Juzuu 4
- 3:93٩٣
Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israili isipo kuwa alicho jizuilia Israili mwenyewe kabla haijateremshwa Taurati. Sema: Leteni Taurati muisome ikiwa nyinyi ni wasema kweli. [93]
Tanbihi
[93] Mayahudi waliwatoa kombo Waislamu kwa kuhalalisha baadhi ya vyakula kama nyama ya ngamia na maziwa yake. Wakadai kuwa hayo yaliharimishwa na sharia ya Ibrahim. Mwenyezi Mungu Subhanahu aliwarudi madai yao hayo kwa kubainisha kuwa vyakula vyote vilikuwa halali kwa Wana wa Yaakub (ndiye Israil) kabla ya kuteremka Taurati, ila alicho jizuia Yaakub mwenyewe kwa sababu zilizo mkhusu yeye tu, basi na wao wakijiharimishia nafsi zao. Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii wake awatake walete uthibitisho wa Taurati kuwa sharia ya Ibrahim imeharimisha hayo kama wao wanasema kweli. Wakashindwa, wakanywea.
- 3:94٩٤
Na wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo, basi hao ndio madhaalimu. [94]
Tanbihi
[94] Ilipo thibiti kuwa wameemewa basi wenye kumsingizia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hoja hizo, hao ndio walio selelea na udhaalimu wao, na wanastahiki kuitwa Madhaalimu.
- 3:95٩٥
Sema: Mwenyezi Mungu amesema kweli. Basi fuateni mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina. [95]
Tanbihi
[95] Baada ya kushindwa kwao Mwenyezi Mungu amemuamrisha Nabii wake awabainishie kuwa ukweli wa Mwenyezi Mungu umethibiti katika ayasemayo. Basi ifuateni Sharia ya Ibrahim anayo kutakeni muifuate, na nyinyi mnaikanusha. Hii ni mbali kabisa na hizo Dini za uwongo, kwani Ibrahim hakuwa miongoni mwa washirikina.
- 3:96٩٦
Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, (Makka) iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote. [96]
Tanbihi
[96] Katika kufuata mila ya Ibrahim ni kuelekea wakati wa Swala Nyumba aliyo ijenga, na kwenda kuhiji huko. Mwenyezi Mungu amebainisha hayo kwa kusema: Hakika Nyumba ya awali kwa ukongwe na utukufu aliyo ijaalia Mwenyezi Mungu iwe ni ya ibada kwa watu ni hiyo iliyoko Makka (au Bakka kama pia inavyoitwa). Nayo ina kheri nyingi na manufaa, na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameijaalia iwe na baraka. Nayo Nyumba hiyo ni pahali pa uwongofu kwa watu kwa kuhiji na kuelekea wakati wa Swala.
- 3:97٩٧
Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu. [97]
Tanbihi
[97] Zipo dalili wazi za kuonyesha utakatifu wake huo Msikiti wa Makka na kuzidi fadhila zake. Miongoni mwa hizo ni hapo alipo kuwa akisimama Nabii Ibrahim a.s. kwa kuswali. Na pia kuwa anaye ingia humo huwa amesalimika halimpati ovu. Na kuhiji Makka ni waajibu wa kila mtu awezae kwenda. Na mwenye kukataa, akaiasi amri ya Mwenyezi Mungu, na akaipinga Dini yake, basi khasara itamuangukia mwenyewe, na Mwenyezi Mungu anajitosha, hawahitajii watu wote.
- 3:98٩٨
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha ishara za Mwenyezi Mungu, na ilhali kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi kwa yote mnayo yatenda? [98]
Tanbihi
[98] Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la amemuamrisha Mtume wake awahizi Watu wa Kitabu kwa kuendelea kwao kukufuru na kupotoka na kupotosha, akasema: Enyi Watu wa Kitabu! Huo ukafiri wenu hauna sura wala maana. Kwa sababu gani mnakanusha dalili, na hoja za Mwenyezi Mungu zenye kuthibitisha Unabii na Ukweli wa Muhammad? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvijua vitendo vyenu na atakulipeni malipo yake.
- 3:99٩٩
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia aliye amini Njia ya Mwenyezi Mungu mkiitafutia kosa, na hali nyinyi mnashuhudia? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda. [99]
Tanbihi
[99] Enyi Watu wa Kitabu! Vipi mnajaribu kumgeuza mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuifuata Haki aache Njia Iliyo Nyooka ya Mwenyezi Mungu wa Kweli, na mnajaribu kuikosoa Njia hiyo, na nyinyi mnajua kuwa hiyo ndiyo Haki? Wala Mwenyezi Mungu hakughafilika na vitendo vyenu, naye atakulipeni kwavyo.
- 3:100١٠٠
Enyi mlio amini! Mkiwat'ii baadhi ya walio pewa Kitabu watakurudisheni kuwa makafiri baada ya Imani yenu. [100]
Tanbihi
[100] Mwenyezi Mungu anawahadharisha Waumini na vitimbi vya baadhi ya Watu wa Kitabu,(Mayahudi na Wakristo), vya uchochezi wao wa udanganyifu kwa kusema: Mkiwat'ii baadhi ya Watu wa Kitabu katika yale wanayo yaeneza ya kutilisha shaka katika Dini yenu, itakuwa mnarajea tena kwenye upotovu baada ya uwongofu, na wakurejezeni muwe makafiri baada ya kuwa ni Waumini.
- 3:101١٠١
Na vipi mkufuru hali nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume yuko kati yenu? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi huyo ameongozwa kwenye Njia Iliyo Nyooka. [101]
Tanbihi
[101] Hebu izingitieni hali yenu ya ajabu, kuwa mnapotoka na mnakufuru baada ya Imani, na hali mnasomewa Qur'ani, na Mtume mnaye, anakubainishieni na anakukingeni na upotovu katika Dini yenu. Na mwenye kumkimbilia Mola wake Mlezi, na akashikamana na Dini yake, basi huyo amefanya vyema. Mola wake Mlezi amemwongoa kwenye Njia ya kufuzu na kufaulu.
- 3:102١٠٢
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu. [102]
Tanbihi
[102] Hakika mlango wa shari uwazi ikiwa hamumchi Mwenyezi Mungu. Basi enyi mlio amini! Mkhofuni Mwenyezi Mungu kwa khofu inayopasa, kwa kutenda anayo amrisha, na kuyaepuka anayo yakataza. Na dumuni juu ya Uislamu mpaka mtakapo kutana na Mwenyezi Mungu.
- 3:103١٠٣
Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka. [103]
Tanbihi
[103] Nyote nyinyi shikamaneni na Dini ya Mwenyezi Mungu, wala msifanye jambo litalo leta mfarakano baina yenu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlivyo kuwa wakati wa ujahili nyinyi kwa nyinyi maadui. Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zenu kwa Uislamu, mkawa mnapendana, na ilhali kwa sababu ya ukafiri wenu na kufarikiana kwenu mlikuwa juu ya ukingo wa Moto, akakuokoeni kwa Uislamu. Kwa mfano wa bayana kama hii ya pekee Mwenyezi Mungu anakubainishieni daima njia za kheri, ili mdumu katika uwongofu.
- 3:104١٠٤
Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa. [104]
Tanbihi
[104] Hakika njia ya kuungana kuliko kamilika juu ya Haki katika kivuli cha Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kivuli cha Mtume wake, ni kuwa muwe nyinyi Umma unao lingania (unao itia) watu waje wafuate mwendo utao waletea maslaha ya Dini na dunia, uamrishe ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, ukataze maasia. Na hapo ndipo mtakuwa mlio fuzu, kufuzu kulio kamilika.
- 3:105١٠٥
Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa. [105]
Tanbihi
[105] Wala msiwe kwa kupuuza kwenu kuamrisha mema na kukataza maovu--mambo ambayo ndiyo yanayo kukusanyeni katika kheri na Dini ya Haki--kama wale walio puuza kuamrisha mema na kukataza maovu,wakagawika mapande mbali mbali, wakakhitalifiana katika Dini yao baada ya kuwafikilia hoja zilizo wazi, zenye kubainisha Haki. Na hao walio farikiana wakakhitalifiana, watapata adhabu kuu.
- 3:106١٠٦
Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zitasawijika (kuwa nyeusi). Ama hao ambao nyuso zao zitasawijika wataambiwa: Je! Mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mnakufuru. [106]
Tanbihi
[106] Adhabu kuu hiyo itakuwa Siku zitapo nawiri nyuso za Waumini kwa furaha, na kusawijika kwa masikitiko na huzuni nyuso za makafiri. Wataambiwa kwa kuwatahayarisha: Je, mmekufuru baada ya kuwa mlikulia juu ya Imani na ut'iifu wa haki, na mkaletewa hoja zilizo wazi? Basi onjeni adhabu kwa sababu ya ukafiri wenu!
- 3:107١٠٧
Ama wale ambao nyuso zao zitanawiri watakuwa katika rehema ya Mwenyezi Mungu. Wao humo watadumu. [107]
Tanbihi
[107] Ama wale nyuso zao zimekuwa nyeupe, yaani zimenawiri, kwa kufurahi, hao watakuwa katika Pepo ambayo Mwenyezi Mungu amewapa kwa rehema yake, wadumu humo milele.
- 3:108١٠٨
Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu walimwengu. [108]
Tanbihi
[108] Na hizo Aya zilizo kuja za kueleza kuwa mwema na mwovu watalipwa tunakusomea, nazo zimekusanya haki na uadilifu. Na Mwenyezi Mungu hataki kumdhulumu yeyote kati ya watu na majini.
- 3:109١٠٩
Na kila kilichomo Mbinguni na kilichomo Ardhini ni cha Mwenyezi Mungu; na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu. [109]
Tanbihi
[109] Na vyote viliomo Mbinguni na Ardhini ni vya Mwenyezi Mungu peke yake, ni vyake kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kuvisarifu. Na marejeo ya mambo yao ni kwake Yeye. Kwa hivyo humlipa kila mmoja kama anavyo stahiki.
- 3:110١١٠
Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu. [110]
Tanbihi
[110] Nyinyi Umma wa Muhammad ni bora ya umati alio umba Mwenyezi Mungu kwa manufaa ya watu, maadamu mtaamrisha ut'iifu na mtakataza maasi, na mtakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu kwa Imani safi na ya kweli. Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeli kuwa ni wakweli katika imani yao kama nyinyi, basi ingeli kuwa ni bora kwao kuliko walivyo. Walakini baadhi yao ni Waumini, na wengi wao wameikiuka mipaka ya Imani na yanayo pasa.
- 3:111١١١
Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na wakipigana nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa. [111]
Tanbihi
[111] Hao wapotovu hawawezi kukudhuruni nyinyi kama walivyo kuandalieni, wala hawakuathirini. Ijapo kuwa mtapata maudhi kwao, lakini athari yake haiselelei. Na hata wakipigana nanyi wataingia kiwewe wakimbie wasipambane nanyi, na hapo mwishoe hawatopata ushindi juu yenu maadamu nyinyi mtashikamana na kuamrisha mema na kukataza maovu.
- 3:112١١٢
Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu. Na wakastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na wamepigwa na unyonge. Hayo ni kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasina haki; hayo ni kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka. [112]
Tanbihi
[112] Na Mwenyewe Subhana ameeleza kuwa lazima watapata madhila popote watapo kutikana, ila wakifungamana kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya Waislamu. Na wao wamestahiki wapate ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pia Mwenyezi Mungu amewajaalia lazima uwafikie unyonge na unyenyekevu kwa wengineo. Na hayo ni kwa sababu ya kukataa kwao Ishara zote za Mwenyezi Mungu zinazo onyesha Unabii wa Muhammad s.a.w. na vile kuridhi kwao hapo zamani kuuliwa Manabii ambako hakuwezi kuwa ni kwa haki, bali ni kwa uasi wao na uadui wao.
- 3:113١١٣
Wote hao si sawa sawa. Miongoni mwa Watu wa Kitabu wamo watu walio simama baraabara, wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za usiku, na pia wanasujudu. [113]
Tanbihi
[113] Watu wa Kitabu si wote sawa sawa. Miongoni mwao wapo walio simama msimamo mwema, wa uadilifu, wanakisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu nyakati za usiku wakiswali.
- 3:114١١٤
Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanakimbilia katika mambo ya kheri. Na hao ndio miongoni mwa watenda mema. [114]
Tanbihi
[114] Wanaamini kweli kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwa Yeye ni Mmoja tu. Wanaamini Mitume wote, hawamuabudu ila Mwenyezi Mungu. Na wanaamini kuwa itafika Siku ya Kiyama; wanaamrisha ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, na wanakataza maasi, na wanawania kutenda mambo ya kheri. Hawa kwa Mwenyezi Mungu huhisabiwa miongoni mwa watenda wema.
- 3:115١١٥
Na kheri yoyote wanayo ifanya hawatanyimwa malipwa yake. Na Mwenyezi Mungu anawajua wachamngu. [115]
Tanbihi
[115] Kheri yoyote wanayo ifanya watu hao hawatonyimwa thawabu zake. Na Mwenyezi Mungu amezizunguka kwa kuzijua na kuziweza hali zao na malipo yao.
- 3:116١١٦
Hakika wale walio kufuru hazitawafaa kitu mali zao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio watu wa Motoni - humo watadumu. [116]
Tanbihi
[116] Wale walio kufuru, mali yao na wangayatoa kuwa ni fidia hayatowafaa kitu, wala watoto wao na wangawataka msaada hawatoweza kuwasaidia hata chembe kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu katika Akhera. Na hawa ndio walio lazimika kuingia Motoni na waselelee humo.(wadumu)
- 3:117١١٧
Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la watu walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao. [117]
Tanbihi
[117] Hakika hali ya wanacho kitoa makafiri duniani kuwa ni sadaka au cha kuwakaribisha mbele ya Mwenyezi Mungu Akhera mfano wake, kwa kuwa ni kazi bure katika ujira wa vitendo, ni kama hali ya shamba la watu walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi. Shamba hilo likakumbwa na upepo wenye baridi kali ya barafu, likateketea shamba lote kuwa ni malipo yao. Wala Mwenyezi Mungu siye aliye wadhulumu ujira wa kazi yao, lakini ni wao wenyewe ndio walio jidhulumu nafsi zao kwa kufanya yaliyo sabibisha hayo. Nayo ni kuzipinga dalili na ushahidi wa Imani na kumkufuru Mwenyezi Mungu.
- 3:118١١٨
Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo kudhuruni. Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia akilini. [118]
Tanbihi
[118] Enyi mlio amini! Msitafute kuwafanya marafiki wa ndani watu wasio wa Dini yenu mkatumai msaada kwao, na mkawa mkiwapa siri zenu. Hao hawatoacha kuyafisidi mambo yenu, kwani wao wanapenda mno kukutieni taabuni na kukudhuruni kwa madhara makubwa. Zimekwisha dhihiri ishara za bughdha yao kukuchukieni nyinyi katika kuropokwa ndimi zao. Na yaliyo ficha nyoyo zao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kuonyesheni alama za kumtambua rafiki na adui kama nyinyi ni watu wa akili na utambuzi wa kweli.
- 3:119١١٩
Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala wao hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani. [119]
Tanbihi
[119] Enyi nyinyi Waumini! Mnawapenda hawa makafiri na wanaafiki kwa ajili ya ujamaa, au urafiki au mapenzi tu. Na wao, lakini, hawakupendeni kwa sababu ya kuing'ang'anilia dini yao. Na nyinyi mnaamini Vitabu vyote vilivyo teremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanapo kutana nanyi hujitia imani ili kukudanganyeni. Na wakisha kuacheni huziuma ncha za vidole vyao kwa chuki na kukasirika. Ewe Nabii! Waambie: Endeleeni na hiyo chuki yenu mpaka mfe! Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyajua yanayo fichikana vifuani, na atakulipeni kwavyo.
- 3:120١٢٠
Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo. [120]
Tanbihi
[120] Nyinyi mkipata neema, kama vile kushinda vitani na ngawira, wao husikitika. Mkipata msiba kama ukame na kushindwa, wao hufurahia msiba wenu. Lakini nyinyi mkisubiri juu ya maudhi yao, na mkajizuilia na kule kuwafanya urafiki mliko katazwa, basi maudhi yao na uadui wao hautakudhuruni kitu. Kwani Yeye Aliye tukuka anavijua vyema vitimbi wanavyo vifanya, wala Yeye hashindwi kukulindeni nao.
- 3:121١٢١
Na pale ulipo toka asubuhi, ukaacha ahali zako uwapange Waumini kwenye vituo kwa ajili ya vita - na Mwenyezi Mungu anasikia na anajua. [121]
Tanbihi
[121] Na hebu taja Ewe Nabii! Pale ulipo toka asubuhi mapema ukaacha ahali zako, watu wako wa nyumbani, ukenda mpaka Uhud kwa makusudi ya kuwaweka Waumini katika makao yao kwa ajili ya vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia kauli zenu, ni Mwenye kuzijua niya zenu.
- 3:122١٢٢
Makundi mawili miongoni mwenu yakaingiwa na woga kuwa watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao; na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. [122]
Tanbihi
[122] Ilipo tokea kuwa vikundi viwili vya Waumini kuingiwa na khofu ya kushindwa na wakataka kurejea nyuma, Mwenyezi Mungu aliwalinda akawapa moyo wa kuthibiti, wakasonga mbele katika vita. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye utawala katika mambo yao mawili, na ndiye wa kuwalinda na kuwawezesha kwa kuwapa tawfiqi. Basi Waumini nawachukue funzo kutokana na haya, na wamtegemee Yeye ili awanusuru.
- 3:123١٢٣
Na Mwenyezi Mungu alikwisha kunusuruni katika Badri nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru. [123]
Tanbihi
[123] Mwenyezi Mungu amewakumbusha Waumini ile neema ya nusura aliyo wapa katika vita vya Badri waliposubiri. Akawahakikishia kuwa Yeye ndiye aliye wapa ushindi katika vita vile na ingawa walikuwa wachache na wapungufu wa silaha; akawataka wamt'ii kuwa ni shukrani kwa neema hiyo. Badri ipo mwendo wa kiasi ya maili 120 kusini magharibi ya Madina. Mpambano hapo baina ya Waislamu na Makureshi ulikuwa siku ya Jumaane 17 Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra (13 Machi 624 B.K.). Mtume s.a.w. na Masahaba wake walitoka Madina taarikh 8-9 ya Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra (5 Machi 624 B.K.) Idadi ya wapiganaji wa Kiislamu katika vita hivi ilikuwa kiasi watu mia tatu au zaidi kidogo, na Washirikina walizidi mara tatu kuliko hao. Mwenyezi Mungu alitimiza ahadi yake katika vita hivi, Waumini wakashinda juu ya kuwa ni wachache, kwa kuwa Imani yao juu ya haki na uadilifu ilikuwa kubwa. Na kuungwa mkono na Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa na moyo wenyewe kulikuwa ni sababu za ushindi kuliko wingi wa watu na ubora wa silaha. Ushindi huu ulio dhaahiri ukawa ndio sababu ya kuenea Neno la Imani na kutukuka likawa juu. Na hichi ni chanzo cha yaliyo kuja baadae, na kivuli cha Uislamu kikatanda Arabuni kote, na kisha kwengineko ulimwenguni.
- 3:124١٢٤
Ulipo waambia Waumini: Je, haitakutosheni ikiwa Mola wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tatu walio teremshwa? [124]
Tanbihi
[124] Ushindi ulipatikana Mtume alipo waambia Waumini: Haitatosha kukutulizeni nafsi zenu Mola wenu Mlezi ikusaidieni kwa Malaika elfu tatu watakao letwa ili kukutieni nguvu?
- 3:125١٢٥
Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu. [125]
Tanbihi
[125] Ndio! Msaada huo unakutosheni. Na pindi mkivumilia vita, na mkashikilia uchamngu, na hata maadui zenu wakikutokeeni kwa ghafla, Mola wenu Mlezi atawaongeza hao Malaika mpaka wafike elfu tano ili kukupeni nguvu.wakikutokeeni kwa ghafla, Mola wenu Mlezi atawaongeza hao Malaika mpaka wafike elfu tano ili kukupeni nguvu.
- 3:126١٢٦
Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikima. [126]
Tanbihi
[126] Na wala Mwenyezi Mungu hakujaalia huko kukuleteeni msaada wa Malaika ila iwe ni bishara tu kwenu ya ushindi, na zipate kutulia nyoyo zenu. Na hapana ushindi ila unao tokana na Mwenyezi Mungu Mwenye Kushinda wote, ambaye anapanga kila kitu kwa pahala pake, na anaye wapangia mambo waja wake Waumini.
- 3:127١٢٧
Haya ni kwa ajili awakate sehemu katika walio kufuru, au awahizi wapate kurejea nyuma nao wamepwelewa. [127]
Tanbihi
[127] Naye Mwenyezi Mungu amekupeni ushindi ili wateketee baadhi ya wale walio kufuru kwa kuuwawa, au wadhalilike na awakasirishe kwa kushindwa na aibu na hizaya, wapate kurejea nao wameemewa.
- 3:128١٢٨
Wewe huna lako jambo katika haya - ama atawahurumia au atawaadhibu, kwani wao ni madhaalimu. [128]
Tanbihi
[128] Huna lako katika ninayo wafanyia waja wangu, kwani mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Ama atawasamehe kwa Imani, au atawaadhibu kwa kuuwawa na hizaya na mateso ya Siku ya Kiyama, kwani hao ni madhaalimu.
- 3:129١٢٩
Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika Mbingu na vilivyomo katika Ardhi. Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye kurehemu. [129]
Tanbihi
[129] Bila ya shaka vitu vyote vilioko katika Mbingu na katika Ardhi ni vya Mwenyezi Mungu peke yake, kwa kuviumba na kuvimiliki. Na Yeye ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu, kila kitu kimo mikononi mwake. Yeye humsamehe ampendaye na akamuadhibu amtakaye. Lakini kusamehe kwake ndiko kulio karibu zaidi, na rehema yake ni ya kutarajiwa sana zaidi. Kwani Yeye hakika ni mwingi wa kusamehe na kurehemu.
- 3:130١٣٠
Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa. [130]
Tanbihi
[130] Enyi mlio amini! Mkikopesha msichukue katika deni ila rasilmali yenu tu. Msifanye kuzidisha juu ya deni faida ya kuzidi mwaka kwa mwaka ikawa kuzidi juu kwa juu. Msiyale mali ya watu kwa upotovu. Hakika nyinyi mtaongokewa na mtafuzu pindi mkiepukana na riba, ikiwa ndogo au kubwa.
- 3:131١٣١
Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya makafiri. [131]
Tanbihi
[131] Tahadharini na Moto ulio andaliwa kwa ajili ya makafiri kwa kujiepusha kutafuta kuihalalisha riba.
- 3:132١٣٢
Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa. [132]
Tanbihi
[132] Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume katika kila wanacho amrisha na kila wanacho kikataza ili mpate kurehemeka duniani na Akhera.
- 3:133١٣٣
Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni Mbingu na Ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu, [133]
Tanbihi
[133] Na kuweni wa mbele katika kutenda mema ili mpate kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote, maghfira makubwa ya kufutiwa dhambi zenu, na Pepo yenye wasaa, na upana wake ni kama upana wa Mbingu zote na Ardhi. Hayo wametengenezewa wale wanao mcha Mwenyezi Mungu na wakaiogopa adhabu yake.
- 3:134١٣٤
Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema; [134]
Tanbihi
[134] Hao wachamngu ndio wale wanao toa mali yao kwa kumridhi Mwenyezi Mungu wanapo kuwa na neema na wasaa, na pia wanapo kuwa na shida na dhiki na uzito, na wanazuia ghadhabu zao wanapo kasirishwa wasiwaadhibu wale wanao wakosa, bali wanawasamehe walio watendea mabaya. Hao kwa haya huhisabiwa kuwa ndio watenda mema. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwalipa mema hao watenda mema na huwa radhi nao.
- 3:135١٣٥
Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua. [135]
Tanbihi
[135] Watu hao nao pindi wakifanya makosa makubwa au dhambi ndogo tu, mara humkumbuka Mwenyezi Mungu na Utukufu wake, na adhabu zake na malipo yake mema, na rehema yake na ghadhabu zake. Tena hapo hujuta kwa waliyo tenda na wakaomba msamaha wake, na hapana anaye samehe madhambi ila Mwenyezi Mungu. Na hao wachamngu hawabaki kuendelea juu ya jambo baya na ilhali wanajua ubaya wake.
- 3:136١٣٦
Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao. [136]
Tanbihi
[136] Basi hao wenye kusifika kwa sifa hizi ujira wao ni maghfira makubwa kutokana na Mola wao Mlezi, Mwenye kumiliki mambo yao yote, na Bustani zipitazo mito kati ya miti yake, na humo watadumu daima. Na hayo ni malipo ya neema kubwa ilioje kwa watendao amri za Mwenyezi Mungu.
- 3:137١٣٧
Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanao kanusha. [137]
Tanbihi
[137] Enyi Waumini, kabla yenu shani ya Mwenyezi Mungu imewapitia kaumu zilizo kadhibisha kwa mapuuza yao. Mwenyezi Mungu akawashika kwa madhambi yao. Basi zingatieni vipi yalikuwa matokeo ya vitendo vya walio kadhibisha.
- 3:138١٣٨
Hii ni bayana kwa watu wote, na ni uwongofu, na mawaidha kwa wachamngu. [138]
Tanbihi
[138] Kwa kutajwa sifa za Waumini na kueleza shani ya Mwenyezi Mungu iliyo pita kwa walio kwisha tangulia lipo Bayana na Uwongozi kwa watu wafuate njia ya kheri, na kuwaachisha njia ya shari.
- 3:139١٣٩
Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini. [139]
Tanbihi
[139] Wala nyinyi msilegelege mkadhoofika katika Jihadi Fi Sabili Llahi kwa yanayo kupateni, na wala msihuzunike kwa wanao uliwa miongoni mwenu, kwani nyinyi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na Imani yenu na nguvu za Haki mnayo ipigania mko juu. Ushindi ni wenu ikiwa Imani yenu ni ya kweli, na maadamu mtadumu nayo.
- 3:140١٤٠
Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu; [140]
Tanbihi
[140] Ingawa katika vita vya Uhud wameuwawa au kujuruhiwa vibaya baadhi yenu na kwa hayo mkaathirika nafsi zenu, lakini msilegee na kuhuzunika. Kwani hao makhasimu zenu yaliwapata kama hayo katika vita vya Badri. Nyakati za ushindi huendeshwa na Mwenyezi Mungu kwa watu kama apendavyo, pengine hawa hushinda, na pengine hawa, ili awatie mtihani na kuwajaribu Waumini, awateuwe wenye kusimama imara juu ya Imani yao, na apate kuwatukuza baadhi yao kwa kuwafisha mashahidi katika Sabili Llahi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi washirikina wenye kudhulumu na wangashinda kwa kusaidiwa na wengineo.
- 3:141١٤١
Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri. [141]
Tanbihi
[141] Kwa huku kushindwa kwa muda, Mwenyezi Mungu anawasafisha jamaa Waumini, na anawat'ahirisha kutokana na wale wenye nyoyo mbaya na imani dhaifu, na wenye kueneza moyo wa kushindwa na wasiwasi; na kwa hivyo ndio anaung'olea mbali ukafiri na makafiri wenyewe pia.
- 3:142١٤٢
Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri? [142]
Tanbihi
[142] Enyi Waumini! Msidhani kuwa mtaingia Peponi bila ya kubainika kati yenu wepi Mujahidiina, Wapigania Haki, wenye kusubiri na kuvumilia ambao wanat'ahirishwa na misukusuko na shida.
- 3:143١٤٣
Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama. [143]
Tanbihi
[143] Nyinyi mlikuwa mkitaka kufa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kabla hamjayaona mauti na mkajua kitisho chake. Sasa basi nyinyi mmekwisha yaona mauti walipo uliwa ndugu zenu mbele yenu nanyi mnaangalia.
- 3:144١٤٤
Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao mshukuru. [144]
Tanbihi
[144] Katika vita vya Uhud ulitoka uvumi kuwa ati Mtume Muhammad s.a.w. kauwawa. Baadhi ya Waislamu walidahadari wakaingiwa kiwewe wakataka kurtadi, kuuacha Uislamu. Mwenyezi Mungu aliwakaripia kwa kuwaambia: Muhammad si chochote ila ni Mtume tu, na kabla yake wamekufa Mitume mfano wake yeye. Naye atakufa kama walivyo kufa wao, na atapita kama wao walivyo pita. Je, akifa au akauliwa ndio mtarejea nyuma kwenye ukafiri wenu? Na mwenye kurejea kwenye ukafiri baada ya kwisha amini, basi hatomdhuru kitu Mwenyezi Mungu, ila atakuwa anajidhuru nafsi yake kwa kujipeleka kwenye mateso. Na Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema wale wenye kusimama imara juu ya Uislamu, wenye kuishukuru neema yake.
- 3:145١٤٥
Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye kushukuru. [145]
Tanbihi
[145] Hayumkini mtu kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye amekwisha viandikia viumbe ajali yao. Na atakaye starehe ya dunia Mwenyezi Mungu atampa, na atakaye malipo ya Akhera atayapata. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao shukuru neema yake wakamt'ii kwa aliyo waamrisha ikiwa ni kupigana Jihadi au mengineyo.
- 3:146١٤٦
Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri. [146]
Tanbihi
[146] Na Manabii wangapi wamepigana vita na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi kwa Mola wao Mlezi! Nyoyo zao hazikuingia woga, wala azma zao hazikudahadari, wala hawakuwanyenyekea maadui zao kwa sababu ya masaibu yaliyo wapata katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu. Haya ni kwa sababu wamo katika ut'iifu wake, na Mwenyezi Mungu huwalipa wanao vumilia ikiwafika balaa.
- 3:147١٤٧
Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri. [147]
Tanbihi
[147] Na kauli yao vilipo kuwa vita vikali haikuwa ila kusema: Mola wetu Mlezi! Tusamehe dhambi zetu kubwa na ndogo. Na tusimamishe imara katika midani za vita, na utunusuru na hawa maadui wa Dini yako, wenye kukukanya Wewe na ujumbe wa Mtume wako.
- 3:148١٤٨
Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema. [148]
Tanbihi
[148] Mwenyezi Mungu akawapa ushindi na tawfiqi katika dunia, na akawadhaminia malipo mema kwa Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwalipa wale wafanyao vitendo vyema.
- 3:149١٤٩
Enyi mlio amini! Ikiwa mtawat'ii walio kufuru watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri. [149]
Tanbihi
[149] Enyi mlio amini! Mkiwat'ii maadui zenu makafiri, walio tangaza ukafiri wao au wakauficha, kwa hayo wanayo kuitieni kwa maneno au vitendo, watakuja kugeuzeni muingie ukafirini. Na hapo tena itakuwa mmekhasiri dunia na Akhera.
- 3:150١٥٠
Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye bora wa wasaidizi. [150]
Tanbihi
[150] Mwenyezi Mungu ndiye wa kukunusuruni, basi msiwaogope hao binaadamu wenzenu, kwani Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kunusuru.
- 3:151١٥١
Tutazitia khofu nyoyo za walio kufuru kwa vile walivyo mshirikisha Mwenyezi Mungu na washirika ambao hakuwateremshia hoja yoyote. Na makaazi yao ni Motoni; na maovu yaliyoje maskani ya wenye kudhulumu! [151]
Tanbihi
[151] Yasikutieni unyonge yaliyo kupateni siku ya Uhud. Sisi tutaingiza khofu na vitisho katika nyoyo za maadui zenu kwa kuwa wao wamemshirikisha Mwenyezi Mungu na miungu mengine ambayo Mwenyezi Mungu hakuwateremshia hoja yoyote. Kwani Miungu hiyo hainufaishi wala haidhurishi kitu. Na makao yao yatakuwa Motoni Akhera, na maovu mno hayo makao ya madhaalimu.
- 3:152١٥٢
Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile mlivyo kuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipo legea na mkazozana juu ya amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu wanao taka dunia, na wapo miongoni mwenu wanao taka Akhera. Kisha akakutengeni nao (maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwisha kusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya Waumini. [152]
Tanbihi
[152] Nusura ya Mwenyezi Mungu ni jambo la hakika ya kweli. Mwenyezi Mungu ametimiza miadi yake kuwa alikupeni ushindi pale mara ya kwanza mlipo wauwa maadui wengi kwa radhi yake; mpaka yalipo dhoofika maoni yenu katika vita na mkakhitalifiana kuifahamu amri ya Nabii aliyo kupeni msiondoke kwenye vituo vyenu. Baadhi yenu mkaacha vituo vyenu mlipo ona mnashinda, na wengine wakabaki mpaka mwisho. Kikundi kimoja kikaasi amri ya Mtume kikenda kuwania ngawira baada ya kwisha kuonyeshwa mkipendacho, nao ni ushindi. Mkawa makundi mawili, wanao taka raha ya dunia, na wanao taka malipo ya Akhera. Ilivyo kuwa hivyo Mwenyezi Mungu akaondoa kwenu nusura yake, mkashindwa, ili akujaribuni, atambulikane mwenye ikhlasi na asiye kuwa nayo. Lakini sasa amekusameheni kwa kuwa mmejuta. Na Mwenyezi Mungu ana fadhila kwenu kwa kukusameheni na kukubali toba yenu.
- 3:153١٥٣
Pale mlipo kuwa mkikimbia mbio wala hamumsikilizi yeyote, na Mtume anakuiteni, yuko nyuma yenu. Mwenyezi Mungu akakupeni dhiki juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yaliyo kukoseeni wala kwa yaliyo kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda. [153]
Tanbihi
[153] Enyi Waumini! Hebu ikumbukeni hali yenu wakati ule mlipo kuwa mkitoka mbio wala hamumsikii mtu kwa shida ya kukimbia; na Mtume anakuiteni nyuma yenu mrejee. Mwenyezi Mungu akakujazini huzuni ya kufudikiza kama wingu lilio funika nafsi zenu, ili msisikitike kwa ngawira mlizo zikosa wala kushindwa kuliko kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema makusudio yenu na vitendo vyenu.
- 3:154١٥٤
Kisha baada ya dhiki alikuteremshieni utulivu - usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jengine nafsi zao ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyo kuwa ya haki, dhana ya kijinga. Wakisema: Hivyo tuna lolote sisi katika jambo hili? Sema: Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyo kubainishia. Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusinge uliwa hapa. Sema: Hata mngeli kuwa majumbani mwenu, basi wangeli toka walio andikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe. (Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani. [154]
Tanbihi
[154] Kisha Mwenyezi Mungu baada ya dhiki akakupeni neema ya utulivu, ambao ulidhihiri kwa usingizi ulio wafunika wale walio wa kweli katika Imani yao na kumtegemea kwao Mwenyezi Mungu. Ama kile kikundi kingine, hamu yao ni juu ya nafsi zao tu hawana jenginelo; kwa hivyo wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbovu za kijahiliya, wakisema kwa kuchukiwa: Tumepata ushindi wowote sisi huo tulio ahidiwa? Sema ewe Nabii: Mambo yote ya kushinda na kushindwa yako kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kuyaendesha mambo kwa waja wake pindi wao wakichukua khatua za ushindi, au wakifanya mambo ya kusabibisha kushindwa. Na wao wanapo sema hayo wana jambo wanalo lificha katika nafsi zao, wala hawalidhihirishi. Kwani wao husema: Ingeli kuwa sisi tuna khiari yetu tusingeli toka, basi tusingeli shindwa. Waambie: Hata mngeli kuwa ndani ya majumba yenu na kama wapo walio andikiwa kuuliwa basi hapana shaka wangeli toka mpaka pahala pao pa kufa wakauliwa. Na Mwenyezi Mungu amefanya aliyo yafanya hapo Uhud kwa maslaha makubwa, ili apate kutoa ndani yenu ikhlasi, na azitahirishe nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua vilivyo yaliyo fichika ndani ya nyoyo zenu.
- 3:155١٥٥
Hakika wale walio rudi nyuma miongoni mwenu siku yalipo pambana majeshi mawili, Shet'ani ndiye aliye watelezesha kwa sababu ya baadhi ya makosa waliyo yafanya; na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole. [155]
Tanbihi
[155] Enyi jamaa wa Kiislamu! Wale miongoni mwenu walio acha kusimama imara pale pahali pao walipo wekwa wasimame hakika ni Shetani ndiye aliye wavuta kwenye utelezi na kukosea kwa sababu ya makosa yao kumkhaalifu Mtume. Lakini Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe, kwani Yeye ni mwingi wa maghfira, na mwingi wa upole.
- 3:156١٥٦
Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio kufuru na wakawasema ndugu zao walipo safiri katika nchi au walipo kuwa vitani: Wangeli kuwa kwetu wasingeli kufa na wasingeli uwawa. Ili Mwenyezi Mungu afanye hayo kuwa ni majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo. [156]
Tanbihi
[156] Enyi mlio amini! Msiwe kama walio kufuru wakasema, kwa mintarafu ya wenzao wanapo ondoka kwenda safarini kutafuta maisha wakafa, au wakenda vitani wakauwawa: Lau wangeli bakia nasi hapa wasingeli kufa, na wasingeli uwawa. Mwenyezi Mungu amejaalia kauli yao hiyo na dhana yao iwe ni majuto ya nyoyoni mwao. Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha, na kudra ya kila kitu imo mikononi mwake. Yeye anayajua yote myatendayo, ya kheri na shari. Na Yeye ndiye wa kukulipeni.
- 3:157١٥٧
Na pindi mkiuliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au mkifa, hakika maghfira na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yote wanayo yakusanya. [157]
Tanbihi
[157] Na mkiuwawa katika Jihadi au mkafa wakati huo, basi hayo hakika ni kupata maghfira ya Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi zenu, na kupata rehema itokayo kwake. Hayo ni bora kuliko starehe za dunia ambazo mnge zikusanya lau mngeli bakia.
- 3:158١٥٨
Na mkifa au mkiuliwa ni kwa Mwenyezi Mungu ndio mtakusanywa. [158]
Tanbihi
[158] Na lau mtakufa au mtauliwa katika Jihadi hazitopotea bure a'mali zenu, kwani mtakusanywa kwa Mwenyezi Mungu akulipeni kwa Jihadi yenu na ikhlasi yenu.
- 3:159١٥٩
Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea. [159]
Tanbihi
[159] Ilikuwa ni rehema ya Mwenyezi Mungu kwako wewe (Muhammad) na kwao (Waumini) kwa kuwa wewe umekuwa laini kwao wala hukuwatolea neno la ukali kwa kukosea kwao. Na lau kuwa wewe ungeli kuwa unawachukulia kwa ukavu, na moyo mgumu wangeli kukimbia. Basi nawe yapuuze makosa yao, na waombee msamaha, na ushauriane nao katika mambo ili upate maoni yao katika mambo ambayo siyo ulio teremshiwa ufunuo, Wahyi. Ukisha funga azimio lako juu ya jambo baada ya kushauriana, basi endelea nalo na huku ukimtegemea Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu humpenda anaye mwakilisha mambo yake Yeye.
- 3:160١٦٠
Akikunusuruni Mwenyezi Mungu hapana wa kukushindeni, na akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye ataye kunusuruni? Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. [160]
Tanbihi
[160] Mwenyezi Mungu akikuungeni mkono kwa nusura yake, kama ilivyo tokea siku ya Badri, hatokushindeni yeyote. Na akikuacheni mkono kwa kuwa nyinyi hamkuchukua khatua zifaazo za ushindi, kama yaliyo pita siku ya Uhud, basi hamtakuwa na wa kukunusuruni mwenginewe. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio yawapasa Waumini wategemeze mambo yao yote.
- 3:161١٦١
Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa. [161]
Tanbihi
[161] Haisihi kuwa Nabii yeyote kukhuni katika ngawira kama walivyo eneza kwa uzushi wanaafiki waongo. Kwani khiyana ni kinyume na Unabii. Basi isikupitikieni dhana hiyo. Na mwenye kukhuni atakuja Siku ya Kiyama na mzigo wa dhambi wa khiyana yake, tena kila nafsi italipwa ilicho tenda, kwa ukamilifu. Na wala hawatadhulumiwa kwa kupunguzwa thawabu zao wala kuzidishiwa adhabu yao.
- 3:162١٦٢
Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea. [162]
Tanbihi
[162] Hawawezi kuwa sawa, anaye piga mbio kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa vitendo na ut'iifu, na yule anaye stahiki ghadhabu kuu ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya uasi wake. Na mwenye kuasi ataishia Jahannamu, na kuovu kulioje huko!
- 3:163١٦٣
Hao wana vyeo mbali mbali kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote wayatendayo. [163]
Tanbihi
[163] Makundi mawili hayo hayawi sawa, bali yametafautiana mbele ya Mwenyezi Mungu kwa daraja mbali mbali. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zao na daraja zao, na atawalipa kwa mujibu wake.
- 3:164١٦٤
Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi. [164]
Tanbihi
[164] Mwenyezi Mungu amewafadhili Waumini wale wa mwanzo walio kuwa na Nabii s.a.w. kwa kuwapelekea Mtume aliye tokana na wao wenyewe, akiwasomea Aya za Kitabu, na akiwat'ahirisha na itikadi mbovu, akiwafundisha Qur'ani na Sunna za Mtume, na ilhali kabla ya kuletwa Mtume, walikuwa katika ujinga na ubabaishi na upotovu.
- 3:165١٦٥
Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi mmekwisha watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka kwenu wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. [165]
Tanbihi
[165] Hivyo mnapigwa na mshangao na kuemewa pale yalipo kupateni siku ya Uhud masaibu ambayo nyinyi mlikwisha wapa maadui mara mbili mfano wa hayo katika siku ya Badri, hata mnasema kwa mastaajabu: Yamekuwaje mauwaji haya na kushindwa huku, na sisi ni Waislamu na Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nasi? Sema: Yaliyo kupateni yametokana na nafsi zenu kwa vile mlivyo mkhalifu Mtume. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, naye amekulipeni kwa mujibu wa mlivyo tenda.
- 3:166١٦٦
Na yaliyo kusibuni siku yalipo pambana majeshi mawili yalikuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ili awajue Waumini. [166]
Tanbihi
[166] Enyi Waumini! Yaliyo kusibuni lilipo pambana jeshi lenu na jeshi la Washirikina katika Uhud yametokana kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu, na ili awadhihirishie watu Imani ya Waumini ya kweli aliyo ifunza.
- 3:167١٦٧
Na ili awapambanue walio kuwa wanaafiki, wakaambiwa: Njooni mpigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu au lindeni. Wakasema: Tungeli jua kuna kupigana bila ya shaka tungeli kufuateni. Wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anajua kabisa wanayo yaficha. [167]
Tanbihi
[167] Na hayo ili pia udhihiri unaafiki wa wanaafiki. Nao hawa ni wale walipo kuwa wanaondoka wanaacha vita wakaambiwa: Njooni mpigane kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu, au kwa ajili ya kujilinda nafsi zenu. Wakasema: Lau kuwa tunajua kuwa mtakutana na vita, tungeli kwenda nanyi. Na wao walipo sema kauli hiyo walikuwa karibu zaidi na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao: Huko hakuna vita. Na hali wanaitakidi ndani ya nyoyo zao kuwa vita kweli vitakuwepo. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema unaafiki wanao uficha, kwani Yeye anajua matokeo ya siri zao.
- 3:168١٦٨
Hao ndio walio waambia ndugu zao na wao wenyewe wakakaa kitako: Lau wengeli tut'ii wasingeli uliwa. Sema: Ziondoleeni nafsi zenu mauti kama mnasema kweli. [168]
Tanbihi
[168] Na hao ndio walio baki nyuma wesende vitani wakakwepa, na wakasema kwa mintarafu ya ndugu zao walio toka wakauliwa: Lau wangeli tufuata sisi wakakaa nyuma kama tulivyo kaa sisi wangeli okoka kama tulivyo okoka. Waambie: Zizuieni nafsi zenu basi zisife, kama mnasema kweli kuwa hadhari inazuia kadari.
- 3:169١٦٩
Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi. [169]
Tanbihi
[169] Wala usidhani kabisa kuwa walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti, bali hao wahai kwa uhai anao ujua Mwenyewe Mwenyezi Mungu, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi, riziki njema anayo ijua Yeye.
- 3:170١٧٠
Wanafurahia aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. [170]
Tanbihi
[170] Nyuso zao zinameremeta kwa furaha na bishara kwa fadhila ya pekee aliyo wapa Mwenyezi Mungu, na wanawafurahia ndugu zao ambao walio waacha duniani wangali wahai, wanashika mwendo wa Imani na Jihadi, na ya kwamba hapana khofu juu yao kupata lolote la karaha wala si wenye kuhuzunika kwa kumkosa mpendwa.
- 3:171١٧١
Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa Waumini. [171]
Tanbihi
[171] Nyuso za Mashahidi zinameremeta kwa neema ya kufa shahidi na neema ya Pepo, na ubora wa karama, na ya kwamba haupotei ujira wa Waumini.
- 3:172١٧٢
Walio mwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya kwisha patwa na majaraha - kwa walio fanya wema miongoni mwao na wakamchamungu utakuwa ujira mkubwa. [172]
Tanbihi
[172] Waumini hao ni wale ambao wameitikia wito wa Mtume wa kuanza upya Jihadi baada ya pigo kubwa walilo lipata katika vita vya Uhud. Kwa hivyo basi wakawa ni wenye kutenda wema, na wakajilinda na kuasi amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakastahiki ujira mkubwa katika Nyumba ya Malipo na Neema.
- 3:173١٧٣
Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. [173]
Tanbihi
[173] Hao ndio walio tiwa khofu na watu kwa kuwaambia: Maadui zenu wamekusanya jeshi kubwa kukupigeni, basi waogopeni. Na wao hawakudhoofika wala hawakulegea, bali walizidi Imani ya Mwenyezi Mungu na wakawa na moyo kuwa atawanusuru. Jawabu yao ikawa: Mwenyezi Mungu anatutosheleza. Yeye ndiye aliye tawala mambo yetu. Na Yeye ndiye anaye tegemezwa mambo yote.
- 3:174١٧٤
Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya lilio wagusa, na wakafuata yanayo mridhi Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu. [174]
Tanbihi
[174] Kisha wakatoka kwenda kwenye Jihadi na kupambana na hilo jeshi kubwa, lakini washirikina wakaingiwa na woga wakakimbia. Wakarejea Waumini kuwa wameshinda kwa neema ya salama ilhali wao wana hamu ya Jihadi, na wana malipo na thawabu na fadhila ya Mwenyezi Mungu kwao kwa vile kutia kitisho katika nyoyo za maadui zao, na wao wasipatikane na maudhi yoyote. Waliitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wao wakaistahiki fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
- 3:175١٧٥
Hakika huyo ni Shet'ani anawatia khofu marafiki zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini. [175]
Tanbihi
[175] Mwenyezi Mungu Aliye takasika anawabainishia Waumini kwamba hao wanao kutieni khofu kuogopa kupambana na maadui zenu si lolote ila ni vibaraka wa Shetani anaye watia khofu wafwasi wake awafanye woga. Na nyinyi si katika hao. Basi msiridhie kutishwa, bali mkhofuni Mwenyezi Mungu peke yake kama nyinyi mna Imani ya kweli, na mnasimamia kutimiza yanayo lazimishwa na Imani hiyo.
- 3:176١٧٦
Wala wasikuhuzunishe wale wanao kimbilia ukafirini. Hakika hao hawamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee sehemu yoyote katika Akhera, na yao wao adhabu kubwa. [176]
Tanbihi
[176] Ewe Nabii! Usihuzunike ukiwaona wale ambao wanazidi ukafiri, na wanawania kuzidisha maovu. Hao hawamletei Mwenyezi Mungu madhara yoyote, kwani Yeye ni Mwenye nguvu juu ya waja wake. Bali Mwenyezi Mungu anataka wasiwe na sehemu yoyote katika thawabu za Akhera, na juu ya kukosa kwao thawabu hizo njema watapata adhabu kubwa.
- 3:177١٧٧
Hakika wale walio nunua ukafiri kwa Imani hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na yao wao ni adhabu chungu. [177]
Tanbihi
[177] Hakika watu hao walio khiari ukafiri badala ya Imani, wakatafuta ukafiri na wakaacha Imani, hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na watapata Akhera adhabu kali ya kutia uchungu mkubwa.
- 3:178١٧٨
Wala wasidhani wale wanao kufuru kwamba huu muhula tunao wapa ni kheri yao. Hakika tunawapa muhula wazidi madhambi. Na yao wao ni adhabu ya kuwadhalilisha. [178]
Tanbihi
[178] Wasidhani hao makafiri kuwa vile kuwapururia tunapo wakunjulia umri wao, na tukawapa njia za starehe katika maisha yao ya duniani, kuwa ndio kheri yao. Kwani kuwaongezea umri na kuwakunjulia riziki huwapelekea kudumu na kuchuma madhambi na kuzidi kustahiki adhabu ya kuwafedhehesha aliyo waandalia Mwenyezi Mungu.
- 3:179١٧٩
Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka apambanue wabaya na wema. Wala haiwi kwa Mwenyezi Mungu kukujuulisheni mambo ya ghaibu. Lakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume wake amtakaye. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake. Na mkiamini na mkamchamngu mtakuwa na ujira mkubwa. [179]
Tanbihi
[179] Haiwi kuwa Mwenyezi Mungu akuacheni enyi jamaa Waumini katika hali mliyo nayo ya mchanganyiko wa Muumini na mnaafiki, mpaka awatenganishe baina yenu kwa misukosuko na taabu ili mumwone mnaafiki khabithi na Muumini mwema. Wala sio mwendo wa Mwenyezi Mungu kumjuulisha yeyote katika viumbe vyake khabari za ghaibu. Walakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume yake ampendaye akamjuvya anacho kitaka katika mambo yake ya ghaibu. Na nyinyi mkiamini na mkamcha Mola wenu Mlezi kwa kujilazimisha kumt'ii atakutieni katika Pepo iwe ndio malipo. Na hayo ndio malipo yaliyo bora na makubwa kabisa.
- 3:180١٨٠
Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili Siku ya Kiyama. Na urithi wa Mbingu na Ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote myatendayo. [180]
Tanbihi
[180] Wasidhani wanao fanya ubakhili kwa mali aliyo waneemesha Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na hawayatoi katika yaliyo waajibu na njia za kheri, kuwa ubakhili huo ni kheri yao. Bali hiyo ni shari yenye matokeo mabaya juu yao. Watalipwa malipo maovu kabisa Siku ya Kiyama, na adhabu itawaganda kama kongwa au mnyororo aliyo fungwa nayo mfungwa shingoni mwake. Kila kiumbe kinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, naye ndiye Mmiliki wao, na Yeye Aliye takasika anajua kila mnacho kitenda, na atakulipeni kwacho.
- 3:181١٨١
Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya walio sema: Mwenyezi Mungu ni masikini, na sisi ni matajiri. Tumeyaandika waliyo yasema, na pia kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya kuungua. [181]
Tanbihi
[181] Juu ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kumiliki kila kiliomo mbinguni na ardhini na Yeye ndiye mrithi wa vyote, wamesema baadhi ya Mayahudi kwa kejeli: Mwenyezi Mungu ni fakiri, ndiyo akatutaka tutoe, na sisi ni matajiri tukitoa au tusitoe. Mwenyezi Mungu amekwisha isikia kauli yao hiyo, na ameisajili dhidi yao, kama alivyo sajili kuwauwa kwao Manabii kwa dhulma na ukhalifu na uadui. Naye atawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya Moto unao waka!
- 3:182١٨٢
Haya ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yenu, na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye mu waja. [182]
Tanbihi
[182] Na hiyo adhabu ni kwa dhambi zao walizo zitenda wenyewe, na malipo ya Mwenyezi Mungu hayawi ila ni kwa uadilifu, wala Yeye kabisa hawadhulumu waja wake.
- 3:183١٨٣
Walio sema: Mwenyezi Mungu ametuahidi tusimuamini Mtume yeyote mpaka atuletee kafara inayo teketezwa na moto. Waambie: Walikujieni Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa hayo mnayo sema, basi kwa nini mkawauwa ikiwa mlikuwa wakweli?. [183]
Tanbihi
[183] Hao ndio walio sema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tusimfuate Mtume yeyote ila akileta dalili ya ukweli wake kwa kutuletea kitu cha kumkurubisha kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu, na uteremke moto kutoka mbinguni ukile hicho kitu. Ewe Nabii! Waambie: Hakika Mitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu wamekwisha kukujieni kabla yangu, wakaja na dalili zilizo wazi, na wakaja na hayo mnayo yasema. Na juu ya hayo mliwakadhibisha na mkawauwa. Kwa nini mkafanya hayo kama nyinyi ni wasema kweli katika ahadi yenu ya Imani yanapo timia mnayo yataka?
- 3:184١٨٤
Na wakikukanusha basi walikanushwa Mitume wengine kabla yako walio kuja na hoja waziwazi na Vitabu vyenye hikima, na Kitabu chenye Nuru. [184]
Tanbihi
[184] Ikiwa watakukadhibisha, Ewe Nabii, wewe usisikitike. Kabla yako wamekutangulia wengi walio kadhibishwa na watu wao kwa chuki na inda, juu ya kuwa walikuja na dalili zilizo nyooka, na Vitabu vya mbinguni vyenye kuthibitisha ukweli wa Ujumbe wao.
- 3:185١٨٥
Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu. [185]
Tanbihi
[185] Hapana hivi wala hivi, kila nafsi lazima ionje Mauti. Na ikiwa hapa duniani mtapata machungu basi Siku ya Kiyama mtalipwa thawabu kwa ukamilifu. Na mwenye kuukaribia Moto akaepushwa nao basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe yenye kupita, haina dawamu.
- 3:186١٨٦
Hapana shaka yoyote mtapata misukosuko katika mali zenu na nafsi zenu, na bila ya shaka yoyote mtasikia udhia mwingi kutokana na walio pewa Kitabu kabla yenu na wale walio shiriki. Na ikiwa mtasubiri na mkamchamungu basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia. [186]
Tanbihi
[186] Kuweni na yakini, enyi Waumini, kuwa mtapata mitihani na majaribio katika mali yenu, kwa kupungua, kutoa au kunyang'anywa, na katika nafsi zenu kwa Jihadi au kuuwawa au kwa maradhi na machungu. Na kadhaalika mtasikia kutokana na Mayahudi na Wakristo na mapagani, washirikina, matusi na uchokozi wa kukuudhini. Na mkiyakaabili hayo kwa kuvumilia na kumcha Mwenyezi Mungu basi itakuwa ni katika mambo mema yanayo wajibika kuazimia kuyatimiliza.
- 3:187١٨٧
Na pale Mwenyezi Mungu alipo fungamana na walio pewa Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho walicho nunua. [187]
Tanbihi
[187] Ewe Nabii! Kumbuka na utaje pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi madhbuti kwa Watu wa Kitabu, kuwa wayaeleze wazi maana ya Kitabu chao, na wala wasiwafiche watu chochote, na wao wakakitupilia mbali nyuma ya migongo yao, na badala yake wakatafuta starehe za dunia. Na starehe za dunia kama zitakavyo kuwa ni kitu chenye thamani duni kabisa kulinganisha na uwongofu na uwongozi. Ama wamejua kutenda uovu! (Hayo yalikuwa zamani na bado yanaendelea. Kuficha na kugeuza na kupotosha Biblia hakusiti. Vipo vitabu vyao vinavyo itwa "Apokrifa", maana yake "Vilivyo fichwa", kwa kuwa hivyo ni marfuku visisomwe ila na mapadri tu, na vingine vimeteketezwa. Miongoni mwa hivyo ni Injili ya Barnaba.)
- 3:188١٨٨
Usiwadhanie kabisa wale wanao furahia waliyo yafanya, na wakapenda kusifiwa kwa wasiyo yatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika na adhabu. Yao wao ni adhabu chungu. [188]
Tanbihi
[188] Usiwadhanie kabisa kuwa wataepuka adhabu wale wanao tenda maovu, na wakapenda kusifiwa kwa wasilo lifanya. Shani yao hao ni kujifungia mlango wa Imani na Haki, kama Mayahudi. Nao watapata adhabu chungu Siku ya Kiyama.
- 3:189١٨٩
Na Ufalme wa Mbingu na Ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. [189]
Tanbihi
[189] Mwenyezi Mungu pekee ndiye Mwenye mamlaka ya kila jambo la Mbinguni na duniani. Naye ni Muweza wa kila kitu. Atawashika wenye dhambi kwa dhambi zao, na atawalipa thawabu watendao mema kwa wema wao.
- 3:190١٩٠
Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili. [190]
Tanbihi
[190] Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na viliomo ndani yao kwa vile vilivyo umbwa tangu mwanzo na mipango yake, na kukhitalifiana usiku na mchana kwa mwangaza na giza, kwa urefu wake na ufupi, zipo dalili na ishara zilizo wazi kwa watu wenye akili na kutambua za kuthibitisha Umoja wa Mwenyezi Mungu na Uwezo wake. "Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana ziko ishara kwa wenye akili" - Aya hii ina ukweli unao onyeshea taadhima ya Muumba. Mbingu ni moja katika Ishara za Mwenyezi Mungu inayo tubainikia kwetu kwa miale ya jua inayo piga juu ya anga linalo izunguka dunia. Miale hii inapo angukia chembe chembe na vumbi vumbi jembamba liliopo angani humulika mianga hiyo na kutawanyika kila upande. Huu mwanga mweupe kwa hakika ni mkusanyiko wa rangi zote zionekanazo. Hizi chembe chembe za angani huzimeza baadhi ya hizo rangi. Imedhihiri kuwa rangi yenye kuenea zaidi ni rangi ya kibuluu. Na hii inazidi kuzagaa linapo kuwa jua liko utosini, na ubuluu wake unapungua kidogo kidogo mpaka jua linapo kuwa upeo wa macho wakati wa magharibi au alfajiri. Wakati huo ile miale ya jua inakwenda masafa makubwa zaidi kabisa. Kwa hivyo zile chembe chembe za angani huzimeza rangi zote isipo kuwa rangi nyekundu. Usafi wa maneno ni: mwangaza wa mchana unahitaji miale ya jua na kuwepo vumbi la kutosha katika anga. Dalili ya hayo ni yale yaliyo tokea mwaka 1944 mbingu ilipo ingia kiza ghafla kati ya mchana. Jinsi ya kiza mchana ukawa kama usiku. Kwa wakati mfupi yakawa hayo, kisha mbingu ikawa nyekundu, kisha kidogo kidogo ikawa rangi ya machungwa, na kisha ya manjano mpaka mbingu ikarejea rangi yake ya tabia, baada ya saa au zaidi. Baadae ilibainika kuwa mambo hayo yalitokana na mripuko mbinguni likatokea jivu, likachukuliwa na upepo mbali mpaka Afrika ya kati na kaskazini, na kufika magharibi ya Asia. Huko ndiko ikaonekana hali hiyo katika pande za Syria. Maelezo yake ni kuwa vumbi lilioko hewani liliifunika nuru ya jua. Lilipo pungua jivu ulidhihiri mwangaza mwekundu na baadae wa manjano n.k. Mwanaadamu akipaa angani katika chombo atapitia matabaka yanayo khitalifiana sifa. Ataiona mbingu inazidi ubuluu mpaka akifika kwenye anga la nje lisio kuwa na hayo mavumbi n.k. ataona mbingu yote ni kiza kitupu kama kwamba ni usiku juu ya kuwa jua lipo juu. Kwa ufupi ni kuwa zipo mbingu nyingi si moja ziliyo pandana tabaka kwa tabaka kama maqubba, zinazo khitalifiana katika sifa zake na rangi zake. Haya ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliye takasika kuwa vyote viliomo mbinguni na ardhini vinamtukuza Yeye. Ama kukhitalifiana usiku na mchana, tumekwisha fahamu kuwa mwanga wa mchana unategemea miale ya jua kuanguka juu ya hili funiko la anga, lenye chembe chembe za vumbi kwa kiasi maalumu. Mwangaza huu ni mkali hata unaficha mwangaza unao toka kwenye nyota n.k. Ama wakati wa usiku mwangaza wa jua unapo fichika, inakuwa hapana katika anga isipo kuwa vumbi linalo tuzunguka na mianga dhaifu ya nyota. Kupishana usiku na mchana ni kwa sababu ya kuzunguka dunia kwa nafsi yake wenyewe, na tafauti ya misimu na kurefuka na kufupika usiku na mchana ni kwa mzunguko wa hii dunia kulizunguka jua. Na katika hikima yake Mwenyezi Mungu na uwezo wake ni kuwa kubadilika usiku na mchana, na kubadilika misimu ya joto na baridi, ni kutengeneza hali ya hewa iwe wastani, yaani kati na kati, kwa kusilihi maisha ya vilivyo hai.
- 3:191١٩١
Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa Mbingu na Ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto. [191]
Tanbihi
[191] Ni shani ya wenye akili kuwa kila pahali wao wanahudhurisha katika nafsi zao adhama na utukufu wa Mwenyezi Mungu, wakiwa wamesimama au wamekaa au wamejinyoosha kitandani, na wanazingatia uumbaji wa mbingu na ardhi pamoja na viliomo ndani yake, na huku wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuumba haya ila kwa hikima uliyo ikadiria. Na Wewe umetakasika na kila upungufu. Bali umeumba hivi vyote kuwa ni dalili ya kudra yako, na ishara ya upeo wa hikima yako. Utuhifadhi na adhabu ya Moto kwa kutuwezesha kukut'ii.
- 3:192١٩٢
Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na walio dhulumu hawana wasaidizi. [192]
Tanbihi
[192] Ewe Muumba wetu, na Mwenye kutusimamia mambo yetu, na Mlinzi wetu! Hakika mwenye kustahiki Moto na ukamuingiza, basi umempa hizaya. Na mwenye kudhulumu akastahiki Moto hana wa kumnusuru nao.
- 3:193١٩٣
Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema. [193]
Tanbihi
[193] Ewe Muumba wetu, na Mwenye kutusimamia mambo yetu, na Mlinzi wetu! Hakika sisi tumemsikia Mtume wako akiita watu wakuamini Wewe, nasi tukamt'ii na tukamuamini. Ewe Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu makubwa, na tufutie maovu yetu madogo madogo, na baada ya kufa kwetu tujaalie tuwe pamoja na waja wako walio bora.
- 3:194١٩٤
Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi. [194]
Tanbihi
[194] Ewe Muumba wetu, na Mwenye kutusimamia mambo yetu, na Mlinzi wetu! Tupe uliyo tuahidi kwa ndimi za Mitume yako, nayo ni ushindi na kuungwa mkono duniani. Wala usituingize Motoni ukatuhizi Siku ya Kiyama. Shani yako ni kuwa huendi kinyume na miadi yako.
- 3:195١٩٥
Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa. [195]
Tanbihi
[195] Mola wao Mlezi aliwaitikia dua yao, akiwabainishia kuwa Yeye hampotezei mtendaji thawabu za vitendo vyake, sawa sawa akiwa mwanamume au mwanamke, kwani mwanamke anatokana na mwanamume, na mwanamume anatokana na mwanamke. Basi wale walio hajiri, wakahama, wakagura, wanatafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wakatolewa makwao, na wakapata mateso katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, wakapigana vita, na wakakhatirisha kuuwawa, bali wakauliwa walio uliwa, Mwenyezi Mungu amejilazimisha Mwenyewe kuwasamehe madhambi yao, na kuwatia kwenye Mabustani yenye kupita kati yake mito, kuwa ni malipo matukufu yaliyo bora kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu peke yake, ndio yako malipo mazuri.
- 3:196١٩٦
Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa walio kufuru katika nchi. [196]
Tanbihi
[196] Usiathirike, ewe Nabii, kwa kuwaona makafiri wamo katika starehe za neema, na biashara na uchumi unawaendea, wakienda huku na huku katika nchi.
- 3:197١٩٧
Hiyo ni starehe ndogo. Kisha makaazi yao yatakuwa Jahannamu. Na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia. [197]
Tanbihi
[197] Hizo ni starehe za kupita njia, na kila kipitacho ni duni. Kisha marejeo ya daima watayo ishia ni Jahannamu. Na hapana makaazi maovu kama Jahannamu.
- 3:198١٩٨
Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata Mabustani yanayo pita mito kati yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na vilioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema. [198]
Tanbihi
[198] Hayo ndiyo malipo ya makafiri. Ama walio muamini Mwenyezi Mungu wakamwogopa Mola wao Mlezi watapata Mabustani yapitayo mito kati yake, watadumu humo daima, kuwa ni wageni walio pokewa kwa ukarimu na Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye takasika. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio mazuri kwa watu wema kuliko hayo wanayo starehea makafiri ambayo yataondoka, hayadumu.
- 3:199١٩٩
Hakika miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na yaliyo teremshwa kwenu na yaliyo teremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawabadili Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani duni. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. [199]
Tanbihi
[199] Hakika baadhi ya Watu wa Kitabu, Mayahudi na Wakristo, wanamuamini Mwenyezi Mungu, na wanaamini aliyo teremshiwa Nabii Muhammad s.a.w. na walio teremshiwa Mitume walio kuwa kabla yake. Utawaona wanamnyenyekea Mwenyezi Mungu, na wanakuwa wanyonge kwake, wala hawabadilishi bayana zilizo dhaahiri kwa ajili ya kutafuta pato la duniani. Hilo nalingawa kubwa ni kitu duni. Hawa wana malipo ya ukamilifu kwa Mola wao Mlezi katika makaazi ya kuridhisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu, hashindwi kuzidhibiti 'amali zao zote na kuwahisabia. Yeye ni Muweza wa hayo na malipo yake yatawafika bila ya shaka.
- 3:200٢٠٠
Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa. [200]
Tanbihi
[200] Enyi mlio amini! Shikamaneni na subira, na mwashinde maadui zenu katika kusubiri. Na kaeni macho kuilinda mipaka, na mkhofini Mola Mlezi wenu. Katika haya yote ndio mtaraji kufanikiwa. (Jee! Baada ya kuijua Qur'ani yamfalia Muislamu kusema kuwa dini ni kitu mbali na siyasa? Vipi uamrishe mema, ukataze maovu, uhukumu, ukatibiane mikataba na dola nyengine, ukusanye zaka na kuzigawa, upigane Jihadi, ulinde mipaka n.k., n.k. na uiepuke siyasa? Amesema Prof. Khurshid Ahmad: "Uislamu si dini kwa maana ya ovyo ovyo kama lilivyo potoshwa neno hilo, yaani kuwa umemkhusu mtu maisha yake ya binafsi tu. Ni mwendo kaamili wa maisha, unao angalia kila midani ya uhai wa binaadamu. Uislamu ni uwongozi katika kila nyendo za maisha - za binafsi na za jamii, za kimwili na kiroho, za uchumi na siyasa, za sharia na mila, za taifa na za mataifa."--Uislamu, Maana na Ujumbe wake uk. 37)
Sura An-Nisaa
سُورَةُ النساء- 4:1١
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni. [1]
Tanbihi
[1] Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na kutokana na nafsi hiyo akamuumba mkewe, na kutokana na hao wawili, wakaenea wanaume na wanawake wengi. Basi nyote mnatokana na nafsi moja. Mcheni Mwenyezi Mungu mnaye mtaka msaada kwa kila mnacho kihitajia, na kwa jina lake ndio mnaombana nyinyi kwa nyinyi katika mambo yenu. Pia tahadharini na kuacha kuwasaidia jamaa zenu, wa karibu na wa mbali. Kwani Mwenyezi Mungu daima anakuangalieni. Hapana chochote katika mambo yenu kinacho fichikana kwake. Na Yeye ndiye Mwenye kukulipeni.
- 4:2٢
Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa. [2]
Tanbihi
[2] Na wapeni mayatima mali yao wanayo stahiki, na yalindeni mali yao vizuri, wala msiwape kilio duni mkawanyima kizuri. Wala msichukue mali yao mkaongezea kwenye mali yenu. Hakika kitendo hicho ni dhambi kubwa.
- 4:3٣
Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana. [3]
Tanbihi
[3] Ilivyo kuwa mnakhofu kuwadhulumu mayatima kwa kuwa hiyo ni dhambi kubwa, basi kadhaalika khofuni machungu ya wake zenu kwa kuacha kuwafanyia uadilifu baina yao, na kuzidisha juu ya wane. Basi mnaweza kuoa wawili, au watatu, au wane, ikiwa mna imani kuwa mtaweza kufanya uadilifu. Mkiogopa kuwa hamtaweza kufanya uadilifu basi oeni mmoja tu, au jitoshelezeni na wajakazi walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hayo ni afadhali kuliko kwenda kuingia katika dhulma na ujeuri . Na ni afadhali msije mkawa na watoto wengi bila ya kiasi hata mshindwe kuwatazama. (Wafasiri wengi wamependelea kufasiri "Alla Tau'luu" kuwa "Kutofanya jeuri au dhulma." Lakini hii AL MUNTAKHAB imekhiari tafsiri hii ya "msikithirishe wana", ambayo ndiyo aliyo ifuata Imam Shaafii r.a., naye alitanguliwa na Maimamu wanazuoni wa Kiislamu, Zayd bin Aslam r.a.na Jabir bin Zayd r.a. kama alivyo simulia Daar Qut'ni, na imetajwa katika Tafsir ya Qurt'uby juzuu ya 5 sahifa 22.) Sharia ya Kiislamu si peke yake inayo ruhusu kuoa wake wengi, miongoni mwa sharia za dini za mbinguni. Sharia ya Taurati inamruhusu mwanamume kuoa idadi ya wanawake atakao. Na imetaja kuwa Manabii walikuwa wakioa wake kwa makumi na makumi. Na Taurati ni katika Agano la Kale la Biblia ambalo linafuatwa pia na Wakristo katika mambo ambayo hayakukatazwa katika Injili au Barua za Mitume. Na hakika iliopo ni kuwa hapana popote katika Agano Jipya panapo pinga sharia hiyo ya kuruhusu kuoa wake zaidi ya mmoja. Kanisa katika Karne za Kati liliruhusu hayo, na wafalme wa Ulaya wa Kikristo walio kuwa na wake wengi ni maarufu katika taarikh (historia). Khitilafu iliyopo ni kuwa Uislamu ndiyo dini ya kwanza kuweka idadi maalumu, isipindukiwe. Imeweka kiwango kwa mambo matatu. (Kwanza) wasipindukie hao wake kuliko wane. (Pili) asidhulumike mmoja katika hao wake, (Tatu) awe mtu anaweza kuwakimu hao wake. Shuruti mbili za mwisho zimelazimu kila ndoa, ijapokuwa ni ya kwanza. Wanazuoni wa Kiislamu wa sharia na wanga khitalifiana wanakubaliana pamoja kuwa mume ambaye anajua kuwa hawezi kuwafanyia uadilifu wakeze ni haramu kwake kidini kuongeza wake. Ila uharamu huu ni wa kidini, watawala na mahakimu hawawezi kumuingilia. Kwani uadilifu ni jambo la nafsi yake mtu, na dhamiri yake, na uwezo wa kutazama ni jambo la mnasaba halifungamani na mizani mojapo. Ni yeye mwenyewe atakaye pata adhabu Siku ya Kiyama akikhalifu amri hiyo. Dhulma au kutokuweza kukimu kunategemea hali ya siku zijazo, na mikataba haifungamani na mambo ambayo huenda yakawa au yasiwe, bali ni juu ya yaliyoko, na ilivyo kuwa dhaalimu huenda akawa muadilifu, na asiye weza sasa hueza akaweza baadae, kwani mali huja na kuondoka, juu ya hivyo Uislamu unasema mwanamume akimdhulumu mkewe au akashindwa kumkimu, basi mwanamke anaweza kutaka kufarikishwa na mume huyo, lakini hazuiliki na kuandikiana mkataba akifanya hayo kwa radhi yake na khiari yake. Na Uislamu kwa kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya mmoja lakini kwa mikazo kama hivyo ilivyo elezwa imekuwa umepiga vita magonjwa ya kijamii: Kwanza - Huenda ikawa idadi ya wanaume wanao faa kuoa ikawa chini kuliko wanawake wanao faa kuoelewa. Khasa huwa hayo baada ya vita. Imeonakana katika baadhi ya nchi za Ulaya imewahi kufika idadi ya wanawake kuwazidi wanaume baada ya vita kwa mara saba! Kwa hivyo ni hishima ya mwanamke katika hali kama hizo kuwa mke-mwenza kuliko kuwa akibahashika kama malaya, bila ya mume. Pili - Huenda kutokea baina ya mwanamume na mwanamke hali inayo walazimisha ama waingiane kiharamu au waoane kisharia. Ni maslaha kwa umma yawe hayo kwa mujibu wa sharia. Na ni bora kwa mwanamke kuwa mke kuliko kuwa hawara wa mwanamume huyu baada ya huyu. Ikiwa hii ni sura mbaya ya kuoa wake wengi, basi juu ya hivyo ni afadhali kuliko kuwa na mke mmoja. Kwani kuoa wake zaidi ya mmoja kama itavyo kuwa vibaya kunakinga shari kubwa zaidi kwa umma, nayo ni umalaya na maovu yanayo pandana nayo. Tatu - Mwanamke hakubali kuolewa na mume mwenye mke ila ikiwa ni kwa dharura iliyo kweli. Ikiwa mke wa kwanza atapata madhara kwa uke-wenza, basi huyu mwenzie atapata madhara makubwa zaidi kwa kuharimishwa mume kabisa, kwa kuwa ama ufe uke wake au apotee kwa wanaume majiani. Madhara makubwa hukingwa kwa madhara yaliyo akali (Kidogo). Nne - Imeonakana kuwa vijana wengi hawapendi kuoa, hata inakisiwa kuwa vijana wanao oa kwa kulinganisha na wafaao kuoa hawazidi kuliko 60%. Na haya yanazidi kila mwaka. Kupinga khatari hii hapana ila kuruhusu kuoa wake wengi. Tano - Huenda mke akapata maradhi ambayo hayamruhusu kulala na mumewe, au huenda akawa tasa. Ni maslaha ya umma na maslaha ya binafsi kuoa mke mwengine. (Wakati huo huo ikawa kumpa talaka huyo mke ni madhara makubwa zaidi kwa mke na ukatili kwa mume kufanya.) Kwa sababu kama hizi na nyenginezo Uislamu umeufungua mlango kwa shida na dhiki, na haukuufunga kabisa. Hivi sasa tunamwona Askofu Mkuu katika Uingereza anaona kuwa dawa ya pekee ya kuondoa uharibifu ulio uingilia ukoo wa Kiingereza ni kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya mmoja. Hakika Uislamu ni Sharia ya Mwenyezi Mungu ambaye anajua kila kitu. Kwani Yeye ndiye Mjuzi Mwenye hikima. (Haya tukijua kuwa dini ya Kikristo haikatazi kuoa wake wengi. Ni sharia zilizo tungwa na makanisa ya Kizungu tu kwa kufuata mila zao ndizo zinazo lazimisha kuoa mke mmoja. Basi hiyo ni mila ya Wazungu, wala si sharia ya dini yoyote duniani. Bali Uislamu ndiyo Dini pekee katika dini zote iliyo wekea kiwango, na kudhibiti idadi ya wanawake kuoa, kwa maslaha ya Umma.)
- 4:4٤
Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha. [4]
Tanbihi
[4] Wapeni wanawake mahari yao kuwa ni kipawa, tunza iliyo safi. Na nyinyi hamna haki yoyote katika hayo mahari. Ikiwa hao wanawake kwa radhi ya nafsi zao wenyewe wakakubali kusamehe sehemu yoyote ya mahari mliyo kwisha ahadiana, basi hapo mnayo ruhusa kuchukua na mkatumia kwa kheri na salama.
- 4:5٥
Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno mazuri. [5]
Tanbihi
[5] Wala msiwape wasio na akili ya kutosha kuendesha mambo yao mali yao, nayo ni mali yenu vile vile. Kwani mali ya yatima na ya mchache wa akili yamekulazimuni myatazame yasiharibike. Mwenyezi Mungu ameyajaalia mali hayo ya kukimu maisha. Wapeni kutokana na pato lake sehemu kama wanavyo hitajia kwa kula, na wavisheni na muwatendee vyema, na mseme nao maneno ya kuwaridhisha sio ya kuwaudhi au kuwadhili.
- 4:6٦
Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu. [6]
Tanbihi
[6] Na kabla ya hao mayatima kufika umri wa kubaalighi wajaribuni, mpate kujua akili zao na hali zao na maarifa yao katika kuendesha mambo. Hata wakifika wakati wa kusilihi kuoa na mkauona uwekevu wao, na matayarisho kuchukua jukumu, basi hapo wapeni mali yao wenyewe. Wala nyinyi msiyale mali yao kwa fujo, mkifanya haraka mpatilize kabla hawajabaalighi wakawa watu wazima ikabidi haki yao kurudi. Na akiwa katika mawasii anajitosha kwa utajiri, basi ajizuie asichukue chochote kuwa ni ujira kutazama mali ya mayatima. Na akiwa fakiri muhitaji basi ajitosheleze kuchukua ujira wa uangalizi kwa kadri ya ada ilivyo. Na mnapo wakabidhi mayatima mali yao wekeni mashahidi wa kushuhudia. Na mjue kuwa Mwenyezi Mungu daima yupo nyuma yenu, na Yeye ndiye Mhasibu, na Yeye ndiye Muangalizi. Na Yeye anatosha kuwa Mhasibu na Muangalizi.
- 4:7٧
Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa. [7]
Tanbihi
[7] Wanaume wanalo fungu lao katika mali waliyo yaacha kurithiwa wazazi wawili na jamaa walio karibia. Na wanawake, aidha, wana fungu lao, bila ya kunyimwa au kupunjwa. Na mafungu hayo yamethibiti, na yamefaridhiwa, na yamekadiriwa, yakiwa mali yenyewe kidogo au mengi.
- 4:8٨
Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini, wapeni katika hayo mali ya urithi, na semeni nao maneno mema. [8]
Tanbihi
[8] Na pindi ikiwa wamehudhuria wakati ule wa kugawanya urithi baadhi ya jamaa ambao hawarithi, na ni mayatima na masikini, basi wakirimuni kwa kuwapa chochote katika huo urithi ili kuzipoza nafsi zao, na kuondoa uhasidi katika nyoyo zao. Na ni vizuri pia katika kuwapa kuleta maneno laini na udhuru mwema.
- 4:9٩
Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao watoto wanyonge wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa. [9]
Tanbihi
[9] Watu watahadhari na kuwadhulumu mayatima, na wawaogopee watoto wao wanyonge wasije na wao wakadhulumiwa kwa watendavyo wazee kwa mayatima wa watu wengine. Na wamwogope Mwenyezi Mungu katika kuwatendea mayatima. Na waseme maneno yaliyo kaa sawa yanayo fuata haki, wala wasimdhulumu yeyote.
- 4:10١٠
Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni. [10]
Tanbihi
[10] Hakika wanao wadhulumu mayatima kwa kuchukua mali yao bila ya haki, hakika wanakula yatakayo wapelekea Motoni. Na Mwenyezi Mungu atawaadhibu Siku ya Kiyama kwa moto mkali wenye kutia machungu.(Je, huwaje basi adhabu ya mwenye kudhulumu mali ya Mwenyezi Mungu? Wakfu za misikiti, madrasa n.k.? Na huwaje mwenye kuuwa ili apate kudhulumu mali ya mayatima wa hao alio wauwa?)
- 4:11١١
Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima. [11]
Tanbihi
[11] Mwenyezi Mungu anakuamrisheni katika mambo ya kuwarithisha watoto wenu na wazazi wenu, pindi mtakapo kufa, kwa njia inayo leta uadilifu na maslaha. Nayo ni kuwa sehemu ya mwanamume ni sawa na sehemu ya wanawake wawili, ikiwa watoto wanao rithi ni wanaume na wanawake. Ikiwa watoto wote ni wanawake watupu, na idadi yao imezidi wawili, basi sehemu yao ni thuluthi mbili za tirka, yaani mali yaliyo achwa na maiti. Inafahamika katika madhumuni ya Aya kuwa fungu la binti wawili ni kama fungu la walio zidi hapo. Na akiwa mtu amemuacha binti mmoja tu, basi fungu lake ni nusu ya alicho kiacha. Na akiwa mtu amemuacha baba na mama, basi kila mmojapo kati ya hao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita, ikiwa huyo maiti alikuwa na mtoto mmoja - mwanamume au mwanamke - pamoja na hao wazazi wake. Akiwa hana mtoto na wakamrithi wazazi wake tu, basi mama sehemu yake ni thuluthi, na kilicho baki ni cha baba. Na ikiwa huyo maiti alikuwa na ndugu, basi mama yake atapata sudusi na kilicho baki ni cha baba, na wale ndugu hawapati chochote. Mafungu hayo hupewa wanao stahiki baada ya kwisha lipwa deni lilio kuwa juu ya maiti, na kutimiza yale aliyo yausia katika mipaka aliyo ruhusu Mwenyezi Mungu. Hii ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. Na huu ndio uadilifu na ndio hikima. Na nyinyi hamjui ni nani kwenu mwenye manufaa zaidi kwenu, baina ya wazazi na wana. Na kheri khasa ni aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuyajua maslaha yenu, na ndiye Mwenye hikima katika yale aliyo kulazimisheni.
- 4:12١٢
Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole. [12]
Tanbihi
[12] Fungu la mume ni nusu ya alicho acha mke ikiwa huyo mke hakuacha mtoto kutokana na mume huyo au mwenginewe. Akiwa huyo mke ana mtoto, basi mumewe atapata robo baada ya kutolewa wasia aliye uusia huyo mwanamke au kulipwa deni lake. Na fungu la mke au wake ni robo ya alicho acha mume ikiwa hakuacha mtoto kwa wake hao au wenginewe. Akiwa anaye mwana kutokana na hao au wake wenginewe basi mke huyu au wake hawa watapata thumni ya tirka baada ya wasia alio usia au deni. Na mwana wa mwana, yaani mjukuu, ni kama mwana katika haya yaliyo tangulia. Na akiwa maiti ni mwanamume au mwanamke, naye hana mwana wala mzazi, na kamwacha ndugu mume kwa mama, au ndugu wawili wa kike kwa mama, basi kila mmoja wao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita. Na wakiwa wengi kuliko hivyo watashirikiana katika thuluthi, watagawana sawa sawa wanaume na wanawake kwa mujibu wa ushirika, baada ya kulipa madeni yaliyo kuwa juu yake, na kutimiza wasia ambao haudhuru urithi, nao ni wasia usio pindukia thuluthi iliyo baki baada ya kulipa madeni. Basi, enyi Waumini! Jilazimisheni kufuata aliyo kuusieni Mwenyezi Mungu; kwani Yeye hakika ni Mwenye kujua vyema nani miongoni mwenu anaye dhulumu na nani anaye fanya uadilifu, Yeye ni Mpole hafanyi haraka kutoa adhabu.
- 4:13١٣
Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa. [13]
Tanbihi
[13] Hizo ni hukumu zilizo tajwa kueleza khabari ya mirathi na mengine yaliyo tangulia ni Sharia za Mwenyezi Mungu aliye zipanga kwa ajili ya waja wake wazijue wala wasizikiuke. Na Mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika alivyo hukumu Yeye malipwa yake yatakuwa ni Pepo ipitayo mito kati yake, na atakaa humo daima dawamu. Na huko ndiko kushinda kukubwa. Mpango wa mirathi uliyo bainishwa na Qur'ani Tukufu ni mpango wa uadilifu na haki kuliko kanuni zote za mirathi nyenginezo duniani. Na haya wameyakiri wataalamu wa sharia wote wa Ulaya. Na huu ni mmoja katika ushahidi wa kuwa Qur'ani inatokana na Mwenyezi Mungu, kwani haya au yaliyo karibia haya hayakuwa yakijuulikana kwa Waajemi wala kwa Warumi wala katika sharia zozote za kabla ya Uislamu. Na sharia hii ya Kiislamu imefuata mipango hii ya uadilifu: Kwanza - Umefanywa urithi kwa mujibu apendavyo Mwenyezi Mungu, sivyo apendavyo mwenye mali, bila ya kupuuza kabisa mapenzi yake huyo. Amepewa huyo ruhusa ya kufanya wasia kwa thuluthi ya mali kwa ajili ya mambo mema, kama kutimiza kasoro katika waajibu wake wa dini, kama Zaka ambazo alikuwa hakuzitoa, au kuwajaalia kitu wahitaji alio khusiana nao kwa ujamaa au mapenzi nao hawastahiki urithi. Na amezuiliwa kufanya wasia ikiwa hayo yatapelekea maasi au yatachochea kuendelea maasia. Na thuluthi mbili zilizo baki baada ya wasia, au mali yote ikiwa hapana wasia, Mwenyezi Mungu Mtunga sharia, amejipa Yeye kuzigawa kwa haki. Pili - Katika kuchukua madaraka ya ugawaji tirka, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, amempa aliye karibu zaidi kuliko mwenginewe, bila ya kuzingatia ukubwa au udogo. Kwa hivyo ndio ikawa watoto wana sehemu kubwa zaidi katika mirathi, kwani wao ndio kiendelezo cha yule maiti, na pia kuwa wao aghlabu ni wanyonge. Juu ya hivyo hawakukoseshwa, bali wameshirikiana nao, mama na bibi, baba na babu, ijapokuwa wanachukua akalli kuliko watoto. Tatu - Yaonekana kuwa mirathi ni kwa kadri ya haja. Kwa hivyo sehemu ya watoto ni kubwa kwa sababu haja yao ni kubwa zaidi, na wao ndio wanayakabili maisha, na kina baba na mama wanayapa mgongo maisha. Ama zingatio la haja ndilo lililo pelekea kuwa fungu la mwanamke liwe nusu ya fungu la mwanamume katika aghlabu ya hali za mirathi. Haya ni kwa kuwa mwanamume inambdi zaidi kukabili matumizi, kwa kuwa yeye anatakikana awalishe watoto na awatazame, amtumilie mwanamke. Maumbile ya kibinaadamu yamemfanya mwanamke ndiye asimamie kazi za nyumbani na kulea watoto, kuangalia raha zao, na mwanmume awe ni wa kuhangaika nje kiuchumi alete fedha za kutumia nyumba nzima. Kumpa kila mmoja kwa kadri ya haja ndio uadilifu. Kuweka sawa kwa wenye haja mbali mbali ni udhalimu. Nne - Sharia ya Kiislamu katika kugawa kwake tirka ya maiti inakusudia kugawa sio kurundika. Kwa hivyo haikufanya urithi wende kwa mtoto mkubwa peke yake, wala haikuwapa wanaume tu na kuwachilia mbali wanawake, wala watoto wakaachwa wazazi. Wala hawakukoseshwa wasio kuwa katika uti wa nasaba, kama ndugu, na maami, na banu-ami n.k. Urithi unaendelea mpaka kwa wanao karibia ukoo, lakini aliye karibu hufadhilika zaidi. Na shida kutokea kuwa mrithi ni mmoja tu. Tano - Mwanamke hakoseshwi kurithi, kama ilivyo kuwa ada ya Waarabu. Hivi ni kumhishimu mwanamke na kumpa haki yake. Na juu ya haya Uislamu hauzuii kurithi ujamaa wa mwanamke, bali hurithi jamaa walio kuwa upande wake, kama wanavyo rithi jamaa upande wa baba. Makaka na madada kwa upande wa mama wanachukua pale wanapo chukua ndugu wa baba na mama, bali katika hali nyengine wanachukua watoto wa kwa mama na kuchukua ndugu wanaume na wanawake. Na haya bila ya shaka ni kuutukuza umama, na kuutambua ukaribu wake. Haya hayakuwa yakijuulikana kabla yake, walakini hii ni Sharia ya Mwenyezi Mungu aliye Mjuzi na Mwenye hikima.
- 4:14١٤
Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha. [14]
Tanbihi
[14] Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akaikiuka mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu, na huku akihalalisha kukiuka huko basi mtu huyo atalipwa Moto, na humo atakaa milele, akiadhibiwa mwili wake juu ya kuadhibiwa roho yake.
- 4:15١٥
Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wane katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine. [15]
Tanbihi
[15] Na wale wanawake wanao zini wakishuhudiwa na mashahidi wanaume wane walio waadilifu, basi wazuieni wasitoke nyumbani kwa ajili ya kuwalinda na kuzuia usiendelee ufisadi na shari mpaka wafe, au Mwenyezi Mungu awafungulie njia ya maisha yaliyo sawa kwa kuolewa na kutubu. (Wafasiri wengine wanasema hukumu hii ni kwa wanawake wanao fanya mambo machafu wenyewe kwa wenyewe, sio ya zina baina ya mwanamke na mwanamume. Kwa kuhifadhi heshima ya wanawake inalazimu wapatikane mashahidi wane, badala ya wawili, walio ona kitendo khasa, sio kuwatuhumu watu kwa jambo ovu kama hilo bila ya mashahidi wane walio shuhudia kwa macho yao.)
- 4:16١٦
Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na wakitubia wakatengenea basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu. [16]
Tanbihi
[16] Mwanamume na mwanamke walio zini, nao hawajaoa (au kuolewa), wapewe adhabu maalumu, pindi ikithibiti hiyo zina kwa mashahidi wane waadilifu. Wakitubu baada ya kupewa adhabu, basi msiwatajie hayo maasi waliyo yatenda, wala msiwaaziri. Hakika Mwenyezi Mungu kwa rehema yake anakubali toba ya wenye kutubu.
- 4:17١٧
Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima. [17]
Tanbihi
[17] Hakika toba imedhaminiwa na Mwenyezi Mungu kwa watendao maovu katika hali ya ujinga, na kupitikiwa na kutoangalia vyema, kisha wakafanya haraka ya kutubu kabla ya kufikiwa na mauti. Hawa basi Mwenyezi Mungu anaikubali toba yao, naye ni Mjuzi, haumfichikii ukweli wa toba, ni Mwenye hikima, hakosei katika kupima.
- 4:18١٨
Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale wanao kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu. [18]
Tanbihi
[18] Toba isiyo kubaliwa ni ya wanao fanya maasi kisha hawafanyi haraka kuyajutia mpaka mmoja afikwapo na mauti. Tena hapo husema: Sasa mimi natangaza majuto na toba. Kadhaalika toba haikubaliwi kutokana na wanao kufa katika ukafiri. Mwenyezi Mungu ameyaandalia makundi mawili hayo adhabu ya kutia uchungu huko kwenye nyumba ya malipo, Akhera.
- 4:19١٩
Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake. [19]
Tanbihi
[19] Enyi mlio amini! Haikujuziini kuwafanya wanawake kama bidhaa, mkiwarithi wake zenu bila ya mahari na bila ya ridhaa yao. Wala msiwadhulumu kwa kuwadhikisha ili wapate kusamehe baadhi ya mahari mlio wapa. Wala msiwadhiki ili wapate kukurejesheeni mali mlio wapa, ila ikiwa wakifanya kosa wazi la kuwacha ut'iifu, au la tabia mbovu, au la ukahaba. Hapo mnaweza kuwadhikisha au kuchukua baadhi ya mlicho wapa wakati wa kufarikiana nao. Na ni waajibu wenu, enyi Waumini, kukaa na wake zenu kwa vizuri, kwa maneno mema na vitendo vyema. Ikiwa mtawachukia kwa aibu fulani katika tabia au katika umbo au mengineyo, basi juu ya hivyo subirini. Msifanye haraka kuwaacha, kwani asaa Mwenyezi Mungu akajaalia kheri nyingi katika hicho hicho mkichukiacho. Na ujuzi wa mambo yote uko kwa Mwenyezi Mungu tu.
- 4:20٢٠
Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi? [20]
Tanbihi
[20] Na pindi ikiwa mnataka kubadili mke pahala pa mke mwengine, na ikawa mmempa mmoja wao mali mengi basi si halali kwenu kuchukua chochote katika hayo. Jee mtachukua hayo kwa njia ya upotovu na kwa dhambi iliyo wazi?
- 4:21٢١
Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti? [21]
Tanbihi
[21] Na vipi ikufalieni nyinyi kutaka kurudishiwa mahari mliyo kwisha yatoa, na hali mlikwisha changanyika nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wakafungamana nanyi kwa agano lenye nguvu ambalo kwalo Mwenyezi Mungu amewajibisha muingiane nao kwa ndoa.
- 4:22٢٢
Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo kwisha pita. Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya. [22]
Tanbihi
[22] Wala nyinyi, watoto, msiwaoe wanawake walio wahi kuolewa na baba zenu. Jambo hilo ni uchafu na linachusha, na linakirihiwa na Mwenyezi Mungu na watu. Na hiyo ni njia ovu kabisa. Lakini Mwenyezi Mungu anasamehe yaliyo kwisha tendeka katika zama za ujahili. Waarabu katika zama za ujahili walikuwa na ada zisio mpa heshima mwanamke, bali zikimdhulumu sana, na zikikata makhusiano mema katika ukoo. Ilikuwa mtu akifa baba yake na akawa na wake wasio kuwa mama yake mzazi, akilazimishwa kuwaoa, au akiwarithi wake za baba yake bila ya ndoa mpya. Na ilikuwa mtu akimwacha mke basi humpokonya kwa dhulma na uadui mahari yote aliyo mpa. Na walikuwapo walio kuwa wakimzuia huyo mt'laka asiolewe na mtu mwengine, kwa jeuri na inda. Ukaja Uislamu, ukamlinda mwanamke na dhulma hii iliyo wazi, ukakataza kurithiwa mke, na kumpokonya mahari yake hata chembe, ijapo kuwa ni mali mengi, na ukakataza kumzuia mt'alaka asiolewe, au kumkera ili apate kutaka yeye mke t'alaka kwa kutoa mali. Na katika mtindo wao Waarabu wa jahiliya ilikuwa yafaa mtu kumwoa aliye kuwa mke wa baba yake na akafarikiana naye kwa t'alaka au mfano wake. Uislamu ukakataza hayo, na ukauwita mtindo huo ni uchafu, kwa sababu ni jambo baya analo lichukia Mwenyezi Mungu na kila mwenye akili sawa. Huo ndio uadilifu wa Mwenyezi Mungu.
- 4:23٢٣
Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [23]
Tanbihi
[23] Mwenyezi Mungu amekuharimishieni kuwaoa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu (ndugu wanawake) na shangazi zenu, na khaalati zenu (mama wadogo) na binti wa ndugu, na binti wa dada, na mama walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wakwe. Na walio harimishwa bila ya kunasibiana kwa damu ni: mama wa kunyonyesha, dada wa kunyonya, mama mkwe, binti za wake kwa waume wengine ikiwa hao wake wameingiliwa, na wake wa watoto mlio wazaa, na kuwaoa pamoja ndugu wawili. Yaliyo pita katika siku za ujahili yamesamehewa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe kwa yaliyo pita kabla ya mpango huu, na Mwenye kuwarehemu katika aliyo kuwekeeni sharia. Ni Sharia ya Kiislamu pekee iliyo harimisha kwa sababu ya kunyonyesha. Anaye nyonya anakula kutokana na mwili wa mnyonyeshaji kama anavyo kula kutokana na mama yake ndani ya tumbo lake. Wote hao wawili wanakuwa ni sehemu yake huyo mtoto. Hapana khitilafu baina ya kukua ndani ya chumba na ndani ya tumbo. Na katika kuharimisha kwa kunyonyesha ni kumtukuza mnyonyeshaji, kwani anakuwa kama mama. Na haya ni kuzidi kushajiisha kunyonyesha kimaumbile, sio kwa chupa, kwa watoto wachanga.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani