiana mbele ya Mtume? Ni kwa sababu nafsi zao zimesibiwa na maradhi ya upofu, na kwa hivyo haziridhiki na hukumu yako ya haki? Au ni kwa kuwa wao wanatilia shaka uadilifu wa Muhammad s.a.w. katika kuhukumu? Si lolote katika hayo kabisa. Lakini hao ni madhaalimu walio dhulumu nafsi zao na wengineo kwa sababu ya ukafiri wao na unaafiki wao na kuiacha kwao haki.

  171. 24:51
    ۝٥١

    Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa. [51]

    Tanbihi

    [51] Hakika kauli ya haki ifaayo kwa Waumini wa kweli wanapo itwa wahukumiwe kwa mujibu wa yaliyo kuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kuwa waseme kwa kukubali na kunyenyekea: Tumesikia wito wako, ewe Muhammad! Na tumeridhia hukumu yako. Na hao ndio watao kuwa watu wa kufanikiwa katika dunia yao na Akhera yao.

  172. 24:52
    ۝٥٢

    Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu. [52]

    Tanbihi

    [52] Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na kuridhia anayo yaamrisha Mtume s.a.w. na wakaiogopa dhati ya Mwenyezi Mungu Tukufu, na wakaukumbuka Utukufu wake, na wakaikhofu ghadhabu yake, hao ndio watakao pata radhi ya Mwenyezi Mungu na mapenzi yake, na neema za Pepo, na ndio wenye kupata kheri tupu.

  173. 24:53
    ۝٥٣

    Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba ukiwaamrisha kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. [53]

    Tanbihi

    [53] Na wanaafiki wanaapa kwa ukomo wa nguvu za viapo vyao, kwamba wewe, Muhammad, ukiwaamrisha watoke nawe kwenda vitani watakut'ii. Waambie: Msiape! Kwani mambo yatakikanayo kwenu mnayajua, hapana hata mmoja wenu asiye yajua. Wala yamini zenu za uwongo haziondoi ujuzi huo. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara kila linalo tokana nanyi, na Yeye atakulipeni kwayo.

  174. 24:54
    ۝٥٤

    Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe wazi wazi. [54]

    Tanbihi

    [54] Waambie: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume kwa ut'iifu wa kweli wenye kuonyesha vitendo vyenu. Wanaafiki wakipuuza wasifuate, basi juu ya Muhammad ni waajibu wa aliyo twishwa tu na Mwenyezi Mungu, nayo ni amri ya kufikilisha Ujumbe, wala hakukalifishwa uwongofu wao. Na nyinyi juu yenu ni hayo aliyo kutwikeni Mwenyezi Mungu nayo ni kufuata na kut'ii. Na mtapata adhabu ikiwa mtaendelea na uasi. Na mkimt'ii Mtume mtaongoka kwenye kheri. Na yeye haimpasi ila kufikisha kwa uwazi mukimti au mukiamsi na yeye akaisha fikisha

  175. 24:55
    ۝٥٥

    Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu. [55]

    Tanbihi

    [55] Mwenyezi Mungu amewahidi katika nyinyi, walio sadiki haki na wakaifuata, na wakatenda vitendo vyema, kwa ahadi ya kutia mkazo. Yakwamba atawafanya makhalifa, (wafuatizi) warithi wa wale walio tangulia wawarithi katika kuhukumu na utawala katika nchi, kama ilivyo kuwa hali kwa walio tangulia. na atawasimamishia Uislamu kuwa ndio Dini yako, alio wapendekezea, basi watakuwa na heba na madaraka. Na atabadilisha hali yao ya khofu iwe ya amani, wawe wananiabudu mimi, nao wametua hawanishirikishi mimi na chochote kile katika ibada. Na wenye kukhiyari ukafiri baada ya ahadi hii ya kweli au wakaritadi wakaacha Uislamu, basi hao ndio waliotoka nje walioasi wapizani

  176. 24:56
    ۝٥٦

    Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate kurehemewa. [56]

    Tanbihi

    [56] Na shikeni Swala kwa ukamilifu wa nguzo katika utulivu na unyenyekevu, ili ipate kuwa inazuia uchafu na mambo mabaya. Na wapeni Zaka wanao stahiki. Na mt'iini Mtume kwa yote anayo kuamrisheni, ili mpate kutaraji rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi yake.

  177. 24:57
    ۝٥٧

    Msiwadhanie walio kufuru kwamba watashinda katika nchi. Na makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo yao. [57]

    Tanbihi

    [57] Ewe Nabii! Usidhani kuwa makafiri wataweza kumkwepa Mwenyezi Mungu asiwashike kwa madhambi yao, au watu wa Haki wasiwaone pahala popote pale katika ardhi. Bali Yeye ni Muweza, na marejeo yao Siku ya Kiyama ni Motoni. Na marejeo maovu kabisa ni marejeo yao.

  178. 24:58
    ۝٥٨

    Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. [58]

    Tanbihi

    [58] Enyi mlio amini! Yakupaseni muamrishe watumishi wenu na vijana wenu ambao bado hawajabalighi wasikuingilieni vyumbani mwenu ila baada ya kutaka idhini katika nyakati tatu, nazo ni kabla ya Swala ya alfajiri, na pale mnapo punguza nguo zenu wakati wa kupumzika mchana, na baada ya Swala ya Isha mnapo jitayarisha kulala. Kwani nyakati hizi mtu hubadilisha mavazi ya kulalia badala ya mavazi ya kutokea, na huonekana sehemu za mwili ambazo hazifai kuonekana. Wala hapana ubaya kwenu wala kwao kuingia bila ya ruhusa nyakati nyenginezo, kwa sababu ni jamba la ada watu wa nyumbani kupitiana kwa maslaha yao. Na kwa uwazi wa namna hii Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya za Qur'ani ili akuwekeeni wazi hukumu. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa hikima, anajua yanayo silihi kwa waja wake, na anawatungia Sharia zinazo wanasibu, na kwa kadri ya haja yao. "Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamikiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Swala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Swala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima." Aya hii tukufu ni moja katika Aya zinazo elekeza nadhari ya watu wazingatie yaliyo laiki katika jamii za watu khasa ndani ya ukoo. Nayo kuwa kuchanganyika kwa watumishi na watoto katika aila yao huenda kukapindukia mipaka ya hishima za maingiano, wakawa wanawaingilia wenginewe bila ya kutaka idhini katika nyakati maalumu zilizo tajwa katika Aya. Na kwa kuwa nyakati hizo ni nyakati za faragha na uhuru wa binafsi, na kuvua nguo nzito nzito, Aya hii imekusudia kuweka Sharia ya kutaka idhini katika nyakati hizo kutokana na watumishi na vijana ili wasione ambayo yanahisabiwa kuwa ni siri, ambayo ni kama utupu ambao wapasa kusitiriwa. Na kwa hivyo wanaelekezwa watu wa ukoo wavae mavazi yanayo kuwa laiki ya kukabiliana hata wao kwa wao, ili hishima yao ibaki imehifadhika, na uhuru wao umedhaminika, na adabu zao zimechungika. Na Qur'ani ndio inaayo faa khasa kutuongoza tufuate mwendo ulio bora na wa juu. (Ikiwa watoto wa nyumbani haiwafalii kuwaingilia watu katika nyakati hizo za faragha zilizo tajwa, seuze watu mbali!)

  179. 24:59
    ۝٥٩

    Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake ruhusa, kama walivyo taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. [59]

    Tanbihi

    [59] Na vijana vyenu wakifikilia umri wa kubalighi inawapasa watake ruhusa ya kuingia kila nyumba, na kila wakati, kama ilivyo wapasa wenzao wa kabla yao. Na kwa mfano wa uwazi kama huu Mwenyezi Mungu anakuwekeeni wazi Aya zake alizo ziteremsha. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa hikima. Anajua linalo wasilihi waja wake, na anawaatungia Sharia zinazo wanasibu, na kwa kadri ya haja yao.

  180. 24:60
    ۝٦٠

    Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. [60]

    Tanbihi

    [60] Na wanawake wakongwe ambao hawatumai kuolewa, hawalaumiwi wakipunguza baadhi ya nguo zao, kwa sharti wasiwe wanajishauwa kwa kuonyesha uzuri wa mwili wao ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha usitiriwe. Lakini kujihishimu kwa kujisitiri kwa ukamilifu ni bora kwao kuliko kujifunua. Na Mwenyezi Mungu anawasikia wayasemayo, na anayajua makusudio yao, na atawalipa kwa hayo.

  181. 24:61
    ۝٦١

    Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, (baba mdogo) au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate kuelewa. [61]

    Tanbihi

    [61] Wenye udhuru kama vile vipofu, viguru, wagonjwa hawana lawama, bali hata nyinyi wazima hamna lawama kula katika nyumba za watoto wenu, kwani hizo ni nyumba zenu. Wala kula katika nyumba za baba zenu, na mama zenu, na ndugu zenu wanaume na ndugu zenu wanawake, au nyumba za ami zenu, au mashangazi zenu, au wajomba zenu, au mama wadogo, dada wa mama zenu, au nyumba ambazo mmewakilishwa kuzitazama, au nyumba za rafiki zenu mnao changanyika nao, ikiwa hamna yaliyo harimishwa humo. Na hayo ikijuulikana kuwa mwenye nyumba ameruhusu yeye au mkewe. Wala hapana ubaya kula humo pamoja au mbali mbali. Na muingiapo katika nyumba toeni salamu kwa waliomo ambao hao ni baadhi yenu kwa umoja wa Dini na ujamaa. Kwani hao ni kama nyinyi. Na maamkio haya ni maamkio yaliyo wekewa Sharia, yenye baraka na thawabu, na pia ndani yake nyoyo hupoa. Na kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu anazifafanua Aya kwa ajili yenu mpate kuelewa waadhi na hukumu ziliomo ndani yake, na mpate kuzifahamu na mzitende.

  182. 24:62
    ۝٦٢

    Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na wanapo kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu umtakaye miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu. [62]

    Tanbihi

    [62] Hakika Waumini wenye kusadiki ni wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala hawamwachi Mtume peke yake katika jambo muhimu linalo hitajia wajumuike pamoja kwa ajili yake, kama mfano wa Jihadi. Ila baada ya kumtaka ruhusa ya kuondoka na wakakubaliwa, hakika wanao kukadiri wewe, ewe Nabii, kama unavyo stahiki, na wanatambua umuhimu wa huo mkusanyiko hawaondoki ila baada ya wewe kukubali. Hao ndio wenye kusadiki katika Imani yao kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakikutaka ruhusa hawa kwenda kufanya baadhi ya maslaha yao mpe ruhusa umtakaye katika wao, pindi ukimwona kuwa ana haja kweli ya kuondoka, na si dharura kwa mkutano kuwapo yeye. Juu ya hivyo waombee maghfira kwa Mwenyezi Mungu kwa kuondoka kwao, ambako kwa hakika hakuelekei kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema.

  183. 24:63
    ۝٦٣

    Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho. Basi nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu. [63]

    Tanbihi

    [63] Fanyeni hima kuhishimu wito wa Mtume kukuiteni kukusanyika kwa mambo muhimu. Na muitikieni huo wito wake, wala msifanye wito huo kama mnavyo itana nyinyi kwa nyinyi, kuwa inafaa kupuuza na kuondoka mpendavyo. Wala msiondoke ila baada ya kutaka ruhusa na mkakubaliwa, na tena iwe katika mipaka ya ufinyo kabisa, na dharura za shida. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anawajua wanao ondoka bila ya idhini wakijificha ficha kati ya watu ili ati Mtume asiwaone. Na watahadhari wanao kwenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu asije Subhanahu akawapatiliza kwa uasi wao wakapata mateso makali duniani kama ukame na mitetemeko, au akawapa adhabu yenye wingi wa uchungu aliyo waandalia Akhera, nayo ni ya Motoni.

  184. 24:64
    ۝٦٤

    Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza waliyo yafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. [64]

    Tanbihi

    [64] Zindukaneni enyi watu! Mjue kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi, na viliomo ndani yao. Anayajua mlio nayo, ukafiri wenu na Uislamu wenu, na uasi wenu, na ut'iifu wenu. Basi msiende kinyume na amri yake. Na Yeye atawapa khabari watu, watapo rejea kwake Siku ya Kiyama, kwa yote waliyo yatenda duniani, na atawalipa kwayo. Kwani Yeye amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake.

  185. Sura Al-Furqaan

    سُورَةُ الفرقان
  186. 25:1
    ۝١

    Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote. [1]

    Tanbihi

    [1] Mambo ya Mwenyezi Mungu yametukuka, na kheri yake imezidi. Yeye ndiye aliye iteremsha Furqani, yaani Qur'ani, ya kufarikisha baina ya kweli na uwongo juu ya mja wake, Muhammad s.a.w., ili awe mwonyaji na mwenye kuifikisha hiyo Qur'ani kwa walimwengu wote.

  187. 25:2
    ۝٢

    Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo. [2]

    Tanbihi

    [2] Yeye Subhanahu ndiye peke yake aliye miliki mbingu na ardhi, aliye takasika na haja ya kuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika wowote katika ufalme wake. Na Yeye kaumba kila kitu na akakipima kwa kipimo baraabara kwa sharia zake ili kiweze kutimiza waajibu wake kwa nidhamu. "Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo." Ilimu ya sayansi ya sasa imethibitisha kuwa vitu vyote vinakwenda kwa mujibu wa hukumu za uumbaji wake, na maendeleo yake namna mbali mbali kwa kufuata mpango madhubuti ambao hapana mwenye uwezo juu yake ila Muumbaji mwenye uwezo Mwenye kuanzisha kila kitu. Kwani katika kuwa kwake imebainika kuwa vitu vyote viumbe vyote na vinga khitalifiana umbo lake na sura yake kwa hakika vinatokana na madda chache za asli za kuhisabika, na hisabu ya madda hizo (elements) zinakaribia mia, nazo ni 96 zinazo juulikana mpaka sasa. Nazo zina khitalifiana kwa sifa zao za maumbile (physically ) na za Al Kimyaa (Chemically), na pia katika uzito wake wa chembe (Atomic Weight). Zinaanza kwa madda asli (element) Nambari 1. Nayo ni Hydrogen yenye Atomic weight 1, na kuishia na element ya nambari 96, Borium, ambayo atomic weight yake bado haijuulikani. Na element ya mwisho katika sayansi ni Uranium na atomic weight yake ni 238.57. Na hizi elements hujengeka na kufanyika Compounds kwa mujibu wa kanuni madhubuti zisio weza kuepukwa. Hali kadhaalika mimea na wanyama. Kila mmoja wao amegawika katika koo na makundi na namna (orders, families, species and sub-species) zinazo geuka sifa zake kwa madaraja ya viumbe vilivyo hai mpaka kuishia viumbe vyenye Khalaya au Cell moja (unicellular) kama microbes mpaka viumbe vyenye cells nyingi (multi- cellular) mpaka kufikia binaadamu, naye ndiye aliye kamilika kuliko wote. Na kila namna ya hizi sifa maalumu zinarithika katika kundi kizazi baada ya kizazi. Na yote haya yanakwenda kufuata kanuni na mipango iliyo thibiti madhubuti inayo onyesha kwa uwazi utukufu wa Mwenye kuumba na uwezo wake. Ametakasika, Subhanahu na ametukuka na hao wanao mshirikisha naye.

  188. 25:3
    ۝٣

    Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka. [3]

    Tanbihi

    [3] Na juu ya yote hayo makafiri wakaacha kumuabudu Yeye, wakenda kuchukua miungu mingine kuiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, katika masanamu, na nyota, na watu. Na hao hawanalo waliwezalo kuliumba, bali wao ni viumbe vya Mwenyezi Mungu. Wala hawawezi kujikinga nafsi zao na madhara, wala kujiletea kheri. Wala hawawezi kumfisha yeyote wala kumhuisha, wala kuwafufua maiti kutoka makaburini kwao. Na kila asiye miliki lolote katika hayo basi hastahiki kuabudiwa. Na mjinga wa kutupwa anaye waabudu. Mwenye kustahiki kuabudiwa ni yule Mwenye kumiliki haya yote.

  189. 25:4
    ۝٤

    Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo. [4]

    Tanbihi

    [4] Makafiri wakaitia ila Qur'ani, wakasema kuwa hiyo ati ni uwongo kauzua Muhammad mwenyewe, na akamsingizia Mwenyezi Mungu. Na wakamsaidia baadhi ya jamaa wengine katika Ahli-l-Kitab. Basi hawa makafiri wamefanya dhulma kwa kauli yao hiyo katika hukumu na kuishambulia Haki, wakaleta uzushi usio kuwa na ushahidi wowote. Kwani hao wanao waashiria katika Ahli-l- Kitab lugha yao hata si Kiarabu. Na Qur'an ni kwa lugha ya Kiarabu fasihi.

  190. 25:5
    ۝٥

    Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni. [5]

    Tanbihi

    [5] Wakaisema Qur'ani pia kuwa ati ni uwongo walio andika watu wa kale katika vitabu vyao, kisha akawataka wao wamuandikie na wamsomee asubuhi na jioni mpaka ahifadhi na apate kusema naye hayo hayo.

  191. 25:6
    ۝٦

    Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [6]

    Tanbihi

    [6] Ewe Nabii! Waambie: Hakika Qur'ani ameiteremsha Mwenyezi Mungu ambaye anazijua siri zilizo fichikana katika mbingu na ardhi. Na ameziweka katika Qur'ani ya muujiza kuwa ni dalili ya kwamba hiyo ni Ufunuo wake Subhanahu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema, anawasamehe wenye kuasi pindi wakitubu, wala hafanyi haraka kuwaadhibu.

  192. 25:7
    ۝٧

    Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye? [7]

    Tanbihi

    [7] Wakamkejeli Muhammad, wakasema: Kitu gani kinacho mtengua huyu anaye dai kuwa ni Mtume, hata anakula chakula kama tulavyo sisi, na anazururuka masokoni kutafuta maisha kama watu wengine? Angeli kuwa ni Mtume Mwenyezi Mungu angeli mtosheleza kwa hayo, na yeye angeli mwomba Mola wake Mlezi amteremshie Malaika kutoka mbinguni amsaidie katika uwonyaji na kufikisha Ujumbe, na amsadikishe katika wito wake, tupate sisi kumuamini.

  193. 25:8
    ۝٨

    Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa. [8]

    Tanbihi

    [8] Na hebu lau angeli mtaka amtosheleze chakula cha kutosha asihitajie kuzunguka masokoni, akamtupia khazina kutoka mbinguni ya kutumia, au akamjaalia na bustani ya kumlisha matunda yake? Na wakubwa wa makafiri walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri, wenye kuwapotoa watu wasimuamini Muhammad, na wenye kufanya hila za kuwaingiza shaka Waumini, walisema: Nyinyi hamumfuati ila huyu mtu aliye zugwa akili yake, basi anabwabwatika bila ya kuwa na hakika.

  194. 25:9
    ۝٩

    Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia. [9]

    Tanbihi

    [9] Hebu angalia, ewe Nabii! Vipi wanavyo kupigia mifano hawa! Mara wanakupigia mfano wa mwenye kurogwa, mara nyengine kuwa ati ni mwendawazimu, mara ya tatu kuwa ni mwongo, na mara yane kuwa unaipokea Qur'ani kutokana na wasio kuwa Waarabu. Hao kwa hayo hakika wameipotea njia ya haki, na kuhojiana kulio sawa. Basi hawaitambui njia ya kufikilia yote hayo.

  195. 25:10
    ۝١٠

    Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo,nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari. [10]

    Tanbihi

    [10] Mwenyezi Mungu ametukuka, na izidi kheri yake! Yeye ndiye ambaye pindi akitaka atakujaalia duniani bora kuliko hayo wanayo pendekeza wao. Kwa Akhera Yeye amekwisha kujaalia kama alivyo kuahidi, nayo ni mabustani mengi yapitayo mito pembezoni mwake, na baina ya miti yake, na majumba ya fakhari madhubuti.

  196. 25:11
    ۝١١

    Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa [11]

    Tanbihi

    [11] Na kwa hakika hawa wamepinga kila Ishara. Kwani wao wamekanusha kufufuliwa, na Siku ya Kiyama. Nao kwa hivyo wanayatia ila matakwa haya ili kuwageuza watu washughulikie upotofu wao. Na Sisi tumekwisha waandalia wanao ikanusha Siku ya Kiyama Moto wenye kuwaka vikali mno.

  197. 25:12
    ۝١٢

    Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yakena mngurumo wake. [12]

    Tanbihi

    [12] Wakiuona Moto, na huo Moto ukawaona, wataisikia sauti yenye hasira, yenye hamu kuwateketeza. Na katika hayo ni mfano wa mingurumo inayo toka kifuani mwa aliye kasirika kuwa ni alama ya ukali alio nao.

  198. 25:13
    ۝١٣

    Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataombawafe. [13]

    Tanbihi

    [13] Na watapo tupwa katika pahali pembamba kwa kulingana na unene wao, nao wamefungwa pingu mikono yao kwenye shingo zao, watapiga kelele kuhimiza wateketezwe upesi upesi ili wapate kupumzika na kitisho cha adhabu.

  199. 25:14
    ۝١٤

    Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi! [14]

    Tanbihi

    [14] Wataambiwa kwa kuwahizi na kuwakejeli: Msitake kuangamia mara moja tu, bali takeni muangamie mara nyingi. Hamtopata kusalimika na hayo mliyo nayo. Na hakika namna ya adhabu zao ni nyingi.

  200. 25:15
    ۝١٥

    Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo? [15]

    Tanbihi

    [15] Ewe Nabii! Waambie makafiri: Je! Marejeo haya waliyo ahidiwa makafiri ni bora au Pepo yenye kudumu neema zake, na ambayo wameahidiwa Waumini, wachamngu, kuwa itakuwa yao kama ndio malipo na marejeo ya kwendea baada ya kufufuliwa na kuhisabiwa?

  201. 25:16
    ۝١٦

    Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa. [16]

    Tanbihi

    [16] Humo watapata wakitakacho, wataneemeshwa kwa neema za daima, zisio katika. Na neema hizi ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Walimwomba Mola wao Mlezi itimie, naye akawaitikia kwa walilo liomba; kwani ahadi yake hayendi kinyume.

  202. 25:17
    ۝١٧

    Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia? [17]

    Tanbihi

    [17] Na taja, kwa ajili ya mawaidha, Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya washirikina kwa ajili ya hisabu katika Siku ya Kiyama, pamoja na hao ambao walikuwa wakiwaabudu duniani badala ya Mwenyezi Mungu, kama Yesu (Isa), Ezra (Uzair) na Malaika. Mwenyezi Mungu atawauliza hao waabudiwa: Je! Ni nyinyi ndio mlio wapoteza waja wangu, mkawaamrisha wakuabuduni, au wao wenyewe ndio walio potea Njia kwa khiari yao, wakakuabuduni?

  203. 25:18
    ۝١٨

    Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia. [18]

    Tanbihi

    [18] Jawabu yao itakuwa: Umetakasika, na Umetukuka! Haikutafalia sisi kabisa tumtake mlinzi badala yako atunusuru na aangalie mambo yetu. Basi itakuwaje juu ya haya tumtake yeyote atuabudu sisi badala yako Wewe? Lakini sababu ya ukafiri wao hawa ni kuwa uliwastarehesha kwa muda mrefu duniani, wao na baba zao. Hayo yakawapandisha kichwa, wakasahau kukushukuru, na kukuelekea Wewe tu kwa ibada. Basi wakawa kwa jeuri hiyo na ukafiri huo wanastahiki kuangamizwa.

  204. 25:19
    ۝١٩

    Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa. [19]

    Tanbihi

    [19] Wataambiwa wenye kuabudu, washirikina: Wamekukadhibisheni hao mlio kuwa mkiwaabudu, ambao mkidai kuwa wamekupotezeni. Basi nyinyi leo mnarejea kwenye adhabu. Hamna hila ya kuepukana nayo; wala hamyapati manusura ya kukutoeni. Na wajue waja wote kwamba mwenye kudhulumu kwa ukafiri na uasi kama walivyo fanya hao basi Sisi tutawaadhibu adhabu kali.

  205. 25:20
    ۝٢٠

    Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona. [20]

    Tanbihi

    [20] Na ikiwa washirikina wanakutia ila ewe Nabii, kwa kula kwako chakula, na kwenda kwako masokoni kwa ajili ya kazi na kuchuma maisha, basi huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa Mitume wake walio kuja kabla yako. Hatukumtuma yeyote kati yao ila alikuwa akila chakula, na anakwenda kwenda masokoni. Na enyi watu! Tumewafanya baadhi yenu wawe ni mitihani kwa wenginewe. Na mafisadi wanafanya hila kuziba Njia ya Uwongofu na Haki kwa namna mbali mbali. Basi, enyi Waumini, mtavumilia juu ya Haki yenu, na mtaishikilia Dini yenu, mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake kwa ushindi? Subirini! Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote, na atamlipa kila mtu kwa kitendo chake.

Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani