Juzuu 23
- 36:28٢٨
Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha. [28]
Tanbihi
[28] Na Sisi hatukawaangamiza kwa kuwapelekea maaskari kutoka mbinguni. Wala huo sio mtindo wetu kupeleka majeshi tunapo yahiliki mataifa.
- 36:29٢٩
Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa! [29]
Tanbihi
[29] Kuteketezwa kwao hakukuwa ila ni kwa ukelele mmoja tu tulio wapelekea. Na mara wao wakawa ni maiti, kama moto ulio zimwa.
- 36:30٣٠
Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli. [30]
Tanbihi
[30] Ee khasara yao, inayo faa kusikitikiwa! Hatuwapelekei waja wangu Mtume ila wao huwa wakimfanyia maskhara.
- 36:31٣١
Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao. [31]
Tanbihi
[31] Kwani wao hawayazingatii mataifa mengi yaliyo tangulia tuliyo yahiliki? Hakika hao hawarejei tena kwenye maisha yao ya duniani.
- 36:32٣٢
Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu. [32]
Tanbihi
[32] Hapana katika mataifa yaliyo tangulia na yajayo ila wote watakusanywa mbele yetu, nao wamelazimishwa kuhudhuria mbele yetu.
- 36:33٣٣
Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila! [33]
Tanbihi
[33] Na dalili kwao ya uweza wetu wa kufufua ni kuangalia vipi ardhi yenye ukame tunavyo ihuisha kwa maji, na kutoa ndani yake nafaka wanazo zila.
- 36:34٣٤
Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake, [34]
Tanbihi
[34] Na humo tukafanya vitalu na mabustani ya mitende na mizabibu, na tukapasua humo chemchem ya kumwagia maji kwenye miti yake, na ikatoa matunda, na wao wakala katika hayo. Na hayo si kazi ya mikono yao. Basi kwa nini hawatoi haki ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yao kwa kumuamini na kumshukuru?
- 36:35٣٥
Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru? [35]
Tanbihi
[35] Na humo tukafanya vitalu na mabustani ya mitende na mizabibu, na tukapasua humo chemchem ya kumwagia maji kwenye miti yake, na ikatoa matunda, na wao wakala katika hayo. Na hayo si kazi ya mikono yao. Basi kwa nini hawatoi haki ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yao kwa kumuamini na kumshukuru?
- 36:36٣٦
Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua. [36]
Tanbihi
[36] Wa kutakasika ni Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu kwa mpango wa ume na uke, katika mimea na katika nafsi zao watu, na katika vitu ambavyo watu hawavijui. Hii harufi Min , yaani "Katika" katika Aya hii ni ya kubainisha. Maana yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ameumba madume na majike katika viumbe vyake vyote, sawa sawa katika mimea, na wanyama, na wanaadamu na vyenginevyo ambavyo watu hawavijui na hawavioni.
- 36:37٣٧
Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani. [37]
Tanbihi
[37] Na Ishara pia ya kuwepo Mwenyezi Mungu na uweza wake, ni huu usiku ambao tunautoa ndani yake mchana, kama kuivua nguo inayo sitiri. Mara utaona watu wamo gizani lilio wazunguka kila upande.
- 36:38٣٨
Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. [38]
Tanbihi
[38] Na jua linakwenda katika njia yake maalumu. Mwenyezi Mungu amekwisha kadiria kwa zama na mahala. Huo ndio mpango wake Mwenye kushinda kwa uweza wake, Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
- 36:39٣٩
Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe. [39]
Tanbihi
[39] Na mwezi kwa mpango wetu tumeujaalia una vituo vyake. Mwanzo wa mwezi unakuwa mdogo na mwembamba. Kisha kila usiku unazidi kukua mpaka unatimia kuwa mbaamwezi. Tena unaingia kupungua vile vile, mpaka ukawa kama karara la mtende linapo kuwa kongwe limepindana na limekuwa manjano.
- 36:40٤٠
Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao. [40]
Tanbihi
[40] Haipelekei jua likaacha sharia zake likakutana na mwezi, na likaingia katika njia zake. Wala usiku hauwi kuushinda mchana ukauzuia usije, bali vyote viwili hivyo hupeana zamu. Na vyote, jua na mwezi, na vyenginevyo vyote vinaogelea katika njia zao za mbinguni, wala haviachi njia. Hakika Aya hizi tukufu zinabainisha ukweli wa ki-ilimu ambao wataalamu walikuwa hawaujui ila mwanzo wa karne ya kumi na nne ya kuzaliwa Nabii Isa. Na jua ni moja katika nyota za mbinguni, nalo kama nyota zilizo baki lina mwendo wake wenyewe. Lakini linakhitalifiana na nyota nyengine kwa kuwa lipo karibu na dunia, na kwa kuwa lina kundi la sayari na miezi ya mikia na sayari ndogo ndogo zinazo lifuata daima, na zinat'ii mvuto wake. Kwa hivyo zinakuwa hizo zinazunguka kwa kufuatana kwa utungo kama sura ya yai. Na mkusanyo wote huu unakwenda angani pamoja na jua kwa mvuto wake. Kwa ufupi jua, na ardhi, na mwezi na sayari zote na vyombo vyote hivyo vinakwenda angani kwa mbio maalumu, na kuelekea jiha maalumu. Na yaonekana kuwa jua na mkusanyo wote huo wake, na nyota zilizo karibu nalo zipo katika mkusanyo ulio tanda katika mbingu inayo itwa kwa Kiarabu Sadiimu almajarrah, au kwa Kiingereza Nebula course. Na imebainika kwa masomo ya kisasa sehemu zote za hiyo Nebula zinaizunguka kati yake kwa mbio ya kunasibiana na kinyume cha umbali wake kutoka hapo kati. Pia imeonakana kuwa jua na ardhi na sayari zake na nyota zilio karibu nayo, vyote hivyo vinakwenda mbio, na upande maalumu. Mbio zake zinafika kilomita 700 kila nukta moja. Na kunatimia kuzunguka kwake kukizunguka hicho kituo cha kati kwa kiasi ya miaka milioni 200 ya muangaza. Na kiini cha maneno ni kuwa Aya tukufu iliyo taja kuwa jua linakwenda kwa kiwango chake, hawakujua wataalamu uzuri wake wa ndani mpaka katika mwanzo wa karne hii. Wala hayamkini jua kuupata mwezi, kwani kila kimojapo kinakwenda katika njia zake mbali mbali, basi ni muhali kukutana, kama ilivyo kuwa ni muhali kupitana usiku na mchana. Hayo ingeli takikana ardhi izunguke juu ya msumari-kati wake kutoka mashariki kwendea magharibi, kinyume na ilivyo hivi sasa kutoka magharibi kwendea mashariki. Na mwezi katika kuizunguka kwake ardhi, na ardhi kulizunguka jua, huenda pamoja na mkusanyo wa nyota unao itwa Manaazil Alqamar au Lunar system. Na katika robo ya mwanzo na ya mwisho wa mwezi huonekana sura yake kama karara kongwe au kole lilio kauka, linapo kuwa kongwe na kunyauka.
- 36:41٤١
Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni. [41]
Tanbihi
[41] Na Ishara nyengine kwao ni kuwa Sisi tuliwapakia wanaadamu katika jahazi ilio jaa bidhaa zao na riziki zao.
- 36:42٤٢
Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda. [42]
Tanbihi
[42] Na tukawaumbia mfano wa hiyo marikebu na vyenginevyo wanavyo vipanda kadhaalika.
- 36:43٤٣
Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi, [43]
Tanbihi
[43] Na tukitaka kuwazamisha, tunawazamisha. Na wala hawapati wa kuwaopoa, wala hawapati wa kuwaokoa wasiangamie.
- 36:44٤٤
Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda. [44]
Tanbihi
[44] Lakini Sisi hatuwazamishi, kwa sababu ya rehema inayo tokana nasi, na ili tuwastareheshe kwa muda ulio kwisha kadiriwa.
- 36:45٤٥
Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa [45]
Tanbihi
[45] Na wanapo ambiwa: Yaogopeni mfano wa yaliyo wapata mataifa yaliyo kwisha pita kwa kukadhibisha kwao, na iogopeni adhabu ya Akhera ambayo itakupateni kwa kushikilia kwenu ukafiri, kwa kutaraji kuwa asaa Mola wenu Mlezi akakurehemuni mkimcha Yeye, wao hupuuza.
- 36:46٤٦
Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza. [46]
Tanbihi
[46] Na haiwajii hoja katika hoja za Mola wao Mlezi, yenye kuonyesha Upweke wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, ila wao huipa nyongo, hawaijali.
- 36:47٤٧
Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri. [47]
Tanbihi
[47] Na wakiambiwa: Wapeni mafakiri kutokana na hicho alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu, makafiri huwaambia Waumini: Je! Tuwalishe watu ambao Mwenyezi Mungu Mwenyewe angeli taka angeli walisha? Hivyo inakuwa tunamfanyia inda Mwenyezi Mungu kwenda kinyume na mapenzi yake! Nyinyi mnao taka tutoe, si chochote ila mmo katika upofu ulio wazi, hamuioni Haki.
- 36:48٤٨
Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli? [48]
Tanbihi
[48] Na huwaambia Waumini kwa kuwafanyia kejeli: Lini yatatokea hayo mlio tuahidi, kama nyinyi mnasema kweli katika mnayo ahidi?
- 36:49٤٩
Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana. [49]
Tanbihi
[49] Hawangojei ila sauti moja tu, iwamalize kwa ghafla, nao wakizozana katika mambo ya kidunia, wameghafilika na Akhera.
- 36:50٥٠
Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei. [50]
Tanbihi
[50] Kwa upesi wa hayo yatakayo wateremkia, hawatowahi kuusia chochote, wala kurejea kwa ahali zao.
- 36:51٥١
Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi. [51]
Tanbihi
[51] Na barugumu litapulizwa kwa mpulizo wa kufufua watu. Mara watu watatoka makaburini mwao wakikimbilia kwenda kukutana na Mwenyezi Mungu. Na hilo barugumu, na kupulizwa kwake, ni katika anayo yajua Mwenyezi Mungu Yeye peke yake.
- 36:52٥٢
Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume. [52]
Tanbihi
[52] Watasema watakao fufuliwa kutoka makaburini: Balaa gani lilio tushukia! Nani aliye tuamsha tukauwacha usingizi wetu? Jawabu ya suala lao itawajia: Hii ndiyo siku ya kufufuliwa aliyo waahidia Arrahaman, Mwingi wa Rehema, waja wake, na Mitume wakaisemea kweli kwa waliyo yasimulia.
- 36:53٥٣
Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu. [53]
Tanbihi
[53] Wito wao wa kuwatoa hautakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watakusanywa mbele yetu wahudhurishwe ili tuwahisabie.
- 36:54٥٤
Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda. [54]
Tanbihi
[54] Basi katika hii siku ya leo haipungukiwi nafsi na chochote katika ujira wake kwa kazi iliyo tenda. Na wala hamtopata isipo kuwa jaza ya mliyo kuwa mkiyatenda, ikiwa ni kheri au shari.
- 36:55٥٥
Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. [55]
Tanbihi
[55] Hakika watu wa Peponi hii leo watakuwa wameshughulika kwa neema walizo nazo, wakistaajabia na kufurahia.
- 36:56٥٦
Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari. [56]
Tanbihi
[56] Wao na wake zao wamo katika vivuli vilivyo enea, wameegemea juu ya viti vilivyo pambwa.
- 36:57٥٧
Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka. [57]
Tanbihi
[57] Wao na wake zao wamo katika vivuli vilivyo enea, wameegemea juu ya viti vilivyo pambwa.
- 36:58٥٨
"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu. [58]
Tanbihi
[58] Wataambiwa: "Salama", kuwa ni kauli iliyo toka kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
- 36:59٥٩
Na enyi wakosefu! Jitengeni leo! [59]
Tanbihi
[59] Na wataambiwa wakosefu siku hii ya leo: Jitengeni mbali na Waumini.
- 36:60٦٠
Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. [60]
Tanbihi
[60] Enyi wanaadamu! Sikukuusieni kuwa msimfuate Shetani kwa ut'iifu kama kwamba ni mungu wa kuabudiwa. Hakika yeye ni adui yenu, aliye dhihirisha uadui wake.
- 36:61٦١
Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. [61]
Tanbihi
[61] Na nyinyi mniabudu Mimi peke yangu, kwani kuniabudu Mimi tu ndiyo Njia kuu katika kusimamisha Dini sawa.
- 36:62٦٢
Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri? [62]
Tanbihi
[62] Na Shetani amewapotoa viumbe wengi kati yenu. Nyinyi mmeghafilika na hayo. Basi hamkuwa mkifikiri mlipo mt'ii yeye?
- 36:63٦٣
Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa. [63]
Tanbihi
[63] Wataambiwa: Hii ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa mlipo kuwa duniani. Ndiyo jaza ya ukafiri wenu.
- 36:64٦٤
Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru. [64]
Tanbihi
[64] Ingieni! Na hilikini kwa joto lake hii leo kwa ukafiri wenu!
- 36:65٦٥
Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma. [65]
Tanbihi
[65] Leo vitazibwa vinywa vyao, basi havito tamka kitu. Mikono yao ndiyo itakayo sema nasi, na miguu yao itatamka kwa kutoa ushahidi juu yao kwa waliyo kuwa wakiyafanya.
- 36:66٦٦
Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje? [66]
Tanbihi
[66] Na tungeli taka kuwatia upofu duniani tungeli watia upofu, wakawa wanaipapasa njia ya kupita wasiweze kuiona. Wataionaje nasi tumewapofoa!
- 36:67٦٧
Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi. [67]
Tanbihi
[67] Na lau tungeli taka kuzigeuza sura zao tungeli zigeuza zikawa mbaya, juu ya kuwa wana nguvu na vyeo. Hata wasinge weza kwenda mbele wala kurudi nyuma, kwa kuwa inge kuwa tumevunja nguvu zao.
- 36:68٦٨
Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii? [68]
Tanbihi
[68] Na tunaye mfanyia umri wake ukawa mrefu, tunamrudisha, kutoka nguvu akawa dhaifu. Basi je hawayazingatii haya wakayatia akilini ya uweza wetu kuyafanya haya, na wao wakajua kuwa dunia ni nyumba ya kupita ina mwisho wake, na kuwa Akhera ndiyo nyumba ya kubaki na kudumu? Na tunaye mfanyia umri wake uwe mrefu tunamrejesha awe kinyume na alivyo kuwa. Yaani baada ya kuwa na nguvu anakuwa dhaifu. Hayo ni kwa kuwa maisha ya mwanaadamu yanapitia vipindi vitatu, kukua, kutimia kukua; na ukongwe unaanza kwa kunywea kwa mafigo, ini, Ghudda Ddarqiya au Thyroid gland, na Pancreas, yaani Dongoronya. Na haya huleta athari katika kudhoofika mwili wote. Mishipa ya damu nayo huanza kukacha na kunywea, na kwa hivyo hupunguka damu inayo kwenda katika viungo vyote vya mwili, basi ndio huzidi udhaifu juu ya udhaifu. Na katika sababu za kukonga ni kuzidi nguvu za kubomoka kuliko kujengeka katika mwili, yaani Metabolism. Na hayo ni kwa kuwa Khalaya au Cells, za mwili zote zimo katika hali ya kugeuka, na pia Khalaya za damu, isipo kuwa Khalaya za ubongo wa kichwani na wa katika mifupa. Hizo hazigeuki muda wote wa uhai. Ikiwa kiasi ya kuundika upya ni sawa ya kiasi cha kuharibika, basi hapana madhara yanayo tokea. Lakini ikiwa kuharibika ni kukubwa kuliko kujengeka katika kiungo chochote basi hapo hudhihiri madhara kwenye kiungo hicho. Na kwa hivyo kila umri ukiwa mkubwa kiasi cha kujengeka kinapungua na kinazidi kiasi cha kubomoka kwa Khalaya, na kunadhihiri kunywea, na kupungua nguvu kote. Na hukhitalifiana kiasi cha kujengeka kwa mnasaba wa kubomoka kwa kukhitalifiana namna ya mfumo (Nasiij, Texture). Katika hayo yanayo dhihiri kama ngozi iliyo funika mwili, na zilio funika paipu za kusaga chakula, na paipu za Ghudad, Glands, zinachakaa kwa upesi zaidi kila miaka ya binaadamu ikipita. Na hii ni sababu ya kuonekana upesi alama za kuzeeka.
- 36:69٦٩
Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha. [69]
Tanbihi
[69] Na Sisi hatukumfunza Mtume kutunga mashairi. Wala haifai hivyo, kwa kuzingatia pahala pake na cheo chake awe mtungaji mashairi! Hii Qur'ani iliyo teremka juu yake si chochote ila ni mawaidha, na Kitabu cha mbinguni kilio wazi. Hakikhusiani kabisa na mashairi.
- 36:70٧٠
Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri. [70]
Tanbihi
[70] Hii Qur'ani ni kumtia khofu mwenye moyo ulio hai ulio nawirika kwa akili. Na ipite hukumu ya adhabu kuwashukia wanao ipinga Qur'ani, wenye kukataa uwongofu wake.
- 36:71٧١
Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki. [71]
Tanbihi
[71] Je! Makafiri wameingiwa na upofu hata hawaoni kwamba Sisi tumewaumbia kutokana na iliyo fanya kudra yetu nyama hoa, wanyama wa mifugo, na wao wamekuwa wanawamiliki, wanawatumilia kama wapendavyo? Ngamia, kondoo, mbuzi na ng'ombe.
- 36:72٧٢
Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala. [72]
Tanbihi
[72] Na hao wanyama tumewafanya wawatumikie. Wengine basi wanawapanda, na wengine wanawala.
- 36:73٧٣
Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru? [73]
Tanbihi
[73] Na wanapata kwa hao vitu vya kuwapa manufaa, kama sufi, na manyoya, na nywele, na ngozi, na mafupa, na vinywaji kutokana na maziwa yao. Je! Wanasahau neema hizi hata wamekuwa hawamshukuru aliye waneemesha?
- 36:74٧٤
Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa! [74]
Tanbihi
[74] Na washirikina wamefanya miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu wakiwaabudu kwa kutaraji kuwa ati watawasaidia.
- 36:75٧٥
Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa. [75]
Tanbihi
[75] Hiyo miungu ya uwongo haiwezi kuwasaidia kwa lolote Mwenyezi Mungu akiwatakia madhara. Kwani miungu hiyo haiwezi kunafiisha wala kudhuru. Bali wao kwa hiyo miungu isiyo weza kitu, ni kama askari walio tayarishwa kwa ajili ya kuwakhudumia na wa kuwalinda na madhara.
- 36:76٧٦
Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza. [76]
Tanbihi
[76] Basi yasikuhuzunishe maneno yao kumkhusu Mwenyezi Mungu kwa kumkufuru, na kukukhusu wewe kwa kukwambia mwongo. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Nasi tutawalipa kwa hayo.
- 36:77٧٧
Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri! [77]
Tanbihi
[77] Je! Binaadamu anakataa kuwepo Mwenyezi Mungu na uweza wake, na haoni yeye kwamba Sisi, baada ya kuwa hata hayupo, tulimuumba kutokana na tone la manii dhalili? Na sasa amekuwa mkali wa kutukhasimu kwa uwazi kabisa?
- 36:78٧٨
Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika? [78]
Tanbihi
[78] Tena huyu mpingaji aliye dhaahiri ametupigia mfano ambao kwao anakanya uweza wetu kufufua mafupa baada ya kuoza na kusagika. Na amesahau kuwa Sisi tulimuumba yeye, naye hata hakuwepo aslani. Akasema kwa kukanya na kuona haliwezi kuwa hilo: Ni nani huyo atakaye yafufua mafupa nayo yamekwisha mung'unyika?
- 36:79٧٩
Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba. [79]
Tanbihi
[79] Ewe Muhammad! Sema: Atayafufua yule yule aliye yaumba hapo mara ya kwanza. Kwani aliye anza anao uweza wa kufanya tena. Naye ni Mkubwa wa kujua kila alicho kiumba. Basi haemewi Yeye na kukusanya vipande vipande baada ya kutawanyika.
- 36:80٨٠
Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha. [80]
Tanbihi
[80] Aliye kuumbieni moto kutoka mti mbichi, baada ya kwisha kauka. Nguvu za jua zinaingia ndani ya mimea kwa wasita wa mwangaza. Khalaya zenye madda ya kijani katika mimea Chlorophyl ndizo zinafyonza Carbon dioxide kutokana na hewa, na hii huchanganyika na maji yanayo fonzwa na mimea, na kufanyika Carbohydrates kwa kuathiriwa na nguvu zinazo tokana na mwangaza wa jua. Tena hufanyika mbao, kuni, ambazo sehemu kubwa ni muundo wa kimyaa wa Carbon na Hydrogen na Oxygen. Na kutokana na kuni hizi hufanyika makaa haya ya miti tuyatumiayo. Ukiyachoma makaa hutoka nguvu zilizo kuwamo ndani yake kwa ajili ya kupikia, na kwa kazi nyingi nyenginezo. Na makaa ya mawe si chochote ila ni hiyo hiyo mimea na miti iliyo kuwa na kufanyika kama ilivyo elezwa, na kisha ikazikika kwa njia fulani na kugeuka baada ya kupita mamilioni ya miaka kuwa makaa ya mawe, kwa kuathirika na hali za geology kama joto au mdidimizo au menginewe. Na yapasa kuzingatia kuwa kutajwa katika Aya hii "mti wa kijani" si bure, bali ni ishara ya hiyo Chlorophyll ya kijani ambayo ni lazima kwa ajili ya kuimeza Carbon dioxide katika mimea.
- 36:81٨١
Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi. [81]
Tanbihi
[81] Kwani hao wamepotelewa na akili zao hata hawajui kwamba aliye ziumba mbingu na ardhi, juu ya ukubwa wao, ni Muweza vile vile kurejesha kuwaumba wanaadamu ambao ni wadogo na hali yao ni dhaifu? Kwani? Yeye ni Muweza sana, na Yeye ni Mwingi wa kuumba, ambaye ujuzi wake umeenea kila kitu.
- 36:82٨٢
Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa. [82]
Tanbihi
[82] Hakika shani yake katika kuumba anapo taka kiwe kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Kikawa, na hutokea hapo hapo!
- 36:83٨٣
Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa. [83]
Tanbihi
[83] Basi Mtukufu ametakasika na kila kisicho laiki na dhati yake, yule ambaye katika kudra yake upo Ufalme wa kila kitu, kwa kuumba, na kupanga, na kuendesha - Kwake Yeye peke yake mtarejeshwa, akuhisabuni kwa a'mali zenu.
Sura As-Saaffaat
سُورَةُ الصافات- 37:1١
Naapa kwa wanao jipanga kwa safu. [1]
Tanbihi
[1] Naapa kwa mataifa katika viumbe vyangu, walio jipanga wenyewe kwa safu zilio sawa katika msimamo wa ibada na ut'iifu.
- 37:2٢
Na kwa wenye kukataza mabaya. [2]
Tanbihi
[2] Na kwa wanao zuia wanao pindukia mipaka kwa mzuio mkali, nidhamu ibakie, na ulimwengu uhifadhiwe.
- 37:3٣
Na kwa wenye kusoma Ukumbusho. [3]
Tanbihi
[3] Na kwa wenye kusoma Aya, na wanamdhukuru Mwenyezi Mungu kwa dhikri ya Tasbihi, Kumtakasa, na Kumhimidi, kumsifu.
- 37:4٤
Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. [4]
Tanbihi
[4] Hakika Mungu wenu anaye faa kuabudiwa bila ya shaka ni Mmoja tu. Hana mshirika wake, kwa dhati, wala kitendo, wala sifa.
- 37:5٥
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote. [5]
Tanbihi
[5] Yeye - peke yake - ndiye Muumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao, na ndiye Mwenye kupanga mambo, na ndiye Mwenye kutawala mashariki za kila chenye mashariki. Mwenyezi Mungu ndiye Muumba mbingu saba na viliomo baina yao, navyo ni hivyo vyombo vya mbinguni na nyota zake. Naye ndiye Mwenye kusimamisha, Mwenye kulinda vile vile juu ya mwahali zinapo chomozea jua na nyota zote. Na Yeye ndiye anaye vionyesha hivyo kila siku katika pahala huko upeo wa macho, kila siku pahala mbali na vilipo dhihiri siku iliyo tangulia. Na hayo ni kwa mwendo wa mpango wa jua maalumu kwa inavyo zunguka dunia juu ya msumari-kati wake kutoka magharibi kwendea mashariki kila siku na wakati huo huo inavyo lizunguka jua katika njia yake katika falaki. Na jua na nyota huonekana na wakaazi wa ardhi kila siku kama zinachomoza mwahala mbali mbali. Na kila ardhi ikigeuza mahala pake katika safari yake katika mbingu linaonekana jua linachomoza pahala pengine. Ukiliangalia jua kwa utulivu kuanzia mwishoni wa mwezi wa Machi, yaani linapo kuwa jua lipo kati ya mstari wa Ikweta mwanzo wa musimu wa Rabii, yaani Spring, kwa nusu ya kaskazini ya dunia, utaliona linachomoza pahala katika mashariki juu ya upeo wa macho. Kwa mwenye kupeleleza kila siku ikipita ataona kuchomoza kwake kunajongelea kaskazini. Na mwishoni mwa mwezi wa Juni utaona linachomozea mwisho wa kukaribia kaskazini. Kisha baada ya hapo utaliona jua linarejea linafuata kugeuka kule kule mpaka mwisho wa Septemba (wakati wa kuwa sawa wakati wa Khariif yaani Autumn) utaliona jua linachomoza pale pale lilipo chomoza mwanzo wa Machi. Kisha litaendelea kuelekea kusini kuchomoza kwake mpaka mwisho wa Desemba linakuwa linachomoza karibu kabisa na kusini. Baada ya hapo huanza tena kurejea kuelekea kaskazini mpaka limalize safari yake ya kufika kati sawa katika Rabii ya pili. Na safari hii yote inachukua siku 365 na robo siku. Na inaonekana kuwa nyota nazo zinachomoza mwahala mbali mbali katika upeo wa macho inapo kuwa dunia imo katika safari yake ya mbinguni, na khasa nyota za buruji (au vituo) 12 vinavyo pitiwa na jua katika mwendo wake wa mwaka.
- 37:6٦
Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota. [6]
Tanbihi
[6] Sisi tumeipamba hii mbingu ya karibu na watu wa duniani kwa mapambo, nayo ni hizo nyota zinazong'ara, zenye ukubwa mbali mbali, na mwahala pao mbali mbali kwenye anga la ulimwengu kama ionekanavyo kwa macho.
- 37:7٧
Na kulinda na kila shet'ani a'si. [7]
Tanbihi
[7] Na tukaihifadhi hiyo mbingu na kila shetani jabari aliye a'si.
- 37:8٨
Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande. [8]
Tanbihi
[8] Hao majabari wa kishetani hawawezi kusikiliza yanayo pita katika ulimwengu wa Malaika. Na wao hupopolewa kwa kila kinacho faa cha kuwazuia.
- 37:9٩
Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. [9]
Tanbihi
[9] Hufukuzwa hao kwa nguvu wasifikilie kuweza kusikiliza khabari za mbinguni. Na Akhera watapata adhabu kali ya kudumu.
- 37:10١٠
Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng'ara. [10]
Tanbihi
[10] Isipo kuwa anaye lipata neno moja hivi katika khabari za mbinguni kwa kuibia. Na huyo naye tunamwandama kwa mwenge wa moto unao murika anga kwa mwangaza wake, ukamuunguzilia mbali.
- 37:11١١
Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata. [11]
Tanbihi
[11] Ewe Nabii! Hebu waulize hao wanao kanya kufufuliwa wanao ona hayawi hayo: Je! Kwani kuwaumba wao hawa ni kugumu zaidi au kuziumba mbingu, na ardhi, na nyota, na vyenginevyo, tulivyo viumba Sisi?
- 37:12١٢
Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara. [12]
Tanbihi
[12] Hakika Sisi tumewaumba wao kutokana na udongo unao gandana. Basi kwa nini wanaona ajabu kurejezwa tena wao?
- 37:13١٣
Na wanapo kumbushwa hawakumbuki. [13]
Tanbihi
[13] Na wanapo kabiliwa kwa dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kufufua, hata hawazishughulikii wakanufaika kwa hizo dalili.
- 37:14١٤
Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara. [14]
Tanbihi
[14] Na wanapo ona ushahidi wa kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu huitana wapate kupita mipaka katika kumkejeli.
- 37:15١٥
Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri. [15]
Tanbihi
[15] Na makafiri husema juu ya Ishara zinazo onyesha uweza wa Mwenyezi Mungu: Haya tunayo yaona si chochote ila ni uchawi tu.
- 37:16١٦
Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? [16]
Tanbihi
[16] Hivyo sisi tukisha kufa tukawa udongo na mafupa tutatolewa tena makaburini kwetu tuwe wahai?
- 37:17١٧
Hata baba zetu wa zamani? [17]
Tanbihi
[17] Sisi tuwe wahai, na pia watafufuliwa baba zetu wa zamani walio kufa kabla yetu, na wakapotea, na wakateketea?
- 37:18١٨
Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili. [18]
Tanbihi
[18] Ewe Nabii! Waambie: Ndio mtafufuliwa nyote, nanyi ni madhalili na wanyonge.
- 37:19١٩
Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona! [19]
Tanbihi
[19] Kwani hakika kufufuliwa ni Ukelele mmoja tu, mara wote watakuwa wahai wakiyaona waliyo ahidiwa.
- 37:20٢٠
Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. [20]
Tanbihi
[20] Na washirikina watasema: Ee msiba wetu huu! Hii ndiyo Siku ya Hisabu na Malipo kwa a'mali zilio tendwa!
- 37:21٢١
Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha. [21]
Tanbihi
[21] Watajibiwa: Hii ndiyo Siku ya Hukumu na kufarikisha vitendo, mliyo kuwa mkiikadhibisha.
- 37:22٢٢
Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu. [22]
Tanbihi
[22] Enyi Malaika wangu! Wakusanyeni walio jidhulumu nafsi zao kwa kufuru, pamoja na wake zao wa kikafiri, na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, yakiwa masanamu au watu, na waonyesheni njia ya kwendea Motoni waingie humo.
- 37:23٢٣
Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu! [23]
Tanbihi
[23] Enyi Malaika wangu! Wakusanyeni walio jidhulumu nafsi zao kwa kufuru, pamoja na wake zao wa kikafiri, na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, yakiwa masanamu au watu, na waonyesheni njia ya kwendea Motoni waingie humo.
- 37:24٢٤
Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: [24]
Tanbihi
[24] Na wazuieni hapo hapo; kwani wao hakika watahojiwa juu ya imani zao na vitendo vyao.
- 37:25٢٥
Mna nini? Mbona hamsaidiani? [25]
Tanbihi
[25] Enyi washirikina! Mna nini? Mbona hamsaidiani kama mlivyo kuwa mkisaidiana nyinyi kwa nyinyi duniani?
- 37:26٢٦
Bali hii leo, watasalimu amri. [26]
Tanbihi
[26] Leo hii hawasaidiani, bali leo wanaongozwa tu, wamekwisha salimu amri.
- 37:27٢٧
Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. [27]
Tanbihi
[27] Watakuwa wakikabiliana kulaumiana na kusutana, na wakiulizana khabari za mwisho wao muovu.
- 37:28٢٨
Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. [28]
Tanbihi
[28] Wanyonge watawaambia walio jipa ukubwa: Nyinyi mlikuwa mkitujia upande tulio udhania ni wa kheri na mafanikio, ili mtugeuze njia tuache Haki twende kwenye upotovu.
- 37:29٢٩
Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini. [29]
Tanbihi
[29] Watasema walio jipa ukubwa: Sisi hatukukugeuzeni njia, lakini nyinyi wenyewe mliikataa Imani, na mkaipuuza kwa khiari yenu.
- 37:30٣٠
Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. [30]
Tanbihi
[30] Na sisi hatukuwa na madaraka juu yenu hata tuweze kukunyang'anyeni uweza wenu wa kukhiari. Bali nyinyi wenyewe mlikuwa watu mlio iacha Haki.
- 37:31٣١
Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. [31]
Tanbihi
[31] Basi neno la Mola wetu Mlezi limethibiti juu yetu. Hakika hapana shaka sisi tutaionja adhabu ya Siku ya Kiyama.
- 37:32٣٢
Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. [32]
Tanbihi
[32] Tukakuiteni kwenye maasi na upotovu na nyinyi mkaitikia wito wetu. Kazi yetu ni kufanya hila ya kuwaita watu wafuate upotovu tulio nao. Basi hatuna lawama.
- 37:33٣٣
Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja. [33]
Tanbihi
[33] Kwani hakika wafuasi na wenye kufuatwa wote watashiriki pamoja katika adhabu ya Siku ya Kiyama.
- 37:34٣٤
Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu. [34]
Tanbihi
[34] Hakika mfano wa adhabu hiyo Sisi tunawapa wale walio fanya makosa katika Haki ya Mwenyezi Mungu kwa ushirikina na kutenda maasi.
- 37:35٣٥
Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa 'Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna. [35]
Tanbihi
[35] Hakika watu hao walikuwa wakiambiwa: La ilaha illa 'Llah, Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakakataa kukiri kwa kiburi na majivuno.
- 37:36٣٦
Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu? [36]
Tanbihi
[36] Na husema: Sisi tuache kuabudu miungu yetu kwa kufuata kauli ya mtunga mashairi aliye zugwa asiye kuwa na akili?
- 37:37٣٧
Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume. [37]
Tanbihi
[37] Bali Mtume wao amewaletea Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, ambayo ndiyo wito wa Mitume wote, naye akasadikisha kwa hivyo wito wa hao Mitume.
- 37:38٣٨
Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu. [38]
Tanbihi
[38] Enyi washirikina! Hakika nyinyi hapana shaka mtaionja adhabu kali ya Akhera.
- 37:39٣٩
Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya. [39]
Tanbihi
[39] Na hamtapata malipo Akhera ila malipo ya vitendo vyenu vya duniani.
- 37:40٤٠
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. [40]
Tanbihi
[40] Ila waja wangu walio safika; hao hawataionja adhabu kwa sababu wao ni watu wa Imani na ut'iifu.
- 37:41٤١
Hao ndio watakao pata riziki maalumu, [41]
Tanbihi
[41] Hawa watu wa ikhlasi watapata Akhera riziki maalumu kwa Mwenyezi Mungu.
- 37:42٤٢
Matunda, nao watahishimiwa. [42]
Tanbihi
[42] Matunda ya namna mbali mbali. Nao watastareheshwa na kutukuzwa,
- 37:43٤٣
Katika Bustani za neema. [43]
Tanbihi
[43] Katika Bustani zenye neema.
- 37:44٤٤
Wako juu ya viti wamekabiliana. [44]
Tanbihi
[44] Wakikaa humo juu ya viti wakikabiliana.
- 37:45٤٥
Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem. [45]
Tanbihi
[45] Watawazungukia watoto na chombo chenye kinywaji kilicho toka kwenye chemchem zisio katika.
- 37:46٤٦
Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao. [46]
Tanbihi
[46] Kinywaji chenyewe ni cheupe kinapo changanywa, na kitamu kwa wenye kukinywa.
- 37:47٤٧
Hakina madhara, wala hakiwaleweshi. [47]
Tanbihi
[47] Hakiwaumizi kichwa na kuwaletea ghururi, wala kwa kukinywa hicho haiwapotei akili yao kidogo kidogo, yaani hakileweshi.
- 37:48٤٨
Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri. [48]
Tanbihi
[48] Na watu hawa wat'iifu walioko Peponi watakuwa nao mahuruleini walio safi, wema, macho yao hayawatazami ila waume zao tu, basi hawayatafuti matamanio maovu, jicho la mwema haliangalii ila mema.
- 37:49٤٩
Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika. [49]
Tanbihi
[49] Hao wanawake wenye macho ya staha ni kama mayai ya mbuni, yaliyo hifadhiwa na mbawa zake. Basi hayaguswi na mikono, wala hayapati vumbi.
- 37:50٥٠
Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe. [50]
Tanbihi
[50] Hao watu wema watakuwa wakiingia kuulizana hali, na walikuwaje duniani?
- 37:51٥١
Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki. [51]
Tanbihi
[51] Hapo mmoja wao atasema: Mimi nalikuwa na rafiki katika washirikina, akijadiliana nami katika mambo ya Dini na yaliyo kuja katika Qur'ani.
- 37:52٥٢
Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki. [52]
Tanbihi
[52] Akisema: Ati wewe ni katika hao wanao sadiki kuwa kupo kufufuliwa na kuhisabiwa na kulipwa baada ya kufa?
- 37:53٥٣
Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa? [53]
Tanbihi
[53] Ati baada ya kwisha teketea, tukawa udongo na mafupa, tutakuja kuwa hai mara nyengine, tuhisabiwe na tulipwe kwa vitendo tulivyo kwisha vitenda?
- 37:54٥٤
Atasema: Je! Nyie mnawaona? [54]
Tanbihi
[54] Muumini awaambie wenzie alio kaa nao: Enyi watu wa Peponi, mnawaona watu wa Motoni nipate kumwona rafiki yangu?
- 37:55٥٥
Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu. [55]
Tanbihi
[55] Jicho lake lipige duru kuelekea Motoni, na huko amwone sahibu yake wa zamani yuko katikati akiadhibika kwa Moto.
- 37:56٥٦
Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza. [56]
Tanbihi
[56] Akimwona aseme: Wallahi! Ulikaribia kule duniani kunihilikisha lau ningeli kufuata katika ukafiri wako na maasiya yako!
- 37:57٥٧
Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa. [57]
Tanbihi
[57] Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi kwa hidaya yake na kuniwezesha kwake nikamuamini Mwenyezi Mungu na kufufuka, basi ningeli kuwa mfano wako wewe katika walio hudhurishwa katika hiyo adhabu.
- 37:58٥٨
Je! Sisi hatutakufa, [58]
Tanbihi
[58] Je! Sisi tutakaa milele tukineemeka katika Pepo, wala hatufi kabisa isipo kuwa kule kufa kwetu mara ya kwanza duniani, na wala hatuadhibiwi baada ya kwisha ingia Peponi?
- 37:59٥٩
Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. [59]
Tanbihi
[59] Je! Sisi tutakaa milele tukineemeka katika Pepo, wala hatufi kabisa isipo kuwa kule kufa kwetu mara ya kwanza duniani, na wala hatuadhibiwi baada ya kwisha ingia Peponi?
- 37:60٦٠
Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa. [60]
Tanbihi
[60] Hakika haya aliyo tupa Mwenyezi Mungu katika ukarimu wa Peponi bila ya shaka ndiyo kufuzu kukubwa, na kuvuka kukuu na hiyo adhabu tuliyo kuwa tunatahadhari nayo tangu duniani.
- 37:61٦١
Kwa mfano wa haya nawatende watendao. [61]
Tanbihi
[61] Ili wapate ukarimu wa Akhera kama walio bahatika kuupata Waumini, basi nawafanye kazi duniani hao wafanyao kazi, ili wapate kama walio pata wao.
- 37:62٦٢
Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum? [62]
Tanbihi
[62] Je! Hiyo riziki maalumu iliyo andaliwa kwa sababu ya watu wa Peponi ni bora, au mti wa Zaqqum ulio andaliwa kwa ajili ya watu wa Motoni?
- 37:63٦٣
Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu. [63]
Tanbihi
[63] Hakika Sisi tumeujaalia mti huu uwe ni mtihani na adhabu ya Akhera kwa ajili ya washirikina.
- 37:64٦٤
Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu. [64]
Tanbihi
[64] Hakika huo ni mti ulioko katikati ya Jahannamu, umekulia huko Motoni, na umeumbwa kutokana na huko huko.
- 37:65٦٥
Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet'ani. [65]
Tanbihi
[65] Matunda yake mabaya kuyatazama, yana sura ya kukirihisha, macho hayapendi kuyatazama, kama vichwa vya mashetani ambavyo kwa hakika watu hawajaviona, lakini mtu humpitikia tu katika dhana jinsi ya ubaya wake.
- 37:66٦٦
Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo. [66]
Tanbihi
[66] Na wao watakuwa wanakula matunda ya mti huo, na wajaze matumbo yao kwayo. Kwani hawanacho kinginecho cha kukila.
- 37:67٦٧
Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka. [67]
Tanbihi
[67] Kisha washirikina hao juu ya kula mti wa Zaqqum watapewa maji yaliyo changanywa, yamoto, ya kuwababua nyuso zao, na kukatakata matumbo yao.
- 37:68٦٨
Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu. [68]
Tanbihi
[68] Tena mwisho wao ni Motoni. Wao watakuwa katika adhabu ya milele. Wataletwa kutoka Motoni waje kula mti wa Zaqqum kisha wanyweshe kinywaji hicho, na tena warejeshwe mahala pao katika Jahannamu.
- 37:69٦٩
Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. [69]
Tanbihi
[69] Wao waliwakuta baba zao wamepotoka, na wao wakafanya haraka kufuata zile zile nyayo za baba zao. Wakawa mbioni kwendea njia yao, wakifuata tu wala hawachungui, kama walio timuliwa na wakihimizwa wende mbio mbio kuwafuata hao baba zao bila ya kupima wala kuzingatia.
- 37:70٧٠
Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao. [70]
Tanbihi
[70] Wao waliwakuta baba zao wamepotoka, na wao wakafanya haraka kufuata zile zile nyayo za baba zao. Wakawa mbioni kwendea njia yao, wakifuata tu wala hawachungui, kama walio timuliwa na wakihimizwa wende mbio mbio kuwafuata hao baba zao bila ya kupima wala kuzingatia.
- 37:71٧١
Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao. [71]
Tanbihi
[71] Na hakika walipotea njia ya sawa na njia ya Imani wengi katika mataifa yaliyo kwisha tangulia kabla ya hawa washirikina wa Makka.
- 37:72٧٢
Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji. [72]
Tanbihi
[72] Na bila ya shaka Sisi tuliyatumia Mitume hayo mataifa yaliyo tangulia ili wawaonye na wawahadharishe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, nao wakawakadhibisha.
- 37:73٧٣
Basi hebu angalia ulikuje mwisho wa walioonywa. [73]
Tanbihi
[73] Basi angalia, ewe uliye jaaliwa kuangalia, ulikuwaje mwisho wa walio onywa na Mitume? Bila ya shaka waliteketezwa, wakawa ni mazingatio kwa watu.
- 37:74٧٤
Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliokhitariwa. [74]
Tanbihi
[74] Lakini walikuwapo Waumini ambao aliwakhitari Mwenyezi Mungu wamuabudu Yeye, ili wapate fadhila za ukarimu wake. Basi hao walizipata thawabu zake, na wakaepukana na adhabu yake.
- 37:75٧٥
Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji. [75]
Tanbihi
[75] Na hakika Nuhu alitwita alipo kwisha kata tamaa na watu wake, basi na Sisi tukawa ni wabora wa kuitikia wito wake, tulipo muitikia ombi lake, na tukawaangamiza watu wake kwa tofani.
- 37:76٧٦
Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa. [76]
Tanbihi
[76] Na tukamwokoa Nuhu na walio amini pamoja naye, wasizame na kuteketea kwa tofani.
- 37:77٧٧
Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia. [77]
Tanbihi
[77] Tukawajaalia vizazi vya Nuhu ndio walio bakia katika ardhi baada ya kuteketea watu wake.
- 37:78٧٨
Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye. [78]
Tanbihi
[78] Na tukamwachilia Nuhu kutajwa kwa wema na watu walio kuja baada yake wakimdhukuru mpaka Siku ya Kiyama.
- 37:79٧٩
Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote! [79]
Tanbihi
[79] Maamkio ya Salama na Amani kumuamkia Nuhu kutokana na Malaika, na watu, na majini.
- 37:80٨٠
Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. [80]
Tanbihi
[80] Hakika Sisi huwalipa walio tenda mema mfano wa haya. Basi aliingia katika Jihadi kulinyanyua Neno letu, na akavumilia maudhi kwa ajili yetu.
- 37:81٨١
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. [81]
Tanbihi
[81] Hakika yeye ni miongoni mwa waja wetu walio tuamini, na wakatimiza ahadi yetu, na wakaufikisha Ujumbe wetu.
- 37:82٨٢
Kisha tukawazamisha wale wengine. [82]
Tanbihi
[82] Kisha tukawazamisha wenginewe katika makafiri wa kaumu yake.
- 37:83٨٣
Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake, [83]
Tanbihi
[83] Na hakika bila ya shaka Ibrahim alikuwa akifuata ile ile njia yake na mwenendo wake katika kuitia Tawhidi, Imani
- 37:84٨٤
Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima. [84]
Tanbihi
[84] Alipo mkabili Mola wake Mlezi kwa moyo ulio kuwa nadhifu hauna ushirikina, umemsafia ibada Yeye tu.
- 37:85٨٥
Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini? [85]
Tanbihi
[85] Alipo chukia kuwa baba yake na watu wake wanaabudu masanamu, akawaambia: Ni nini haya masanamu mnayo yaabudu?
- 37:86٨٦
Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu? [86]
Tanbihi
[86] Si mnazua uwongo tu ulio wazi kwa haya myatendayo, kwa kuwa mnamuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Na si mnataka kuzua uzushi huu bila ya udhuru wowote ila kupenda kwenu tu?
- 37:87٨٧
Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote? [87]
Tanbihi
[87] Mnamdhania nini huyo ambaye ndiye Mwenye haki ya kuabudiwa kwa kuwa Yeye ndiye Muumba walimwengu wote, mtapo kutana naye na hali nyinyi mmemfanyia washirika wenginewe katika ibada?
- 37:88٨٨
Kisha akapiga jicho kutazama nyota. [88]
Tanbihi
[88] Basi akazitupia jicho nyota kuzitazama ili apate kuona dalili ya Muumba ulimwengu. Akaziona zinageuka, zinabadilika
- 37:89٨٩
Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa! [89]
Tanbihi
[89] Akajikhofia nafsi yake asiwe ana upotovu na maradhi ya itikadi.
- 37:90٩٠
Nao wakamwacha, wakampa kisogo. [90]
Tanbihi
[90] Watu wake wakamwachilia mbali, na wakapuuza maneno yake.
- 37:91٩١
Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli? [91]
Tanbihi
[91] Akayaendea kwa haraka yale masanamu kwa kificho, na akayapa chakula ambacho wale washirikina walikiweka mbele yao ili nao wapate baraka yao kwa mujibu wa madai yao. Akasema kwa maskhara na kejeli: Mbona hamli?
- 37:92٩٢
Mna nini hata hamsemi? [92]
Tanbihi
[92] Mna nini hata mmeshindwa kusema lolote, hata ndio au sio?
- 37:93٩٣
Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia. [93]
Tanbihi
[93] Akayaingilia yale masanamu kuyapiga kwa mkono wa kulia, kwa kuwa ndio wenye nguvu, akayabomoa.
- 37:94٩٤
Basi wakamjia upesi upesi. [94]
Tanbihi
[94] Walipo baini kwamba kuvunjwa miungu yao ni kwa kitendo cha Ibrahim, basi walimkimbilia ili wamtese kwa alivyo watendea miungu yao.
- 37:95٩٥
Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe [95]
Tanbihi
[95] Ibrahim akawaambia kwa kuwahizi: Hivyo nyinyi mnaabudu mawe mliyo yachonga nyinyi wenyewe kwa mikono yenu? Akili zenu zimekwenda wapi?
- 37:96٩٦
Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya! [96]
Tanbihi
[96] Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, na akayaumba hata hayo masanamu mnayo yaunda kwa mikono yenu. Basi Yeye peke yake ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.
- 37:97٩٧
Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo! [97]
Tanbihi
[97] Hoja ilipo wapata wale wanao abudu masanamu, wakaona hawana ila waingie kutumia nguvu; wakaazimia kumchoma moto. Basi waliambizana: Mjengeeni jengo, na mlijaze moto, na mtupeni katikati yake!
- 37:98٩٨
Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini. [98]
Tanbihi
[98] Kwa haya walikusudia kumteketeza, lakini Mwenyezi Mungu alimwokoa na ule moto baada ya wao kwisha mtumbukiza humo. Hadhi yake ikawa juu kwa utukufu ule, na Mwenyezi Mungu akawafanya wao ndio watu wa chini.
- 37:99٩٩
Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa. [99]
Tanbihi
[99] Ibrahim alipo kata tamaa nao, kuwa hawaamini tena, alisema: Mimi ninahama kwendea pahala alipo niamrisha Mola wangu Mlezi nende. Mola wangu Mlezi atanihidi aniongoze mpaka nifike pahala pa utulivu, penye amani, na nchi nzuri.
- 37:100١٠٠
Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema. [100]
Tanbihi
[100] Ewe Mola wangu Mlezi! Nipe dhuriya walio wema wa vitendo, wasimamie hii kazi ya wito kuwaitia watu kwako Wewe, baada yangu.
- 37:101١٠١
Basi tukambashiria mwana aliye mpole. [101]
Tanbihi
[101] Malaika wakampa bishara ya kwamba atapata mwana atakaye pambwa kwa akili na upole.
- 37:102١٠٢
Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri. [102]
Tanbihi
[102] Akazaliwa huyo mwana, na alipo kuwa kijana wa kwenda naye baba yake katika kutafuta haja za maisha, Ibrahim alipewa mtihani kwa ndoto aliyo iota. Ibrahim akasema: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini ufunuo kutokana na Mwenyezi Mungu ananitaka nikuchinje! Basi wewe tazama unaonaje? Yule mwana mwema alisema: Ewe baba yangu! Tekeleza amri ya Mola wako Mlezi. Utaniona mimi katika wanao subiri, Inshallah!
- 37:103١٠٣
Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji. [103]
Tanbihi
[103] Yule baba na mwanawe walipo iridhia hukumu ya Mwenyezi Mungu, na akamweka juu ya fungu la mchanga na akamlaza juu yake, kipaji chake kikawa juu ya ardhi, akawa tayari kumchinja.
- 37:104١٠٤
Tulimwita: Ewe Ibrahim!. [104]
Tanbihi
[104] Na Mwenyezi Mungu akajua umadhubuti wa Ibrahim na mwanawe katika majaribio, Mwenyezi Mungu alimwita Ibrahim kwa wito wa kirafiki: Ewe Ibrahim! Hakika umeuitikia kwa utulivu huo ufunuo wa ndoto, na wala hukusitasita katika kufuata amri. Basi haya yanakutosha. Sisi tunakupunguzia haya majaribio yetu kuwa ni malipo kwa wema wako, kama tunavyo walipa walio wema kwa wema wao.
- 37:105١٠٥
Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema. [105]
Tanbihi
[105] Na Mwenyezi Mungu akajua umadhubuti wa Ibrahim na mwanawe katika majaribio, Mwenyezi Mungu alimwita Ibrahim kwa wito wa kirafiki: Ewe Ibrahim! Hakika umeuitikia kwa utulivu huo ufunuo wa ndoto, na wala hukusitasita katika kufuata amri. Basi haya yanakutosha. Sisi tunakupunguzia haya majaribio yetu kuwa ni malipo kwa wema wako, kama tunavyo walipa walio wema kwa wema wao.
- 37:106١٠٦
Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri. [106]
Tanbihi
[106] Hakika majaribio haya tuliyo mjaribia Ibrahim na mwanawe bila ya shaka ni majaribio yaliyo dhihirisha undani wa Imani yao na yakini yao kwa Mola Mlezi wa walimwengu.
- 37:107١٠٧
Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. [107]
Tanbihi
[107] Na tukamkomboa kwa mhanga wenye cheo kikubwa, kwa kuwa hayo ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
- 37:108١٠٨
Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye. [108]
Tanbihi
[108] Na tukaacha atajike kwa sifa nzuri katika ndimi za walio kuja baada yake.
- 37:109١٠٩
Iwe salama kwa Ibrahim!. [109]
Tanbihi
[109] Maamkio ya amani na salama kwa Ibrahim!
- 37:110١١٠
Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. [110]
Tanbihi
[110] Mfano wa malipo kama haya ya kuwakinga na balaa ndivyo tunavyo walipa walio wema katika kufuata amri za Mwenyezi Mungu.
- 37:111١١١
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. [111]
Tanbihi
[111] Hakika Ibrahim ni katika waja wetu wanao ifuata Haki.
- 37:112١١٢
Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema. [112]
Tanbihi
[112] Na kwa amri yetu, Malaika walimbashiria kuwa ataruzukiwa mwana, Is-haqa juu ya kukata tamaa na kuwa mkewe ni tasa. Na kwamba yeye hakika atakuwa Nabii miongoni mwa walio wema.
- 37:113١١٣
Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi. [113]
Tanbihi
[113] Nasi tukamtunukia yeye na mwanawe baraka na kheri duniani na Akhera. Na miongoni mwa vizazi vyao watatokea watakao jifanyia wema nafsi zao kwa Imani na ut'iifu, na watakao jidhulumu kwa upotovu wa ukafiri na maasi.
- 37:114١١٤
Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni. [114]
Tanbihi
[114] Na bila ya shaka tuliwaneemesha Musa na Haruni kwa kuwapa Unabii na neema kubwa kubwa.
- 37:115١١٥
Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa. [115]
Tanbihi
[115] Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa iliyo kuwa iwashukie kutokana na Firauni na kaumu yake.
- 37:116١١٦
Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda. [116]
Tanbihi
[116] Na Sisi tukawanusuru na adui zao, wakawa wao ndio wenye kushinda.
- 37:117١١٧
Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha. [117]
Tanbihi
[117] Na tukampa Musa na Haruni Kitabu kilicho wazi chenye kubainisha hukumu za Dini, nacho ni Taurati.
- 37:118١١٨
Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. [118]
Tanbihi
[118] Na tukawaongoza waifuate Njia iliyo sawa.
- 37:119١١٩
Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. [119]
Tanbihi
[119] Na tukabakisha sifa njema za kutajika wote wawili hao kwa watu wengineo walio kuja baada yao.
- 37:120١٢٠
Iwe salama kwa Musa na Haruni!. [120]
Tanbihi
[120] Maamkio ya Amani na Salama kwa Musa na Haruni.
- 37:121١٢١
Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. [121]
Tanbihi
[121] Hakika mfano wa malipo tuliyo mjazi Musa na Haruni ndivyo tunavyo wajazi wote walio wema.
- 37:122١٢٢
Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini. [122]
Tanbihi
[122] Hakika wawili hao ni katika waja wetu wenye kuifuata Haki.
- 37:123١٢٣
Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume. [123]
Tanbihi
[123] Na hakika Ilyas ni katika hao tulio watuma kwenda waongoa watu wao.
- 37:124١٢٤
Alipo waambia watu wake: Hamwogopi?. [124]
Tanbihi
[124] Ilyas alipo waambia watu wake, nao walikuwa wakiyaabudu masanamu yao: Je! Mnaendelea juu ya makosa yenu, na wala hamumkhofu Mwenyezi Mungu mkajikinga na adhabu yake?
- 37:125١٢٥
Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji,. [125]
Tanbihi
[125] Mnaliabudu sanamu linalo itwa Baa'li, na mkaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu aliye uumba ulimwengu na akaufanya mzuri uumbaji wake?
- 37:126١٢٦
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani?. [126]
Tanbihi
[126] Mwenyezi Mungu amekuumbeni na amekuhifadhini nyinyi na baba zenu wa zamani. Yeye basi ndiye Mwenye haki ya kuabudiwa.
- 37:127١٢٧
Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa;. [127]
Tanbihi
[127] Lakini walimkadhibisha, basi jaza yao ni kuhudhurishwa kwenye Moto Siku ya Kiyama.
- 37:128١٢٨
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. [128]
Tanbihi
[128] Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safisha Imani yao. Hao basi ndio wenye kufuzu.
- 37:129١٢٩
Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye. [129]
Tanbihi
[129] Na tukamjaalia awe anatajwa kwa wema na ndimi za walio kuja baada yake.
- 37:130١٣٠
Iwe salama kwa Ilyas. [130]
Tanbihi
[130] Salamu juu ya Ilyasi, au juu yake yeye na watu wake, kwa kuwa kawashinda.
- 37:131١٣١
Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. [131]
Tanbihi
[131] Hakika mfano wa malipo tuliyo mlipa Ilyas tunamlipa kila aliye mwema kwa sababu ya wema wake.
- 37:132١٣٢
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. [132]
Tanbihi
[132] Hakika Ilyas ni katika waja wetu walio amini.
- 37:133١٣٣
Na hakika Lut'i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume. [133]
Tanbihi
[133] Na hakika Lut'i ni katika Mitume tulio watuma ili afikishe Ujumbe wetu kwa watu.
- 37:134١٣٤
Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote,. [134]
Tanbihi
[134] Kwa hakika Sisi tumemwokoa yeye na ahali zake wote kutokana na adhabu iliyo wasibu watu wake.
- 37:135١٣٥
Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma. [135]
Tanbihi
[135] Ila mkewe mkongwe. Yeye bila ya shaka aliteketea pamoja na walio teketea.
- 37:136١٣٦
Kisha tukawaangamiza wale wengineo. [136]
Tanbihi
[136] Kisha tukawaangamiza wote isipo kuwa Lut'i na walio muamini.
- 37:137١٣٧
Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi,. [137]
Tanbihi
[137] Na hakika nyinyi, watu wa Makka, mnayapitia majumba ya hao kaumu Lut'i katika safari zenu za kwendea Sham asubuhi au usiku. Je! Mmepotelewa na akili zenu hata hamwezi kuzingatia yaliyo wapitia hao kuwa ni malipo ya ukanushaji wao?
- 37:138١٣٨
Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini?. [138]
Tanbihi
[138] Na hakika nyinyi, watu wa Makka, mnayapitia majumba ya hao kaumu Lut'i katika safari zenu za kwendea Sham asubuhi au usiku. Je! Mmepotelewa na akili zenu hata hamwezi kuzingatia yaliyo wapitia hao kuwa ni malipo ya ukanushaji wao?
- 37:139١٣٩
Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. [139]
Tanbihi
[139] Na hakika Yunus ni miongoni mwa tulio watuma wawafikishie Ujumbe wetu watu.
- 37:140١٤٠
Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. [140]
Tanbihi
[140] Alipo wahama watu wake bila ya amri ya Mola wake Mlezi, akaliendea jahazi ambalo lilio kwisha sheheni pomoni, akalipanda. Jahazi likapatikana na mambo ikawajibikia lazima mmoja katika abiria atoswe kupunguza shehena yake. Kura ikamuangukia Yunus, akashindwa kwa kura. Akatoswa baharini kwa mujibu wa ada yao zama zile.
- 37:141١٤١
Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. [141]
Tanbihi
[141] Alipo wahama watu wake bila ya amri ya Mola wake Mlezi, akaliendea jahazi ambalo lilio kwisha sheheni pomoni, akalipanda. Jahazi likapatikana na mambo ikawajibikia lazima mmoja katika abiria atoswe kupunguza shehena yake. Kura ikamuangukia Yunus, akashindwa kwa kura. Akatoswa baharini kwa mujibu wa ada yao zama zile.
- 37:142١٤٢
Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. [142]
Tanbihi
[142] Samaki akammeza, naye hakika alistahiki lawama kwa kuikimbia kazi yake ya Daa'wa, Wito, kuwaitia watu wafuate Haki, na kuacha kuwasubiria wale walio kwenda kinyume naye..
- 37:143١٤٣
Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu,. [143]
Tanbihi
[143] Na lau kuwa Yunus hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, wanao dumu kumdhukuru, angeli kufa ndani ya samaki, wala asingeli toka humo mpaka siku ya kufufuliwa.
- 37:144١٤٤
Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa. [144]
Tanbihi
[144] Na lau kuwa Yunus hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, wanao dumu kumdhukuru, angeli kufa ndani ya samaki, wala asingeli toka humo mpaka siku ya kufufuliwa.
- 37:145١٤٥
Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa. [145]
Tanbihi
[145] Tukamtupa pahali patupu kwenye nchi pasipo kuwa na miti wala majumba, naye ni mgonjwa kwa yaliyo mpata. Yaliyo mtokea Sayyidna Yunus a.s. ni muujiza. Lakini nayo si muhali kutokea mtu kumezwa na samaki, na akabakia yuhai ndani yake kwa muda fulani. Mawili yaweza kuwa - Kwanza, ni kuwa huyo samaki ni namna asiye kuwa na meno katika kabila ya nyangumi wakubwa kabisa, kama nyangumi wanao onekana sana katika Bahari ya Kati (Mediterranean). Urefu wake huweza kufika Mita 20. Alibaki Yunus katika mpandikizi wa kinywa chake huyo nyangumi mpaka alipo mtema kwenye ufukwe mtupu, kwani koo ya nyangumi ni nyembamba hawezi kupita mtu. Pili, yaweza kuwa huyo samaki ni namna ya wenye meno pia, kama nyangumi wa ambari, na ambaye pia urefu wake hufika mita 20. Hawa mara kadhaa wa kadhaa huonekana katika Bahari ya Kati. Nyangumi hao yawezekana kwa kawaida kuwameza wanyama wakubwa wanao pita urefu wa mita tatu.
- 37:146١٤٦
Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung'unye. [146]
Tanbihi
[146] Tukauotesha mmea wa kutambaa, usio simama juu ya kigogo, ukamfunika na kumkinga na madhara ya hali ya hewa.
- 37:147١٤٧
Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi. [147]
Tanbihi
[147] Hata alipo pata nafuu kutokana na yaliyo msibu, tukamtuma awaendee watu wengi. Wanasema walio waona kuwa wanapata laki moja au zaidi.
- 37:148١٤٨
Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda. [148]
Tanbihi
[148] Wakauwitikia wito wake, nasi tukawakunjulia neema zetu kwa muda maalumu.
- 37:149١٤٩
Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume?. [149]
Tanbihi
[149] Ewe Nabii! Waulize watu wako: Ati Mwenyezi Mungu aliye kuumba ana watoto wa kike kinyume na wao; na wao ndio wana watoto wanaume kinyuma na Yeye?
- 37:150١٥٠
Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia?. [150]
Tanbihi
[150] Ati tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao hao makafiri waliona kwa macho yao kuumba kwao, na ndio wakasimulia walio yaona?
- 37:151١٥١
Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema:. [151]
Tanbihi
[151] Ewe mwenye kusikia! Yazingatie maneno yao. Hakika wao kwa uwongo wao wanasema: Mwenyezi Mungu amezaa! Na hali Yeye ametakasika na upungufu kama huo wa kuwa mzazi au kuzaliwa. Na hakika bila ya shaka hao ni waongo kwa usemi huo, kwa ushahidi wa dalili nyingi za Upweke wake.
- 37:152١٥٢
Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo!. [152]
Tanbihi
[152] Ewe mwenye kusikia! Yazingatie maneno yao. Hakika wao kwa uwongo wao wanasema: Mwenyezi Mungu amezaa! Na hali Yeye ametakasika na upungufu kama huo wa kuwa mzazi au kuzaliwa. Na hakika bila ya shaka hao ni waongo kwa usemi huo, kwa ushahidi wa dalili nyingi za Upweke wake.
- 37:153١٥٣
Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume?. [153]
Tanbihi
[153] Ati Yeye amejichagulia mwenyewe mabinti ambao kwa madai yenu ndio mnawachukia kuliko watoto wa kiume ambao mnawapenda, na hali Yeye ndiye Mwenye kuwaumba wote, watoto wa kike na wa kiume?
- 37:154١٥٤
Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?. [154]
Tanbihi
[154] Ni nini lilio kusibuni hata mkakata hukumu bila ya ushahidi? Vipi mnahukumu hivyo na hali ni upotovu ulio wazi?
- 37:155١٥٥
Hamkumbuki?. [155]
Tanbihi
[155] Je! Mmesahau dalili za uweza wake na kutakasika kwake, ndio msikumbuke mpaka mkaingia katika upotovu?
- 37:156١٥٦
Au mnayo hoja iliyo wazi?. [156]
Tanbihi
[156] Hebu nyinyi mnazo nguvu za ushahidi wa kubainisha wa kuthibitisha hayo mnayo yadai?
- 37:157١٥٧
Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli. [157]
Tanbihi
[157] Basi leteni hoja zenu, ikiwa mnazo hoja za katika Kitabu cha mbinguni, kama nyinyi ni wakweli katika hayo myasemayo na mnayo yahukumia.
- 37:158١٥٨
Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa. [158]
Tanbihi
[158] Wakashikilia katika itikadi zao, na wakazua baina ya Mwenyezi Mungu na majini, ambao hawawaoni, kuwa ati yapo makhusiano ya nasaba. Na bila ya shaka hao majini walikwisha jua kuwa makafiri watahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu ili wapate malipo yao yasiyo kimbilika.
- 37:159١٥٩
Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia. [159]
Tanbihi
[159] Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasika na hizo sifa za kuemewa na za upungufu wanazo mzulia kuwa anazo.
- 37:160١٦٠
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. [160]
Tanbihi
[160] Lakini waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa wakasafishwa hawana makosa ya huo uzushi wa makafiri.
- 37:161١٦١
Basi hakika nyinyi na mnao waabudu. [161]
Tanbihi
[161] Enyi makafiri! Hakika nyinyi, na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu - Nyinyi kwa kuwaabudu kwenu badala yake Yeye, hamtampoteza yeyote kwa upotovu wenu. Isipo kuwa yule ambaye tangu hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamjua ni katika watu wa Motoni, na huko ataingia.
- 37:162١٦٢
Hamwezi kuwapoteza. [162]
Tanbihi
[162] Enyi makafiri! Hakika nyinyi, na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu - Nyinyi kwa kuwaabudu kwenu badala yake Yeye, hamtampoteza yeyote kwa upotovu wenu.
- 37:163١٦٣
Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni. [163]
Tanbihi
[163] Isipo kuwa yule ambaye tangu hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamjua ni katika watu wa Motoni, na huko ataingia.
- 37:164١٦٤
Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu. [164]
Tanbihi
[164] Na Malaika kuwania kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu, wakasema: Hapana yeyote katika sisi ila ana cheo chake maalumu katika ujuzi, na ibada, na wala hakikiuki hicho.
- 37:165١٦٥
Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu. [165]
Tanbihi
[165] Na sisi tumejipanga safu wenyewe katika misimamo ya kutumika daima.
- 37:166١٦٦
Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa. [166]
Tanbihi
[166] Na hakika sisi bila ya shaka yoyote ndio wenye kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisilo kuwa na maelekeo naye katika kila hali.
- 37:167١٦٧
Na walikuwapo walio kuwa wakisema:. [167]
Tanbihi
[167] Na walikuwapo makafiri wa Makka kabla ya kuteuliwa Mtume s.a.w. ambao wakisema:
- 37:168١٦٨
Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani,. [168]
Tanbihi
[168] Lau kuwa sisi tungeli kuwa na Kitabu kama Vitabu vya watu wa zamani, yaani kama Taurati na Injili, nasi bila ya shaka tungeli kuwa waja wa Mwenyezi Mungu wenye kumsafia ibada Yeye.
- 37:169١٦٩
Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi. [169]
Tanbihi
[169] Nasi bila ya shaka tungeli kuwa waja wa Mwenyezi Mungu wenye kumsafia ibada Yeye.
- 37:170١٧٠
Lakini waliukataa. Basi watakuja jua. [170]
Tanbihi
[170] Na Kitabu kikawajia, nao wakakikataa. Basi watakuja jua nini matokeo ya kukataa kwao.
- 37:171١٧١
Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa. [171]
Tanbihi
[171] Ninaapa! Hukumu yetu kwa Mitume tulio watuma imekwisha tolewa mbele, ya kwamba ushindi na matokeo mema ni yao wao dhidi ya makafiri.
- 37:172١٧٢
Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. [172]
Tanbihi
[172] Ninaapa! Hukumu yetu kwa Mitume tulio watuma imekwisha tolewa mbele, ya kwamba ushindi na matokeo mema ni yao wao dhidi ya makafiri.
- 37:173١٧٣
Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda. [173]
Tanbihi
[173] Na kwamba wafuasi wetu na wasaidizi wetu ndio peke yao watakao washinda walio kengeuka.
- 37:174١٧٤
Basi waachilie mbali kwa mda. [174]
Tanbihi
[174] Basi waachilie mbali, nawe ngoja mpaka wakati ujao. Kwani Sisi tutakupa wewe matokeo mema, na manusura, na ushindi.
- 37:175١٧٥
Na watazame, nao wataona. [175]
Tanbihi
[175] Nawe watazame, na uangalie vyema adhabu gani na mateso yatakayo wapata kwa kwenda kinyume nawe na kukukadhibisha. Basi watakuja ona kwa macho yao zitakavyo shindwa safu zao, na wataona nusura ya Mwenyezi Mungu inavyo wafikia Waumini.
- 37:176١٧٦
Je! Wanaihimiza adhabu yetu?. [176]
Tanbihi
[176] Je! Wamepoteza akili zao nini, hata wakawa wanaihimiza adhabu yetu?
- 37:177١٧٧
Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa. [177]
Tanbihi
[177] Basi adhabu hiyo itakapo teremka kwenye uwanja wao mpana, itakuwa asubuhi ovu kweli hiyo kwa hao walio onywa na adhabu.
- 37:178١٧٨
Na waache kwa muda. [178]
Tanbihi
[178] Na waachilie mbali mpaka mambo yatakapo waishia.
- 37:179١٧٩
Na tazama, na wao wataona. [179]
Tanbihi
[179] Na yaangalie yatakayo wafika wao na yatakayo kufika wewe. Wao watakuja yaona hayo wanayo yahimiza.
- 37:180١٨٠
Subhana Rabbi'l'Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia. [180]
Tanbihi
[180] Mwenyezi Mungu, aliye kuumba wewe na aliye ziumba nguvu na ushindi, ametakasika na huo uzushi wanao muambatisha naye.
- 37:181١٨١
Na Salamu juu ya Mitume. [181]
Tanbihi
[181] Na salamu zishuke juu ya Mitume wapenzi walio safika.
- 37:182١٨٢
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. [182]
Tanbihi
[182] Na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu peke yake, Muumba wa viumbe vyote, na Mwenye kuwaangalia makhaluku wote.
Sura Saad
سُورَةُ ص- 38:1١
S'ad, Naapa kwa Qur'ani yenye mawaidha. [1]
Tanbihi
[1] S'ad: Ni harufi iliyo anzia Sura hii kama zilivyo anzia baadhi ya Sura nyengine kwa mpango wa Qur'ani katika kuanzia kwa harufi moja moja. Naapa kwa Qur'ani yenye utukufu na shani kubwa kuwa hakika hii ni Kweli isiyo na shaka yoyote.
- 38:2٢
Lakini walio kufuru wamo katika majivuno na upinzani . [2]
Tanbihi
[2] Lakini walio kufuru wamo katika majivuno, hawataki kufuata Haki, na wanawafanyia inda watu wa Haki.
- 38:3٣
Mataifa mangapi tumeyaangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwisha pita. [3]
Tanbihi
[3] Mataifa mengi tuliyateketeza kabla yao, wakapiga kelele kutaka msaada ilipo wafikia adhabu. Lakini huo haukuwa wakati wa kuiepuka adhabu.
- 38:4٤
Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anaye tokana nao wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo. [4]
Tanbihi
[4] Na walistaajabu watu hawa kuwa amewajia Mtume binaadamu kama wao, na wakasema hao wanao upinga Ujumbe wake: Huyu ni mdanganyifu, mwongo.
- 38:5٥
Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu. [5]
Tanbihi
[5] Ati amewafanya miungu yote kuwa ni Mungu mmoja tu! Ama hakika jambo hili ni la ajabu, mwisho wa kustaajabisha.
- 38:6٦
Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililo pangwa. [6]
Tanbihi
[6] Wakubwa wao wakakimbilia kuusiana wao kwa wao wakiambiana: Endeleeni na njia yenu hiyo hiyo, na shikilieni kuiabudu miungu yenu. Kwani hakika tumepangiwa jambo kubwa hili.
- 38:7٧
Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu. [7]
Tanbihi
[7] Hatujapata kusikia haya mambo ya Tawhidi, kumfanya Mungu mmoja tu, katika dini ya baba zetu tulio wawahi kuwaona. Haya si chochote ila ni uwongo tu ulio zuliwa.
- 38:8٨
Ati yeye tu ndiye aliye teremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu. [8]
Tanbihi
[8] Basi katika sote sisi, amechaguliwa Muhammad tu peke yake kupewa hishima ya kuteremshiwa Qur'ani?
- 38:9٩
Au wanazo wao khazina za rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji? [9]
Tanbihi
[9] Bali sisi tunawauliza hawa wanao kuhusudu: Kwani wao wanazo khazina za rehema ya Mola wako Mlezi Mwenye nguvu, Mwingi wa kutoa, hata wao wawe ndio wa kuteua nani wa kumpa Unabii kwa mujibu wa mapenzi ya nafsi zao?
- 38:10١٠
Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo kati yao? Basi nawazipande njia za kwendea huko! [10]
Tanbihi
[10] Tena tunawauliza: Kwani wao wanao ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao? Ikiwa hivyo basi nawazipande ngazi mpaka wafikie pahala ambapo watakuwa wakitoa hukumu kama watakavyo, kama wanaweza!
- 38:11١١
Hao ni askari watao shindwa miongoni mwa makundi yatayo shindwa. [11]
Tanbihi
[11] Hao ni askari wanyonge walio shindwa, hapana hivi wala hivi, kama walivyo shindwa mfano kama wao walio jikusanya kuwapinga Manabii.
- 38:12١٢
Walikanusha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A'adi na Firauni mwenye majengo. [12]
Tanbihi
[12] Kabla ya hawa, walikadhibisha kaumu ya Nuhu, kina A'adi na Firauni aliye kuwa na majengo makubwa yaliyo simama imara kama milima, na kina Thamudi na Kaumu Lut'i na Kaumu ya Shuaibu, na watu wa Machakani, kwenye miti mingi iliyo shikamana. Hao ndio walio jumuika kuwapinga Mitume wao kama walivyo jumuika watu wako.
- 38:13١٣
Na Thamud na kaumu Lut'i na watu wa Machakani. Hayo ndiyo makundi. [13]
Tanbihi
[13] Na kina Thamudi na Kaumu Lut'i na Kaumu ya Shuaibu, na watu wa Machakani, kwenye miti mingi iliyo shikamana. Hao ndio walio jumuika kuwapinga Mitume wao kama walivyo jumuika watu wako.
- 38:14١٤
Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahiki adhabu yangu. [14]
Tanbihi
[14] Hapana mmoja katika hao wote ila alimkadhibisha Mtume wake, na kwa hivyo ikawashukia adhabu yangu.
- 38:15١٥
Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda. [15]
Tanbihi
[15] Na hao walio jiunga kuwapinga Mitume hawangojei ila ukelele mmoja usio hitajia kukaririwa.
- 38:16١٦
Na wao husema: Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hisabu. [16]
Tanbihi
[16] Na makafiri husema kwa kejeli: Mola wetu Mlezi! Tuhimizie sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Malipo.
- 38:17١٧
Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia. [17]
Tanbihi
[17] Ewe Muhammad! Yastahamilie hayo wanayo yasema juu yako washirikina. Na mkumbuke mja wetu, Daudi, mwenye nguvu katika Dini na dunia. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika hali zote.
- 38:18١٨
Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye. [18]
Tanbihi
[18] Hakika Sisi tuliidhalilisha milima pamoja naye, yeye akichuma manufaa kutoka humo, na hiyo milima ikimtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kila upungufu, wakati wa mwisho wa mchana na mwanzo wake.
- 38:19١٩
Na pia ndege walio kusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake. [19]
Tanbihi
[19] Na pia tukamdhalilishia ndege walio kusanywa kutokana na kila namna na kila pahali. Vyote hivyo, milima na ndege, vikimwitikia Daudi kama atakavyo, akivisarifu kama apendavyo kwa maslaha ya umma.
- 38:20٢٠
Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na kukata hukumu. [20]
Tanbihi
[20] Tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa Unabii na kupambanua baina ya Haki na baat'ili.
- 38:21٢١
Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo pindukia ukuta kuingia chumbani? [21]
Tanbihi
[21] Ewe Muhammad! Ati imekujia khabari ya makhasimu wagombanao, walio mjia Daudi kwa kupindukia kuta za mihrabuni palipo kuwa pahala pake pa ibada? Hawakupita mlangoni.
- 38:22٢٢
Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa. [22]
Tanbihi
[22] Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa, akababaika. Wakasema: Usikhofu kitu. Sisi ni wenye kuzozana, tumedhulumiana. Basi tuhukumu kwa uadilifu wala usiupindukie huo uadilifu. Na tuongoze kwenye njia iliyo sawa sawa.
- 38:23٢٣
Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na amenishinda kwa maneno. [23]
Tanbihi
[23] Mmoja wa hao wagombanao alisema: Hakika huyu ndugu yangu anao kondoo wa kike tisiini na tisa, na mimi ninaye kondoo mmoja tu. Akasema: Nache niwe nakuchungia kama ninavyo wachunga wangu. Na akanishinda katika usemi.
- 38:24 ۩ Sijida٢٤
Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia. [24]
Tanbihi
[24] Daudi akasema kabla hajasikia maneno ya yule mwenye ugomvi mwengine: Hakika huyo amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako amchanganye na wale wake. Na hakika wengi wenye kushirikiana hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa wale ambao Imani yao imetulia katika nyoyo zao, na wakawa wanatenda mema. Na watu kama hao ni wachache, shida kupatikana. Na Daudi akajua kuwa jambo hili si chochote ila ni mtihani tuliyo mfanyia Sisi. Basi akaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, na akainama kurukuu kwa Mwenyezi Mungu, na akarejea kwa Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu.
- 38:25٢٥
Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu. [25]
Tanbihi
[25] Na Sisi tukamsamehe kule kufanya haraka ya kutoa hukumu. Na hali yeye ana hadhi na marejeo mazuri kwetu.
- 38:26٢٦
Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu. [26]
Tanbihi
[26] Na Mwenyezi Mungu alimfunulia kwa kumwambia: Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa, yaani Naibu, wetu katika ardhi. Basi wahukumu watu kwa sharia niliyo kupa, wala usiendeshe hukumu kufuata matamanio yao, yakakupotosha njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wendao pogo na njia ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata matamanio yao wao watapata adhabu kali kwa kughafilika kwao na Siku ya Malipo.
- 38:27٢٧
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata. [27]
Tanbihi
[27] Wala Sisi hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa mchezo. Hayo ndiyo wanayo yadhania makafiri. Na kwa hivyo wakapitisha hukumu kwa mujibu wa pumbao zao. Basi hao walio kufuru watapata adhabu kali ya Moto.
- 38:28٢٨
Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu? [28]
Tanbihi
[28] Inaelekeana vipi na hikima yetu na uadilifu wetu tuwafanye sawa baina ya Waumini wenye kutenda mema, na wale wanao fanya uharibifu katika ardhi? Au yaelekea vipi tuwaweke sawa baina ya wenye kuikhofu adhabu yetu na wakaiogopa ikabu yetu na wale walio waasi wakenda kinyume na hukumu zetu?
- 38:29٢٩
Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili. [29]
Tanbihi
[29] Ewe Muhammad! Hichi tulicho kuteremshia ni Kitabu chenye manufaa mengi, ili wenye akili nzuri na nyoyo za kufahamu wapate kuzielewa Aya zake, na wawaidhike kwazo.
- 38:30٣٠
Na Daudi tukamtunukia Suleiman. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia. [30]
Tanbihi
[30] Na Daudi tulimtunukia mwana, aitwaye Suleiman, mwenye kustahiki sifa nzuri, ambaye anafaa kuitwa, "Mja mwema kweli". Kwa sababu yeye alikuwa mwingi mno wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika kila hali.
- 38:31٣١
Alipo pelekewa jioni farasi wasimamao kidete, tayari kutoka shoti; [31]
Tanbihi
[31] Na hebu taja katika khabari za Suleiman kuwa alipelekewa alasiri farasi wa asli ambao hutulia wanapo simama, na huenda mbio wanapo kwenda.
- 38:32٣٢
Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Kisha wakafichikana nyuma ya boma. [32]
Tanbihi
[32] Suleiman akasema: Hakika mimi nimenyweshwa mapenzi ya farasi, kwa sababu hawa ni katika matayarisho ya mambo ya kheri, nayo ni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Mapenzi haya yametokana na kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Na hakusita kushughulika kuwaangalia mpaka wakapotea machoni mwake.
- 38:33٣٣
Nirudishieni! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo. [33]
Tanbihi
[33] Akaamrisha warudishwe tena kwake apate kujua hali yao. Akaingia kuwapapasa miundi ya miguu yao na shingo zao kwa upole na mapenzi juu yao.
- 38:34٣٤
Na tulimtia mtihanini Suleiman, na tukauweka mwili juu ya kiti chake, kisha akarejea kwa kutubu. [34]
Tanbihi
[34] Na hakika Sisi tulimfanyia mtihani Suleiman ili asighurike na heba ya ufalme. Tukaweka juu ya kiti chake kiwiliwili kisicho weza kuendesha mambo. Akautambua mtihani, akarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akatubu.
- 38:35٣٥
Akasema: Mola wangu Mlezi! Nisamehe na unipe ufalme usio mwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mpaji. [35]
Tanbihi
[35] Suleiman alimwomba Mola wake Mlezi kwa kurejea kwake: Mola wangu Mlezi! Nighufirie yaliyo toka kwangu kwa ghafla, na unitunukie ufalme usio elekea yeyote kuupata baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mwingi wa kutunukia, na ndiye Mwingi wa kutoa.
- 38:36٣٦
Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri yake, popote alipo taka kufika. [36]
Tanbihi
[36] Tukamdhalilishia upepo, ukenda kama anavyo taka maridhawa, kokote aliko kusudia na kutaka.
- 38:37٣٧
Na tukayafanya mashet'ani yamtumikie, wote wajenzi na wapiga mbizi. [37]
Tanbihi
[37] Na tukamdhalilishia kila mjenzi na mpiga mbizi katika bahari kuu miongoni mwa mashetani maasi.
- 38:38٣٨
Na wengine wafungwao kwa minyororo. [38]
Tanbihi
[38] Na wengine katika hao mashetani wamefungwa wao kwa wao kwa minyororo, kuwazuia na wenginewe wasifanye ufisadi wao.
- 38:39٣٩
Hichi ndicho kipawa chetu. Basi toa au zuia, bila ya hisabu. [39]
Tanbihi
[39] Na akamfunulia kwa wahyi : Haya tuliyo kuneemesha kwayo ni kipawa kilicho toka kwetu. Yaani ni Sisi tulio kupa. Basi mpe umtakaye, na mnyime umtakaye. Hapana hisabu juu yako kwa kutoa au kunyima.
- 38:40٤٠
Na hakika yeye kwetu Sisi ana cheo cha kukaribishwa kwetu, na pahala pazuri pa kurejea. [40]
Tanbihi
[40] Hakika Suleiman kwetu Sisi ana ukaribisho mkubwa, na marejeo mazuri.
- 38:41٤١
Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shet'ani amenifikishia udhia na adhabu. [41]
Tanbihi
[41] Ewe Muhammad! Mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwomba Mola wake Mlezi kwa kusema: Hakika Shetani amenipatisha taabu na machungu.
- 38:42٤٢
(Akaambiwa:) Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Basi haya maji baridi ya kuogea na ya kunywa. [42]
Tanbihi
[42] Tukamuitikia na tukamwambia: Ipige ardhi kwa mguu wako, yatatimbuka maji baridi, utakoga na utakunywa hayo, na kwa hivyo yatakuondokea machofu na adhabu.
- 38:43٤٣
Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili. [43]
Tanbihi
[43] Tukamkusanyia watu wake walio kuwa wametapanyika mbali naye siku zile za mateso yake. Na tukamzidishia wenginewe kama wale. Na tulifanya hayo kuwa ni rehema kutokana nasi, na ili yawe ni mawaidha kwa wenye akili, wapate kujua kuwa matokeo ya subira ni faraji.
- 38:44٤٤
Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, kisha ndio upigie nacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu. [44]
Tanbihi
[44] Ayubu alikuwa kaapa kuwa atampiga mmoja wapo katika ahali zake fimbo kadhaa wa kadhaa. Mwenyezi Mungu alimhalalishia aondoe kiapo chake kwa kuchukua kifungu cha fimbo idadi ile ile alio apia kuwa atampigia. Basi kwa kile kifungu cha fimbo ampige aliye apa kuwa atampiga, na hapo yamini yake itakuwa imetimia kwa uchache wa machungu. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mneemesha kwa neema hizi, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimwona kuwa ni mtu aliye vumilia masaibu yake. Kwa hivyo amestahiki sifa. Mbora wa kusifiwa kwa ibada ni yeye, kwa sababu yeye ni mwingi mno wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika kila jambo.
- 38:45٤٥
Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Yaa'qubu walio kuwa na nguvu na busara. [45]
Tanbihi
[45] Na mkumbuke mja wetu Ibrahim, na Is-haqa, na Yaa'qubu, wenye nguvu katika Dini na dunia, na wenye busara ya mwangaza.
- 38:46٤٦
Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera. [46]
Tanbihi
[46] Hakika Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa, nayo ni kuwa wanaikumbuka Nyumba ya Akhera, wao wanaikumbuka nao wanakumbukwa kwayo.
- 38:47٤٧
Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora. [47]
Tanbihi
[47] Na hakika wao kwetu Sisi ni wenye kukhitariwa walio bora.
- 38:48٤٨
Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifli, na wote hao ni katika walio bora. [48]
Tanbihi
[48] Na mkumbuke Ismail, na Alyasaa, na Dhalkifli - na wote hao ni miongoni mwa walio bora.
- 38:49٤٩
Huu ni ukumbusho. Na hakika wachamngu wana marudio mazuri. [49]
Tanbihi
[49] Haya tuliyo kusimulia ni khabari za baadhi ya Mitume ili kukukumbusha wewe na kuwakumbusha watu wako. Na hakika wachamngu walio jikinga na kumuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu watapata marejeo mazuri na natija njema.
- 38:50٥٠
Bustani za milele zitazo funguliwa milango yao kwa ajili yao. [50]
Tanbihi
[50] Wameandaliwa bustani za milele zilizo funguliwa milango yao hapana wa kuwazuia wasiingie humo.
- 38:51٥١
Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji. [51]
Tanbihi
[51] Watakuwa wamekaa humo wakiegemea juu ya makochi na vitanda kama wafanyavyo wenye taanusi, wakistarehe kwa kutaka matunda ya kila namna na vinywaji.
- 38:52٥٢
Na pamoja nao wake zao wenye kutuliza macho, hirimu zao. [52]
Tanbihi
[52] Na huko Peponi watakuwa na wake ambao macho yao hayawatazami ila waume zao tu, hawawaangalii wengineo, nao ni wa miaka sawa na waume zao. Kwa hivyo wameelekeana kuwafikiana.
- 38:53٥٣
aya ndiyo mliyo ahidiwa kwa Siku ya Hisabu. [53]
Tanbihi
[53] Raha hii ndiyo mliyo ahidiwa kuipata Siku ya Kiyama.
- 38:54٥٤
Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyo malizika. [54]
Tanbihi
[54] Hakika haya bila ya shaka ni tunayo yatoa Sisi, na wala hayana ukomo.
- 38:55٥٥
Ndio hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marudio maovu kabisa; [55]
Tanbihi
[55] Neema hizi ni malipo ya wachamngu. Na hakika majabari wenye kuwaasi Manabii wao bila ya shaka watakuwa na marejeo na mwisho muovu.
- 38:56٥٦
Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nacho hicho ni kitanda kiovu mno cha kulalia. [56]
Tanbihi
[56] Na mwisho huo ni Jahannamu watakayo iingia, na moto wake uwatese. Na malalio maovu mno hayo!
- 38:57٥٧
Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha! [57]
Tanbihi
[57] Haya maji ya moto, mwisho wa umoto, na usaha wa watu wa Jahannamu wataamrishwa wayaonje.
- 38:58٥٨
Na adhabu nyenginezo za namna hii. [58]
Tanbihi
[58] Na adhabu nyengine mfano wa hizi, za namna kwa namna zilizo changanyika.
- 38:59٥٩
Hili ndilo kundi litakalo ingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho mema kwao. Hakika hao wanaingia Motoni. [59]
Tanbihi
[59] Na majabari, wale marais wa washirikina, wataambiwa: Hawa chungu ya watu wanao ingia Motoni pamoja nanyi kwa kusukumana na kwa shida, ni wafwasi wenu. Wale marais watasema: Hawana mapokezi mema hao! Hakika hao wanaingia Motoni wapate kuteseka kwa mvukuto wake.
- 38:60٦٠
Waseme: Lakini nyinyi! Hamna mapokezi mazuri! Nyinyi ndio mlio tusabibisha haya, napo ni pahala paovu kabisa! [60]
Tanbihi
[60] Na wafwasi hao watasema: Bali nyinyi ndio mnastahiki zaidi hayo maapizo mnayo tuapizia sisi, kwani nyinyi ndio mlio tuletea adhabu hii kwa vile mlivyo tudanganya na mkatuitia ukafirini, nasi tukakufuru kwa sababu yenu. Basi nyumba ovu kabisa ya kukaa ni Jahannamu!
- 38:61٦١
Waseme: Mola wetu Mlezi! Aliye tusabibisha haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni. [61]
Tanbihi
[61] Wafwasi watasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Aliye kuwa ni sababu ya adhabu hii, mzidishie adhabu mara mbili katika Moto.
- 38:62٦٢
Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ndio katika waovu? [62]
Tanbihi
[62] Na watu wa Motoni watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tulikuwa duniani tukiwahisabu kuwa ndio katika waovu, na wa duni, wasio kuwa na jema lolote? Na watu hao ni wale mafakiri wa Kiislamu.
- 38:63٦٣
Tulikosea tulipo wafanyia maskhara, au macho yetu tu hayawaoni ? [63]
Tanbihi
[63] Imekuwaje kuwa sisi tukiwakejeli na wala hawakuingia Motoni pamoja nasi? Au wamekwisha ingia na macho yetu yakazibwa tusiwaone tu?
- 38:64٦٤
Hakika hayo bila ya shaka ndiyo makhasimiano ya watu wa Motoni. [64]
Tanbihi
[64] Hakika hayo tuliyo yataja ya hadithi ya watu wa Motoni ni kweli ambayo haina budi kutokea, nayo ni ya kugombana kwa watu wa Motoni wao kwa wao.
- 38:65٦٥
Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mungu ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda nguvu, [65]
Tanbihi
[65] Ewe Muhammad! Waambie washirikina: Hakika mimi ni mwenye kukuonyeni na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu Mmoja ambaye hana mshirika wake, Mtenda nguvu, Mwenye kumshinda kila mwenye madaraka.
- 38:66٦٦
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe. [66]
Tanbihi
[66] Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao, Mwenye nguvu asiye shindika, Mwenye kusamehe, akazifuta dhambi za mwenye kumuamini.
- 38:67٦٧
Sema: Hii ni khabari kubwa kabisa. [67]
Tanbihi
[67] Ewe Muhammad! Waambie: Haya ninayo kuambieni ni khabari kubwa, ambazo nyinyi mnazipuuza. Msizikanye!
- 38:68٦٨
Ambayo nyinyi mnaipuuza. [68]
Tanbihi
[68] Ewe Muhammad! Waambie: Haya ninayo kuambieni ni khabari kubwa, ambazo nyinyi mnazipuuza. Msizikanye!
- 38:69٦٩
Sikuwa na ilimu ya mambo ya viumbe wakuu watukufu walipo kuwa wakishindana. [69]
Tanbihi
[69] Mimi sikuwa nikijua khabari za watukufu walio juu walipo kuwa wakizozana juu ya shauri ya Adam, kwa sababu mimi sikupitia njia za kupata ilimu zilizo zowewa na watu za kusoma vitabu au kupokea masomo kwa wataalamu. Njia yangu mimi ya kujua ni kwa kufunuliwa kwa Wahyi.
- 38:70٧٠
Haikufunuliwa kwangu isipo kuwa ya kwamba hakika mimi ni mwonyaji dhaahiri. [70]
Tanbihi
[70] Na mimi sikufunuliwa kwa Wahyi ila kwamba hakika mimi ni Mtume wa kukufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi kwa njia iliyo wazi kabisa.
- 38:71٧١
Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo. [71]
Tanbihi
[71] Watajie pale alipo sema Mola wako Mlezi kuwaambia Malaika: Mimi nataka umba mtu, naye ni Adam a.s., kutokana na udongo.
- 38:72٧٢
Na nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayo tokana nami, basi muangukieni kwa kumt'ii. [72]
Tanbihi
[72] Nikisha timiza kumuumba na nikampulizia siri ya uhai, nayo ni roho, muangukieni kwa kusujudu sijida ya kumtukuza na kumuamkia.
- 38:73٧٣
Basi Malaika wakat'ii wote pamoja. [73]
Tanbihi
[73] Malaika wote wakafanya kama walivyo amrishwa, wakamuangukia wakisujudu, isipo kuwa Iblisi. Yeye hakusujudu, na akajiona bora na akapanda kiburi, na akawa miongoni mwa makafiri.
- 38:74٧٤
Isipo kuwa Iblisi; alijivuna na akawa katika makafiri. [74]
Tanbihi
[74] Malaika wote wakafanya kama walivyo amrishwa, wakamuangukia wakisujudu, isipo kuwa Iblisi. Yeye hakusujudu, na akajiona bora na akapanda kiburi, na akawa miongoni mwa makafiri.
- 38:75٧٥
Mwenyezi Mungu akamwambia: Ewe Iblisi! Kipi kilicho kuzuia kumt'ii yule niliye muumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli? [75]
Tanbihi
[75] Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Ewe Iblisi! Nini kilicho kuzuilia kumsujudia niliye muumba Mimi mwenyewe bila ya kuingiliwa na yeyote kati yake! Umejiona mkubwa hali nawe si mkubwa, au hakika wewe nafsi yako ni katika walio shinda ukubwa?
- 38:76٧٦
Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo. [76]
Tanbihi
[76] Iblisi akasema: Mimi ni bora kuliko Adam; kwani Wewe umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo. Basi vipi mimi nimsujudie yeye?
- 38:77٧٧
Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umelaanika. [77]
Tanbihi
[77] Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kumlipa Iblisi kwa kiburi chake cha kukataa amri ya Mola wake Mlezi, alimwambia: Basi toka kwenye kundi la watukufu walio juu, kwani wewe umekwisha fukuzwa kutokana na rehema yangu!
- 38:78٧٨
Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo. [78]
Tanbihi
[78] Na hakika wewe umetengwa mbali na kila kheri mpaka Siku ya Malipo. Hapo utalipwa kwa sababu ya kunikufuru Mimi na kunifanyia kiburi.
- 38:79٧٩
Akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watayo fufuliwa viumbe. [79]
Tanbihi
[79] Iblisi akasema: Mola Mlezi! Nipe muhula, wala usinifishe mpaka Siku ya kufufuliwa viumbe.
- 38:80٨٠
Mwenyezi Mungu akasema: Basi umekwisha kuwa miongoni mwa walio pewa muhula, [80]
Tanbihi
[80] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi wewe utaakhirishwa, utapewa muhula, mpaka siku ya wakati tunao ujua Sisi, nao ni kumalizika dunia.
- 38:81٨١
Mpaka siku ya wakati maalumu. [81]
Tanbihi
[81] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi wewe utaakhirishwa, utapewa muhula, mpaka siku ya wakati tunao ujua Sisi, nao ni kumalizika dunia.
- 38:82٨٢
Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote, [82]
Tanbihi
[82] Iblisi akasema: Basi naapa kwa Ukubwa wako na Utukufu wako, kwa yakini nitawapoteza watu wote, isipo kuwa waja wako ulio wateuwa kwa ajili ya kukut'ii Wewe. Hao sina madaraka nao.
- 38:83٨٣
Isipo kuwa wale waja wako miongoni mwao walio khitariwa. [83]
Tanbihi
[83] Isipo kuwa waja wako ulio wateuwa kwa ajili ya kukut'ii Wewe. Hao sina madaraka nao.
- 38:84٨٤
kasema: Haki! Na haki ninaisema. [84]
Tanbihi
[84] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Haki ndiyo yamini yangu na kiapo changu; na wala sisemi ila Haki. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa jinsi yako ya kishetani na watakao kufuata katika vizazi vya Adam wote. Hapana khitilafu kwangu baina ya wafuasi na wanao fuatwa.
- 38:85٨٥
Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao. [85]
Tanbihi
[85] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Haki ndiyo yamini yangu na kiapo changu; na wala sisemi ila Haki. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa jinsi yako ya kishetani na watakao kufuata katika vizazi vya Adam wote. Hapana khitilafu kwangu baina ya wafuasi na wanao fuatwa.
- 38:86٨٦
Sema (Ewe Mtume) : Sikuombeni ujira juu ya haya, wala mimi si katika wadanganyifu. [86]
Tanbihi
[86] Ewe Muhammad! Waambie umma wako: Mimi sikuombeni ujira kwa ajili ya haya niliyo amrishwa nikufikishieni yaliyomo katika Qur'ani na Wahyi. Wala mimi si katika hao wanao jipamba na yasiyo kuwa yao, hata nijidai Unabii.
- 38:87٨٧
Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. [87]
Tanbihi
[87] Haikuwa Qur'ani ila ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote.
- 38:88٨٨
Na bila ya shaka mtajua khabari zake baada ya muda. [88]
Tanbihi
[88] Na hapana shaka nyinyi, mnao ikadhibisha Qur'ani, mtakuja jua karibuni hivi ukweli uliomo ndani yake wa ahadi, na maonyo, na khabari za mambo yatakayo kuja, na Ishara za ulimwengu.
Sura Az-Zumar
سُورَةُ الزمر- 39:1١
Mteremsho wa Kitabu hiki umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima. [1]
Tanbihi
[1] Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu, ambaye hana wa kumshinda kwa atakayo; Mwenye hikima katika vitendo vyake na utungaji wa sharia zake.
- 39:2٢
Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu. [2]
Tanbihi
[2] Hakika Sisi tumekuteremshia wewe, Muhammad, Qur'ani hii yenye kuamrisha Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia ibada Yeye tu peke yake.
- 39:3٣
Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanao wafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika wanayo khitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye mwongo kafiri. [3]
Tanbihi
[3] Jueni na mtambue kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye Dini isiyo kuwa na ila. Na washirikina walio wafanya wenginewe kuwa ni wasaidizi wa kuwanusuru, wanasema: Sisi hatuwaabudu hawa kwa kuwa ni waumbaji, bali tunawaabudu wapate kutukaribisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa mkaribisho wa kutuombea sisi kwake Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina ya hawa washirikina na Waumini wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja katika yale wanayo khitalifiana katika matatizo ya shirki na Tawhidi. Hakika Mwenyezi Mungu hamjaalii afikie Haki mtu ambaye mtindo wake ni uwongo na kukanya.
- 39:4٤
Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, basi bila ya shaka angeli teua amtakaye katika alio waumba. Subhanahu, Ametakasika na hayo! Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda atakalo. [4]
Tanbihi
[4] Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, kama wasemavyo Wakristo kwa Masihi, na washirikina kwa Malaika, basi angeli jichagulia amtakaye katika viumbe vyake, la sio kama mtakavyo nyinyi. Mwenyezi Mungu ametakasika na upungufu wa kuhitajia mwana. Yeye ni Mwenyezi Mungu asiye kuwa na mfano kama Yeye. Mtenda kama apendavyo, ukomo wa kutenda.
- 39:5٥
Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Hufunika usiku juu ya mchana, na hufunika mchana juu ya usiku. Na amefanya jua na mwezi vitumike. Kila kimojapo kinakwenda kwa kipindi kilicho wekewa. Jueni mtanabahi! Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe! [5]
Tanbihi
[5] Ameumba mbingu na ardhi kwa kushikamana na Haki na kuwa sawa kwa kufuatana na sharia zilizo thibiti. Usiku unaufunika mchana, na mchana unaufunika usiku kwa mfululizo. Na amedhalilisha jua na mwezi kwa mujibu atakavyo na kwa mujibu wa maslaha ya waja wake. Kila kimojapo katika hivyo vinakwenda katika njia yake mpaka ufike wakati aliyo uwekea Yeye, nao ni Siku ya Kiyama. Jueni basi kuwa Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye kushinda kila kitu. Basi hapana kitu chochote kilicho tokana na atakavyo Yeye, ambaye amefikilia ukomo wa kuwasamehe wenye kutenda madhambi katika waja wake. Aya hii tukufu inaonyesha kuwa ardhi ina sura ya mviringo kama mpira, na inazunguka wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake. Kwani kule kutumiwa neno Yukawwiru katika Kiarabu na ikafasiriwa Hufunika, maana yake ni kufunika kitu kwa kitu kwa namna ya kufuatana, kukariri, mara kwa mara. Na lau kuwa ardhi haina sura ya mpira, kwa mfano kuwa batabata tu, usiku ungeli enea kote kwa ghafla, au mchana ungeli angaza dunia nzima kwa mara moja.
- 39:6٦
Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi? [6]
Tanbihi
[6] Enyi watu! Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na nafsi moja, naye ni Adam, baba wa watu wote. Na amemuumba kutokana na nafsi hiyo mkewe, Hawa. Na amekuteremshieni kwa ajili ya maslaha yenu namna nane za nyama hoa, wanyama wa mifugo, madume na majike. Nao ni ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi. Naye anakuumbeni matumboni mwa mama zenu kwa kukua na kugeuka geuka, katika viza vitatu, navyo ni kiza cha tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio. Huyo aliye kuneemesheni kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu, Mlezi wenu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote. Ni Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye utawala wa pekee. Hapana wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi yawaje hata wanaacha kumuabudu Yeye wakenda kuwaabudu wenginewe? Huzuka yai katika mwahala pa kufanyika mayai kwa mwanamke, hata likisha kuwa tayari hutumbukia katika mojapo ya paipu za Filopia likapita humo mpaka kufikia kwenye tumbo la uzazi Rahimi (Womb). Halifiki huko ila kupita siku kidogo, na huenda kijidudu cha manii (Sperm) ya mwanamume kikaliingia hilo yai, na hapo huanza viwango vya kugeuka na kukua kwa mwanzo. Na katika tumbo la uzazi hubaki mtoto muda wa mimba, na hujifanyia vifuniko viwili, na sehemu ya funiko moja hufanyika zalio, placenta. Na funiko jingine ndio humfunika yule mtoto khasa. Yapo maoni mbali mbali juu ya hivyo "viza vitatu" kama ilivyo tajwa katika Aya hii tukufu. Katika hayo ni Tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio, yaani mfuko unao mfunika mtoto. (2)Tumbo la uzazi, na ile mifuniko miwili. (3) Tumbo na mgongo na tumbo la uzazi. (4) Panapo toka mayai (Mabiidh, au Ovaries), na paipu ya kupitia mayai, Fillopian tube, na tumbo la uzazi (Rahimi au Womb). Na dhaahiri ni kuwa hii ya mwisho ndiyo rai yenye nguvu zaidi, kwa sababu ni mahala patatu mbali mbali. Ama zile rai nyengine zinaonyesha kwa hakika kiza kimoja katika pahala pamoja palipo zungukwa na t'abaka kadhaa. Na Muumbaji Mtukufu ameashiria katika Kitabu chake ukweli huu wa kisayansi katika zama walipo kuwa watu hawajavumbua hayo mayai ya mwanamke na mwendo wake katika mwili ulio kuwa hauwezi kuonekana kwa macho.
- 39:7٧
Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi. Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo vifuani. [7]
Tanbihi
[7] Enyi watu! Mkizikataa neema za Mwenyezi Mungu, basi Yeye hakika si mhitaji wa imani yenu na shukrani zenu. Lakini Yeye hapendi waja wake wakufuru, kwa sababu hayo yanawadhuru wenyewe. Na mkimshukuru kwa ajili ya neema zake, Yeye huwa radhi nanyi kwa shukra hiyo. Wala mtu mwenye madhambi hayabebi madhambi ya mwenginewe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi, na hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda duniani. Hakika Yeye anayajua mnayo yaficha katika nyoyo zenu ziliomo vifuani. Haya yaliomo katika Qur'ani Tukufu yanaweka wazi msingi wa kutoa adhabu, kama ilivyo vile vile katika Surat Yusuf katika kauli yake Mtukufu: "Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali sisi kumshika yeyote ila tuliye yakuta mali yetu kwake; hivyo basi tutakuwa madhaalimu." Na haya katika Qur'ani ni kusimamisha msingi ulio kwisha tajwa, nao ni msingi ambao haukuthibiti katika kanuni (sharia) za kutungwa na binaadamu ila katika zama za karibuni. (Haya ni kinyume cha ilivyo katika imani aliyo itumbukiza Paulo katika Ukristo, kwamba wanaadamu wamerithi dhambi ya Adam, wanayo ita "Dhambi ya asili", na kwamba Nabii Isa, Yesu, kafa msalabani kwa kubeba dhambi za wanaadamu. Biblia yenyewe inapinga haya. Tazama: Jeremiah 31:29-30; Ezekieli 18 Kwa nadhariya ya Paulo Mungu amedhulumu mara mbili: 1. Kutubandika wanaadamu wote dhambi za Adam, 2. Kumbebesha "mwanawe" Yesu dhambi za walimwengu wote!)
- 39:8٨
Na taabu inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia yake. Sema: Starehe na ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. [8]
Tanbihi
[8] Na mtu akifikiwa na shida yoyote katika shida za dunia humwomba Mola wake Mlezi, na hurejea kwake, baada ya kuwa akimpuuza. Kisha Mola wake Mlezi akimpa neema kubwa husahau zile taabu alizo kuwa akimwombea Mola wake Mlezi amwondolee na amfarijie kabla hajamneemesha kwa neema hizo. Na humfanyia Mwenyezi Mungu miungu washirika walio sawa na Yeye kwa kuwaabudu. Huyo mtu hufanya haya ili ajipoteze yeye na wenginewe waiache Njia ya Mwenyezi Mungu. Ewe Muhammad! Mwambie huyo mwenye sifa hizi kwa kumwonya: Starehe na huko kuzikanya kwako neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe ni katika watu wa Motoni.
- 39:9٩
Je! Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake MleziSema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili. [9]
Tanbihi
[9] Je! Mwenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu nyakati za usiku anao upitisha na hali yeye yumo kusujudu na kusimama, akiiogopa Akhera, naye anataraji rehema ya Mola wake Mlezi, ni kama anaye mwomba Mola wake Mlezi wakati wa shida na akamsahau wakati wa neema? Ewe Muhammad! Waambie: Ati wanakuwa sawa wenye kujua haki za Mwenyezi Mungu wakamuabudu Yeye tu peke yake, na wale wasio jua wakapuuza kuziangalia Ishara? Hakika wenye akili nzuri ndio wanao waidhika.
- 39:10١٠
Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu. [10]
Tanbihi
[10] Ewe Nabii! Sema kwa kufikisha Ujumbe unao toka kwa Mola wako Mlezi: Enyi waja wangu mlio niamini! Jikingeni na ghadhabu za Mola wenu Mlezi. Mwenye kutenda mema atalipwa mema, duniani kwa kusaidiwa, na Akhera kwa Pepo. Wala msikae katika unyonge, kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu ina wasaa. Na subirini kwa kufarikiana na nchi zenu na wapenzi wenu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wenye kusubiri ujira wao mara zisio ingia katika hisabu za wanao hisabu.
- 39:11١١
Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia Dini Yeye tu. [11]
Tanbihi
[11] Sema: Mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ibada yangu isiwe na shirki ndani yake wala riya ya kujionyesha kwa watu.
- 39:12١٢
Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu. [12]
Tanbihi
[12] Na nimeamrishwa amri iliyo tokana naye Mtukufu, amri ya nguvu, ya kwamba niwe wa mwanzo wa kufuata amri zake.
- 39:13١٣
Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu Mlezi. [13]
Tanbihi
[13] Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku Kubwa yenye vitisho ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi.
- 39:14١٤
Sema: Mwenyezi Mungu tu namuabudu kwa kumsafishia Yeye tu Dini yangu. [14]
Tanbihi
[14] Ewe Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na ibada yangu haina shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia yangu nanyi hamnit'ii, basi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie: Hakika wenye kupata khasara ni wale walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe, na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao Siku ya Kiyama. Ama hakika kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo dhaahiri.
- 39:15١٥
Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Sema: Hakika walio khasirika ni wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo khasara iliyo dhaahiri. [15]
Tanbihi
[15] Ewe Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na ibada yangu haina shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia yangu nanyi hamnit'ii, basi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie: Hakika wenye kupata khasara ni wale walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe, na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao Siku ya Kiyama. Ama hakika kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo dhaahiri.
- 39:16١٦
Yatawekwa juu yao mat'abaka ya moto, na chini yao mat'abaka. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawakhofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni Mimi! [16]
Tanbihi
[16] Hawa walio khasirika watakuwa na mat'abaka ya Moto yalio rindikwa juu yao, na chini yao hali kadhaalika. Kwa namna ya adhabu hiyo ndio Mwenyezi Mungu anawahadharisha waja wake. Enyi waja wangu! Basi yaogopeni mateso yangu.
- 39:17١٧
Na wale wanao jiepusha na ibada potovu, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu. [17]
Tanbihi
[17] Na wale wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu katika mwahala mote. Basi Ewe Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili zilizo nawirika.
- 39:18١٨
Ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao. Hao ndio alio waongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili. [18]
Tanbihi
[18] Na wale wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu katika mwahala mote. Basi Ewe Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili zilizo nawirika.
- 39:19١٩
Je! Yule mwenye kustahiki hukumu ya adhabu, je, wewe unaweza kumwokoa aliyomo katika Moto? [19]
Tanbihi
[19] Je! Unaweza kuniingilia katika Ufalme wangu? Iliyo kwisha pita juu yake hukumu ya kumuadhibu, je, wewe unaweza kuizuia? Unayo nguvu hiyo wewe? Je! Unaweza kuwaokoa na Moto baada ya kwisha wathibitikia?
- 39:20٢٠
Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa zilizo jengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. [20]
Tanbihi
[20] Lakini wenye kumkhofu Mola wao Mlezi watapata vyeo vya juu Peponi na majumba yake ya fakhari, yenye kupitiwa chini yake na mito. Hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu haendi kinyume na ahadi yake.
- 39:21٢١
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi, kisha kwa maji hayo akatoa mimea yenye rangi mbali mbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano, na kisha huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa wenye akili. [21]
Tanbihi
[21] Ewe usemezwaye! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, akayapitisha kwenye mito na chemchem za katika ardhi, kisha kwa maji hayo akaotesha mimea ya namna mbali mbali. Kisha baada ya kustawi kwake hiyo mimea, ikayabisika ukaiona imekuwa rangi ya manjano baada ya kustawi kwake. Kisha akaifanya imevurugika na kukatika vipande vipande. Hakika kutoka kwenye hali moja na kuingia hali nyengine ni mazingatio kwa wenye akili zilizo nawirika. Huku kuzunguka maji katika maumbile kutoka mbinguni na kufika kwenye ardhi na huko yakenda chini na kutimbuka katika chemchem, hakukuwa kunajuulikana kabla ya katikati za karne ya nane tangu kuzaliwa Nabii Isa a.s. Fikra iliyo zagaa kabla ya hapo ni kuwa maji ya chemchem na mito yanatimbuka kutoka chini ya ardhi kutoka kwenye mashimo na visima katika vina vya bahari.
- 39:22٢٢
Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisio mkumbuka Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika upotofu wa dhaahiri. [22]
Tanbihi
[22] Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kufunguliwa kifua chake na Mwenyezi Mungu kwa Uislamu kwa kupokea mafunzo yake, na akawa na utambuzi unao tokana na Mola wake Mlezi, huyo basi ni kama yule anaye kataa kuangalia Ishara zake? Basi hao ambao nyoyo zao zimekuwa ngumu hata hawamkumbuki Mwenyezi Mungu watapata adhabu kali! Hao wenye nyoyo ngumu wameitupa Haki iliyo wazi.
- 39:23٢٣
Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa. [23]
Tanbihi
[23] Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, nayo ni Kitabu ambacho zimeshabihiana maana zake na matamko yake kwa kufikilia ukomo wa kuwashinda watu kuleta mfano wake, na hukumu zake. Mawaidha na hukumu zinakaririwa, kama kunavyo kaririwa kusomwa kwake. Kinapo somwa Kitabu hicho na kikasikiwa maonyo yake, ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi hukunjika, na kisha hulainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hicho Kitabu kilicho kusanya sifa hizi ni Nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo kwayo humwongoa amtakaye, ikamwezesha kufikilia kumuamini Yeye. Na anaye achwa na Mwenyezi Mungu apotee kwa kumjua kuwa tangu hapo ataiacha Haki, basi hapati mwongozi wa kumwokoa na upotofu wake.
- 39:24٢٤
Je! Atakaye kuwa anapambana kwa uso wake na adhabu mbaya kabisa Siku ya Kiyama (ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye kudhulumu: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyachuma! [24]
Tanbihi
[24] Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kuikinga adhabu ovu, kali, kwa uso wake Siku ya Kiyama baada ya kuwa mikono yake imetiwa pingu, ni kama anaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Na wenye kudhulumu wataambiwa: Onjeni laana ya vitendo vyenu!
- 39:25٢٥
Walio kuwa kabla yao walikadhibisha , na ikawajia adhabu kutoka pahala wasipo patambua. [25]
Tanbihi
[25] Walikanusha walio kuja kabla ya washirikina hawa, ikawajia adhabu kutoka upande wasio utaraji.
- 39:26٢٦
Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangeli jua! [26]
Tanbihi
[26] Mwenyezi Mungu akawaonjesha unyonge katika maisha ya duniani. Ninaapa: Hakika adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi kuliko ya duniani, lau kwamba walikuwa ni watu wa kujua na kuangalia!
- 39:27٢٧
Na bila ya shaka tumewapigia watu mifano ya kila namna katika hii Qur'ani ili wapate kukumbuka. [27]
Tanbihi
[27] Na bila ya shaka tulikwisha wabainishia watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano wa kuwakumbusha Haki, kwa kutaraji kuwa watakumbuka na watawaidhika.
- 39:28٢٨
Qur'ani ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu. [28]
Tanbihi
[28] Tumeiteremsha Qur'ani ya Kiarabu kwa ulimi wao, haina upungufu, kwa kutaraji kuwa watamcha na watamwogopa Mola wao Mlezi.
- 39:29٢٩
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana washirika wanao gombana, na wa mtu mwengine aliye khusika na bwana mmoja tu. Je! Wako sawa katika hali zao? Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! Lakini wengi wao hawajui. [29]
Tanbihi
[29] Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mshirikina kama mtumwa aliye milikiwa na watu kadhaa wenye kushirikiana, na wenye kumgombania. Na mfano wa mwenye kuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kama mtu ambaye amemilikiwa na mtu mmoja tu. Je hao wanakuwa sawa? Alhamdulillahi kwa kusimama hoja mbele ya watu. Lakini watu wengi hawaijui Haki.
- 39:30٣٠
Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa. [30]
Tanbihi
[30] Hakika wewe, Muhammad, na wao wote mtakufa.
- 39:31٣١
Kisha bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi. [31]
Tanbihi
[31] Kisha baada ya kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa nyinyi.
Tafsiri: Ali Mohsin Al-Barwani (Ali Mohsin Al-Barwani) — Chanzo: QuranEnc.com · v1.0.1 · Translated by Ali Mohsen Al-Barwani